Chapter 9 - KOCHA

Gema alivalishwa mavazi ya usiku na kupanda kitandani. Hakuwa na usingizi lakini ratiba haikumruhusu kufanya jambo lolote hivyo aliona ni bora akae kitandani na kuutafuta usingizi ulipo. 

Mone, muhudumu wake, alianza kuzima mshumaa mmoja baada ya mwingine. Kabla ya kuzima mshumaa wa mwisho ilisikika hodi mlangoni. Mone aliacha mshumaa uwake na kwenda kufungua mlango. Macho yake yalipokutana na macho ya mbisha hodi, alipigwa na butwaa. Mgeni alikuwa Avana, mwana wa mfalme, mme mtarajiwa wa Gema.

Mone aliinamisha kichwa haraka;

"Nimekuja kumuona mke wangu mtarajiwa.", alisema Avana.

Gema aliposikia maneno hayo alitoka kitandani mbio na kukimbilia kwenye kioo. Mwanga ulikuwa hafifu kwani ni mshumaa mmoja tu uliokuwa unawaka, lakini aliweza kujiangalia na kurekebisha pale alipoona hapako sawa.

Gema alirudi kusimama pembeni ya kitanda chake akisubiri. Avana aliingia ndani na macho yake hayakutazama kitu kingine zaidi ya Gema. Ukweli ni kwamba, Gema alikuwa na mvuto wa ajabu, na wala Avana hakuhitaji mishumaa hamsini kuona hilo.

"Karibu, mume wangu mtarajiwa.", Gema alitamka kwa upole.

Sauti yake ilimsisimua Avana na kumuacha akitabasamu, "Nimeshakaribia. Naomba unisamehe kwa kutokuja kukutembelea siku zote hizi. Nilikuwa sitaki kuja mikono mitupu hivyo hizi siku zote nilikuwa nikitafuta zawadi itakayokufaa.", alisema.

Mone alijua kuwa Gema hatolala muda wowote wa karibu, "Mnahitaji kitu chochote?", aliwauliza,

"Tutahitaji chai na tende.", alisema Avana.

Mone aliondoka kwenda kufata alichotumwa. Huku, Gema alimkaribisha Avana waketi. Avana alitoa cheni nzuri ya dhahabu kutoka kwenye mfuko wa vazi lake.

"Naweza kukuvalisha?", aliuliza,

"Ndiyo.",

Gema alikusanya nywele zake na kuzilaza begani kisha Avana alifunga cheni shingoni mwa Gema. Ilimpendeza sana. Avana alirudi kwenye kiti chake na kuketi.

"Umeipenda?", aliuliza tena,

"Nimeipenda sana.", Gema alitamka kwa furaha isiyo na kifani, "Asante sana.",

"Itabidi uzoee. Takuwa nakupa zawadi mpaka ukose sehemu ya kuziweka.",

Gema alicheka. Sasa moyo wake ulikuwa umesuuzika. Mawazo yote ya kukata tamaa na kurudi kijijini yaliyeyuka kama barafu juu ya chungu cha moto. Alisahau dhiki na misongo ya mawazo iliyokuwa ikimsumbua tangu mguu wake ukanyage ardhi ya ikulu. Kitu pekee alichokuwa akiwaza sasa ilikuwa ni jinsi ya kumridhisha mume wake mtarajiwa.

Sinta aligeuza kiti chake dirishani ili atazame mwezi. Yurie, muhudumu wake, alisimama nyuma ya kiti akichana nywele za Sinta kwa umakini mkubwa. Mezani kulikuwa na kikombe cha maziwa ya uvuguvugu yaliyochanganywa na binzari ya manjano; kinywaji ambacho Sinta alikunywa kila usiku kabla ya kulala. Muhudumu alijitahidi sana nywele zisirukie ndani ya kikombe cha mkuu wake maana adhabu yake isingekuwa ya kitoto.

"Nini kinaendelea upande wa pili?", Sinta aliuliza,

"Mfalme Bazi alionwa akimkumbatia Aera.", alisema Yurie.

Ukiachana na uhudumu, Yurie pia alikuwa jasusi wa Sinta.

"Aera ndio nani?", Sinta aliuliza,

"Dada wa konsoti Gema.",

"Anhaa, yule msichana?",

"Ndiyo.",

"Kwahiyo unasema baba yangu ameonwa akikumbatiana nae?",

"Ndiyo. Ledi Erini na ledi Kompa walikuwepo hayo maeneo na kuwaona.",

"Mama yangu alikuwepo pia?",

"Hapo sijajua.",

Sinta alicheka kidogo kisa kusonya, "Unahisi mfalme anafikiria nini?", aliuliza.

"Sifahamu. Kitu nachofahamu ni kwamba leo jioni mfalme Bazi alikwenda kumuona kuhani mkuu.", Yurie alieleza,

"Tarura?", Sinta aliuliza kwa mshangao, "Mfalme kaenda kumuona Tarura?",

"Ndiyo. Hivyo Tarura atakuwa na majibu ya maswali yako yote.",

"Bila shaka.",

"Unataka nifanyeje?",

"Fatilia nyayo za Tarura kisha uniletee majibu.", Sinta alitoa amri.

"Sawa, binti mfalme.",

Sinta alinyanyua kikombe chake cha maziwa na kuanza kunywa taratibu.

***