Chereads / THE PRIESTESS' PROPHECY (Book 1) / Chapter 10 - TETEMEKO

Chapter 10 - TETEMEKO

Njia nzima, Gema alikuwa akitetemeka mwili kwa hofu. Dakika chache zilizopita alipokea wito kutoka kwa mama mkwe mtarajiwa akitaka wale chakula cha asubuhi pamoja. Kilichomuogopesha zaidi ni kwamba mualiko ule haukumuhusu yeye tu bali ledi Erini pia alikuwepo. Bila shaka Gema alijua kuna jambo. 

Aliwasili kwenye makazi ya ledi Kompa na kuwaacha wahudumu wake nje kisha yeye aliingia ndani. Kama mategemeo yake yalivosema, aliwakuta ledi Erini na ledi Kompa tayari wamekwishaketi wakinywa chai taratibu. Gema aliinamisha kichwa;

"Salamu ledi Kompa. Salamu ledi Erini.", alisema kwa utaratibu.

"Salamu, konsoti Gema.", ledi Erini alijibu.

Ledi Kompa alikaa kimya huku akimuangalia Gema kwa macho ya hasira. Gema aliona na hakusema kitu. Alisita kuvuta kiti na kukaa maana alihisi ataongeza hasira yao, hivyo alibaki amesimama wima.

"Umeongea na dada yako hivi karibuni?", ledi Kompa aliuliza,

"Hapana. Mama alikuja kuniona peke yake.", Gema alijibu.

"Dada yako hana adabu hata robo!", ledi Erini alidakia, "Huko mlipotoka mlifundwa?",

"Ndiyo, ledi Erini _",

"Sasa mbona anakuja na kuanza kuharibu mipangilio ya familia yetu?",

Moyo wa Gema ulimwenda mbio. Alianza kukumbuka maneno ya mama yake;

"Samahani ledi Erini na ledi Kompa. Ningependa kujua dada yangu alichokifanya kama hamtojali.", aliomba taarifa zaidi.

"Unajua kilichokuleta hapa?", ledi Kompa alimuuliza,

"Ndiyo, ledi Kompa. Nimekuja kuwa mke wa Avana, mwana wa mfalme.", Gema alijibu,

Ledi Erini alicheka kwa kejeli, "Hii ndio shida ya kukaribisha masikini kwenye familia yetu. Mmoja kakaribishwa, mwingine naye akaona kwanini abaki nyuma? Hivi ameshindwa kutega wanaume wote hapa ikulu mpaka mfalme?",

"Unasema?", Gema alishangaa, "Aera amemtega mfalme?", 

"Tumemuona dada yako akimkumbatia mfalme bwawani.", ledi Kompa alieleza, "Tabia za kimalaya kabisa. Mwenendo wa dada yako unanifanya nipate mashaka kuhusu wewe pia, maana samaki mmoja akioza _ nahisi unajua msemo unavyosema.",

Gema alilengwalengwa na machozi.

"Kama mmekuja ikulu kwa nia mbaya, nakuahidi kuwa mtakosa vyote.", ledi Erini aliapa, "Siwezi kukaa na kushuhudia nzi wawili wakisambaratisha kila kitu tulichokihangaikia.",

Gema alijishusha na kupiga magoti. Alijikaza kutokumwaga machozi mbele yao;

"Nawaahidi ya kuwa mimi na familia yangu hatujaja kwa nia mbaya. Ninakubali kuwa kitendo alichofanya dada yangu ni kosa na mimi mwenyewe tamkanya.", alisema,

"Na kama akikataa kukusikiliza?", ledi Kompa aliuliza,

Gema alikunja mikono kwa hasira, "Kama akikataa kunisikiliza basi tamuacha mikononi mwenu, nanyi mtaamua cha kumfanya.", alitamka.

Ledi Kompa na ledi Erini walitabasamu. Kauli ya Gema ndiyo kauli waliyokuwa wakiisubiri.

Gema alitoka kwenye chumba cha ledi Kompa akiwa amefura kwa hasira. Mone na wahudumu wake walimfwata kwa nyuma.

"Konsoti Gema, upo sawa?", aliuliza Mone.

"Naomba mmoja wenu aende kumleta Aera kwenye makazi yangu.", Gema aliongea kwa hasira, "Tena mwambieni asinipotezee muda. Afike haraka iwezekanavyo.",

Muhudumu mmoja aligeuza na kupita njia nyingine kuelekea kwenye makazi ya familia ya Gema. Waliobaki waliambatana na Gema kurudi kwao.

Aera aliacha alichokuwa akifanya na kumfata muhudumu wa Gema. Alikuwa na shauku ya kumuona mdogo wake kwani ni mambo mengi sana alitaka kuongea naye. Makazi ya familia ya Aera na makazi rasmi ya familia ya mfalme yalitenganishwa na daraja, kisha geti. Umbali ulikuwa wa dakika kumi na tano. 

Walipokuwa wakikaribia darajani, walimuona mzee mmoja akiwa amesimama. Mavazi yake yalimfanya Aera agundue kuwa hakuwa masikini kama wao bali mtu wa uchumi wa juu. Mkongoja wake ulikuwa mweusi na mistari kadhaa ya rangi ya dhahabu. Nywele zake zilikuwa nyeupe pe, na ndevu zake zilikuwa nyingi na ndefu. Aera hakumjua ni nani, na Tarura hakuwa na mpango wa kujitambulisha.

Kadiri walivyokuwa wakikaribiana, Tarura aliweza kumuona Aera kwa ukaribu. Alishindwa kujizuia, mdomo ulimwagika wazi;

"Stara!", Tarura aliropoka.

Aera alicheka kidogo, "Hapana. Naitwa Aera.", kisha aliendelea kumfata muhudumu.

Tarura alibaki akimshangaa Aera mpaka walipoingia getini na kupotea. Hakuamini macho yake. Mfalme Bazi alisema ukweli. Hivyo bila kupoteza muda, Tarura alielekea kwenye madhabahu yao ili azungumze kiundani na mizimu yao. Kitendawili kile kilihitaji kutegwa.

Je, kwanini Aera alikuwa akitabasamu peke yake huku Gema akiwa amefura? Aera alidhania ya kwamba mkutano wao utajaa furaha maana wamekumbukana sana, lakini Gema alikuwa amekaa kitandani, mikono kifuani, na hasira kali. Muhudumu aliyemsindikiza Aera alitoka nje na kuwaachia nafasi ya kuzungumza. 

"Macho yangu yananidanganya au ni kweli kwamba umekasirika?", Aera aliuliza akiwa amesimama mbali kidogo na kitanda.

"Kwanini unahisi nimekasirika? Unaweza kunipa sababu yoyote?", Gema aliuliza kwa sauti ya mkazo.

Aera alitikisa mabega kwa kukataa, "Sifahamu. Unaweza kuniambia?",

"Bwawani, ulikwenda kufanya nini pale? Tena usiku.",

"Basi. Nimeshajua unachotaka kusema.",

"Hujajibu swali langu.",

Gema hakuwai kumuongelesha Aera kwa sauti na namna kama ile. Kwa kawaida, Aera alitakiwa amkanye maana yeye ni mkubwa, lakini aliona ajishushe.

"Sikwenda kukutana na mfalme, kama ndicho kitu unachouliza. Nilikuwa kwenye matembezi tu nikishangaa maeneo ya ikulu. Mfalme alinikuta nimeshakaa.", Aera alijibu.

"Ngoja nibadilishe swali ili unielewe; Aera, kwanini umemkumbatia mume wa watu?",

"Gema, tafadhali. Unanikosea adabu.",

Gema alinyanyuka na kumkaribia Aera, "Adabu?", aliuliza kwa hasira, "Hivi unajua maisha nayoishi? Nimetoka kukutana na ledi Kompa na ledi Erini, wote wamejaa hasira. Nimekosa hata cha kujieleza kwasababu sijui kinachoendelea kichwani mwako.",

"Gema _",

"Sikutegemea kabisa kuwa kuna siku nitapitia changamoto na wewe utakuwa sababu. Unaniaibisha na kunizaririsha mbele za watu.",

"Sina mpango wowote wa kukuaibisha, mdogo wangu. Nipo hapa kwa sababu nakuthamini na ninakupenda. Siwezi kufanya jambo la kukuweka hatarini.", Aera alieleza,

"Mama ameniambia kuwa mimi kuchumbiwa na mtoto wa mfalme hakujakufurahisha. Sasa nieleze; ni wivu au chuki?",

"Inaonekana hutaki kunielewa, Gema. Sio peke yako, hata mama pia anajitenga na mimi. Nini sababu?",

"Unashika visivyokuhusu!", Gema aliunguruma, "Kama ulikuwa unataka mwanaume ungemkubalia Pim. Yani kisa mimi nimechumbiwa na mtoto wa mfalme, wewe unakwenda kumtega mfalme? Malaya!",

Aera alinyanyua mkono wake na kumchapa Gema kibao cha shavu. Gema aliyumba na kuweza kusimama wima baada ya kushikilia kiti. Bumbuwazi ilimpiga. Aera hakuwahi kumpiga hata kwa utani. Alishikilia shavu lake, mdomo ukiwa wazi kwa mshangao.

Aera hakujutia kumpiga, hakujuta hata kidogo.

"Humu wewe ni konsoti lakini haimaanishi nitakaa nikusikilize hata ukinivunjia heshima.", Aera aliongea, "Mimi ni dada yako, na hata siku moja usijione kuwa upo juu yangu. Ninakuheshima, na ninakujali lakini hii haimaanishi mimi ni dhaifu.",

"Umethubutu kunipiga?", Gema aliuliza, sura ikibadilika kuwa nyekundu kwa hasira.

"Na ninaweza kukupiga tena.", alisema Aera, "Hivi kisa unalala kwenye hichi chumba kizuri na kisa una wafanyakazi wako unajiona umebahatika? Huu ni mtego. Hakuna mtu anayekupenda ndani ya hii ikulu zaidi ya sisi familia yako.",

"Avana ananipenda. Kanizawadia hii cheni.", Gema alimuonesha Aera cheni iliyopo shingoni kwake kwa kujidai, "Sina shida ya upendo wako wa masharti.",

"Mbuzi wa kafara!", maneno yalimponyoka Aera, lakini baada ya hapo hakutaka kubadilisha mada. Maji yalikwishamwagika. Hayazoleki. "Wanakuchekea na kukupa zawadi za gharama kwa sababu wewe ni mbuzi wa kafara. Hujaja hapa kuwa mke wa milele wa Avana, bali umekuja kuolewa, kufariki usiku wa ndoa yako na kutolewa kafara kwa mizimu yao. Bahati?", Aera alicheka, "Labda bahati mbaya.",

"Unase-unasemaje wewe?", Gema alitetemeka sauti. Maneno ya dada yake yalimtisha.

"Avana hajawahi kukuona nje ya ikulu. Mara yake ya kwanza kukuona ilikuwa ile siku tuliyowasili hapa. Pia nasikitika kukutaarifu kuwa hakupendi. Ukishatolewa kafara atapata nafasi ya kuoa mwanamke atakayempenda na ambaye hatafariki.", 

Aera aliitazama meza iliyopo pembeni yao. Kulikuwa na mabakuli ya vitafunwa vitamu na majagi ya juisi. Aliguna.

"Unalishwa unenepe, upendeze ili mizimu yao ifurahie sadaka. Hujawahi kula vizuri hivi, mdogo wangu. Unajiona upo peponi kumbe wanakupumbaza. Eti unapendwa? Unajua maana ya upendo wewe?",

"Muongo!", Gema alisema, "Wivu ndio unakufanya utunge maneno.",

Aera alimsogelea Gema, "Fikiria mdogo wangu. Hakuna kitu cha bure duniani. Kwanini hawajachagua binti tajiri lakini wamekuchagua wewe masikini? Kwa sababu nguvu ya kukataa raha hauna. Wanataka kukuua. Baada ya hapo na sisi tutauliwa na hakuna hata atakayetukumbuka. Unahisi kwanini Badri alituambia tusiwaambie watu kuwa unakuja kuolewa na mtoto wa mfalme? Hii ndiyo sababu.",

Hofu ilimuingia Gema. Kulikuwa na sauti mbili zilizokuwa zikikinzana. Sauti moja ilikuwa ya juu ikimwambia kuwa maneno ya Aera ni ya uongo na asiyaamini. Sauti ya pili ilikuwa ndogo, ya chini sana, nayo ilimwambia asikilize maneno ya dada yake maana yanamtakia mema. Sauti hizi zilifanya kichwa kianze kumuuma ghafla na kumpatia kizunguzungu. Moyo ulimwenda mbio hadi akashindwa kuhema. Aliyumba, nusura aanguke.

"Ondoka!", Gema alimuamuru Aera,

"Siwezi kwenda. Ona hali yako _",

"ONDOKA! TOKA!", Gema alipayuka.

Wahudumu wake walirudi ndani haraka baada ya kusikia sauti ya Gema. Mone na msaidizi mwingine walimchukua Gema na kwenda kumlaza kitandani kwa ajili ya huduma ya kwanza. Aera aliogopa sana kumuona mdogo wake kwenye ile hali.

"Tafadhali, tunaomba uondoke.", muhudumu mmoja alimwambia Aera, "Usiwe na wasiwasi, tutamuangalia vizuri.",

Katika pirikapirika zilizokuwa zikiendelea, Aera alisukumwa nje kisha mlango ulifungwa. Hakuweza kurudi ndani hata angejaribu. Hakuwa na budi kuondoka, japo kuwa moyo ulikataa. 

"Nimefanya makosa.", alisema kimoyomoyo, "Sikupaswa kumwambia.",

Alisahau kuwa Gema alikuwa na roho nyepesi. Njia nzima alijilaumu.

***