Chapter 6 - SALAMU

Wahudumu walitenga chakula cha mchana mezani. Kusini mwa meza aliketi ledi Kompa, na kaskazini mwa meza alikaa Gema. Yalikuwa matembezi yake ya pili. Tayari alikwishakunywa chai ya asubuhi na malkia. Sasa alikuwa na mama mkwe mtarajiwa. 

Huku wakila, ledi Kompa alimkagua Gema kwa macho. Kila kona ya mwili wa Gema iliyoonekana, ledi Kompa alipitisha macho yake hapo. Japo kuwa Gema hakuwa kwenye mipango ya kuwa mke wa milele wa Avana, bado mama mkwe hakutaka binti wa ovyo.

Katika ukaguzi wake, hakuona kasoro hata moja. Gema alikuwa msafi mpaka kwenye kucha. Alikuwa mrembo na wasaidizi wake walimchagulia mavazi mazuri ya siku hiyo. Alikuwa na nidhamu. Vyote hivyo vilimuongezea alama.

"Umekipenda chumba chako?", ledi Kompa alimuuliza, "Mimi ndiye niliyekichagua kwa ajili yako.",

"Ndiyo, ledi Kompa. Nimekipenda sana.", Gema alijibu kwa utaratibu,

"Ulilala vizuri?",

"Ndiyo, ledi Kompa.",

Ledi Kompa alitabasamu na kutikisa kichwa.

"Una bahati sana kupata hii nafasi.", aliendelea, "Mabinti wengi wamepambana ila wewe ndiye mshindi. Una kila haki ya kuhisi umebarikiwa na miungu. Bila mwanangu kukupenda, wewe na familia yako mngekuwa bado mpo shambani mnalima sasa hivi. Avana ndiye mkombozi wako. Unatambua hilo?",

"Natambua, ledi Kompa.", Gema alijibu bila hiana,

"Hivyo mwanangu akikuomba chochote mpe. Usimbishie. Muheshimu. Mtii. Msujudu kama unavyosujudia wazazi wako. Umesikia?",

"Ndiyo, ledi Kompa.",

Gema alitamani sana kumuuliza ledi Kompa kuhusu mwanae lakini alijua lisingekuwa jambo la busara.

"Dada yako anaitwa nani? Nimesahau jina lake.", ledi Kompa aliuliza.

Alikuwa mtu wa pili sasa kumuuliza Gema kuhusu Aera. Ledi Kompa ndiye alikuwa mke mdogo wa mfalme. Alipendelewa kuliko wake wote wa mfalme na hii ni kwasababu alikuwa mke wa mwisho. Alihofia kuwa mfalme akiongeza mke mwingine, zile starehe zake zote zitapungua. Hakutaka itokee.

Upande mwingine, Gema hakufahamu kwanini Aera alikuwa kwenye hoja ya kila mazungumzo. 

"Dada yangu anaitwa Aera.", alijibu,

"Aera. Jina zuri.", alisema ledi Kompa, "Aera amechumbiwa?",

"Hapana, ledi Kompa.",

"Hayupo kwenye mahusiano?",

"Ndiyo, ledi Kompa.",

Ledi Kompa alinuna. Aera alikuwa tishio ila hakutaka liwe tishio kubwa kwani yeye alikuwa na nguvu zaidi yake.

Kabla ya kurudi kwenye makazi yake, Gema alikwenda kumsalimu mtu wa mwisho; Sinta. Tayari ilikuwa jioni, giza limeingia. Njia nzima alikuwa akiiwaza familia yake. Je, wameshindaje? Wamekula? Wanafanya nini sasa hivi? Kiujumla, Gema alikumbuka sana familia yake. Ingawa wote waliishi ikulu, utenganisho ule haukuwa na afadhali.

Makazi ya Sinta yalikuwa mbali na makazi mengine. Ikulu ilikuwa kubwa. Walipowasili, muhudumu wa Sinta aliwazuia mlangoni. Macho yake yalionesha hofu.

"Tumekuja kumuona Sinta, binti wa mfalme.", alisema Mone, muhudumu wa Gema.

Gema alikuwa amesimama nyuma yake akisubiri. 

"Hamuelewi? Sinta yupo na mgeni.", alisema muhudumu wa Sinta,

"Huyo mgeni ni muhimu kuliko konsoti Gema?",

"Hap-hapana. Lakini _",

"KUNA NINI HUKO NJE?", ilisikika sauti ya Sinta kutoka ndani ya chumba.

Muhudumu wake alikimbilia mlangoni na kuinamisha kichwa, "Konsoti Gema amekuja kukusalimu.", aliongea kwa kutetemeka kidogo, "Nimemwambia una mgeni.",

Hasira ya Sinta ilikuwa mbaya hivyo wahudumu wake hawakupenda kumkwaza. Sinta alikuwa na cheo cha unyanyasaji. Hakuwa mtu wa kuridhika kirahisi na hakupenda kasoro ya aina yeyote. Wahudumu wake walipewa adhabu nzito kwa makosa madogo madogo, hivyo wengi hawakudumu na kupoteza maisha. Waliobaki walipambana na kufanya kila wawezalo kikamilifu.

"Mruhusu aingie.", alisema Sinta,

"Lakini binti mfalme upo _",

"Nimesema mruhusu aingie.", Sinta aliamuru.

Gema alijongea mlangoni na mhudumu wa Sinta alimfungulia mlango. Gema aliingia ndani lakini alisita kupiga hatua nyingine mbele. Kwa haraka aliinamisha kichwa chini na kufumba macho. Hakuamini alichokikuta.

Sinta alikuwa kajilaza kitandani kwake akiwa uchi. Pembeni ya kitanda alisimama mwanaume mwenye mwili wa kishupavu. Naye pia alikuwa uchi wa mnyama. Nguo za mwanaume zilikuwa sakafuni. Hazikuwa nguo za gharama. Alikuwa ni miongoni mwa wanaume wa uchumi wa chini ambao Sinta aliwalipa ili wamburudishe kimwili.

Gema alianza kurudi nyuma taratibu, lakini;

"Unakwenda wapi?", Sinta alimuuliza,

"Naona upo _",

"Na mgeni? Muhudumu wangu aliwaambia nipo na mgeni ila mkawa ving'ang'anizi. Sasa unajifanya unaogopa nini? Nigeukie.",

"Siwezi.", Gema aligoma,

"Nimesema nigeukie!",

"Mpo uchi.",

"Kwani kitu gani ni kigeni? Hata wewe maziwa unayo, kila nilichonacho unacho. Usijifanye una aibu. Nimesema niangalie. Usipofumbua macho takuadhibu kwa kutonitii.",

Aliposikia hivyo, Gema alinyanyua uso haraka na kufumbua macho. Haikuwa picha nzuri kuitazama lakini alijitahidi. Sinta aliangua kicheko huku akipiga makofi.

"Umeshawahi kumuona mwanaume akiwa uchi?", aliuliza.

Gema alitikisa kichwa kukataa. Sinta alicheka zaidi.

"Hivi una miaka mingapi?",

"Kumi na nane.",

"Mtu mzima kabisa alafu hujawahi? Haya, leo umepata nafasi ya kumuona mwanaume akiwa uchi. Nimekupa ruhusa ya kumshika.",

Gema alimtazama mwanaume yule machoni na kuona kuwa alikuwa na hali kama yake. Alimuhurumia.

"Hutaki kumshika?", Sinta aliendelea kuuliza,

"Hapana, siwezi. Mimi ni mke mtarajiwa wa kaka yako. Ni mwili wake pekee ndio naruhusiwa kuushika.", alisema Gema.

Sinta alimsonya, "Unajua nachukia sana watu kama nyie.", alisema, "Mnajifanya wapole kumbe mnajua mambo kuliko sisi. Nafahamu mabinti wengi kama wewe.",

Gema hakuweza kujibu. Alitamani sana aondoke lakini alishindwa kutokana na amri aliyopewa.

"Najua unajiuliza kwanini nalala na wanaume wa uchumi wa chini na sio wale wa juu.", Sinta alieleza, "Hawa wa uchumi wa chini wanachapa kazi. Wakulima, wavuvi wana nguvu ya ziada. Hawa wanaume matajiri kazi yao ni kunenepeana tu. Hawajui chochote kuhusu mwili wa mwanamke.",

"Naweza kuondoka sasa?", Gema aliuliza. Hakutaka kubaki mule ndani hata sekunde moja.

"Kabla hujaondoka nina swali.", 

Gema alimuangalia, "Swali gani?",

"Utamwambia mtu yeyote ulichokiona na kukisikia humu ndani?",

Gema alitikisa kichwa, "Hapana.",

"Na iwe hivyo. Nikisikia minong'ono ya aina yeyote, takata kichwa cha baba, mama na dada yako mbele ya macho yako. Huo mdomo wako utumie kula tu.",

Gema alisikia jinsi damu yake ilivyokuwa ikichemka ndani. 

"Unaweza kwenda.",

Bila kusubiri, Gema alitoka nje ya chumba kile na hakugeuka nyuma. Alichapa mwendo kwa hasira. Wahudumu wake walimfata nyuma kwa kasi maana Gema alikuwa akitembea haraka. Machozi yalimlengalenga. Hakuwahi kudharirika namna ile. Alitamani sana awe na familia yake. Wao pekee ndiyo wangeweza kumliwaza.

***