Himaya ya Natron iliongozwa na mfalme Bazi, kiongozi mchapakazi na mwenye upendo kwa wananchi wake. Mfalme alikuwa na wake watatu na watoto wanne. Mke wa kwanza, malkia, aliitwa Omuro. Alimzalia mfalme watoto wawili; wa kwanza wa kiume aitwaye Noro, na wa pili wa kike aitwaye Sinta. Kuzaliwa kwa Sinta, binti, kulipelekea mfalme na wazee wa baraza kupitisha pendekezo la mke wa pili. Na wa tatu.
Wake wa pili na watatu wa mfalme walipewa vyeo vya Ledi, yaani, wanawake pendwa wa mfalme baada ya malkia. Mke wa pili aliitwa Ledi Erini naye alimpatia mfalme mtoto wa kiume aliyeitwa Antivo. Mke wa tatu, Ledi Kompa, alibahatika kupata mtoto wa kiume pia na kumuita Avana. Hiyo ndiyo iilikuwa familia ya mfalme Bazi.
Japokuwa familia hiyo ilibarikiwa mali nyingi, utashi na afya njema, walikuwa na mila moja; sheria iliyoamua hatima zao wote. Mila hiyo ilikuwa; kila mke wa kwanza wa mwanamume mwenye damu ya kifalme ndani yake alipaswa kutolewa sadaka kwa mizimu yao. Ndiyo; ukoo mzima wa mfalme uliabudu mizimu. Kutokana na hili, mtoto wa kiume afikishapo umri wa kuoa, familia nzima na makuhani walifanya tambiko ili mizimu iwaoneshe mwanamke watakaependezwa naye ili aolewe kama mke wa kwanza kisha kufanywa sadaka.
…
Giza zito lilitanda. Mvua nyingi zilinyesha na radi ziliunguruma kila pembe. Miti ilikuwa kwenye hatihati za kupoteza matawi yake kwa upepo mkali uliovuma. Wananchi wa Natron waliichukulia kama hali ya hewa ya kawaida kwani himaya yao ilizungukwa na milima mirefu.
Mfalme Bazi na familia yake walizunguka madhabahu. Meza ilifunikwa na vitambaa vyeusi na vyekundu na juu yake kulikuwa na fuvu la binadamu lililozungukwa na mishumaa kumi. Familia nzima ilivaa mavazi meusi. Wote walikuwa wakinena maneno yasioleweka ili kuita mizimu yao. Avana, mwana wa Kompa, alikuwa amefikia umri wa kuoa. Tambiko lile lilimuhusu yeye. Walihitaji mizimu iwaelekeze kwa binti watakaependezwa naye kwa kafara.
Kuhani aliyekuwa akiongoza tambiko alishika mbuzi aliyewakilishwa na familia ya mfalme. Mbuzi alikuwa mweusi na aliyenona. Kuhani alikamata kisu na kuchinja mbuzi kwa umakini mkubwa. Alikinga bakuli na kuacha damu ichuruzikie ndani. Bakuli ilipojaa aliiwasilisha mbele ya madhabahu.
"Naita mizimu yote ya familia hii tukufu. Jongeeni kwetu mtuoneshe muelekeo. Kijana wetu, Avana, mwana wa Bazi, amefikisha umri wa kuoa, na kwa heshima ameitikia wito wa kumtoa kafara mke wake wa kwanza kwenu. Tunaomba mtuelekeze sisi tulio hai, ili tuweze kuwaridhisha.", kuhani alitamka maneno yale kwa sauti.
Radi ilipiga ndani ya bakuli ya damu na moshi ulifuka. Wote waliacha kunena. Kuhani aliusoma moshi ule kwa umakini. Yeye pekee ndiye aliyeweza kuona maono ya mizimu. Mizimu iliweka wazi mapendeleo yao. Kuhani alioneshwa binti mweupe, mrefu, mnene kidogo, na mwenye mvuto. Binti huyo alikuwa shambani akisaidiana na wazazi wake kuvuna mahindi. Alionekana kuwa mchangamfu, lakini pia masikini.
"Mizimu imejibu.", alisema kuhani kwa furaha,
Familia nzima ilivuta pumzi ya auheni. Ledi Kompa alimshika Avana mkono kwa kujivunia. Avana alikuwa ni mtoto wa mwisho wa mfalme. Mizimu kumjibu ilionesha kuwa ilimtambua Avana kama sehemu ya ukoo mtukufu hivyo mapenzi ya mfalme kwake yataongezeka.
"Umeweza kumtambua huyo binti?", mfalme alimuuliza kuhani,
"Bila shaka, mfalme. Namfahamu yeye na familia yake.",
"Basi tunakuachia kazi ya kumleta ikulu.",
"Sitakuangusha.",
Sinta alitupa jicho la husuda kwa Ledi Kompa na Avana.
***