Chereads / THE PRIESTESS' PROPHECY (Book 1) / Chapter 12 - MDOMO WA MAMBA

Chapter 12 - MDOMO WA MAMBA

Ledi Kompa na Avana walifika kwenye makazi ya Gema muda mchache baada ya kujulishwa kuhusu hali yake. Gema alikuwa kalala kitandani kinyonge huku kitambaa cha uvuguvugu kikiwa kimewekwa kwenye paji lake la uso. Maumivu yalikuwa yamepungua na nguvu zilikuwa zikirudi taratibu. Alipomuona mume wake mtarajiwa alivaliwa na wimbi la furaha. 

Kwa mara nyingine tena maneno ya Aera yalirudi akilini na kutengeneza mtafaruku. Je, ni kweli kuwa alikuwa kwenye shimo lenye moto? Kama kweli Avana hampendi, mbona alikuwa na macho ya majonzi akimtazama? Je, angekuwa hamjali angefikaje kwenye makazi yake kwa muda mfupi tu? Alipofika kitandani, Avana alishika mkono wa Gema na kuubusu;

"Mchumba wangu, nini tatizo?", Avana aliuliza, huzuni ikitoka kwenye sauti yake.

"Naendelea vizuri, mume wangu mtarajiwa.", Gema alijibu.

"Kwanini upo kwenye hali hii? Nini kimesababisha?",

Gema aliogopa kujibu maana ingemaanisha kuwa angemuweka Aera hatarini. Lakini ledi Kompa alikuwa mbele yake kiakili. Alifahamu kuwa Gema asingeweza kufungua mdomo wake na kusema kilichojiri. Hivyo alimgeukia Mone.

"Wewe.", ledi Kompa aliita.

Mone alimgeukia na kuinamisha kichwa, "Abee, ledi Kompa.", 

"Konsoti Gema alikuwa na nani kabla ya hali yake kutetereka?",

"Dada yake alikuja kumtembelea, ledi Kompa.",

Gema aliuma meno kwa hasira. Ama kweli hakuwa na mtu wa kumuamini, hasa wahudumu wake. Kuficha siri ndani ya ikulu ilikuwa ni changamoto, tena kubwa sana. Ledi Kompa alijongea kitandani kwa Gema.

"Dada yako alikwambia nini mpaka ukataka kupoteza fahamu?", aliuliza,

"Haikuwa sababu.", Gema alijitetea.

"Sikujua kama wewe ni dhaifu namna hii. Kama mazungumzo tu yanakufanya unyondee hivi; Je, utaweza kumzalia mwanangu watoto kweli?", ledi Kompa alibadilisha muelekeo wa mada.

Gema alianza kuogopa maana alijua anakwenda kutelekezwa.

"Tulitakiwa kuhakikisha kuwa umefanyiwa uchunguzi na matabibu kabla hatujakukaribisha kwenye familia yetu. Familia ya mfalme inatakiwa kukua.", ledi Kompa aliendelea kumkandamiza Gema kwa maneno, "Kwa kuwa umri wako mdogo, tulitegemea kuwa ungemzalia hata watoto watano. Lakini kwa hizi dalili, hata mmoja itakuwa ni miujiza.",

"Hapana!", Gema alisema kwa shauku, "Nina afya imara, ledi Kompa. Aera alinipa taarifa mbaya ambazo zilishtua moyo wangu. Nakuahidi kuwa mimi sio dhaifu na kuwa ninaweza kumudu changamoto zote za ujauzito.",

Ledi Kompa alisogea karibu, "Ni habari gani hizo alizokwambia?",

Sasa Gema alianza kufanya mahesabu akilini. Habari aliyopewa na Aera ilikuwa ni hukumu ya kifo. Lakini alikuwa na chaguzi mbili; Amtetee dada yake kisha afukuzwe warudi kijijini, ama aseme ukweli ili ndoto zake zitimie. 

"Konsoti Gema.", Avana alimshika mkono wake wa pili na kuuweka kifuani kwake, "Nakupenda sana, mchumba wangu, na ninatamani sana uwe mke wangu. Upendo wangu kwako unazidi milima mirefu. Kwa ajili yako naweza hata kumwaga damu yangu. Nataka kuwa na wewe mpaka kifo kitutenganishe. Je, na wewe unataka hilo pia?", 

Maneno yake yalikuwa kama sumu kali iliyosambaa kwa kasi ndani ya mwili wake. Kupendwa namna ile kulizidi utajiri. Ubongo wake ulichora mizani; upande mmoja alikaa Avana, na upande mwingine alikaa Aera. Aera alikuwa dada yake tu, tena aliyethubutu kumchapa kofi la shavu. Avana alikuwa mchumba wake aliyemzawadia cheni ya dhahabu. Ametoka kukiri hisia zake na kumfanya Gema ajione kama malkia. Aliona kuwa atapata vitu vingi zaidi akimchagua Avana. Aera hakuwa na cha kumpatia. Hakuweza kupoteza vyote hivyo kisa dada yake.

"Aera hajapenda mimi kuchumbia na wewe.", Gema alianza kueleza, "Anasema kuwa ni mtego.",

"Anamaanisha nini?", ledi Kompa aliuliza,

"Kaniambia kuwa nimekuja kutolewa kafara kama wake wote wa kwanza wa wahusika wa kiume wenye damu ya kifalme ndani yao.",

Ledi Kompa na Avana walitazamana. Walijua kuwa wakionesha mwitikio tofauti basi Gema atayaamini maneno ya dada yake. Avana alikuwa kama zuzu akimtegemea mama yake aokoe jahazi. Na alipatia; ledi Kompa aliweza kujiongeza.

"Dada yako ametuita sisi wachawi?", aliuliza kwa hasira ya kuigiza.

"Hapana, ledi Kompa. Ame_",

"Ameikashfu familia tukufu ya mfalme na kutuita wachawi? Kafara _",

Mlango ulifunguliwa na mjumbe wa mfalme aliingia ndani kwa kasi.

"TANZIA! TANZIA!", alisema kwa sauti ya juu.

Wote waliokuwa ndani walimtolea macho.

"Kuhani mkuu Tarura ametangulia mbele za haki.", mjumbe alitangaza.

Gema hakumfahamu Tarura lakini wote waliobaki walimjua na waliingiwa na majonzi. Pamoja na habari hiyo mpya, bado ledi Kompa alikuwa akitafakari Gema alichosema. Kama ingekuwa ni msituni, basi Aera angekuwa simba mwindaji maana alikuwa ni mgumu kushindwa. Alifanya ledi Kompa aanze kujenga mawazo mabaya kumlenga.

Familia ya mfalme na viongozi wote walikutana kwenye ukumbi wa mkutano kwa ajili ya mipango ya msiba. Habari ya kufa kwa kuhani mkuu ilikuwa imesambaa kila kona. Japo kuwa wengi walikuwa na huzuni, majonzi ya mfalme yalizidi kila mtu. Tarura alifariki kipindi ambacho mfalme Bazi alimuhitaji zaidi. Alihisi miungu ilimtelekezea msala.

"Kifo cha Tarura hakikuwa cha kawaida.", mfalme Bazi alitamka akiwa juu kwenye kiti chake.

Malkia Omuro alikaa mkono wake wa kulia na Noro, mwana wa kwanza wa mfalme alikaa mkono wa kushoto. Ledi Erini na ledi Kompa walisimama nyuma ya kiti cha malkia, huku watoto wao na familia zao wakiwa wamesimama msitari wa mbele kabisa pamoja na viongozi wengine.

Sentensi aliyotamka mfalme ilitengeneza gumzo.

"Matabibu wamegundua kuwa Tarura alipewa sumu bila kujua na ndiyo sababu iliyopelekea kifo chake.", mfalme Bazi aliendelea, "Hivyo, ninatangaza; Mpaka mwenye hatia apatikane, kila mtu aliyemo humu ndani ni mtuhumiwa.",

Minong'ono ilisambaa ukumbini. Kila mtu alishika moyo wake mkononi. Inamaanisha kuwa ndani ya ikulu kulikuwa na muuaji, hivyo hakuna aliyekuwa salama, hadi mfalme. 

Baada ya kikao kuisha, watu walianza kuondoka. Avana alimfata mama yake na kumvuta pembeni.

"Mama, tunafanyaje kuhusu Aera?", Avana aliuliza kwa kunong'ona.

"Aera ni mtu hatari sana. Kwanza amejuaje kuhusu hii laana?", ledi Kompa alijiuliza bila jibu, "Sio mtu wa kawaida huyu binti. Tucheze nae kwa umakini.",

"Gema akiamini maneno ya dada yake, tumekwisha. Hili jambo halijawahi kutokea tangia enzi za mababu zangu. Likitokea sasa, tena kwenye zamu yangu unajua maana yake?",

"Ninajua mwanangu, na ndio maana nipo nahangaika kutafuta suluhisho.",

Huku Avana akipepesa macho alimuona malkia Omuro akiondoka ukumbini na wahudumu wake. Alipata wazo.

"Mama, kaongee na malkia Omuro.", alisema.

"Nini? Huoni kama ni hatari?", ledi Kompa aliuliza,

"Hapana. Usimwambie ya Aera kufahamu kuhusu laana. Mwambie kuhusu Aera kumkumbatia mfalme. Naamini malkia atakasirika sana na kumuadhibu Aera. Isitoshe, anaweza kumfukuza kabisa ikulu.",

"Alafu kweli.", ledi Kompa alifurahia, "Kwanini sikuwaza hivi tokea zamani? Una akili sana, Avana.",

"Asante mama. Haya, nenda sasa hivi kabla hajapata ugeni mwingine.",

"Sawa. Uwe na usiku mwema, mwanangu. Nakuahidi, kesho asubuhi ukiamka kila kitu kitakuwa sawa.",

"Nakuamini mama.",

Ledi Kompa aligeuka upande wa pili na kuondoka na muhudumu wake. Muda huo huo Avana aliona ni vyema kurudi kwenye chumba cha Gema ili asiruhusu mashaka yasombe akili ya Gema na kuchafua hali ya hewa ya ikulu. 

***