Chapter 21 - STARA 8

Jolani alifika na kila kifaa kilichohitajika katika uzalishaji. Muda aliowasili alimkuta Stara tayari anatapatapa na uchungu. Mwili ulilowana jasho. Jolani alifika kitandani na kumshika mkono;

"Tuko pamoja.", alimwambia, "Usiwe na shaka.",

Jolani aliwageukia wasaidizi wa Stara.

"Samahani ila naomba mtupishe.", aliwaambia, "Pia msiende kuiamsha familia ya mfalme mpaka nitakapowaambia. Stara anaweza asijifungue muda huu.",

Bila kubisha, wasaidizi walitoka nje. Aisha alipitia dirishani ili watu wasimuone. Alikuwa na kikapu kilichojazwa vitambaa mpaka juu. Ndani ilikuwa maiti ya kichanga.

 Jolani alimwingiza mkono Stara ili kupima njia kisha alitikisa kichwa, "Njia imefunguka.", alimtaarifu, "Hatuna muda wa kupoteza.",

Aisha alitoa kitambaa kizito na kukiweka katikati ya meno ya Stara ili aking'ate.

"Anza kusukuma.", 

Stara alivuta pumzi na kufanya kama alivyoambiwa. Kitambaa kilidhibiti kelele. Alipumzika sekunde chache kisha kusukuma tena. Mchakato ulitumia dakika kumi nzima, hatimaye mtoto alitoka. Jolani alimwacha alie kidogo kisha alimziba mdomo. Kwa bahati mbaya, sauti ya kilio chake ilisikika mpaka nje. Msaidizi mmoja aliondoka haraka kwenda kuitaarifu familia ya mfalme.

Stara aliangalia uso wa mwanae, katoto ka kike kalikomfanana. Hakuwahi kumpenda mtu kama alivyompenda mwanae. Uchungu ulimkabili pale Aisha alipokitoa kichanga maiti kwenye kikapu na kuweka kichanga cha Stara ndani. Alikifunika na vitambaa.

"Natakiwa kuondoka.", aliwajuza,

Stara alishindwa kujikaza. Aluangua kilio kizito. Sura yake nzima ilibadilika na kuwa nyekundu. Aisha aliwaaga na kutoka mbio kupitia dirishani tena. Jolani alifunika vizuri maiti ya kile kichanga na kumshikisha Stara mikononi.

"Mshike vizuri, lia kwa sauti zaidi, usioneshe unafuu wowote. Lia mama, usijikaze.", alimwambia.

Kilio cha Stara hakikuwa cha uongo. Maumivu ya moyo yalikuwa makali mno. Familia ya mfalme na baadhi ya viongozi waliwasili kwenye makazi ya Stara. Kilio chake kilisikika mpaka nje. Malkia na mfalme walitizamana na kuficha tabasamu zao. Bazi alifika haraka, na kilio cha Stara kilimvunja moyo mara mia. 

Sasa chumba cha Stara kilikuwa kimejaa watu, lakini Bazi aliwasukuma wote na kukimbilia kitandani. Hakuuliza mtu yoyote kilichotokea kwani ilikuwa wazi. Alichukua maiti kutoka mikononi mwa Stara na kuikumbatia, wote wakilia kwa uchungu.

Omuro aliwasili ikulu muda huo na kituo cha kwanza kilikuwa nyumbani kwa Stara. Alishangaa kukuta watu wengi sana nje ya chumba chake. Bazi alikuwa kazungukwa na mfalme na wanaume wengine wakimliwaza. Wanawake walibaki ndani kushuhudia Stara akisafishwa.

Hofu ilimvaa Omuro. Alimfata muhudumu mmoja;

"Nini kimetokea?", aliuliza,

"Konsoti Stara amejifungua, lakini kwa bahati mbaya mtoto amefariki.",

Sasa Omuro alielewa maana ya ndoto yake. Dada yake alikuwa akimuhitaji kuliko mtu yeyote. Aliifata njia mpaka mlangoni na kuingia bila hata kubisha hodi. Stara alikuwa kajilaza kitandani kama mfu. Sauti ilikuwa imemkauka, machozi tu ndiyo hayakuacha kububujika. Omuro alipanda kitandani na kumkumbatia dada yake bila kusema neno lolote. 

"Stara mwanangu, hakuna kitu kizuri kama uhai.", malkia Waridi alisema, "Mkunga mkuu anasema sio kawaida mtoto kutoka kabla ya siku zake, na mara nyingi hii ikitokea, mama na mtoto wote huwa hatarini. Hivyo ni bora upo salama. Watoto watakuja tu.",

Stara hakuweza hata kuongea.

Malkia alimpongeza Jolani kisirisiri akiamini kuwa Jolani alifanya kama alivyomwambia. Alimpatia Jolani mifuko miwili iliyojaa dhahabu na fedha.

***