Chapter 24 - WITO

Malkia alitoka mbio kuelekea kwa mfalme Bazi, lakini alipotoa mguu wake kwenye geti la jela, alikutana na Sinta akimsubiri. 

"Tupishe. Nataka kuongea na mama yangu.", Sinta alimwambia msaidizi wa malkia.

Msaidizi alikwenda kusimama mbali kidogo.

"Unataka kuniambia nini?", malkia alimuuliza Sinta kwa haraka.

"Ulikuja kumuona nani?", Sinta aliuliza, kama kawaida akiwa amevaa tabasamu lake la kejeli.

"Unajua niliyekuja kumuona. Sema unachotaka kuniambia haraka, kuna sehemu natakiwa kwenda.",

"Kwa mfalme Bazi?",

"Umejuaje?",

Sinta alitikisa mabega, "Chochote alichokwambia Aera, baki nacho moyoni. Usiende kumwambia mfalme.",

Malkia Omuro alikunja uso, "Mbona unaongea kama unajua kilichoongelewa?",

Sinta hakukwepesha macho yake, bali alizidi kumtazama mamaye kiundani. Malkia hakutaka kuamini. Vitu vingi sana vilianza kuleta maana.

"Sinta, tayari unajua kuhusu uhusiano wa Aera na baba yako, sio?", malkia aliuliza kwa kuotea.

"Ndiyo.", Sinta hakubisha.

"Na aliyekwambia alikuwa Tarura, sio?",

Hapo Sinta alisita kujibu. Malkia alimsogelea karibu, "Wewe ndiye ulimuua Tarura ili ukweli ubaki nao mwenyewe, sio?",

"Baba hatakiwi kujua ukweli.", Sinta alijitetea, "Ikigundulika kuwa Aera ni mtoto wa kwanza wa baba, yeye ndiye atarithi kiti cha mfalme, kiti ambacho kinamtazama Noro, kijana wako. Unataka mtu baki aiongoze himaya yetu?",

Hasira ilianza kumpanda malkia Omuro taratibu, "Aera sio mtu baki.", alisema akiuma meno.

"Ni mtu baki!", Sinta alifoka, "Yeye ni tofauti na sisi. Hatustahili kukaa meza moja.",

"Bila yeye usingekuwepo. Bila yeye nisingekuwepo. Bila mama yake kujitoa sadaka tusingekuwepo!",

"Mama yake alikuwa ni mbuzi wa kafara tu _",

Malkia alimkata kibao Sinta, tena cha nguvu. Sinta hakuwahi kupigwa na mama yake hata siku moja. Alishika shavu kwa mshangao, macho yakimtoka kama mjusi aliyebanwa na mlango.

"Mama _",

"Kimya! Utakwenda kumwambia baba yako kila ulichofanya; kuanzia kumuua Tarura na kumsingizia kesi mwenzio. Utamwambia baba yako kwanini umemuua Tarura na utakwenda kumuomba Aera msamaha kwa ushetani ulioufanya.", malkia alimuamuru kwa ukali.

"Siwezi!", Sinta alitetemeka kwa hasira, "Kwanini unatetea mkosi?",

"Kabla asubuhi haijafika, ukweli uwe umemfikia baba yako. Usiposema wewe, tasema mimi. Nakuhesabia muda.",

"Mimi ni mwanao!",

"Nimeshafeli kama mama, sitafeli kama malkia.",

Malkia Omuro aliondoka kwa hasira na kumwacha Sinta akiuma meno. Alianza kupika cha kufanya ili kujikomboa na wazo lilimjia. Alirudi kwenye makazi yake na kuchukua mfuko wa fedha. Wazo lake lilikuwa kwenda kuwashawishi walinzi wamuue Aera kabla asubuhi haijafika.

Aera alijikunyata kwenye kona ya ukuta, akitetemeka na baridi. Usingizi wa ajabu ulimvaa na kumsafirisha kwenye bustani nzuri ya maua. Akiwa anatembea aliona mtu kwa mbali akimpungia mkono. Aera alikimbia mbio kumfwata. Alipokuwa akimkaribia, aliona kuwa alikuwa mwanamke mzuri sana, lakini sura yake haikuwa ngeni. Aliposogea karibu zaidi, aligundua kuwa alikuwa bibi yake aliyemuacha milimani. Alimkumbuka sana.

Bila kungoja, alikwenda kumkumbatia bibi yake na kuanza kulia.

"Nimeshindwa bibi.", Aera alilia kwa uchungu, "Nimeshindwa kuokoa maisha ya familia yangu. Nanyongwa kesho asubuhi.",

"Bado unaweza, mjukuu wangu.", bibi alimliwaza, "Nilikwambia kuwa hii vita hautaweza kuishinda kwa nguvu zako mwenyewe. Sasa hivi umeanguka na huwezi kusimama.",

Aera alimuachia bibi yake na kumuangalia vizuri.

"Nifanyeje bibi? Nahitaji msaada wako.", aliomba,

"Mjukuu wangu Aera, hauna muda. Watu wametumwa kuja kukuua. Ikishindikana, kesho asubuhi unakwenda kunyongwa. Itikia wito wa miungu.",

"Bibi, siwezi kuwa kuhani. Sijui chochote kuhusu ukuhani.",

"Wala haukuzaliwa kuwa kuhani, Aera. Wito wa miungu utakuonesha kusudi lako la kuzaliwa. Ukweli ni kwamba tangia ukiwa tumboni mwa mama yako, miungu ilikuchagua. Itikia wito wao na utaoneshwa kila lililojificha.",

Bibi alifungua kiganja chake na juu kulikuwa na mkufu wenye almasi iliong'aa kama jua. 

"Sikulazimishi kukubali. Uamuzi huu unatakiwa uufanye mwenyewe.", alimtaarifu.

Aera alitazama mkufu ule, na kila sekunde, moyo, mwili na nafsi yake vilioana nao. Ni kama ulikuwa umetengenezwa kwa ajili yake. Vitu vingi sana alivyofanya vilikuwa kama makosa; ni mkufu ule pekee uliokuwa kitu sahihi. 

"Nimekubali.", alitamka, "Nimekubali wito wa miungu.",

Bibi alifurahi mno. Alimvalisha Aera mkufu ule shingoni kisha alimbusu shavuni.

"Unakwenda kuwa mtu mkubwa sana, mjukuu wangu. Najivunia sana.",

Aera aliamka usingizini na kujikuta ndani ya gereza lilelile chafu. Kitu kilichobadilika ilikuwa ni mkufu shingoni mwake. Alidhani ni ndoto tu, kumbe ni kweli. Cha kushangaza zaidi, madonda yake yote yalipotea. Alikuwa na nguvu, tena zaidi ya kawaida.

Akiwa katika harakati za kujua cha kufanya, alisikia sauti za walinzi wakinyatia gereza lake. Aliweza kusikia mawazo yaliyomo vichwani mwao. Alisikia mapigo ya moyo ya kila mtu aliyekuwa karibu yake na kelele ilikuwa kali.

Walinzi walifungua kufuli la gereza lake na kuingia ndani. Nyuso zao wote zilivaa swali.

"Yuko wapi?", aliuliza mlinzi mmoja,

"Hee! Amekwenda wapi?", aliuliza mwingine.

Aera alikuwa mulemule lakini hawakumuona. Walinzi waligongana vikumbo wakimtafuta huku na huku lakini hawakumuona. Walitoka mbio kwenda kutoa taarifa ya kupotea kwa Aera.

Aera alishika mkufu wake na kufumba macho. Popote alipofikiria kwenda alifika. Na muda huo ni sehemu moja tu aliyotaka kwenda. Ndani ya sekunde alikuwa amesimama nje ya boma ya bibi yake milimani. Alifurahi sana.

"Bibi!", aliita, "Bibi nione.",

Alifungua mlango na kuingia ndani. Kwa mshtuko mkubwa alimkuta bibi yake kitandani, akiwa amevaa mavazi yake ya ukuhani. Aera hakusikia mapigo ya moyo wala mawazo ya bibi yake. Mauti yalikuwa yamemkuta. Wala ile haikuwa ndoto, bali roho ya bibi yake ilikuja kumuaga na kumhamasisha.

Aera alibusu paji la uso wa bibi yake;

"Asante bibi. Sitakuangusha.",

***