Chapter 23 - MPASUKO

Asubuhi na mapema, usingizi ukiwa ndio unafifia, ndoto za Aera na familia yake zilikatishwa baada ya mlango wa chumba chao kubomolewa ghafla. Walinzi walifurika ndani, bila kujali hali ya waliolala. Aera na familia yake walikuwa kwenye mshtuko uliowapa kigugumizi. Hawakufahamu kilichokuwa kinaendelea. Walinzi walikwenda kumnyakua Aera kutoka kitandani kwake kama mwizi. Walimshika huku na huku.

"Aera, upo chini ya ulinzi kwa kosa la kupuuzia ombi la mfalme Bazi.", mlinzi mkuu alisema.

Aera alichanganyikiwa, "Mnaongelea nini? Ombi gani?",

"Tunza maneno yako kwa ajili ya baraza.",

Walimvuta Aera kwa nguvu na kumtoa nje. Walimswaga kama mfugo kuelekea kwenye baraza la mfalme. Njia nzima, watu walisimama na kushangaa. Haikuwa kawaida tukio kama hilo kutokea ndani ya ikulu. Aera alijitahidi kuomba maelezo lakini hakuna aliyejisumbua kumuongelesha. Familia yake ilikuwa ikiwafata kwa nyuma, wote wakiwa na hali pacha na yeye.

Milango ya baraza ilifunguliwa kisha Aera alivutwa ndani. Mfalme na malkia walikaa kwenye jukwaa lao. Kwa haraka haraka, familia nzima ya mfalme ilikuwa mule ndani, kasoro watoto wadogo. Isitoshe, Gema pia alikuwa kasimama mkono wa kulia wa Avana. 

Walinzi walimsukuma Aera chini na kumpigisha magoti kilazima. Aera alitazama macho ya kila aliyemwangalia. Hakukuwa na jicho hata moja lililomuhurumia. 

"Aera, binti wa Heya, unamfahamu Tarura?", mfalme aliuliza.

Aera alitikisa kichwa, "Hapana, mfalme wangu. Simfahamu Tarura.", alijibu.

"Unathubutu kunidanganya mimi?", mfalme aliongea kwa ukali, "Taarifa zilizonifikia ni kwamba wewe ulikuwa mtu wa mwisho kumuona Tarura. Kwanini unadanganya baraza?",

"Amini maneno yangu, mfalme. Siwezi kukudanganya.",

Mfalme Bazi alimpa ishara ledi Kompa kuendelea kumuhoji Aera. Ledi Kompa alipiga hatua moja mbele.

"Aera, unamfahamu huyu?", alielekeza kidole chake kwa Gema.

"Ndiyo. Ni mdogo wangu Gema.", Aera alijibu.

"Umekosea sana. Huyu sio mdogo wako Gema bali ni konsoti Gema, mchumba wa Avana, kijana wa mfalme. Kwenye ngazi, cheo chake ni kikubwa na unahitaji kumuheshimu. Lakini jana ulithubutu kumchapa kibao na kufanya hali yake kudorola.",

Migumo ilianza kusikika, yote kama inamzomea Aera. Aera aligeuza uso wake kwa Gema, na Gema alimkazia macho. Ah! Hapo Aera alijua kilichokuwa kikiendelea. Bila shaka, Gema aliwaambia alichomwambia bila hata kufikiria hatari aliyomweka mwenzie. Njia ya kushinda kesi ile salama ilikuwa ndogo kama tundu la sindano.

"Tangia ufike ikulu, umekuwa ni mada.", ledi Kompa aliendelea, "Umekwenda pasipoendeka, umeshika visivyoshikika na kuonesha maadili mabovu sana. Isitoshe, ulionekana ukienda kumuona Tarura muda mchache kabla mfalme hajafika. Damu ya Tarura i mikononi mwako. Kama sio wewe, basi unamjua aliyemuua.",

"Aera, ninakupa mpaka usiku wa leo kusema ukweli wote. Ikifika asubuhi mdomo wako umefungwa, utakwenda kunyongwa mpaka kifo.", mfalme Bazi alitangaza.

Familia ya Aera iliangua kilio, kasoro Gema aliyejikaza. 

"Utakwenda kuwekwa jela chini ya ulinzi mkubwa ili usitoroke. Kabla ya hapo utapigwa viboko kumi na tano.", mfalme alimalizia.

Walinzi walikuja kumnyanyua Aera. Lakini kabla ya kumsomba nje, Aera alimgeukia Gema tena.

"Hongera, konsoti Gema.", alisema kwa sauti ambayo kila mtu alisikia, "Hongera mdogo wangu. Umeniua.", 

Kauli ilimchoma Gema hadi nafsini. Lakini si yeye tu; maneno ya Aera yalimuingia malkia Omuro na kufanya amkumbuke dada yake. Ni yeye pekee, baraza zima aliyetaka kumuamini Aera maana ni kama historia ilikuwa ikijirudia taratibu. Alimtazama Gema, kisha Aera aliyekuwa akisukumwa nje ya malango. Malkia Omuro aliweza kuhisi maumivu na mashaka yao wote wawili kwani haikuwa hisia ngeni kwake.

Jioni ilipofika, Aera alikuwa hoi. Majeraha ya viboko yalimjaa mwili mzima. Gauni yake ililowana damu. Maumivu yalizidi pale nguo ilipogandamana na madonda yake mabichi. Gereza lake halikuwa na afadhali; Ardhi ilikuwa tope na vinyesi. Vijidudu vilikuwa vikimpandia na kutapakaa kwenye vidonda. Aliona ni afadhali asubuhi ifike anyongwe yaishe. Alikuwa amekwisha kata tamaa.

Kwa mbali alianza kusikia sauti za hatua zikijongea kwenye gereza lake. Machozi yalifanya macho yake yaone ukungu. Hata watu hao wawili waliposimama mbele ya nondo za gereza, hakuweza kujua ni akina nani.

"Aera.", malkia Omuro alimuita, "Ni mimi malkia wako. Sogea kwenye nondo, mwanangu.", 

Aera alitambaa kama mtoto na kuzifikia nondo. Msaidizi wa malkia alikwenda kumnywesha maji. Aera aliguguma maji yote kama samaki. Kwa bahati mbaya hawakuweza kuleta chakula. 

"Unaweza kuongea, mama?", malkia alimuuliza.

Aera alitikisa kichwa.

"Vizuri. Naomba unisikilize, Aera. Lengo langu ni kukusaidia, lakini sitaweza kufanya hivyo kama hutaniambia ukweli.", alisema,

"Ukweli gani, malkia Omuro?", aliuliza Aera kwa unyonge.

"Ni kweli kwamba ulimpiga mdogo wako kibao?",

"Ndiyo.",

"Kwa sababu gani?",

"Malkia Omuro, nimemlea Gema. Cheo chake kisimfanye asahau na kunivunjia heshima.", Aera alieleza.

"Nakubaliana na wewe. Hata mimi nilikuwa na dada yangu tuliyelingana umri lakini hatukuwahi kuvunjiana heshima.", malkia alisema, "Jana usiku, ledi Kompa alikuja kuniona na kuniambia kuwa alikuona ukimkumbatia mfalme. Ni kweli?",

Aera aliogopa kujibu, lakini hakuwa na jinsi, "Ndiyo, malkia Omuro. Lakini mfalme ndiye aliomba kunikumbatia kwani alisema nimekumbusha rafiki yake wa zamani aliyetangulia mbele za haki.",

"Alikutajia jina la huyo rafiki yake?",

"Hapana. Malkia Omuro, naomba utambue kuwa sina nia mbaya. Nipo hapa kwa ajili ya mdogo wangu tu.",

"Aera, ni kweli kwamba ulikwenda kumuona Tarura?", malkia alimuuliza,

"Hapana. Nilikutana na Tarura mara moja darajani na wala sikujua kuwa ni yeye. Aliniita jina lisilo langu nami nikapuuzia.", 

"Jina gani?",

Aera alichangamsha akili kukumbuka jina aliloitwa. Hatimaye kumbukumbu zilimpata.

"Aliniita Stara.",

Malkia Omuro alishtuka nusura akalie matope. Stara? Ni kweli kwamba aliona ufanano wa Aera na dada yake lakini alipuuzia tu kwasababu sio mara ya kwanza kwake kufananisha mabinti na marehemu dada yake. Miaka yote hiyo bado alikuwa akijilaumu na kifo cha dada yake, hivyo aliiona sura ya Stara kwenye nyuso mbalimbali. Mwanzoni ilimsumbua lakini alizoea. Hivyo hata alipomuona Aera, alijua ni picha tu iliyotengenezwa na akili yake kama njia moja ya kukabiliana na upotevu wake.

Alihisi kuwa yeye pekee ndiye aliyeona ufanano huo, lakini kumbe mfalme aliuona, na Tarura aliuona pia.

"Aera, una miaka mingapi?", malkia aliuliza kwa hamasa,

"Ishirini na tano, malkia.", Aera alijibu.

"Je, hawa ni wazazi wako wa kukuzaa?",

"Mfalme pia aliniuliza hilo swali. Bila shaka, malkia. Hawa ni wazazi wangu na Gema ni mdogo wangu wa damu.",

Malkia Omuro alianza kupiga mahesabu kimoyomoyo. Ufanano, miaka, usiri kati ya mfalme Bazi na Tarura; jibu lilimjia bila itirafu. Aera alikuwa binti wa Stara na mfalme Bazi. Kama Stara alijua kuhusu kifo chake, basi alifahamu kuhusu ubaya uliomwelekea mwanae, na hivyo alifanya ujanja kumuondoa mapema na kumficha. 

Lakini hatima ni kitu cha ajabu sana; pamoja na Stara kumficha binti yake kijiji cha mbali, bado ulimwengu ulimrudisha Aera palepale alipozaliwa. Bila shaka kulikuwa na sababu ya Aera kurudi, na sio kufa siku iliyofuata.

***