Akiwa chumbani Ed alichukua simu na kumpigia Linus akimuuliza kama yuko nyumbani tayari, lakini Li alikuwa njiani akirejea. Ed ilibidi amsubiri ndugu yake huyu, alihitaji kuzungumza nae juu ya mambo mawili, kwanza juu ya taarifa aliyoipokea kwenye simu yake wakati akirudi, na pili alitaka kujua kuhusu Aretha.
Akiwa mawazoni simu yake iliita, ilikuwa ni simu kutoka kwa Joselyn, Ed aliiangalia kwa sekunde kisha akapokea,
"Edrian umepatwa na nini siku hizi, hadi nikupigie?" Lyn alisikika akilalamika mara baada ya Ed kupokea simu
"Hello Lyn" Ed alimsalimu na hakuonekana kuwa na muda wa kujibu malalamiko yaliyoelekezwa kwake
"I swear babe, nikijua unanifanyia kusudi nitakuja kukaa hapo" kama kawaida yake Lyn alimpa vitisho maana alijua Ed hakubaliani na hilo
"Lyn hivi huwezi kuongea bila kulalamika?" Aliuliza Ed akionesha kukereka
"Nalalamika sababu hunichukulii serious, toka mchana hujanitafuta wala kunijulisha wikiendi itakuwaje?" Lyn alizungumza kwa upole baada ya kuona Ed amembadilikia.
"Mmmmm" akaguna Ed
"Umeanza na kutonijali, hujanipa ratiba ya kwa mama, umenyamaza tu" aliendelea Lyn
Ed akashusha pumzi kisha akamwambia,
"Lyn tutaonana Jumatatu nitakupitia kuelekea kwa mama, hii wikiendi nitakuwa na ratiba ya kazi na vitu binafsi." Ed kwa sauti iliyoonesha kuchoka alimjibu Lyn na kuegama kwenye ubao wa kitanda
"Ooooh, jumamosi yote na jumapili utakuwa na nani Ed?" Lyn aliuliza kuonesha kukerwa na kile alichoambiwa.
"Mmmmmm" aliguna Ed kisha akaendelea
"Lyn nina kazi na watu kwenye maisha yangu, unataka nikuombe ruhusa kila nikiwa na ratiba nao?" Mtetemo kwenye sauti ya Ed sasa ulitisha na kumfanya Lyn upande wa pili wa simu kugundua na kuamua kusawazisha mambo.
"Am sorry Ed, mpenzi ninakupenda hadi naona wivu usiponitafuta" Lyn alibadilisha sauti kumrudisha Ed
"Mmmmm" aliguna Ed
Lakini kabla ya kumjibu sauti ya mtu akigonga mlango wa Ed ilisikika...
"Nitakupigia asubuhi, goodnight" alipomaliza kusema hivi, hakusubiri Lyn aitikie alikata simu. Aliinuka na kuelekea mlangoni ambapo alikutana na Li baada ya kufungua.
"Za jioni Bro..." Li alisalimia
"Salama, habari ya kazi?" Aliendelea Ed huku akirudi nyuma kidogo kumruhusu Li kuingia.
"Safi, leo mapema sana umeniwahi!" Li alimdodosa Ed maana siku chache nyuma alichelewa kurudi na wakati mwingine alilala huko huko.
"Nimewahi walau nilale mapema leo, japokuwa mpango wangu umeshaharibiwa" alijibu na kuketi kitandani wakati Li akikaa kwenye kochi la watu wawili lililokuwa pembeni kidogo kwenye chumba hiki.
"Nambie Bro!"
"4D wamepata taarifa kutoka Boric inayoonesha kuna mtu wa Martinez ambaye yuko ndani na kazi yake ni kupinga kila proposal zinazotoka kwetu" Ed alikunja uso kuonesha taarifa hizi zilimkera
"Ooohh, si ajabu sana Bro sababu kuna namna tulishamhisi... tunafanyaje hapo? Aliuliza Li huku akishika simu yake
"Nasubiri taarifa ndani ya hizi siku mbili halafu nitajua cha kufanya. Kesho atakutana na Waziri, Captain yuko nae tayari.. "
"Well, hatua nzuri. Kuna kitu nahisi anakitaka ni aidha tusiwepo kwenye hii business abaki yeye maana sisi ndio kampuni pekee inayokwenda sambamba nae" Li alimtafakarisha Ed ambaye alitulia na macho yake yaliangukia kwenye picha ya marehemu baba yake iliyoning'inia karibu na kabati la nguo..
"I miss you babaa" alisema moyoni mwake nyakati kama hizi baba yake angekuwa msaada wa karibu.
"Tutamsogelea pasipo kujua, hidden agenda yake tutaifunua taratibu" alijibu kwa uthabiti kitu ambacho kilimfanya Li ajue kazi imeanza.
"Utafanyaje sasa kuhusu Joselyn?" Aliuliza Li
Sura ya Ed ilibadilika na meno yake yalibana sehemu ya chini ya mdomo wake kisha akajibu
"Nitamuuliza"
"Sio kwa kufanya hivyo utamfanya Martinez awe makini zaidi?" Aliuliza kwa mshangao
"Exactly nachotaka, nataka kujua kama anashirikiana na baba yake". Tabasamu jepesi lilionekana upande mmoja wa mdomo wa Ed
"Ha ha ha nimekuelewa Bro" Li alijibu
Kimya kifupi kilipita kisha Ed akaendelea
"Nashukuru kwa kuja na ile taarifa kuhusu Aretha, lakini usingesumbuka na mambo yasiyokuhusu Li" taratibu Ed alisema huku akimwangalia mdogo wake