Usiku huo, malkia Omuro alikwenda kwenye makazi ya Gema. Haikuwa kawaida malkia kutembelea nyumba za makonsoti hivyo hata wahudumu hawakujua wafanyeje. Malkia aliomba usiri na Gema.
Gema alimimina chai kwenye vikombe vyao huku mikono ikimtetemeka. Alikuwa na mashaka juu ya vingi.
"Unajisikiaje?", malkia Omuro alimuuliza,
"Kuhusu nini, malkia?", Gema nae aliuliza,
"Hali ya dada yako?",
Gema alijikaza, "Amefanya uhalifu hivyo anastahili kuadhibiwa.",
"Kwa kunyongwa?",
"Siwezi kutoa maoni juu ya hukumu ya mfalme.",
Malkia alicheka kidogo.
"Aera alikwambia nini jana?", aliuliza,
"Alini-aliniambia kitu cha uongo, na cha _ na cha kutisha.", Gema alisema kwa kigugumizi.
"Kiseme.",
"Malkia, ni kitu kibaya _",
"Nimesema kitaje hicho kitu.",
Gema alimeza fundo zito la mate lililomkaba kooni.
"Aera alisema kwamba nimekuja hapa kutolewa sadaka.", Gema alieleza.
Cha kushangaza, malkia Omuro hakushtuka.
"Nisamehe malkia. Najua ni uongo hivyo _",
"Kama ni kweli je?", malkia alimuhoji.
"Sio kweli. Haiwezi kuwa kweli?",
"Kwanini?",
"Kwa sababu nyie ni watu wazuri na wenye busara.",
Malkia alicheka tena, "Umekutana na sisi siku chache tu zilizopita. Unaacha kuamini maneno ya dada yako, unatuamini sisi? Eti kisa tuna busara? Nani kakwambia?",
Gema aliwekwa njia panda.
"Dada yako anakwenda kunyongwa kesho lakini huoneshi hata huruma. Mimi malkia nipo mbele yako lakini sijasikia ukiniomba niokoe maisha ya dada yako. Je, hivi ndo ndugu wanavyotakiwa kuishi?",
"Malkia, mimi _",
"Hivi unahisi dada yako akifa utaweza kusonga mbele? Hapana. Utaishi siku zako chache kwa majonzi na majuto. Utatamani kumuomba msamaha lakini hautaweza. Tamaa zako zitakufanya ukose kila kitu.",
Gema alijisikia vibaya lakini sauti zilikuwa zikikinzana. Hakuwaza ya sasa bali yajayo.
"Malkia, ninakwenda kuwa mke wa Avana. Mchumba wangu ananipenda. Aera amechagua mwenyewe njia yake nami nimeshachagua njia yangu.",
"Gema, nisikilize kwa makini; kila kitu kinachoendelea hakikuhusu wewe bali Aera. Sababu ya wewe kufika hapa ilikuwa ni kumleta Aera karibu, hivyo unaweza kuondoka na janga lolote lisikukumbe.",
"Siwezi kuondoka!", Gema alicharuka, "Hii ni bahati yangu.",
"Unaiita bahati wakati dada yako anakwenda kunyongwa? Mpumbavu nini? Fumbua macho yako, binti.",
Gema alianza kulia, "Malkia, tafadhali usinipokonye baraka yangu.", aliomba.
"Tayari nimeshafanya uamuzi. Nakupa siku chache sana za kujiandaa. Nakurudisha kijijini kwenu.",
Gema aliangukia magoti na kuanza kulia kwa uchungu.
"Hapana, malkia. Naomba usiniondoe. Tafadhali.", alilia.
Malkia Omuro alinyanyuka na kuondoka bila kumuhurumia.
Gema alipiga sakafu kwa hasira.
…
Asubuhi ilipofika, ikulu nzima ilikuwa imeshajua kuhusu kupotea kwa Aera. Hakuna iliyemuingia akilini. Wengi waliamini kuwa alitoroshwa, lakini zilikuwa hoja za chinichini. Walinzi walitumwa kila kona ya ikulu na nje ili kumtafuta maana kwa hali aliyokuwa nayo, uwezekano wa kufika mbali ulikuwa haupo. Walinzi wa zamu waliadhibiwa vilivyo kwa uzembe wao. Kwa bahati nzuri, Sinta na mchezo wake haukuwekwa wazi.
...
Siku iliisha haraka zaidi ya ilivyoanza. Jua lilipozama, familia ya mfalme ilikutana bwaloni kwa ajili ya chakula cha usiku cha pamoja. Nje mvua kali ilikuwa ikinyesha na radi ziliunguruma. Mezani, malkia Omuro na Sinta waliangaliana kila dakika kwa wizi kwani walikuwa wakifikiri kitu kimoja. Sinta hakuwa amemwambia mfalme ukweli, hivyo malkia alikuwa akielekea kuliweka jukumu mikononi mwake mwenyewe.
Kawaida, meza huwa na vistori mbalimbali vya kuwachangamsha wakiwa wanakula, lakini usiku huo kila mtu alikuwa kimya, hadi mfalme Bazi.
Ghafla, zilisikika sauti za vurugu nje ya malango ya bwalo la chakula. Zilikuwa kelele za mbio za walinzi wakielekea sehemu moja. Hiyo ilikamata umakini wa kila mtu. Wote walitaka kujua kilichokuwa kikiendelea. Ghafla kukawa kimya tena, sauti ya mvua na radi ikirejea masikioni mwao. Kisha ilisikika hodi, mara moja, na baada ya hapo milango ilifunguliwa na upepo mkali.
Wote waligeukia mlangoni, na midomo yao ilibaki wazi baada ya kumuona Aera kasimama. Alionekana wa tofauti sana; hakuwa na baka wala upele. Nywele zake zilikuwa safi, ndefu, na laini, zikipepea kama upepo. Alivaa gauni refu, jeusi la hariri, na mkufu wake wa almasi ulitakasa shingo yake. Alikuwa ametakata.
Walinzi walianza kumfata kwa kasi, lakini Aera alinyanyua kidole chake na papo hapo miguu ya walinzi iliganda sakafuni. Hakuna aliyeweza kupiga hatua mbele. Woga uliivaa familia ya mfalme kama sunami. Hakuna aliyethubutu kunyanyuka.
"Salamu, familia tukufu ya mfalme.", alisema Aera huku akijongea meza taratibu, "Msishangae sana. Ulimwengu una mambo mengi.",
"Umefata nini?", mfalme aliunguruma, "Umekuja kutudhihirishia uchawi wako?",
"Oh, hapana, mfalme mtukufu Bazi. Nimekuja kuwajuza kuhusu uhalisia wa wote mliopo mezani. Miungu imenifumbua macho na kunionesha maono.", aliwajuza, "Ndani ya familia hii kuna roho nne; roho ya nyoka, roho ya simba, roho ya nge, na roho ya mwezi. Mwezi utauliwa na nyoka, nyoka ataumwa na nge, na hatimaye nge atakanyagwa na simba.",
Aera alikamata jagi la maji na kuyageuza kuwa damu. Wachache walipiga kelele ila wote waliogopa sana. Haja ndogo na kubwa ziliwabana. Aera alimwaga damu juu ya sahani ya mfalme Bazi.
"Janga kuu linajongea familia yako mfalme. Wengi wenu mtapoteza maisha. Watakaobaki watakuwa zaidi ya vichaa.", Aera alitabiri.
"Kila janga linaweza kuepukika.", malkia Omuro alisema, "Hivyo tafadhali, tunaomba utueleze jinsi ya kuepuka janga hili.",
Aera alitabasamu, "Utabiri wangu utaanza leo usiku. Nyoka atakwenda kumuuma mwezi na kumuua. Bila mwezi, familia ya mfalme itaingia kwenye giza kali. Hivyo njia pekee ya kuepuka janga hili ni kuokoa maisha ya mwezi. Mwezi ukiiona asubuhi ya kesho, kila kitu kitakuwa sawa.",
Aera aliweka jagi chini na kuondoka bwaloni. Milango ilijifunga yenyewe na walinzi walirudishiwa uwezo wao wa kutembea. Kila mtu alilowa jasho.
"Mfalme ndiye mtu mkuu kuliko wote kwenye himaya yetu.", alisema Noro, kijana wa kwanza wa mfalme, "Bila shaka yeye ndiye mwezi.",
"Mmesikia maneno ya Aera.", Antivo aliongezea, "Tukifanikisha kuwa mfalme anaamka asubuhi akiwa salama salmini, utabiri wake hautatimia.",
Wote walikubaliana nao.
"Mfalme atakwenda kupumzika akiwa na ulinzi mara kumi zaidi. Wengine tukeshe tukiomba. Mtabiri mmoja hawezi kuwa na nguvu zaidi yetu.", alisema Noro.
Wote walirudi kwenye makazi yao haraka. Karibia walinzi wote walizunguka makazi ya mfalme kumlinda na hatari yoyote. Wana wa kiume wa mfalme walikuwa karibu na baba yao, wote wakimtazama na kukataa kusinzia. Usiku ulikwenda taratibu na hatimaye jua lilichomoza.
…
"TANZIA! TANZIA!", alisema mjumbe wa mfalme akikimbia huku na huku kwa jazba na hamasa, "AMKENI! TANZIA! TANZIA!",
Watu wote walikurupuka vitandani mwao na kutoka nje.
"TANZIA! TANZIA! MALKIA OMURO AMEAGA DUNIA!".
***