Tarura alimaliza kuandika ujumbe kwenye kipande cha karatasi na kumkabidhi muhudumu wake wa kiume.
"Mfikishie mfalme Bazi. Akisoma atakuja kuniona haraka iwezekanavyo.", alimtuma muhudumu yule.
"Sawa, kuhani mkuu.",
Muhudumu alianza kuondoka. Alipofungua mlango alisitisha mwendo. Kulikuwa na mgeni nje. Tarura aliona muhudumu wake akiinamisha kichwa, naye alidhani kuwa labda ni mfalme. Hivyo, alijitahidi kutembea haraka ili akamsalimu. Alipofika mlangoni alishangaa kumkuta Sinta. Mshangao wake, Sinta alifurahishwa nao. Sasa alikuwa na uhakika kuwa kuna kitu kilikuwa kikiendelea nyuma ya pazia.
"Tarura, mbona unashangaa kuniona?", Sinta aliuliza akitabasamu,
"Haujawahi kuja kwenye makazi yangu.", alijibu Tarura.
"Kila kitu kina mwanzo.",
Sinta alishusha macho chini na kuona karatasi mikononi mwa muhudumu. Bila kusubiri alilinyakua na kulifungua kisha kusoma kilichoandikwa ndani;
"Mfalme Bazi, nimepata jibu la kitendawili chetu.", Sinta alisoma kwa nguvu, "Mh, napenda vitendawili.",
Ingawa Tarura hakumkaribisha ndani, Sinta alijialika mwenyewe. Muhudumu alitoka nje. Tarura alihisi dalili mbaya ikimnyemelea, hivyo kijanja alimpatia ishara mlinzi wake kuwa aende kumuita mfalme. Kijana yule alipoanza safari, Tarura alifunga mlango.
Sinta alikuwa tayari ameshaketi mezani akimsubiri. Tarura alijivuta na kwenda kukaa pia. Kikombe chake cha chai bado kilikuwa kikitoa mvuke hivyo aliendelea kunywa taratibu kabla hakijapoa.
"Kama unahitaji chai, kuwa huru.", Tarura alisogeza kikombe kitupu na chupa ya chai kwa Sinta.
Lakini, "Hapana. Sina kiu.", Sinta alisogeza vyombo pembeni, "Ila nina swali.",
"Uliza.",
"Tarura, Stara ni nani?",
Tarura alipaliwa na chai ghafla. Alikohoa kwa muda mfupi kidogo, "Umejuaje hilo jina?", aliuliza,
"Nina masikio kila kona ya hii ikulu. Sasa bila kupoteza muda, Stara ni nani? Bila shaka atakuwa anahusika na hichi kitendawili ulichoandika kwenye hili karatasi.",
"Hii ni siri yangu na mfalme Bazi. Siwezi kukwambia.",
"Tarura, nimekuona ukimtuma muhudumu wako aende kumuita mfalme. Najua muda utakaomchukua baba yangu kutoka kwenye makazi yake mpaka hapa, hivyo akikaribia, tavua nguo yangu na kusema ulikuwa unataka kunibaka.",
"Mimi ni mzee nisiye na nguvu ya kukukandamiza. Hakuna atakayekuamini.",
"Nina njia zaidi za ishirini ya kukufanya uonekane mbakaji.", Sinta alianza kufungua kamba za gauni yake, "Wewe ni mwanaume. Huna nguvu ya kujizuia.",
Tarura alimeza mate.
"Mara yako ya mwisho kuona kifua cha mwanamke ni lini, Tarura?",
Macho ya Tarura yalifwata vidole vya Sinta vilivyokuwa vikijiburuza kifuani taratibu. Hakuhitaji kugusa ngozi yake kujua kuwa ilikuwa laini kama hariri.
"Sinta, tafadhali. Acha.", Tarura aliomba,
"Stara ni nani, Tarura? Usiponiambia utakuwa kwenye wakati mgumu sana.",
Sinta alianza kushusha gauni taratibu. Jasho jembamba liliteremka usoni mwa Tarura. Joto liliongezeka. Ilikuwa vita ngumu, na hatimaye alikata tamaa;
"Stara alikuwa ni mke wa kwanza wa baba yako!", aliropoka.
Sinta alitabasamu, "Endelea.".
…
Mfalme aliwasili kwenye makazi ya Tarura bila kuchelewa. Mguu wake ulipokanyaga ndani na macho yake kukamata picha ya mbele yake, mfalme alipigwa na butwaa. Tarura alikuwa mwili tu kasoro roho, yaani marehemu. Vazi lake lilikuwa limeloweshwa na damu iliyomtoka mdomoni na puani. Hakukuwa na mtu ndani zaidi yake, na wala lile karatasi la ujumbe pia halikuwepo.
Walinzi walifurika ndani kwenda kugomboa mwili wa Tarura. Mfalme hakuwa na nguvu hata ya kumsogelea. Moyo wake ulivunjika kwa mengi.
***