Familia ya mfalme ilikutana kwa ajili ya mazungumzo ya pamoja. Wahudumu walitenga chai na vitafunwa mbalimbali juu ya meza ndefu. Tayari Ledi Kompa, mke wa tatu na mwanae Avana walikuwa wamekwishafika mezani. Huku wakisubiri wengine wawasili, Ledi Kompa alisogea karibu ya mwanae;
"Hakikisha hauongei neno la kumkwaza baba yako.", Ledi Kompa alimuonya huku akinong'ona,
"Usijali mama.", Avana alimuhakikishia,
"Unajua wewe ni mtoto wa mwisho wa mfalme, macho mengi yapo kwako. Wengi wanatamani hili swala lako lisikamilike ili mimi na wewe tufedheheke. Kuwa makini.",
"Mama, usiwe na shaka.",
Malango yalifunguliwa kisha Ledi Erini, mke wa pili, na kijana wake Antivo waliwasili. Kwa ukimya, walikwenda kwenye siti zao maalumu na kuketi. Hakuna aliyemuongelesha mwenzie. Mahusiano yao yalikuwa ya mashaka.
Muda mfupi baadae, malkia Omuro na Noro, mtoto wake wa kiume, walifika kwenye bwalo hilo la chakula. Wote waliokuwemo ndani walinyanyuka na kuianamisha vichwa vyao kama ishara ya heshima kwa malkia. Malkia alipoketi, nao pia waliketi.
Sasa ni viti viwili tu vilikuwa wazi; kiti kikuu cha mfalme, na kiti cha Sinta, binti wa mfalme. Malkia Omuro aligeuza jicho lake kwa Noro. Bila kuongea chochote, macho yake yalikuwa yakimuuliza dada yake yu wapi. Noro alitikisa mabega yake. Hata yeye hakufahamu Sinta alipokuwa. Malkia alisali kimoyomoyo, akiomba Sinta awasili bwaloni kabla ya mfalme maana akifika baada ya baba yake haitaleta picha nzuri kwake yeye kama mama.
Kukiwa na ukimya mkubwa, wote walianza kusikia hatua zikijongea malango ya bwalo. Malkia alitamani sana hatua hizo ziwe za binti yake, huku wake wenzie wakiomba ziwe ni hatua za mfalme. Kulikuwa na mashindano yasiyoonekana kati ya wake wale watatu. Walijua ya kuwa kila jambo walilofanya, mfalme aliwapatia alama, na mwishowe mfalme humpongeza mke aliyefanya vizuri kuliko wote. Ledi Erini na Kompa walitaka sana kupunguza alama za malkia ili wao pia wapandishwe vyeo.
Malango yalifunguliwa na kwa bahati mbaya kwa malkia, alikuwa ni mfalme Bazi na wasaidizi wake. Wote walisimama na kuinamisha vichwa vyao mpaka mfalme alipofika kwenye siti yake. Kabla mfalme hajakaa, alitupa macho kwenye kiti cha Sinta, ambacho bado kilikuwa kitupu. Hakupendezwa na jambo lile hata kidogo. Aliketi kisha wengine kufanya vivyo hivyo.
Malkia hakujua atumie sababu gani ya kujitetea yeye na binti yake, ila aliona ni heri akae kimya.
"Avana anakwenda kupata mke wa kwanza.", mfalme Bazi alianza, "Kama ilivyozoeleka, sisi sote tunapaswa kushirikiana ili jambo hili likamilike. Ledi Kompa?",
Ledi Kompa alimgeukia mfalme, "Abee, mfalme wangu.",
"Wewe ndiye utakayesimamia swala hili zima mpaka mwisho. Gema atawasili ikulu siku tatu zijazo.",
"Bila shaka, mfalme mtukufu.",
"Ledi Erini.", mfalme aliita,
"Abee, mfalme wangu.", Ledi Erini aliitika,
"Hizi hatua zote umeshazipitia kipindi Antivo anaoa mke wake wa kwanza. Nitapenda kama utamuonesha Ledi Kompa usaidizi.",
"Ondoa shaka, mfalme.",
Kabla mfalme hajasema kingine, malango ya bwalo yalifunguliwa na Sinta aliingia ndani. Wote walimgeukia. Sinta hakuonesha dalili yoyote ya woga wala majuto kwa kuwasili baada ya mfalme. Alifika na kuvuta kiti chake kisha kuketi. Malkia Omuro aliuma meno kwa hasira, hasa alipoona kuwa binti yake hakujali.
Mfalme hakuweza kuficha hasira zake;
"Unafika sasa hivi kama nani?", mfalme Bazi aliunguruma,
Sinta alitabasamu kwa kejeli kidogo, "Kwani mimi kutokuwepo kumeharibu lolote?", aliuliza,
Aliacha kila mdomo wazi kwa jibu lake.
Sinta alikuwa ni binti pekee wa mfalme. Katika upekuzi wake, aliweza kujua kuwa yeye ndiye sababu ya mfalme kumuoa Ledi Erini na Kompa. Kuzaliwa kwake hakukumfurahisha mfalme hivyo moja kwa moja Sinta alijiwekea kuwa baba yake alimchukia. Japo kuwa alipenda kuishi kama binti wa mfalme ndani ya ikulu, na kula raha zote zilizokuwepo, hakupenda kujihusisha kiundani kabisa na mambo ya familia yake.
Sinta alikuwa na miaka 23 lakini hakuwa ameolewa na wala hakuwa na mtoto. Starehe yake ilikuwa ni kulala na mwanaume yoyote aliyemvutia, hivyo alitungiwa jina la siri na wale waliofahamu tabia yake; walimwita 'Hanidi', maana yake 'mwenye ulimi wa asali'. Vivyo hivyo alibarikiwa akili nyingi na za haraka hivyo ilikuwa ngumu kumuingia na kumshawishi kwa lolote.
"Utake usitake, wewe ni sehemu ya hii familia.", mfalme alimfokea, "Iwe mwanzo na mwisho hii tabia kujirudia.",
"Ndiyo, mfalme mtukufu.", Sinta aliongea kwa utofanyaji, akijua fika kuwa maneno ya mfalme yaliingilia sikio la kulia na kutokea sikio la kushoto.
"Wifi yako atawasili siku tatu zijazo. Tengeneza ukaribu naye.",
"Kuna ulazima wowote wa mimi kutengeneza urafiki na marahemu?",
"Sinta!", malkia Omuro alimuita kwa ukali,
Sinta alizungusha macho.
Tayari mfalme alikuwa amekwishakwazika. Alinyanyuka na kuondoka na wasaidizi wake. Ledi Erini na Kompa nao pia waliondoka na watoto wao. Ndani alibaki malkia, Sinta pamoja na wasaidizi wao tu.
"Una shida gani, Sinta?", malkia aliuliza, "Mbona unapenda kunitia aibu?",
"Mama tafadhali, usijifanye hujui sababu.", alisema Sinta huku naye akijiandaa kuondoka,
"Unahisi wewe ndiyo mwenye maumivu kuliko mimi? Kitendo alichofanya baba yako kiliniumiza pia, lakini tunasonga mbele. Haya ndio maisha.",
"Sawa, malkia mtukufu.", alisema tena kwa utofanyaji,
Malkia alimjua mwanae nje na ndani. Pamoja na mapungufu ya Sinta, malkia alimpenda sana. Alinyanyuka na kumfata Sinta kwenye kiti chake.
"Wanasema dawa ya mjinga ni kukaa kimya.", alisema malkia Omuro, "Muda mwingine hutakiwi kufanya chochote.",
"Ndiyo maana wake wenzio wanakudharau sana, mama. Umezidi upole.", alisema Sinta kwa kukereka,
"Najua kila kinachoendelea, wote wanayoyasema nayasikia. Lakini mimi ndiye malkia, na wao ni Ledi tu. Watasema yote lakini bado mimi ni mkuu. Inatosha.",
"Kuliko niolewe alafu niishi kama wewe, bora niendelee kuishi kama navoishi sasa hivi.",
"Na mimi wala sijakukataza. Ila kuwa makini habari zako zisimfikie baba yako. Atakuua na kuichemsha mifupa yako kama supu.", Malkia alimbusu Sinta shavuni, "Nakupenda mwanangu. Kuwa makini.",
"Nakupenda pia, mama.",
Malkia Omuro na wasaidizi wake waliondoka. Sinta alimpenda sana mama yake. Alikuwa ni mtu pekee aliyemsikiliza na kuwa upande wake.
…
Siku mbili zilikuwa zimebaki kabla ya familia ya Gema kuhamia ikulu. Waliweza kujitahidi kuficha siri hiyo hivyo hata majirani zao hawakujua kilichoendelea. Huku familia ikiwa na hamasa kubwa ya safari, Aera bado alikuwa akitafuta ufumbuzi. Hakuweza kuwaambia familia yake ukweli kwani alijua ya kuwa hawatomwamini. Hivyo alivaa swala la ukombozi mikononi mwake mwenyewe.
Usiku na mchana hakuweza kulala. Ubongo wake ulikuwa ukifanya kazi ya ziada kutafuta ufumbuzi. Hatimaye aliweza kuona mwangaza. Asubuhi na mapema aliamka na kuelekea ziwani. Hakukuwa na mtu yeyote njiani, watu wote walikuwa wamelala kasoro wavuvi. Yeye alikuwa na shida ya mvuvi mmoja tu.
…
Pim alisukuma mtumbwi wake mpaka ng'ambo ya ziwa. Alishangazwa sana na uwepo wa Aera mahali pale kwani haikuwa kawaida yake.
"Ni macho yangu au ndoto?", Pim aliuliza huku akimkaribia Aera,
"Huwezi kuota ndoto nzuri kama hii.", Aera alifanya utani,
"Vipi? Umekuja kufundishwa kuvua samaki?",
"Natamani ingekuwa hivyo, ila nipo hapa na shida nyingine.",
Pim aliangalia kushoto na kulia. Kwa bahati nzuri hakukuwa na watu wengi eneo hilo.
"Niambie, nakusikiliza.", Pim alisema,
"Ni kitu kikubwa, Pim. Nahisi wewe pekee ndiye utakaeweza kunisaidia.",
"Bila shaka. Kama kipo ndani ya uwezo wangu lazima nikusaidie.",
Halikuwa jambo rahisi kusemwa, ila Aera alipiga moyo konde. Maisha ya familia yake yalikuwa matatani.
"Pim, nafahamu kuhusu hisia zako kwangu.", Aera alianza,
Pim hakushtuka wala kuona aibu, "Ni kweli Aera, nakupenda.",
"Najua hilo, lakini kwa bahati mbaya sitaweza kukubali ombi lako kutokana na jambo linaloendelea kwenye familia yangu.",
"Jambo gani?",
"Naomba haya tayokwambia yawe siri yetu mimi na wewe tu.",
"Ondoa shaka.", Pim aliahidi,
"Kesho kutwa mimi na familia yangu tutaondoka kijijini hapa kuelekea sehemu isiyojulikana. Gema amepata mchumba.",
Pim alicheka kwa furaha, "Hii ni habari njema, Aera.",
"Hapana, Pim. Mwanaume anayetaka kumuoa sio mtu mzuri. Yeye na familia yake wana nia ya kumuangamiza Gema na sisi sote kwa pamoja.",
Kauli ya Aera ilimchanganya, "Kwanini unasema hivyo? Umesikia wapi?", aliuliza,
"Habari zao zimenifikia na ninashindwa kuwaambia familia yangu kwasababu familia ya huyo mwanaume ni tajiri. Baba na mama yangu hawasikii wala hawaelewi. Ni mimi pekee ndiye naeweza kuwakomboa.", alisema Aera,
"Ni familia gani hii kwani?",
"Siwezi kukwambia kwasababu nitakuweka hatarini.",
"Sasa ni msaada gani unaotaka kutoka kwangu.",
Aera alimtazama Pim machoni na kushika mkono wake. Mikono ya Aera ilitetemeka. Hii ilionesha kuwa alikuwa kwenye wakati mgumu. Pim hakupenda kumuona Aera akiwa kwenye ile hali.
"Pim_", Aera alianza, "Naomba ukutane na Gema kimwili.", alitamka,
Pim alivaa mshangao mkubwa. Hakuamini kile alichosikia, "Unasema nini?", aliuliza tena.
Hata Aera hakupenda yale aliyotamka lakina hakuwa na jinsi. Njia pekee ya kuokoa maisha yao ni kama Gema akigundulika kuwa hana usichana wake. Mabinti walioolewa kwenye familia za kifalme walihitajika kuwa na bikra zao. Hii ilikuwa ni kielelezo cha malezi yao mazuri na huleta heshima kwa familia yake. Gema akipoteza usichana wake, familia ya mfalme haitataka aibu ile iwaangukie hivyo itawabidi watafute binti mwingine.
Gema hakuwa kwenye mahusiano wala hakuwa na mazoea na vijana wa kiume. Aera alitaka kumpa kazi hiyo Pim kwani alimfahamu tangia wakiwa watoto. Pim alikuwa mstaarabu, mchapakazi na mwenye roho nzuri sana, tofauti na vijana wote ambao Aera aliwafahamu. Aliamini ya kuwa Gema atakuwa kwenye mikono salama.
"Hata mimi sipendi kusema haya.", Aera aliendelea, "Lakini sina jinsi, Pim. Hii ndiyo njia pekee.",
Pim aliingiwa na hasira lakini hakutaka kuionesha. Alitoa mkono wake kutoka kwenye mikono ya Aera na kupiga hatua moja nyuma.
"Umenidharau sana.", Pim alimweleza, "Unanichukuliaje?",
"Pim tafadhali, naomba unisikilize _",
"Kwani nimefanya makosa kukupenda?"
Maumivu ya moyo yalimfanya Aera aanze kububujikwa na machozi, "Hapana Pim. Naheshimu hisia zako.",
"Sasa mbona unanipa masharti magumu hivi? Mimi nakupenda wewe, sitaki kulala na mwanamke mwingine yeyote zaidi yako. Kama hunitaki ni bora uniambie kuliko kunitupia kwa mdogo wako.",
"Sifanyi makusudi. Hata mimi naumia.", Aera alizidi kulia.
Pim alitikisa kichwa na kurudi kwenye mtumbwi wake. Alianza kuusukuma tena kurudi ziwani. Alihitaji kuwa mbali na Aera ili apate nafuu kwa muda. Aera alimfata kwa nyuma huku akiendelea kumuomba;
"Mimi na familia yangu tutakufa, Pim. Zimebaki siku mbili tu.",
"Aera niache tafadhali.",
Pim alirukia mtumbwini na kuelea nao mbali na ng'ambo ya ziwa. Mawimbi madogo yaligonga miguu ya Aera. Alikuwa kama mtu aliyepigwa ganzi. Njia pekee ya kuokoa maisha yao imeshindikana. Je, ni kweli kuwa kifo kilikuwa kimeshinda vita ile?
***