Aera alishuka milimani asubuhi na mapema kurudi nyumbani. Mvua ilikuwa imeacha kunyesha lakini bado wingu lilitanda. Njia nzima alikuwa akifikiria mazungumzo ya usiku uliopita na bibi yake na alicheka kwa kuwa hakuamini hata kitu kimoja kilichosemwa.
Kijiji chao hakikuwa na watu wengi, hivyo kukiwa na tukio kwenye boma fulani, lazima kila mtu ajue. Aera alipopita senyenge zilizozunguka kijiji chao, alishangazwa kuona watu wengi wakiitazama boma yao. Nje ya boma yao kulikuwa na farasi watatu. Familia yao ilikuwa masikini. Mifugo pekee waliyokuwa nayo ilikuwa ni kuku. Hakujua farasi wale wametokea wapi hivyo aliongeza mwendo ili afike haraka.
Aera alipoingia ndani, alikutana na familia yake, lakini pia kulikuwa na sura tatu ngeni. Ingawa familia yake ilionekana kuwa na furaha, Aera aliwazingatia wageni wale wanaume ambao umri wao ulikuwa umekwenda. Mavazi yao yalikuwa maridadi. Pia walibeba zawadi zenye vifungashio vya gharama.
"Njoo uketi mama.", alisema Heya, baba yake,
Kwa utii, Aera alikwenda kuketi pembeni ya Gema.
"Endelea mkuu.", Heya alisema huku akimtazama kiongozi wa wageni.
Kiongozi huyu alikuwa kuhani aliyeongoza tambiko la familia ya mfalme siku chache zilizopita. Jina lake lilikuwa Badri.
"Kama nilivyosema awali, sisi ni makuhani kutoka ikulu. Kazi yetu ni kuiombea familia ya mfalme na himaya yetu kwa ujumla. Lakini pia, mfalme hupenda kutupa kipaombele likija swala la ndoa. Hivyo sisi huvua mavazi ya kikuhani na kuvaa mavazi ya washenga.", alieleza Badri,
"Bila shaka tunaheshimu sana uwepo wenu.", alisema Heya, "Lakini ningependa kujua nia na dhumuni la ugeni wenu kama hautojali.",
"Natumaini kuwa mnamfahamu mfalme na familia yake.",
Wote walitikisa vichwa kukubali.
"Basi mtoto wa mwisho wa mfalme, Avana, amefikia umri wa kuoa. Alipoulizwa anataka kumuoa nani, alitaja jina la binti yako.",
Macho yote yaligeuka kwa Aera wakidhani ndiye muhusika, lakini Badri aliingilia kati kabla mawazo yao hayajafika mbali.
"Nani ni Gema kati yao?", aliuliza,
Gema alinyanyua mkono kisha kuushusha. Badri alitabasamu, "Gema, binti wa Heya, umeweza kukamata moyo wa kijana wa mfalme. Tumetumwa na familia ya mfalme kuleta ombi la ndoa.",
Mazungumzo ya bibi yake yalimrudia Aera kwa mara nyingine. Huku familia yake ikifurahia bahati iliyowaangukia, Aera alitambua fika kuwa haikuwa bahati bali janga. Alielewa umaskini wa familia yao, ya kuwa wasingeweza kukataa ombi la mfalme. Ndoa ya Gema ilikuwa njia pekee ya kuwapandisha kwenye ngazi za uchumi. Lakini kitu alichoambiwa na bibi yake kilimpa mashaka.
"Mtoto wa mfalme alimuona wapi Gema kwa mara ya kwanza?", Aera aliuliza na kusababisha ukimya wa ghafla. Kila mtu alimtazama kwa mshangao.
"Familia ya mfalme inamfahamu kila mmoja wetu.", alisema Badri,
"Naelewa, lakini nataka kujua ni wapi mtoto wa mfalme alimuona mdogo wangu, akampenda na kufanya uamuzi wa kumtaka awe mke wake.",
"Aera!", aliita Foni kwa ukali wa chini chini, "Una matatizo gani?",
Badri alimsoma Aera huku akitabasamu. Alihisi mgomo ukiwanyemelea.
"Naelewa kwa nini una maswali mengi.", alisema Badri, "Hata mimi ningekuwa ni wewe ningeuliza. Nachotaka utambue ni kwamba tangia mwanzo mpaka sasa, familia ya mfalme haijawahi kukaribisha binti kutoka kwenye familia masikini. Avana ndiye wa kwanza, na amefanya kazi kubwa sana kushawishi familia yake kukubali ombi lake. Ningependa ufahamu ya kuwa hii ni bahati ambayo kila mtu anaihitaji.",
"Kweli kabisa!", Heya alisisitiza, "Tutakuwa wapuuzi tukikataa ombi lenu.",
Aera alikuwa njia panda; Je, aamini maneno ya bibi yake au aruhusu familia yake kupokea bahati ile? Moyo wake ulikuwa mgumu kama chuma. Kutokana na sababu asizozielewa, kila kitu kilichotamkwa na Badri kilimjia kama uongo mwingine.
"Tungependa kujua utaratibu, mkuu.", Heya aliendeleza mada,
"Mfalme ametuma zawadi hizi. Ni mavazi ambayo Gema atapaswa kuvaa siku atakayowasili ikulu. Pia familia yake nzima itaandaliwa boma ndani ya ikulu kwani sasa hamtakuwa watu wa kawaida bali mtakuwa na uhusiano na familia ya mfalme.", Badri alieleza,
"Ni siku gani hiyo, mkuu?",
"Tutarudi tena kuwasindikiza ikulu baada ya siku tano.",
"Tumeelewa mkuu.",
"Onyo.", Badri alitamka kwa mkazo, "Hamruhusiwi kusema kitu chochote kwa mtu yoyote kuhusu hili jambo. Mambo mengi yanaendelea katika himaya yetu na wenye wivu ni wengi. Ikigundulika kuwa Gema, binti wa Heya, ndiye atakuwa mke wa kijana wa mfalme, mtauliwa kabla siku tano hazijaisha na watu wasiojulikana na sisi wala mfalme hatutaweza kuwasaidia kwa lolote. Hivyo mnatakiwa kuwa makini.",
Kwa hofu, Heya, Foni na Gema walikubali. Zawadi zilipokelewa kisha familia nzima ilisindikiza makuhani wale hadi walipoondoka kijijini kwao. Aera alipata hisia mbaya sana rohoni.
…
Gema alipewa likizo kwa kutofanya kazi ya aina yoyote. Aliwekwa ndani kama mwali ili aanze kujitunza. Hawakutaka afanye kazi ya aina yoyote asije akapata kovu mwilini. Hivyo ilipofika jioni, Aera na mama yake ndiyo waliokuwa jikoni wakiandaa chakula. Foni aliweza kusoma akili ya binti yake na kujua ya kuwa hakufurahishwa na swala la ndoa ya mdogo wake. Hakutaka kulaza zege.
"Aera mwanangu.", Foni alianza,
Aera alimtazama mama yake kwa upole.
"Macho yangu yananiambia kuwa hujafurahishwa na pendekezo la ndoa ya Gema kwa mtoto wa mfalme.", alisema,
"Macho yako yanasema kweli.", Aera hakubisha,
"Naelewa kwa nini unajisikia hivyo.",
"Kwa nini?",
"Kutokana na tamaduni zetu, ulitakiwa uolewe wa kwanza kabla ya Gema.",
"Hapana mama.", Aera alimkanusha, "Siku zote nilijuwa ya kuwa Gema ataolewa kabla yangu.", alimweleza.
"Basi niambie kwa nini upo hivi. Umesikia maneno ya kuhani; wote tutapewa boma ikulu hivyo wewe na Gema bado mtaendelea kuonana kila siku. Sasa ni nini kinakupa majonzi mwanangu?",
Aera alisitisha kukoroga mboga, "Mama, hivi hamna wasiwasi? Himaya yetu ina vijiji kumi na mbili, kijiji chetu ni cha nane. Tangia Gema azaliwe, ameishia kijiji cha tatu. Hatujawahi kufika mji mkuu. Sasa huyo mtoto wa mfalme amemuona wapi?",
Foni alicheka kidogo, "Aera, unajua tangia uzaliwe mpaka sasa umeonwa na wanaume wangapi? Nikikwambia uwataje kwa majina utaweza? Macho ya binadamu yapo mbele, hayapo kisogoni wala mashariki. Hatujui majira, sehemu wala siku mtoto wa mfalme alipomuona Gema, lakini cha muhimu ni kwamba amemuona, amempenda na anataka kumuoa.",
Aera aliona kuwa anapiga debe tupu. Mtu pekee ambaye alimuelewa na angeweza kumsaidia alikuwa ni bibi yake.
"Mama, kesho asubuhi taenda milimani kumuona bibi.", alimjulisha.
"Si umetoka kumuona jana?",
"Nataka kumuona tena.",
Aera aliokota mwiko na kuendelea kukoroga mboga, akitamani asubuhi ifike papohapo.
…
"Bibi!", Aera aliita akiwa nje ya boma ya bibi yake.
Ilikuwa asubuhi, baridi jepesi likipapasa ngozi yake. Lakini kutokana na hali aliyokuwa nayo, damu ilichemka na kumtengenezea joto mwilini. Bibi alifungua mlango taratibu kisha kuchungulia nje. Alimtazama mjukuu wake juu hadi chini. Bila shaka alitambua dhumuni la Aera kufika kwake mapema yote ile.
"Yametimia?", bibi aliuliza,
"Naomba msaada wako bibi.", Aera aliongea, huzuni ikisikika kwenye sauti yake.
"Pita ndani.",
Aera alimfata bibi yake mpaka ndani. Yale mavazi ya kikuhani ambayo bibi aliyavaa zamani yalikuwa yametandazwa juu ya kitanda. Kulikuwa na mkufu na njuga, hereni na bangili za rangi ya dhahabu. Aera hakuzingatia hivyo;
"Bibi, ulijuaje kuhusu pendekezo la harusi ya Gema na mtoto wa mfalme?", Aera aliuliza kabla hajaketi,
"Nilikupa jibu lakini haukutaka kuniamini. Mimi ni chombo ambacho miungu hutumia kufikishia ujumbe kwa viumbe vyao.", bibi alimweleza, "Huwa siambiwi kila kitu, lakina vile ambavyo miungu hunifunulia mimi hupaswa kutafuta ufumbuzi kwa msaada wao.",
"Familia yangu haijui kinachoendelea. Wao wanaiona hii kama baraka na mimi nimeshindwa kuwaeleza. Lakini bibi nahitaji msaada wako. Nataka kuikomboa familia yangu.",
"Jana usiku nilikuwa kwenye maombi. Miungu yetu imenionesha suluhisho.",
"Lipi hilo?", Aera aliuliza kwa haraka, macho yakimtoka,
Bibi alinyoosha kidole kwenye mavazi ya kikuhani. Aera hakuelewa maana yake.
"Unamaanisha nini?", aliuliza,
"Familia ya mfalme ni familia yenye nguvu sana, sio kiuchumi tu, bali hata kiroho. Kuna sababu kwanini makuhani wenzangu waliuawa baada ya siri yao kujulikana. Wewe kufahamu mipango yao tayari ni hatari. Huwezi kupambana nao hivihivi.", bibi alimwambia, "Suluhisho ni wewe kuitikia wito wa miungu na kuwa kuhani.",
Aera alipigwa na butwaa, "Bibi unasemaje?", aliuliza kwa kituo,
"Nisikilize mjukuu wangu. Wewe ni dhaifu, unanielewa? Huwezi kuokoa maisha ya familia yako bila msaada kutoka juu. Hivi hujajiuliza kwa nini Gema ndiye aliyechagulia na sio wewe?",
"Ninajua kwa nini Gema amechagulia na si mimi?",
"Sababu ni ipi?",
"Gema ni mdogo, pia ana mvuto zaidi yangu _",
Bibi alianza kucheka na kumkatisha Aera. Aera hakuielewa familia yake. Kila kitu kilichokuwa kikifanyika sasa kilimuweka roho juu. Maneno aliyokuwa akiyatamka bibi yake yalimfanya akumbuke maneno ya watu; au bibi yake kweli ni mchawi?
"Aera, familia huwa zina siri kubwa sana. Kitu pekee nachoweza kukwambia ni kwamba wewe ni mtu tofauti na familia yako. Sasa hivi wewe ndiye mwenye nguvu ya kuikomboa familia yako ama kuiacha iangamie. Fanya uamuzi.", alisema bibi,
"Hakuna njia nyingine ya kuwasaidia mpaka niwe kuhani?",
"Ndiyo. Itikia wito Aera. Hii ndiyo njia pekee. Siku zangu za kuishi zinakaribia kufika mwisho. Nahitaji mtu wa kunirithi na wewe ndiye mtu sahihi.",
"Siwezi!", Aera alitamka kwa msisitizo,
"Aera, sikiliza _",
"Bibi, kama miungu yako inaweza kutusaidia basi itusaidie bila masharti. Kama hawawezi basi taikomboa familia yangu kwa uwezo wangu mwenyewe.",
Aera alianza kuondoka ila bibi alimkamata mkono, "Aera, amini maneno yangu. Vita hii hautashinda. Huo uwezo hauna.",
"Ninaweza na nitafanikiwa.",
Aera alifungua mlango na kuondoka. Bibi alirudisha macho yake kwenye mavazi yaliyopo kitandani. Alivuta pumzi nzito na kuketi. Ilikuwa ngumu kumshawishi mjukuu wake. Hata yeye alitamani kama kungekuwa na njia nyingine lakini dawa ya moto ni moto.
Uwezo wa kumrithisha majukumu Aera kwa lazima alikuwa nao, lakini sharti la miungu lilikuwa ni utayari wa Aera, kitu ambacho sasa kilikuwa kimeshindikana.
***