Wakiwa juu ya farasi, Aera aligeuka nyuma na kuitazama boma yao tena kwa mara ya mwisho. Siku ya kuhamia ikulu ilikuwa imefika na tayari safari ilianza. Wanakijiji wenzao walisimama vikundi wakiwapungia mikono ya kwaheri, lakini kati yao, Pim hakuwepo. Aera aliumia sana moyoni. Mipango yake yote ilikuwa imefeli lakini pia alikuwa amempoteza rafiki ampendaye. Familia yake ilijawa furaha kasoro yeye. Mambo mengi yalikuwa yakiingia na kutoka kwenye akili yake.
Kwa mbali alitazama milima aishipo bibi yake, "Sitakata tamaa.", Aera alijisemea kimoyomoyo, "Tafanya kila niwezalo ili niokoe maisha ya familia yangu.", aliapa.
…
Familia nzima ya mfalme, ndugu na jamaa, walikuwa kwenye ukumbi wa sherehe. Meza zilijazwa vyakula na vinywaji vya kila aina. Kwaya ya mfalme iliburudisha kwa nyimbo nzuri. Ilikuwa tayari ni jioni, jua likizama taratibu. Hatimaye Badri aliwasili ukumbini na moja kwa moja alielekea kwenye kiti cha mfalme. Aliinamisha kichwa kwa heshima;
"Mfalme, mtumishi wako nimewasili. Kama nilivyokuahidi, wageni wetu wapo salama.", alisema Badri,
Mfalme alitoa kicheko cha kuridhika. Hii ilifanya kila mtu ajue kuwa jambo lao lilikuwa linaenda kukamilika.
"Wakaribishe wageni ndani.", mfalme alitoa amri.
Walinzi walifungua malango. Kila mtu aligeukia mlangoni na kusubiri kuwaona wageni hao kwa hamu. Familia ya Aera iliingia ndani. Walikuwa wamevaa mavazi mazuri na ya kuvutia. Gema alikuwa amefunikwa uso kwa mtandio mrefu hivyo hakuna aliyeweza kumuona sura. Walitembea polepole, wakiona macho ya kila aliyewatazama; Yalikuwa macho ya furaha. Lakini Aera hakushawishika.
Walifika mbele ya kiti cha mfalme na kuinamisha vichwa vyao. Mfalme alivaa tabasamu nene, hasa alipokuwa akimtazama Gema. Hakuhitaji kuiona sura yake kujua kuwa ni mrembo. Kila kitu kuhusu yeye kilimvutia sana.
"Mfalme mtukufu, naileta kwako familia ya Heya.", Badri aliwatambulisha, "Huyu ni Heya, baba.",
Heya alinyanyua uso wake na kumtazama mfalme.
"Karibu ikulu, Heya.", alisema mfalme.
"Asante, mfalme mtukufu.".
"Huyu ni Foni, mke wa Heya.", Badri aliendelea,
Foni pia alinyanyua uso na kumpatia mfalme heshima yake.
"Afuataye ni binti wa kwanza wa Heya, Aera.",
Aera alinyanyua uso kama alivyotakiwa lakini ghafla mfalme alipoiona sura ya Aera kwa karibu alishtuka. Kitendo kile kilishuhudiwa na wengi waliokuwa karibu yao. Mfalme alifanana na mtu aonaye mzimu. Aera alichanganywa kwa namna alivyoangaliwa na mfalme. Hakupenda.
Ili kumuokoa mfalme asiaibike, Badri aliingilia kati, "Na sasa, mfalme wangu, namtambulisha kwenu binti aliyekamata hisia za kijana wetu.",
Gema alinyanyua mtandio na kumuangalia mfalme. Uzuri wake uliwaacha wengi mdomo wazi. Gema aling'aa kama mwezi. Macho yake ya goroli na midomo yake myekundu ilitengeneza wivu ndani ya wadada. Kama neno 'mrembo' lingekuwa na ufafanuzi, basi Gema ndiye angekuwa kielelezo sahihi.
Avana alisisimkwa kwa uzuri wa Gema. Ilikuwa ndiyo mara yake ya kwanza kumuona na alimtamani papo hapo. Mfalme pia alipenda muonekano wa Gema, lakini kila baada ya dakika chache alirudisha macho yake kwa Aera. Kitendo kile kilishuhudiwa na ledi Kompa na ledi Erini. Malkia alikipuuzia.
…
Asubuhi.
"Konsoti Gema, amka.", alisema Mone, binti mdogo na mtaratibu ambaye sasa alifanywa kuwa miongoni mwa wasaidizi wa Gema.
Konsoti ilikuwa ni cheo walichopewa wake na wachumba wa watoto wa mfalme.
Gema alifumbua macho taratibu. Harufu ya marashi ilijaa hewani. Mishumaa ya rangi mbalimbali iliwashwa kwenye kila pembe ya chumba chake. Kitanda alicholalia, mito na mashuka vyote vilikuwa vya gharama. Hakuwahi kumiliki hata kimoja.
Gema alinyanyuka na kukaa kitako. Aliona ya kuwa kulikuwa na wasaidizi wengine wanne waliokuwa wamesimama mlangoni. Mmoja alibeba beseni, mwingine alibeba taulo, mmoja alibeba mafuta ya mwilini na wa mwisho alibeba mahitaji yote ya nywele. Gema alikiangalia chumba chake kwa mara nyingine tena. Kilikuwa kikubwa zaidi ya boma lao waliloliacha. Hakujua ni kitu gani amefanya kupata hii bahati.
"Konsoti Gema, tunatakiwa kukuandaa ili uanze shughuli ya kusalimia familia yako mpya rasmi.", alisema Mone,
"Mbona nimeshawasalimia wote jana?", Gema aliuliza,
"Jana ilikuwa ni salamu ya ujumla. Leo utakwenda kumsalimia mmoja baada ya mwingine. Utaanza kwenda kumsalimia malkia Omuro, kisha ledi Kompa, mama yako mkwe. Baada ya hapo utakwenda kumsalimia ledi Erini, mke wa pili wa mfalme, na mwisho utakwenda kumsalimu Sinta, binti wa mfalme.",
"Familia yangu je _",
"Leo hautaweza kukutana na familia yako, ila usijali. Wao pia wako salama kwenye makazi yao mapya.",
"Mume wangu mtarajiwa tamuona lini?", Gema aliendelea kuuliza,
"Hakuna ratiba maalumu. Atakuja kukuona muda wowote atakaojisikia.",
Hakikuwa ni kitu kizuri Gema kusikia. Japo kuwa hakufahamu swala la mapenzi, kitu alichojua ni kwamba mtu akimpenda mtu mwingine huwa na hamasa ya kumuona kila wakati. Hakuelewa kwanini Avana hakuja kumtembelea.
…
Wahudumu walimimina chai kwenye kikombe cha malkia Omuro, kisha kwenye kikombe cha Gema. Walipomaliza waliondoka kwenye chumba cha malkia na kuwaacha peke yao.
Kutokana na aibu, Gema alishindwa kumuangalia malkia machoni. Hii ilimfanya aonekane mpole kwa malkia. Bila kusubiri, malkia Omuro aliokota kikombe chake cha chai;
"Chai yako itapoa.", alimwambia.
"Familia yetu ina utaratibu wa kuwa watoto wanakula baada ya wazazi wao, hivyo nitakunywa chai yangu baada yako, malkia.", alisema Gema,
Malkia alitabasamu na kunywa chai yake. Alitokea kumpenda Gema, na kwa ndani alimuhurumia kwani hatima yake haikuwa nzuri kama alivyodhania.
"Niambie.", malkia alirudisha kikombe chake mezani, "Unajisikiaje?",
"Najisikia vizuri, malkia wangu. Najiona ni binti mwenye bahati sana kupendwa na mtoto wa mfalme. Daima nitakuwa kwenye deni lenu.", Gema alijibu.
"Mabinti wengi walikuwepo kwenye nafasi yako lakini hawakufika mbali. Takupa siri moja ya kuishi vizuri ndani ya ikulu; Kuwa makini na maneno yatokayo mdomoni mwako. Tafuta mtu mmoja tu na huyo ndiye umfanye awe rafiki na msiri wako. Ukweli ni kwamba itakuwa ngumu kwani mambo mengi yanaendelea humu ndani. Jitahidi. Macho, masikio na akili yako vifanye kazi zaidi ya mdomo wako.",
"Maneno yako nimeyasikia na kuyaelewa, malkia wangu. Nakushukuru sana kwa ushauri wako.",
Malkia alitikisa kichwa na kunywa chai tena.
"Niambie. Dada yako anaitwa nani?", malkia aliuliza baada ya kuweka kikombe chini tena,
"Anaitwa Aera, malkia.", Gema alijibu,
"Unaweza kuniambia kidogo kuhusu yeye?",
"Ndiyo, malkia. Dada yangu ni mtu mwenye upendo kwa kila mtu. Pia ni mchapakazi na mwenye busara. Amenifundisha mambo mengi sana tangia nikiwa mdogo. Ninaweza kusema kuwa yeye ni mama yangu wa pili.", Gema alielezea.
"Vizuri sana. Inaonekana mnapendana sana na dada yako.",
"Sana. Ni mtu pekee ninayemuamini.",
"Unafahamu kama yupo kwenye mahusiano?",
Malkia aliona jinsi mfalme alivyokuwa akimuangalia Aera kila wakati usiku uliopita. Kama mke ambaye alikwishaongezewa washindani wawili, alitamani sana kuweza kuisoma akili ya mume wake. Kwa sasa alikuwa akihisi kuwa mfalme alimtamani Aera hivyo alitaka afahamu nafasi ya Aera kwenye maisha yake; Je, amchukulie kama binti tu wa kawaida, au mke mwenza mtarajiwa wa tatu?
"Hapana, malkia. Dada yangu hayupo kwenye mahusiano yoyote.", Gema alijibu.
Malkia alitikisa kichwa na kuendelea kunywa chai yake.
***