Derrick aliendesha pikipiki mawazo yake yakifikiri namna ambavyo Aretha ameleta changamko la ghafla katika ugumu uliokuwa ukiendelea kati yake na kaka yake.
Baada ya dakika kumi za kupambana na foleni ya hapa na pale, waliingia mtaa wa Moon. Derrick akapunguza mwendo na kufungua sehemu ya juu ya kofia yake kumuuliza Aretha mwelekeo wa mwisho wa safari.
Baada ya kumpa maelekezo Derrick alifuata njia aliyoelekezwa na kufanikiwa kufika katika geti la rangi ya kijivu. Akaegesha pembeni na kumruhusu Aretha kushuka huku akivua kofia yake.
"Kumbe unaishi hapa, basi mara nyingi huwa nakuja barabara ya pili nyuma yako" alimshangaza Aretha
"Oooh karibu wakati mwingine ukija na asante kunileta" huku akimkabidhi mfuko aliyapokea maneno yale kwa furaha. Derrick alijua sasa ana namna njema ya kuwa karibu na Aretha.
Na kwa namna ya tofauti aliona ishara nzuri ya mafanikio mbele yake maana rafiki yake wa kike, Emmy anaishi upande kwa pili tu kutokea alipo. Na mara kadhaa amekuwa akifika mahali hapa.
Wakati anajiandaa kuwasha pikipiki yake mlango mdogo katika geti ulifunguliwa, akatoka mama mmoja wa makamo ambaye alipomuona Derrick alishtuka. Akamtupia jicho mwanae lililoonesha swali, lakini kabla ya Aretha kujitetea tayari alikurupushwa na sauti ya mwanamke huyu
"Aretha mbona humkaribishi mgeni anaishia nje tu?" aliuliza huku tabasamu jepesi likionekana usoni mwake.
Aretha alishtushwa na sentensi hii akapiga hatua kumsogelea yule mama
"Mama ni mtu tu kanisaidia wakati narudi" alisema Aretha kwa aibu huku akishika bega la mama yake
Derrick hakuacha nafasi hii ipotee, akashuka na kumsalimia mama yule
"Oooh samahani sana mama, niliona nisiwasumbue huko ndani, nilimsindikiza dada Aretha baada ya ajali ndogo niliyoisababisha"
Mama huyu akashtuka, lakini Aretha akawahi kuongezea alipoishia Derrick hakutaka mama yake ajue alipokuwa
"Aaah usihofu mama ni kugongana wakati tukitembea" alijibu Aretha huku akimwangalia mama yake aliyeanza kuwa na wasi wasi.
"Oooooh basi sawa, karibu mwanangu" maneno haya yalipotoka kinywani mwa mama huyu, Derrick tayari alishajipanga kufahamika zaidi
"Naitwa Derrick mama yangu, nimepata urafiki na binti yako muda mfupi uliopita, nimefurahi kumleta nyumbani" aliongea Derrick akiachia tabasamu lake ushindi ambalo lisipokunasa basi utakuwa umeokoka mdomoni mwa simba
"Hahhahah asante mwanangu Derrick, hakika unakaribishwa hapa kama upendavyo" alicheka mama huyu akimkaribisha kwa ukarimu. Kwa upande wa Aretha aliinama chini huku akichezea majani kwa viatu huku akionekana kuwaza mengine akiwaachia hawa wawili uwanja wa maongezi.
"Asante mama, ngoja niwahi. Nitakuja wakati mwingine" alishukuru Derrick
"Sawa mwanangu, nimefurahi kuona Aretha amepata walau rafiki wa kumtembelea" maneno haya yalimpa Derrick mwanya mdogo wa kumfahamu Aretha kuwa si mtu wa kupenda kampani ya watu.
"Sawa mama. Jioni njema" aliaga Derrick na kupanda tena kwenye pikipiki yake. Akiwapungia mkono na kisha anaondoka.
Huku nyuma Aretha na huyu mama walirudi ndani,
"Retha uwe unakaribisha marafiki kama huyu. Anaonekana ni kijana mwema. Ni mzuri usoni anafaa kweli" alidokeza mama huyu ambaye ni mama mzazi wa Aretha.
"Mama jamani" alisema Aretha na kukimbilia chumbani kwake ambapo alijitupa kitandani na kujaribu kufumba macho kuondoka hali ya aibu aliyohisi baada ya kung' amua maneno ya mama yake alipomsifia Derrick.
"Aaaaargh!! Mama jamani mbona ananikorofisha aliwaza Aretha. Akakumbuka ule mfuko aliotoka nao ofisini kwa Ed. Akainuka na kuchukua biskuti akitafuna huku akitafakari maongezi yake na Ed.
Akaweka biskuti juu ya kitanda huku akitoa kipande na kutafuna kisha akasogea kwenye meza yake ya kuchorea ambayo ilikuwa pembeni katika kona ya chumba chake. Akavuta karatasi moja akaiangalia sana kisha akachukua brashi yake iliyokuwa mahususi kumalizia hatua ya mwisho ya uchoraji.
Akaanza taratibu kucheka, lakini sauti ya mama yake ilimkatiza ambayo ilimuita kutokea jikoni, akashusha pumzi na kurudisha brashi mahali pake. Akachukua taulo na kufuta mikono kabla ya kuelekea jikoni.
********************************