Chapter 8 - SWALI

Kuhani mkuu wa ikulu aliitwa Tarura. Alikuwa na umri wa miaka tisini na miwili. Aliingia madarakani baada ya mauaji ya chinichini ya makuhani wa kike. Kazi nyingi za matambiko alipenda kuwaachia makuhani wengine kama Badri kuyaendesha. Umri wake ulikuwa umekwenda. Alikuwa akifanya kazi ya ziada tu.

Jioni, Tarura alijiandaa kumpokea mfalme Bazi kwenye makazi yake. Mfalme alikuwa na mazungumzo nyeti naye. Tarura alitumia mkongoja wake kunyanyuka na kutembelea mpaka mlangoni kisha alifungua mlango na kumkaribisha mfalme Bazi ndani. Wahudumu wa mfalme walibaki nje ya boma.

"Samahani kwa kuja jioni, Tarura.", alisema mfalme huku akiketi.

"Kwangu ni kwako, mfalme Bazi. Unakaribishwa muda wowote.", Tarura aliketi pia, "Naamini ujio wako mahali hapa sio bure. Nini kinakusumbua?",

"Nahisi nipo kwenye njozi, maana hichi kinachoendelea kinafanana na soga za uwongo na kweli kutoka kwa bibi na babu zetu.",

"Unanipa mashaka. Nini kinaendelea?",

"Nimemuona Stara.",

Tarura alishtuka, "Stara? Unamaanisha _",

"Ndiyo, rafiki yangu mpendwa Stara.",

"Umemuona wapi? Ndotoni?",

"Nimemuona kwa macho yangu mawili.", mfalme Bazi alisema, "Hata mimi nilishangaa na bado ninashangaa. Inatokeaje mtu unafanana na binadamu mwingine namna ile bila hata kuwa na undugu?",

"Mfalme, unamuongelea nani?", Tarura aliuliza, maana maneno ya mfalme yalimpatia kizunguzungu.

"Familia ya mke mtarajiwa wa Avana inaishi ikulu sasa. Iliwasili siku chache zilizopita. Dada wa Gema, Aera, amefanana sana na Stara. Nahisi kama mizimu inanipa kitendawili.",

"Ana miaka mingapi?",

"Ishirini na mitano, miaka kamili tangia Stara afariki.",

"Unahisi nini? Ya kwamba anaweza kuwa mtoto wa Stara?",

"Inawezekana, Tarura.",

"Kama kumbukumbu zangu zipo sawa, mtoto wa Stara alifariki akiwa tumboni. Wakunga waliokwenda kumsaidia walithibitisha kutoa mtoto maiti.",

"Wanaweza kuwa walidanganya.", mfalme Bazi alihoji,

"Unasema huyo Aera ni binti?", Tarura aliuliza,

"Ndiyo.",

"Mtoto wa Stara alikuwa dume, hivyo haiwezekani.",

"Naamini ukimuona Aera utaamini maneno yatokayo kwenye kinywa changu.",

Tarura bado alikuwa na moyo mgumu, "Umekuja ukitaka msaada wangu. Je, ni kipi unataka nifanye?", aliuliza,

"Nataka uniangalizie kama Aera ni binti wa Stara.", alisema mfalme Bazi.

"Kabla ya yote tahitaji kumuona huyo Aera kwanza. Kama kweli amefanana na Stara tafanya kila niwezalo ili nipate jibu.",

"Bila shaka, Tarura. Wewe pekee ndiye tumaini langu kwa sasa.",

Moyo wa mfalme uliota tundu ambalo lingezibika baada ya kufahamu ukweli kuhusu Aera. Subira haikuwemo ndani yake.

Aera aliona utofauti wa mama yake tangia alipotoka kumuona Gema. Hakuwa amechangamka, na kwa mbali ni kama alikuwa akimkwepa Aera. Kitendo kile kilimuhuzunisha Aera. Familia yao ilitakiwa izidishe upendo na ukaribu lakini Foni alikuwa akichora mpaka wa kuwatenganisha taratibu. Walipokuwa wanajiandaa na chakula cha jioni, Aera alimvuta mama yake nje kwa ajili ya maswali. Aliona ni vema kama baba yake hatosikia.

"Mama, kuna shida yoyote?", Aera alimuuliza Foni.

Foni hakutaka kufanya mazungumzo ya aina yoyote na Aera maana tayari alikuwa hamuamini. Lakini kwa bahati mbaya, Aera alikuwa kamuweka kibindoni hivyo hakuwa na budi kuendeleza mjadala ule.

"Mdogo wako anaandamwa na wake wa mfalme.", Foni alitamka, "Na wewe ndio sababu.",

"Mimi?", Aera alishangaa, "Nimefanya nini?",

"Tukuulize wewe maana kila mtu anakuulizia. Bila shaka hawakuongelei kwa mazuri, hivyo naomba uniambie ulichofanya.",

"Mama, sijafanya chochote _",

"Gema hana amani kwa sababu yako. Kaa ukijua kuwa chochote unachofanya kinaenda kumuathiri mwenzio.",

"Mama _",

"Hivi Aera, unajua kabisa maisha yetu yalivyokuwa magumu. Hii ni bahati ambayo haitakuja kujirudia. Tumebahatika kuwa mahali hapa kwa sababu ya Gema, hivi kweli unataka kumuharibia mwenzio? Gema anataka kukata tamaa na kurudi kijijini.",

"Mama embu nisikilize!", Aera aliongea kwa hasira baada ya kuona hapewi nafasi ya kuzungumza, "Sijafanya chochote. Alafu hii mnayoiita bahati sio bahati, ni mtego.",

Alipokwishakusema hayo alifunika mkono juu ya mdomo wake kwa shaka. Hakutaka familia yake ijue kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia mpaka apate suluhisho.

"Unamaanisha nini mtego?", Foni aliuliza,

"Nimemaanisha hivi _ ya kuwa _ ulimwengu una mambo mengi.", Aera alibadilisha muelekeo wa mada, "Vitu vizuri vinaweza kuwa vibaya.",

"Hivi unajielewa kweli? Naomba usituletee balaa, umesikia? Kama unaona huwezi, funga virago vyako urudi kijijini mwenyewe.",

Maneno ya Foni yaliuchoma moyo wa Aera kama bisu. Mama yake hakuwahi kumtamkia maneno kwa uchungu hivyo. Siku zote hakuwahi kujiuliza kuhusu upendo wa mama yake kwake lakini muda huo aliweza kuona kuwa upendo huo ulikuwa ukififia. Aliumia mno.

"Katika matembezi yangu jana usiku, nilikutana na mfalme Bazi.", Aera alisema baada ya kuhisi chimbuko la mtafaruku ule, "Mfalme na mimi tulizungumza kidogo kisha akaomba kunikumbatia.",

"Unasemaje?", Foni alifoka, "Umemkumbatia mfalme?",

"Mfalme aliomba kunikumbatia, ulitaka nifanyeje? Wewe unaweza kumbishia mfalme?", Aera alihoji, "Sisi ni wananchi tu, tena masikini. Hatuna jinsi. Pia huyu ni mfalme, na wala halikuwa ombi la nia mbaya. Mazungumzo yetu yalimpa huzuni, hivyo _",

"Wewe sio malkia na wala sio ledi!", Foni alizidi kumfokea, "Kwanza aliyekutuma uende kutembea mbali huko ni nani? Usituletee shida, Aera. Nakuonya. Wivu wako utatufanya wote tukose. Tena iwe mwanzo na mwisho! Kesho utakwenda kuomba msamaha kwa ledi Kompa na ledi Erini kwa kosa ulilofanya.",

"Kosa gani, mama?",

"Usiniulize maswali! Tii amri.",

Foni alianza kurudi ndani, lakini:

"Mfalme aliniulize kama nyie ni wazazi wangu wa kunizaa.", Aera aliongea taratibu.

Foni aliposikia hivyo miguu yake iliganda ardhini. Uso wake ulivaa swali. Kwa bahati nzuri, Aera hakuweza kuona uso wa mama yake maana Foni alimpa mgongo. 

"Mfalme alisema nimefanana na mtu aliyemfahamu _",

"Wewe ni binti yangu uliyekaa tumboni mwangu miezi tisa. Sisi ni wazazi tuliokuzaa na Gema ni mdogo wako wa damu. Mwisho wa mjadala.",

Foni aliongeza mwendo na kuingia ndani ya nyumba yao. Kwa mbali Aera aliwaona wahudumu wakijongea na chakula, lakini hamu ilikuwa imeondoka. Familia yake ilikuwa ikijitenga na yeye taratibu.

***