Chereads / THE PRIESTESS' PROPHECY (Book 1) / Chapter 7 - ULIMI WA SUMU

Chapter 7 - ULIMI WA SUMU

Baada ya chakula cha usiku, Aera alikwenda kutembea nje. Upande wa ikulu ambao waliwekewa makazi yao ulikuwa kimya sana. Hakukuwa na watu zaidi yao. Mida ya chakula cha asubuhi, mchana na jioni ndipo watu walikuja ili kuwaletea milo. Baada ya hapo waliachwa peke yao.

Aera alitembea polepole huku akipendezwa na kila alichokiona; bustani, nyota za angani na mawe ya ardhini. Kwa muda mrefu aliotembea, aliweza kuona tofauti kati ya masikini na matajiri. Ikulu ilifanana na dunia nyingine ambayo kila kitu kilivutia zaidi ya kingine. Hatimaye alifika kwenye bwawa kubwa la samaki. Maji yalikuwa yametulia tuli. Sauti ya vyura ilitawala eneo hilo. Aera alikaa kitako juu ya jiwe kubwa lililokuwa pembezoni mwa bwawa.

"Sijui Gema anafanya nini sasa hivi?", alijiuliza kimoyomoyo, "Vumilia kidogo tu, mdogo wangu. Tafanya kila kitu kukuokoa.",

Alitumia muda ule kuwaza na kuwazua. Akiwa kwenye msongo wa mawazo, alishindwa kusikia sauti ya hatua zilizokuwa zikijongea bwawani pia. Mtu huyo alisimama nyuma ya Aera kwa muda mfupi akimtazama ila Aera wala hakuhisi uwepo wake.

"Aera?", mtu huyo aliita.

Kwa mshtuko kidogo, Aera aligeuka nyuma. Hakutegemea kukutana macho kwa macho na mfalme Bazi. Aera alinyanyuka haraka na kuinamisha kichwa.

"Mfalme.", alisema, "Nisamehe. Sikujua upo hapa.",

Mfalme Bazi alikuwa peke yake. Yeye pia alikuwa kwenye matembezi ya jioni. Lakini haikuwa kawaida yake kutembelea maeneo hayo ya ikulu. Dhumuni la yeye kufika hapo lilikuwa mbele ya macho yake.

"Usiwe na wasiwasi. Kila mtu ana mawazo.", alisema mfalme Bazi kwa upole, "Mbona upo mahali hapa usiku wote huu peke yako?",

"Nimekuja tu kusafisha macho na kuchangamsha akili, mfalme.", Aera alisema, kichwa kikiwa bado kimeinamishwa,

"Unaweza kunyanyua uso wako. Sitakuhukumu.",

"Hapana, mfalme. Haitaleta heshima _",

"Mimi ndiye nimekuomba uniangalie. Nimekupa ruhusa.",

Aera hakuweza kumbishia mfalme. Alinyanyua sura yake na kumtazama. Kwa mara nyingine tena mfalme Bazi alionesha mshangao japo kuwa haukuwa mkubwa kama alipomuona kwa mara ya kwanza.

"Aera, una miaka mingapi?", aliuliza mfalme Bazi,

"Nina miaka 25, mfalme.",

"Miaka 25?", mfalme Bazi alikunja sura. Alikuwa akichanganua jibu la Aera, "Wewe ndiye mtoto wa kwanza wa baba na mama yako?",

"Ndiyo, mfalme.", Aera alijibu bila kuelewa muelekeo wa mazungumzo hayo.

"Samahani. Naomba kuuliza kama hautojali.", mfalme Bazi aliendelea,

"Bila shaka, mfalme.",

"Hawa ni wazazi wako kweli?", 

"Unamaanisha nini?",

"Huyu ni mama na baba yako wa kukuzaa?", mfalme aliuliza tena,

"Ndiyo, mfalme mtukufu. Hawa ni wazazi wangu wa kunizaa na Gema ni mdogo wangu wa damu. Kwanini unauliza?",

"Kuna mtu umefanana nae sana, sana.", mfalme alisema kwa msisitizo, "Kuanzia uso mpaka sauti.",

"Mtu gani huyo, mfalme wangu?", Aera aliuliza kwa hamu ya kujua.

"Alikuwa rafiki yangu mpendwa. Tangia afariki, sijawahi kupata rafiki mwingine kama yeye.", mfalme alilengwa na machozi, "Naweza kukukumbatia, Aera?",

Aera alitabasamu, "Bila shaka, mfalme.",

Mfalme alimkaribia Aera na kumkumbatia. Aera hakuwa na woga wala wasiwasi. Mfalme alikuwa kama rafiki wa karibu. Alimpa Aera amani ya moyo muda wote alimokuwa kwenye kumbato lake. 

Lakini ikulu ilikuwa na macho kila kona. Mashariki mwa bwawa alikuwepo ledi Erini, na magharibi mwa bwawa alisimama ledi Kompa na muhudumu wake. Wanawake hawa hawakuonana lakini macho yao yalitazama eneo moja tu. Mioyo yao ilipata joto. Hasira zao hazikumuelekea mfalme bali aliyekumbatiwa nae.

Gema alijiangalia tena kwenye kioo. Wahudumu wake walisimama nyuma yake. Tayari walikuwa wamemaliza kumuandaa kwa ajili ya siku mpya. Ila siku hiyo ilikuwa muhimu zaidi kwani hatimaye mama yake alipewa ruhusa ya kuvuka geti na kuja kumtembelea. Hakutaka kumpatia mama yake mashaka, hivyo alitaka aonekane mrembo zaidi na mwenye furaha. Alipenda kazi waliyofanya wahudumu wake. Alipenda muonekano wake.

Wahudumu wa jikoni walitenga chai na vitafunwa mezani kisha kuondoka. Baada ya muda mfupi, Foni aliwasili kwenye makazi ya binti yake. Gema alikimbia kutoka chumbani kwake kwenda kumlaki mama yake. Alidhani ya kuwa ataweza kujikaza, lakini alipomuona mama yake machozi yalianza kumtoka. Alimkumbatia mama yake na kuanza kulia papo hapo. Foni aliweza kujikaza kwa sababu wote wangelia hakuna ambaye angeweza kumnyamazisha mwenzie.

"Usilie, mama yangu.", alisema Foni akimpapasa Gema mgongoni, "Tupo pamoja.",

"Nimewakumbuka sana, mama.", Gema alilia, "Nimefurahi sana kukuona.".

Gema alimkaribisha mama yake kwenye makazi yake rasmi. Waliketi mezani kisha wahudumu wote walitoka nje ili kuwapa nafasi ya kuzungumza kwa amani.

"Mwanangu, unaendeleaje? Upo salama?", Foni aliuliza bila kusubiri,

"Naendelea vizuri, mama. Nyie je?", Gema alisema,

"Mimi, baba yako na dada yako tunaendelea vizuri. Tumekukumbuka sana.",

"Kwanini hamjaja wote? Nataka kuwaona wote.",

"Ili kuepuka usumbufu, ledi Kompa amesema tutakuwa tukikutembelea kwa zamu.",

"Sijui kwanini nahisi hivi, mama.",

"Unahisi nini? Una amani?",

"Nilikuwa sitaki kukwambia lakini sina mtu wa kuongea nae.", Gema alisogeza kiti chake mbele, "Najisikia vibaya. Tokea nifike, mume wangu mtarajiwa hajawahi kuja kuniona. Siku mbili zilizopita nilikwenda kuwasalimu ledi Kompa na Erini pamoja na malkia Omuro. Lakini cha kushangaza kila mmoja alikuwa akiniuliza kuhusu Aera.",

Foni alishangaa, "Kwanini wanamuulizia Aera?",

"Mimi pia sifahamu. Sipendi kwa sababu naanza kujutia kukubali ombi la kuwa konsoti. Bora tungekuwa kijijini kwetu.", Gema alianza tena kulia.

Foni alimshika mwanae mkono, "Gema, hakuna mzazi anayefurahia utajiri huku wanae wakiwa hawana furaha.", alisema Foni, "Hivyo kama unaona huwezi kuwa konsoti sema ili tumwambie kuhani mapema turudi kwenye maisha yetu yenye amani na furaha.",

"Bado sina uhakika, mama. Labda kwa sababu nipo ugenini ndiyo maana.", Gema alijaribu kusuhuzisha mioyo yao,

"Hapana. Naomba ukae upambanue vyote. Ukiona huwezi sema tu usiogope. Mimi nipo pamoja na wewe kwa lolote utakaloamua.",

"Sawa mama. Takujulisha.",

"Pia kuhusu Aera.", Foni aliendelea, "Jaribu kujua ni kwa nini wanawake wa mfalme wanamuongelea. Asije akawa amefanya tukio ambalo hatulijui likaja kukuathiri hadi wewe. Jaribu kuchimbachimba ujue kinachoendelea.",

"Aera sio muharibifu wa mambo. Sidhani kama anaweza kuwa amefanya jambo baya.", Gema alimtetea dada yake.

Foni aliguna, "Sitashangaa nikisia kuwa amefanya chochote.",

"Kwa nini unasema hivyo?",

"Hivi unafahamu ya kuwa Aera hajapenda wewe kuchumbiwa na mtoto wa mfalme?",

"Mh! Ingekuwa hivyo angeniambia _",

"Hapana, nisikilize. Utamaduni wetu unasema kuwa mtoto wa kwanza anatakiwa kuolewa kabla ya wengine. Kitendo cha wewe kuchumbiwa kabla yake kimemkwaza sana, tena haswa kwa sababu umechumbiwa na mtoto wa mfalme. Anaweza kuwa anakuonea wivu ila anashindwa kusema. Ndiyo maana nakwambia uchimbe ujue ni kwanini wake wa mfalme wanamzungumzia. Huwezi jua.", Foni alieleza.

Gema hakutaka kuamini maneno ya mama yake asilimia mia kwa sababu hata yeye pia alimfahamu Aera na aliamini dada yake alimpenda sana hivyo asingeweza kufanya jambo la kumuumiza au kumuharibia.

***