Harusi ilifanywa karibu maana hawakuwa tena na sababu ya kusubiri. Siku chache za maandalizi, Stara alifungua mdomo wake mara chache sana. Kula ilikuwa changamoto mpaka asimamiwe. Usiku usingizi ulimtoroka. Alikesha akiangalia dari mpaka asubuhi. Alidhoofika mwili na nafsi ndani ya muda mchache sana, na wote waliamini kuwa ni matokeo ya msiba wa mwanae. Omuro alikuwa na Stara bega kwa bega. Kwa namna moja au nyingine alijilaumu.
…
Siku ya harusi hatimaye ilifika. Jioni, Omuro alikuwa chumbani akishuhudia dada yake akipambwa. Stara alikuwa kama kisiki akiwaacha wasaidizi wake wamrembe watakavyo. Walipomaliza kumvalisha kila kitu, Stara aliwaomba wamuache na dada yake. Wahudumu waliondoka.
Stara alijiangalia rasmi kwenye kioo. Alijua kuwa ndiyo ilikuwa mara yake ya mwisho kujiona, tena akiwa amerembeka. Alifahamu kuwa hatoiona kesho na wala halikumsumbua sana. Aliweza kufanikisha malengo yake yote. Mwanae alikuwa salama na familia yake mpya ambayo aliweza kupata jina la mama; Foni.
"Nimependeza?", Stara aliuliza,
Omuro alitikisa kichwa, "Sana. Umependeza sana, Stara.", alimwambia.
"Siku si nyingi na wewe utapendeza kama mimi.",
Omuro alishtushwa na ile kauli, "Una-unamaanisha nini?", aliuliza,
"Nataka ufahamu kuwa nashukuru ni mimi naepitia haya na sio wewe.",
Kauli za Stara zilimchanganya Omuro. Stara alinyanyuka na kwenda kusimama mbele ya dada yake. Alifungua mikono yake;
"Naomba nikukumbatie.", alimwambia.
Omuro alisita kidogo ila alinyanyuka na kumkumbatia dada yake, "Nini kinaendelea kwani? Unanitisha.",
"Miungu ilifahamu maisha yangu bila wewe isingewezekana, ndiyo maana tulifichwa pamoja. Wewe ni nusu ya moyo wangu, Omuro. Usinisahau hata siku moja. Pale utakapojihisi uko peke yako, kaa ukijua nipo na wewe na ninakupenda sana.",
"Mbona kama huna furaha wakati unakwenda kuolewa na mwanaume unayempenda?", Omuro aliuliza,
"Sio kila king'aacho ni dhahabu. Usisahau maneno yangu.",
Wahudumu walikuja kumchukua Stara kumpeleka ukumbini. Omuro alikuwa nyuma yao. Ndoa ilishuhudiwa na watu wachache tu wa karibu. Lakini pamoja na furaha ambayo kila mtu alikuwa nayo, Stara hakuonesha hata tabasamu.
Baada ya ndoa, familia ya mfalme, Stara na makuhani waliondoka pamoja kuelekea msituni wakimwambia Omuro kuwa walikuwa wakienda kutoa heshima kwa mababu zao.
...
Omuro hatokuja kusahau alipokuja kuamshwa usiku kwenda kuona maiti ya dada yake kutoka msituni. Stara alilazwa kitandani na kufunikwa mashuka meupe. Hakuwa na donda wala mchubuko. Sura yake ilionekana kuwa na amani.
Sio kila king'aacho ni dhahabu …
Aliposhika mkono wa dada yake na kuhisi ule ubaridi, alikumbuka mazungumzo yao. Stara alikuwa anamuaga. Je, alijua kuwa anakwenda kufariki? Je, hicho ndicho malkia mama alichomaanisha alipomwambia kuwa atakuja kuwa mke wa Bazi na malkia wa Natron? Ya kuwa dada yake ataonja mauti kwanza ili ndoto zake zitimie?
Usilolijua ni kama usiku wa giza. Mtaka yote kwa pupa hukosa yote kwa haraka. Sasa Omuro alikuwa akiangalia maiti ya dada yake, bei iliyolipwa kwa ajili ya ujinga wake. Huo ndio ulikuwa mwisho wa Stara, na mwanzo wa majuto ya Omuro.
***