Chapter 15 - STARA 2

Miaka mitano baadaye, mfalme Zito alitangulia mbele za haki kwa afya mgogoro, na Antivo alitangazwa kuwa mfalme mpya wa Natron. Amani ilirudi nchini mwao. Sheria zilizosababisha mitafaruku na vifo visivyo na hatia zilivunjwa. Sasa mimea ilistawi, mifugo iliongezeka, samaki zilijaa ziwani na mvua zilinyesha. Mfalme Antivo na malkia Waridi walibarikiwa watoto wengine wawili wa kiume. Familia yao ilikuwa na furaha.

Vile vichanga viwili vilivyookolewa na Antivo vilikua; majina yao yalikuwa Omuro na Stara. Makuhani waligundua kuwa hawakuwa ndugu wa damu ila walizaliwa mwaka na mwezi mmoja. Pamoja na hayo, walilelewa kama mtu na dadaye, na walipendana sana. Urafiki wao na Bazi ulinawiri. Alipo Bazi nao walikuwepo. Walishirikiana kwenye kila utoto wao.

Miaka kumi na mmoja ilipita, nao watoto hawa walitimiza miaka kumi na sita. Akili zao za utoto zilibadilishwa na utu uzima. Omuro na Stara waliacha kukimbizana na kupanda miti kama nyani na kuwa na mienendo ya kibinti. Walielezwa umuhimu wa usafi na kufundishwa kupaka vipodozi. Kwa kuwa mfalme Antivo na malkia waliwapenda sana, walizawadiwa vito na mavazi ya thamani. Wahudumu na viongozi waliwapa heshima yao kama mabinti wa mfalme ingawa hawakuwa.

Urafiki ulijenga hisia mpya mioyoni mwao. Omuro na Stara walianza kumpenda Bazi kimapenzi, lakini hisia za Bazi zilikuwa kwa mmoja wao; Stara. Ilijenga mfumo wa kihisia wa pembetatu.

Stara na Omuro walilala chumba kimoja hivyo ilikuwa dhahiri kuwa stori zilikuwa nyingi na kuwachelewesha kulala. Kwasababu kulikuwa na wahudumu nje ya vyumba vyao, waliweza kubana sauti ili zisisikike na kwenda kushtakiwa kwa malkia. 

"Hivi Stara, una ndoto za kuja kuolewa?", Omuro aliuliza.

Stara alitazama dari, "Sisi ni mabinti. Lazima tuwe na ndoto za kuolewa.", alisema.

"Lakini mfalme Antivo hajatufunga. Ametupa uhuru wa kuolewa na mtu yeyote tutakayemtaka.",

"Najua hilo. Lakini kwa sasa ndoa sio kipaombele changu.",

"Wewe unataka nini?",

"Nataka nijifunze utabibu ili niokoe maisha ya watu.",

"Utabibu?", Omuro alishangaa, "Sio kitu rahisi kujifunza. Utatumia muda mwingi sana kusoma. Mpaka unakuja kuwa bingwa, umri wako utakuwa umekwenda. Ndiyo maana matabibu wengi kwanza ni wanaume, na hao wanawake wachache wapo kwenye useja wa milele.",

Stara alicheka, "Maseja ni makuhani tu. Wao ndio wamejiwekea hiyo nadhiri. Hata hivyo nisipoolewa basi haikuwa bahati yangu. Wewe je?",

"Nataka kuolewa haraka iwezekanavyo.", Omuro alisema kwa hamasa, 

"Umeshapata mtu nini?",

"Ndiyo. Tazama; ndani ya mwaka huu au ujao takuwa mke wa Bazi.",

Stara alithibiti mshtuko wake. Ilikuwaje kuwa walimpenda kijana mmoja ingawa wanaume waliowazunguka walikuwa wengi?

"Nampenda sana, yani sana. Ukiingia moyoni mwangu utamkuta yeye amekaa.", Omuro aliendelea.

Stara aligeuka upande wa pili na kulalia ubavu, "Kama unampenda mwambie. Labda anakupenda pia.", roho ilimuuma kusema hivyo lakini hakuwa na jinsi. Alifahamu madhara ya kugombania mwanaume, tena na dada yake.

"Ngoja nitafute wakati muafaka nimwambie.", Omuro alisema kwa furaha, "Na wewe kesho nenda kwa malkia mama ukamwambie kuhusu lengo lako la kujifunza utabibu. Naamini atakukubalia.",

Stara alitabasamu, "Usiku mwema, Omuro.",

"Usiku mwema, Stara.",

Omuro alipuliza mshumaa mmoja uliobaki na kufanya giza. Walilala.

Mfalme Antivo na malkia Waridi walipenda sana ombi la Stara kusomea utabibu. Kama familia zote zilivyokuwa na vichangamoto vidogo, wao pia walikuwa nayo. Kati ya Stara na Omuro, malkia Waridi alimpenda Omuro zaidi. Alitamani sana Omuro angekuwa akijiongeza kama mwenzie kutaka kujifunza ujuzi mbalimbali.

Habari za Stara kuanza chuo cha utabibu zilimfikia Bazi naye hakutaka kupoteza muda, kwani jinsi Stara anavyozidi kusoma ndipo anapozidi kwenda mbali naye. Aliamua kuweka kitu kimoja wazi.

***