Chapter 17 - STARA 4

Bazi alikwenda kwenye makazi ya wazazi wake kwa ajili ya mazungumzo muhimu. Baada ya Stara kumpa jibu kuwa amemkubalia, hakutaka kupoteza hata sekunde. Alitamani ulimwengu mzime utambue hilo, lakini taarifa zilibidi zifike kwa mfalme na malkia kwanza. 

"Baba, mama, nina kitu muhimu sana cha kuwaeleza.", alisema Bazi.

Mfalme na malkia walitizamana kisha kurudisha macho yao kwa Bazi.

"Kitu gani hicho?", mfalme Antivo aliuliza,

"Nimepata mwenza wangu.", 

Mfalme alishangaa lakini malkia Waridi alikuwa akilitegemea hilo. 

"Ni binti gani huyu aliyeweza kumuingia mwanangu kumoyo?", mfalme aliuliza kwa shauku,

"Baba, mama, kipenzi changu ni Stara.",

Mfalme alikohoa ghafla. Stara? Mke wa kwanza wa Bazi? Ubongo wake haukupokea taarifa hiyo vyema.

"Mwanangu, una uhakika kuwa unataka kumuoa Stara?", aliuliza,

"Ndiyo, baba.",

"Tena unampenda kwa dhati?",

"Ndiyo, baba.",

Mfalme alipatwa na kigugumizi. Malkia Waridi alipoona hivyo, aliingilia kati ili kuokoa jahazi.

"Ni habari nzuri sana, mwanangu.", alisema, "Mimi na baba yako tumefurahi sana. Baraka zikishatolewa na makuhani, mipango yenu ya harusi itaanza.",

Bazi alifurahi sana, "Asante mama, shukrani baba.",

Bazi aliondoka kwa shangwe kwenda kumfikishia habari Stara. Huku mfalme alikuwa akihitaji majibu ya kumtuliza moyo.

"Stara? Hivi anafahamu mfumo wa koo zetu?", mfalme alimuuliza malkia Waridi, "Stara ni kama binti yetu. Hatuwezi kuruhusu awe mke wa kwanza wa Bazi.",

"Bazi alipotimiza miaka kumi na sita, nilikwenda kumuona kuhani mkuu Tapa. Naye alinifahamisha mapendekezo ya mizimu. Kwa bahati mbaya, mizimu imemchagua Stara.", malkia alimueleza.

"Unasema?", mfalme alishtuka, "Haiwezekani!",

"Unapinga mapenzi ya mizimu? Unajua matokeo yake?",

"Stara ni _",

"Kama huamini maneno yangu, basi nenda kamuulize Tapa. Lakini kabla hujaenda kutafuta ugomvi na mizimu, fikiria hili; Stara na Omuro ni kitu kimoja, wote ni kama mabinti zetu, hivyo mizimu ikimchukua Stara, bado tutabaki na Omuro.",

"Mbona kama jambo hili halikusumbui kama mimi?",

"Nimeshasali usiku na mchana kuomba mizimu ibadilishe pendekezo lao, lakini jibu halikubadilika. Siwezi tena, Antivo. Inatakiwa ifanyike.",

Mfalme alihuzunika sana, "Bazi anajua kinachoendelea?",

"Hapana, na ni vyema kama ikibaki hivihivi.",

Mfalme Antivo hakuwa na hoja tena. Wao walikuwa binadamu tu. Nguvu ya kubishana na mizimu hawakuwa nayo.

Siku chache baadae, baraka ilitoka kwa kuhani mkuu na mahusiano ya Bazi na Stara yalirasimishwa. Heshima kwa Stara iliongezeka kwani sasa alikuwa ni konsoti, mchumba wa kijana wa mfalme. Alihamishiwa kwenye chumba cha peke yake. Hakupenda kuwa mbali na Omuro lakini hakuwa na jinsi.

Mapenzi yake kwa Bazi yalizidi, na baada ya ujana kuwakabiri, walivuka kiwango na kuingiliana kimwili. Haikuwa mara moja, na kwa kuwa haikuruhusiwa, walifanya kwa siri. Hakuna aliyejuwa kilichoendelea mpaka siku sitini baadaye matabibu walipogundua kuwa Stara alikuwa na ujauzito!

***