Chapter 16 - STARA 3

Darasa lilikuwa limekwisha na wanafunzi walikuwa wameondoka kasoro Stara. Mwalimu alimpatia kazi ya kurudisha dawa zote kabatini. Akiwa bize na upangaji, Bazi alifika na kukaa kwenye kigoda akimtazama. Mapigo ya moyo yalimwenda mbio kwa jambo lililomleta. 

Stara alipogeuka nyuma alishtuka kumuona Bazi, nusura aangushe dawa alizobeba.

"Unafanya nini hapa?", aliuliza haraka,

"Nimekuja kukuona. Kwani kuna shida yoyote?", Bazi naye aliuliza,

"Hakuna shida lakini nina shughuli za kufanya.",

"Hakuna shida. Kuna kitu nimekuja kusema, hivyo endelea na shughuli zako huku ukinisikiliza.",

"Sawa.",

Stara aliendelea kupanga dawa.

"Kuna binti ambaye sichoki kumfikiria. Amekamata moyo, akili na nafsi yangu.", Bazi alieleza.

Stara alianza tena kuumia roho akifikiri kuwa Bazi alikuwa akimuongelea Omuro. Wote wawili walikuwa wakimuumiza maana alijiona wa kukosa. Nayo hii ilimfanya akasirike.

"Natamani sana kujua anachofikiria maana nampenda sana, na nataka awe mke wangu.", Bazi aliendelea.

"Sasa si ukamwambie yeye?", Stara aliongea kwa hasira, "Kwanini unakuja kuniambia mimi? Hivi mnaniona mimi ni jalala la kumwaga hisia zenu? Mnahisi mimi sina moyo au?",

Bazi alinyanyuka na kumsogelea, "Stara _",

Stara alifuta machozi na kuendelea kupanga dawa, "Kama unampenda sana basi nenda kamwambie. Labda na yeye anakupenda pia.",

"Ndicho kitu ninachofanya.", alishika mkono wa Stara, "Stara, nakupenda.",

Stara alimtazama kwa macho yenye swali, "Unasema?", 

"Nakupenda wewe hapo, sio mwingine.", 

Stara aliishiwa maneno. Je, ajisikie furaha, au ajisikie vibaya? Bazi kumpenda yeye ilimaanisha Omuro atakuja kuumia, naye hakutaka hilo litokee. Je, afanyeje maana naye alimpenda sana Bazi.

"Kuna mtu nataka kuongea naye kwanza kabla sijakupa jibu.", Stara alisema.

Bazi alimvuta na kumkumbatia, "Chukua muda wako, lakini usichelewe.",

Kwa bahati mbaya, Omuro alikuwa amekwenda kumuona Stara akiwa darasani. Muda aliofika alimkuta tayari Bazi amekaa, hivyo alijibanza nyuma ya kibanda kusikia maongezi yao.

Chozi refu lilitiririka shavuni pake baada ya kujua kuhusu hisia za Bazi kwa Stara. Hakupendwa yeye. Moyo wake ulivunjika vipisi. Hakuweza kubaki pale na kuzidi kujiumiza. Aligeuka nyuma kwa fosi na kugongana mwili na mtu mwingine. Hakujua kuwa kuna mtu alikuwa amesimama nyuma yake muda wote huo. Aliponyanyua macho alishtuka kumuona malkia Waridi.

"Malkia mama, samahani, sikukuona.", alisema Omuro,

Malkia Waridi alitabasamu, "Nilikuwa najiuliza sana kwanini hutaki kujifunza chochote kama Stara. Kumbe tayari umeshapata ukipendacho.", alisema,

"Sijui unamaanisha nini _",

"Mwanangu, unampenda Bazi, sio?",

Omuro alitazama pembeni kwa aibu, "Haina maana, anampenda Stara.",

"Kwahiyo umekata tamaa?",

Omuro alishindwa kujibu. Malkia alimuhurumia sana. Alisogea karibu na kumkumbatia kwa upendo wa dhati, "Mwanangu, nakuahidi kuwa utakuwa mke wa Bazi na malkia wa himaya yetu.",

"Lakini _",

"Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha Stara anamkubalia Bazi. Vingine niachie mimi.",

"Stara hatodhurika?", Omuro aliuliza maana alimjali sana mwenzie.

"Wala hatodhurika.",

"Sawa malkia mama. Tafanya hivyo.",

Malkia alitupa jicho lake kwa Bazi na Stara kisha kutabasamu zaidi.

Usiku ulipoingia, Omuro alikuwa peke yake chumbani, Stara hakuwepo. Asichofahamu ni kwamba Stara alikuwa nje ya mlango akisita kuingia. Alikuwa amejipanga kwenda kumwambia mwenzie kuhusu Bazi, lakini aliogopa pale alipofikiria jinsi Omuro atakavyopokea hiyo habari. 

Ndani, Omuro nae alikuwa akitembea mbele na nyuma. Malkia alimpa kazi ya kuhakikisha Stara anamkubalia Bazi, hivyo japokuwa roho ilikuwa ikimuuma kupita kiasi, alipaswa kuigiza kama yupo sawa ili mwenzie anase kwenye mtego. Basi wote wawili, roho zao zilikuwa juu juu.

Baadaye Stara alipiga moyo konde na kuingia chumbani kwao. Alimkuta Omuro kasimama dirishani, mdomo wake ukicheza kama anazungumza na mtu, lakini alikuwa akijiongelesha mwenyewe. Alikuwa akitunga sentensi za kutumia ili kumshawishi mwenzie.

"Omuro.", Stara aliita kwa upole.

Omuro alimgeukia, "Mbona umechelewa kurudi chumbani? Nilikuwa nimepatwa na woga.", alisema.

"Nipo salama.", Stara alieleza, "Kuna kitu nataka nikushirikishe kama hautojali.",

"Kabla hujaniambia kitu chako, naomba kwanza nikwambie kitu changu.",

"Kuna kitu unataka kuniambia?", 

"Ndiyo.", Omuro alitikisa kichwa kukubali.

Wote wawili walikwenda kuketi kitandani kwao kwa kuangaliana kama wanacheza mdako. 

"Leo nilifata ushauri wako na kwenda kwa Bazi kukiri hisia zangu.", Omuro alianza, "Lakini nimegundua kuwa Bazi hana mapenzi hayo kwangu bali anampenda mtu mwingine.",

Stara alikauka koo kwa wasiwasi.

"Bazi anakupenda wewe, Stara.", Omuro aliendelea, "Bila shaka na wewe unampenda pia.",

"Omuro, sikutaka _",

"Nimeumia lakini upande mwingine nina amani. Mimi na wewe sio ndugu lakini nakupenda kama dada yangu wa damu. Nimefurahi kuwa Bazi amekupenda wewe na sio binti mwingine wa nje. Najua atakupa furaha sana na wewe utampenda zaidi ya ninavyompenda mimi. Hivyo, nakupa ruhusa ya kuwa naye.",

Machozi yalitiririka mashavuni pa Stara. Maneno ya Omuro yalimgusa sana na kumfanya ajione wa bahati. Jambo lililokuwa likimkereketa sasa lilisawazika.

"Omuro, una uhakika na unachosema? Una uhakika kuwa hautanibebea kinyongo?", Stara aliuliza,

"La hasha! Nipo pamoja na wewe daima, Stara.",.

Stara alimkumbatia Omuro kwa furaha. Alidhani kuwa aliwekwa njia panda; amchague Bazi au Omuro. Ni bahati gani hii ya kuwa alikwenda kuwapata wote bila kumkosa hata mmoja? Kimoyomoyo, alishukuru sana miungu.

Huku, Omuro alijipongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya. Sasa mpira ulikuwa mikononi mwa malkia. Hakufahamu malengo ya malkia Waridi ya kwanini ametaka amkuwadie Stara kwa Bazi maana ilimaanisha yeye anajitoa kwenye mashindano. Lakini pia malkia alimuhakikishia kuwa yeye ndiye atakuwa mke wa Bazi na malkia wa Natron. Alisubiri kwa hamu kurasa zianze kufunguka.

***