Miaka 50 iliyopita himaya ya Natron ilikuwa chini ya uongozi wa Zito, mfalme katiri na mwenye kupenda kumwaga damu. Asili yake ya ukorofi na ukatiri ilitengeneza uadui mkubwa na falme za jirani na kwa bahati mbaya ilisababisha vita kubwa. Jeshi la Natron lilikwenda kupigana vita na himaya ya Ozi. Vita ilichukua miezi kumi na miwili kuisha na kwa bahati nzuri himaya ya Natron ilipata ushindi. Walikamata watumwa na mali nyingi kurudi nazo nyumbani.
Mfalme Zito na kijana wake, Antivo (baba wa mfalme Bazi), walishiriki kwenye vita ili kusaidia jeshi lao lililokuwa matatani kushindwa. Sasa walikuwa wakirudi himayani kwao na ushindi. Ingawa lilikuwa jambo la kusherekea, Antivo hakuwa na raha hata kidogo. Hakupenda uongozi wa baba yake kwani damu nyingi ilikuwa ikimwagwa tena ya watu wasio na hatia. Alitamani zamu yake ifike ili arudishe amani kwa wananchi wao waliokuwa wakiishi kwa mashaka.
Wakiwa njiani, walipita kwenye kijiji kilichokuwa mpakani. Kwa bahati mbaya, kijiji hicho kilikuwa kimetoka kuvamiwa; mifugo ilikuwa imesombwa, watu walikuwa wameuliwa na boma zao zilibaki majivu. Antivo aliumia sana lakini yeye peke yake ndiye aliyekuwa na roho nyepesi. Kila mtu alipita kama haoni.
Ole!
Sauti za vilio vya watoto zilisikika kutoka chini ya makuti ya minazi lakini hakuna hata mmoja kwenye jeshi aliyegeuka. Antivo alimtazama baba yake kwa macho ya kuomba, lakini mfalme Bazi alimpuuza. Hasira ilitengeneza giza kwenye kifua chake. Alikuwa amefika tamati kwenye sekta ya kumridhisha baba yake ili asionekane dhaifu. Alishuka kwenye farasi na kukimbilia kwenye makuti.
"Antivo!", mfalme Zito alimuita kwa hasira, "Rudi!",
"Hapana.",
Antivo alinyanyua makuti na kukuta vichanga viwili vya kike. Mwanga ulipowapiga machoni walilia kwa nguvu zaidi. Iliyeyusha moyo wa Antivo kwani alikuwa amemuacha mke wake na mimba kipindi anaelekea vitani na baba yake. Watoto walikuwa udhaifu wake. Alionea huruma vile vichanga kwani vilimfanya amfikirie mwanae.
Mfalme Zito alishuka kwenye farasi wake na kumfata. Alimvuta bega,
"Unafikiria nini?", alimuuliza,
"Narudi na hawa watoto ikulu.", Antivo alimueleza baba yake,
"Hichi kijiji sio cha himaya yetu. Unataka ulee vichanga vya himaya nyingine?",
"Himaya gani? Unamaanisha himaya hii uliyotoka kuiangamiza?", Antivo alifoka, "Tazama kijiji chao, baba. Wote ni maiti. Walionusurika ni hivi vichanga viwili. Hawakuwa na hatia yeyote, na hawastahili kufa kinyama.",
Antivo alifahamu fika ya kuwa baba yake hakujivunia kuwa naye kwasababu walikuwa na mawazo tofauti ya uongozi. Mfalme Zito alimuona kijana wake kuwa ni dhaifu hivyo hakutaka kumrithisha uongozi, huku Antivo alitamani sana mauti yamkute babaye ili aweze kuimarisha himaya yao.
"Hii ndio sababu inayonifanya nisikupe ufalme. Huruma yako itakuletea migogoro mingi sana.", mfalme Zito alimueleza,
"Baba tazama.", Antivo alinyoosha kidole kwa jeshi lao, "Unafahamu ni watu wangapi wamepoteza maisha kutokana na ukorofi wako? Tunarudi na ushindi lakini kuna watoto wamefanywa yatima, wanawake wamefanywa wajane na wazazi wamepoteza vijana wao. Uwezo wa kuepuka mapigano ulikuwa nao lakini bila kumwaga damu hujisikii raha.",
"Antivo, unathubutu _",
"Nakuahidi kuwa hakutakuja kutokea mfalme mwingine kama wewe, na mimi ndiye nitahakikisha. Sheria zako ulizotunga, njia zako za uongozi, ukifariki utakwenda nazo ahera.",
Mfalme Zito alimtandika Antivo kofi la uso, lakini Antivo hakutetereka. Alizidi kumkazia baba yake macho.
"Mimi ndimi mfalme wa Natron, na ninakuamuru urudi kwenye farasi wako sasa hivi!", mfalme Zito alimuamuru,
"Nami ni Antivo, mwana wa Zito. Natangaza kuwa hivi vichanga vitakuwa chini ya uangalizi wangu kuanzia leo mpaka kifo changu. Kama huwezi kukubali, chukua panga uniue sasa hivi maana hautapata nafasi nyingine.",
Jeshi lilikaa kimya likitazama ugomvi mkuu wa baba na kijana wake. Hakuna aliyethubutu kuingilia kati. Antivo na mfalme Zito walitoleana macho huku moshi ukifuka vichwani mwao. Apende asipende, Antivo alikuwa mwanae, tena mrithi wa kiti cha ufalme baada yake. Hakuweza kumuua, lakini;
"Ukichukua hivi vichanga na kuvileta ikulu, haya ndiyo yatakuwa maneno yangu ya mwisho kwako.", mfalme alimuonya.
"Na ikawe hivyo.",
Antivo alivinyanyua vile vichanga na kurudi navyo kwenye farasi wake. Mwanajeshi alimsaidia kubeba mtoto mmoja na safari iliyokatishwa iliendelea. Na huo ndio ulikuwa mwanzo wa ukimya kati ya mfalme na mwanae.
…
Kulikuwa na mapokezi makubwa ikulu kukaribisha jeshi lao lililowabebea ushindi. Karamu iliandaliwa na malkia pamoja na wakwe zake wakitegemea kuwa mfalme na Antivo watatambua juhudi zao. Lakini kwa sababu wasizozifahamu, sherehe nzima, waliokuwa wakiburudika ni wanajeshi tu. Mfalme na Antivo walikuwa wamenuna, na Antivo hakutaka kukaa meza moja na baba yake.
Ilibidi malkia aende kuzungumza na wanajeshi kujua yaliyojiri. Baada ya hapo alijua kuwa hakukuwa na suluhisho. Antivo alikuwa na hasira mbaya kama ya baba yake hivyo wa kujishusha alikuwa hayupo. Kutokana na asili ya ukorofi wa mumewe, malkia hakuweza kuliongelea swala hilo kwani angejumlishwa kwenye msala. Aliona bora ajikalie kimya, andelee kula matunda ya kimalkia.
…
Usiku, Antivo alikwenda kwenye makazi ya mkewe, konsoti Waridi. Kichanga chake kilikuwa kimelala usingizi kwenye titi la mamaye. Furaha ilimfanya Antivo ajihisi yupo peponi. Hatimaye alikuwa baba. Machungu yote aliyopata kutoka kwa baba yake aliyavua mlangoni.
"Karibu, mume wangu.", alisema Waridi kwa sauti nyororo na auheni ya kumuona mumewe mzima wa afya.
Jambo la Antivo kwenda kupigana vita na babaye kilimpatia uchungu Waridi, kwani vita huja na majanga yake, baya zaidi kuwa kifo. Wakati Antivo alipokuwa akiondoka, Waridi alikuwa na ujauzito wa miezi miwili. Kila siku iitwayo leo alikwenda kuomba miungu imlinde mumewe. Sasa mumewe alirudi mikononi mwake akiya yu hai.
"Nisamehe mke wangu kwa uchungu niliyokupatia.", Antivo alisema, "Pia nakushukuru kwa kuwa shujaa wa mwili na roho.",
Antivo alisogea karibu na kuanza kumtathimini mwanae.
"Tumepata mtoto wa kiume, mume wangu. Nami nilikataa apewe jina na mtu yeyote zaidi yako.", Waridi alieleza,
"Bazi, mtoto wetu ataitwa Bazi. Naye atakuwa mfalme mahiri wa Natron kwa kufata nyayo zangu.",
"Je, tetesi nilizosikia zina ukweli wowote?", aliuliza Waridi, "Kwamba wewe na mfalme Zito mmegombana na kuapa kutokuongeleshana tena?",
"Ni kweli.",
"Kwanini, mume wangu?",
"Kwasababu baba yangu ni katiri sana. Wananchi wetu wanaishi kwa hofu. Unajua ni watu wangapi wamepoteza maisha tangia aingie madarakani? Aliuwa makuhani wetu wanawake _",
"Alikuwa na sababu, Antivo. Siri ingejulikana kuhusu kasoro ya familia yetu ingetuletea hatari.",
"Kungekuwa na njia nyingine.", Antivo aliketi kitandani, pembeni ya mkewe, "Najua wazee wa baraza wanamjaza fikra potofu za kuwa ili himaya iimarike lazima damu imwagike, lakini mimi nakataa.",
"Siku zote wewe na mfalme mlikuwa na mawazo tofauti ya kisiasa, lakini hamkuwahi kugombana na kufikia hili hitimisho. Nini haswa kilitokea huko mlipotoka?",
Antivo alivuta pumzi, "Kijiji cha mpakani kimevamiwa. Watu wameuawa kama wanyama na mifugo yote imesombwa. Boma zao zimechomwa moto na kubaki majivu." alieleza kwa uchungu,
"Kwahiyo?",
"Tulipokuwa tukipita tuliona vichanga viwili.",
Waridi alishangaa, "Vilikuwa hai?",
"Ndiyo. Walifichwa chini ya makuti ya minazi.",
"Masikini. Sasa mkafanyaje? Usiniambie kuwa mliviacha vife.",
"Baba alitaka niviache lakini niligoma na kuvichukua. Ndicho kilichopelekea yeye kuapa kutosema neno lolote kwangu.",
Waridi alishika mkono wa Antivo, "Vyovyote vile, kitendo ulichokifanya ni kikubwa na kizuri. Wewe ni mtu mwema sana, ndio maana ninakupenda. Amini maneno yangu, huo moyo wako utakufanya uwe kiongozi imara sana kwenye himaya yetu.",
Maneno yake yalimfariji Antivo. Ilimpa nafuu kubwa kupata ushirikiano wa mkewe.
"Hivyo vichanga viko wapi?", Waridi aliuliza,
"Nimevikabizi kwa wanawake walezi. Watalelewa vizuri na kuja kuwa mabinti maridadi sana.",
"Isitoshe, Bazi atapata marafiki wakucheza nao.", Waridi aliongeza,
"Haswaa.",
***