Chapter 18 - STARA 5

Makazi ya kuhani mkuu Tapa yalipatwa na ugeni wa ghafla wa mfalme na malkia. Watu wachache tu ndio waliokuwa wakifahamu kuhusu mimba ya Stara, nao walihitaji jibu mapema kabla habari haijaanza kusambaa. Haikuwahi kutokea konsoti kubeba mimba kabla ya ndoa. Walihitaji akili ya ziada.

Kuhani alisoma nyaraka zote zilizoandikwa na makuhani waliokuwepo kabla yake. Ni waraka mmoja tu uliozungumzia swala la ujauzito. Bila kungojea, Tapa alifikisha waraka huo mezani alipo mfalme na malkia. 

"Nini kimeandikwa?", malkia aliuliza,

Tapa alianza kusoma, "Na kama konsoti wa kwanza wa mwana wa kiume akibeba mimba kabla ya ndoa, inatakiwa itolewe. Kwa maana mtoto huyo hubeba damu chafu ndani yake, damu yenye kukasirisha mizimu. Kama ujauzito ni mkubwa, basi mtoto anyongwe shingo na mkunga mara tu atokapo tumboni mwa mamaye.", 

"Wewe unashauri nini?", mfalme aliuliza,

"Mimba yake ni ya miezi miwili sasa kwa taarifa za tabibu.", malkia alieleza, "Mimba ikitoka sasa hivi itaharibu mipango ya harusi. Stara anaweza hata kukataa kuolewa na Bazi kutokana na machungu. Mimi naona tusubiri ajifungue kisha mtoto anyongwe na mkunga.",

"Tapa, unafahamu kuhusu unajimu, sio?", mfalme aliuliza,

"Ndiyo, mfalme.",

"Angalia tarehe ya kujifungua kwa Stara ili tuitegeshe harusi maeneo hayo.",

"Bila shaka, mfalme.".

Mipango ilianza kupikwa mapema.

Jioni, Omuro alikwenda kumuona malkia. Njiani, aliyapita makazi ya Stara. Tayari alikwishasikia habari za ujauzito wake, nazo zilikuwa kama mkuki wa moyo. Hakutaka kuongea nae wala kumuona. Ingawa kuna vitu vichache alivyotegemea, mimba haikuwa miongoni. Aliichukulia kama usaliti wa kiaina.

Aliwasili kwa malkia na kukaribishwa ndani. Malkia alimkaribisha mezani naye Omuro aliketi.

"Salamu, malkia mama. Nimeitikia wito wako.", aliamkia.

"Bila shaka umesikia habari za mwenzio.", malkia Waridi alizungumza, "Maumivu unayoyasikia nayaona ila ni vyema ujikaze maana wakati wako unakaribia.",

"Malkia mama, Stara ana ujauzito wa Bazi. Sina tena nafasi.",

"Nafasi yako ipo wazi. Usivunjike moyo, mwanangu. Nimekuita hapa ili nikupe mtiririko mzima. Kesho asubuhi utaondoka na kwenda kwenye makazi yangu ya siri. Huko utakutana na walimu wa kukufundisha vitu mbalimbali. Utakaa huko kwa muda wa miezi saba kisha nitakutumia ujumbe wa kukutaarifu urudi ikulu.",

Omuro hakuelewa, "Kwani hao walimu hawawezi kuja hapa, malkia mama?", aliuliza,

"Haiwezekani. Kumbuka lengo lako. Utakuwa mke wa Bazi na malkia wa Natron. Kuna vitu vingi mno unahitaji kujifunza. Hivyo ndani ya miezi saba ijayo, utabadilika na kuwa mahiri sana.", malkia alimueleza.

"Stara je?",

"Acha kufikiria kuhusu yeye, bali jifikirie mwenyewe. Waza yajayo. Haya ni maisha yako, wala si ya mwengine. Nenda kajiandae. Utaondoka asubuhi na mapema.",

Omuro hakuweza kumpinga malkia mama. Alimpa heshima yake na kutoka nje. 

Ilipofika asubuhi, Omuro aliondoka na wahudumu wachache kuelekea kwenye makazi ya ufichoni. Umbali kutoka ikulu ulikuwa ni masaa kumi na mawili. Hakumuaga mtu yeyote, hivyo ilikiwa siri yake na malkia Waridi.

Huko, Omuro alifundishwa kila kitu kuhusu uongozi na kuwa malkia. Alielezwa mazuri na mabaya. Alifundishwa ujuzi mbalimbali; kushona, kucheza, mitindo, na michezo migumu ya ubongo ili asitetereshwe na akili za wazee wa baraza. Mwezi wa kwanza ulipita, wa pili, wa tatu, wa nne na wa tano. Kila siku alizidi kuwa imara kuliko siku iliyopita.

***