"Zenaaaaa" Lyn akamuita akiwa amesimama kwenye mlango uliofunguliwa nusu...
Sauti ya miguu iliyokuwa imepanda ngazi taratibu ilisikika.
"Zena fanya upesi kama unajielewa!" Lyn alionesha kabisa kukerwa na hatua zile zilizoonesha Zena hakuwa na haraka alipoitwa...
Lyn akaanza kuchukua hatua kwa hasira lakini kabla ya kukunja kona iliyoelekea mwanzoni kwa ngazi, akashtuka kumuona aliyesimama mbele yake
"Zena anaandaa chai jikoni, unataka nini nikusaidie?" Coletha akiwa ameshika kiuno kwa mikono yake miwili alimuuliza Lyn. Sura yake haikuonesha hisia zozote kuweza kujua amekasirika au ana furaha
Lyn ambaye hakutegemea kukutana na Coletha akamwangalia kisha akamsalimia
"Hujambo wifi" namna alivyoitamka hiyo wifi ni kuonesha msisitizo wa kile anachokisema bila kuficha tabasamu feki usoni...
"Sijambo wifi" kama ambavyo Lyn aliweka msisitizo Coletha naye akaitamka huku akizungusha macho yake....
"Mwambie Zena nahitaji maziwa" Lyn akasema na kugeuka kuanza kuondoka
Kabla Coletha hajajibu akaongeza "Ya moto wifi"
Coletha akatabasamu, "Yasubiri wifi yatakuja huko chumbani"
Kulikuwa na dhihaka katika matamshi ya Coletha ambaye tabasamu lake halikutoka usoni akageuka na kurudi jikoni alipokuwa akimalizia kuandaa maandazi aliyokusudia kuyapeleka chuoni.
"Zena weka chupa ya maziwa mezani na kikombe, akisikia njaa atashuka mwenyewe" Coletha akamwambia Zena ambaye alionekana kuwa na wasi wasi
"Lakini da Coletha mimi sipendi makelele acha tu ni__"
"Fanya kama nilivyokuagiza. Mimi namsaidia yeye ajue jinsi ya kuishi kwa kanuni za nyumba ya 'mumewe'!" Dhihaka ilikuwa wazi kwenye sentensi ya Coletha na kumfanya Zena kucheka...
"Haya"
***********************
Edrian alikuwa na ratiba ngumu kwa siku ya leo na bado mambo ya maisha yake binafsi yalikuwa na msuguano aliokusudia kuumaliza..
"Asante Li" Edrian alimshukuru nduguye kwenye simu
"It's okay bro, ndugu ndivyo tunavyosaidiana...."
Wakaongea mambo mengine yaliyohusu biashara za fedha na madini. Kwa kuwa mkutano wa bodi ya SGC ulikuwa hivi karibuni wakakubaliana kuhakikisha ripoti zinaandaliwa vyema. Bado walikubaliana kuwa na mkutano tofauti kabla ya ule Mkutano mkuu as bodi. Katika mkutano huo wangekutana yeye, Li, Allan, Beno na Ganeteu ambaye anasimamia masuala ya sheria ya SGC.
Beno ni moja wa wafanyakazi ambao walifanya kazi tangu SGC ilipoanza ikiwa chini ya baba yake Edrian. Alijenga uaminifu mkubwa sana kiasi kwamba, familia ya Simunge haikuwa na wasi wasi na utendaji wake. Njama nyingi zilizofanyika kufanya familia ipoteze hisa za umiliki ziligonga mwamba mara kadhaa kwa kuwa Beno na Ganeteu waliweza kuzing'amua mapema.
Edrian alipomaliza kuongea na Li aliendelea na kazi hata muda wa chai hakuweza kutoka ikapelekea Loy kumletea chai ofisini..
"Asante Loy, unapenda kujitaabisha." Alisema Edrian ambaye bado macho yake yakielekezwa kwenye kioo cha kompyuta...
Loy alibaki amesimama hadi Edrian alipoinua uso wake tena na kumuangalia kwa jicho lililobeba swali,
"Bosi maziwa yatapoa, tafadhali kunywa kwanza" Loy akamsihi Ed..
Akatabasamu na kuinuka, akajinyoosha kisha akakaa tena na kuvuta ile sinia iliyobeba kifungua kinywa.. Akanywa huku akiendelea kuzungusha kipanya cha kompyuta yake kusoma taarifa walizokusanya... Loy alipoona bosi wake kumsikiliza akaondoka na kurudi kwenye meza yake kuendelea na kazi.
Wakati Ed akimalizia kipande cha mkate uliotiwa mayai katikati meseji iliingia kwenye simu yake... Tik Tik. .. akafungua huku akiendelea kutafuna taratibu...ghafla akapaliwa na kuanza kukohoa.. akaweka simu na mkate uliobaki kwenye sahani. Akachukua chupa ya maji na kunywa..
Alipokuwa sawa akacheka taratibu huku akifuta mikono yake kwa Tissue zilizowekwa kwenye sinia...
Inawezekanaje... akachukua simu na kuanza kujibu ule ujumbe aliotumiwa. .
"Rian samahani nimetoka darasani sasa, lakini kuna kitu naomba nikuulize?"
Aretha kamtumia meseji, anataka kumuuliza nini, Ed akatabasamu na kuondoka
"Hongera kwa darasa Retha, niulize bila shaka"
Akainuka na kutoa ile sinia iliyobeba kifungua kinywa na kuiweka kwenye meza iliyokuwa pembeni. Akarudi kukaa.