Chereads / Tafadhali, Nipende(Please, Love me) / Chapter 21 - UNAJIUMIZA

Chapter 21 - UNAJIUMIZA

"Hello Lyn" Ed aliipokea simu yake akiwa amejilaza kwenye kochi baada ya kushindwa kuendelea kumpotezea Joselyn.

"Ed, mbona hupokei simu una nini?" Swali ambalo alilitegemea Ed.

"Nina kazi nyingi Lyn, am sorry" maneno haya aliyasema kwa shida huku akifumba macho yake kuonesha alisikitika kusema ambacho sio ukweli wa hali ilivyo.

"Edrian, ukinidanganya nitakuja ofisini hapo na kuuliza kila mtu" kawaida yake Lyn alijua kumfinya Ed panapouma.

Edrian siku zote hapendi mambo yake binafsi yaingilie masuala ya kazi. Kule kusema hivi kwa Joselyn ni wazi alijua atahakikisha ampotezei tena, ikiwa angefika ofisini ingemlazimu Ed kumwambia ukweli. Joselyn alijua wapi pa kumkamata.

"Okay Lyn, nina kazi nyingi tu" alijibu kwa unyonge Ed.

"Nimesikia Coletha anaandaa birthday ya mama, mbona hujaniandaa na ni jumatatu?" Ed alishtushwa na swali hili maana alishapitiwa na akashangaa ni kwa namna gani Lyn alikuwa na taarifa kabla yake.

"Sifahamu kitu, nitauliza" kwa taratibu Ed alijibu swali la Lyn. Akatamani kumuona mama yake lakini alijua kufanya hivyo kutamlazimu kuyaweka wazi yaliyoendelea kwenye moyo wake. Mama yake alimjua vyema Ed na hakika kama tu kule kuongea naye kwenye simu tayari alishamshtukia.

"Ed, nataka kwenda, fanya arrangements nisikose" sauti ya Joselyn ilitia mkazo

"Mmmm" aliguna Ed na kunyamaza kitu pekee hufanya ambapo hapendi kushurutishwa kufanya kitu.

"Babe please, mama anatakiwa aone nashiriki mambo ya familia" alilainisha sauti Joselyn ili kumshawishi Ed akubali

"Sawa, nitafuatilia" hakuwa na namna zaidi ya kukubali.

"Asante Ed. Babe bado uko ofisini hadi saa hii?" Aliuliza Joselyn

"Natoka mida hii" Ed alijibu akijua mwelekeo wa maongezi haya

"Oooh nilitaka nije kukuona toka jumatatu uko busy tu" alianza kulalamika Lyn

Akashusha pumzi ndefu na kukuna ndevu zake zilizokatwa kwa ufupi na kufanya kidevu kutengeneza muonekano wa 'O'.

"Jumapili nitakuona Lyn, nipe muda nimalizie hizi kazi"

"Basi sawa. Nenda nyumbani sasa" alimaliza Joselyn

"Mmmmm" Ed alikata simu na kushusha pumzi kisha akapandisha miguu yake mirefu kwenye kochi na kulala chali akiangalia dari, kisha akifumba macho.

Moyo wake ukaongea

"Aretha"

********************

"Hey za asubuhi" Ed aliweza kusalimia baada ya kukumbana na Li saa 11 alfajiri aliporejea nyumbani ili kubadili nguo na kurudi ofisini.

Li ambaye alikuwa katika mshangao wa kumuona kaka yake aliyeingia nyumbani alfajiri hii alijitahidi kuitika

"Salama bro"

Wakati huo Ed alipiga hatua kupanda kwenye ngazi zilizoelekea chumbani kwake. Li hakuweza tena kuvumilia kumuona kaka yake akiwa hivyo

"Bro" aliita Li

Ed ambaye alishapanda ngazi nne, alijikaza na kugeuka maana alijua kitakachofuata.. Alimuangalia Li kumpa ishara ya kuendelea na alichotaka kusema

"Unahitaji kuongea nae, unajiumiza" Li aliamua kuongea bila kujali matokeo yatakayofuata huku akijua Ed hapendi kabisa kufuatiliwa.

Ed alimuangalia Li kama mtu aliyekurupushwa usingizini asijue cha kujibu. Hakika alijua bila shaka alichomaanisha Li, lakini akaamua kutoangukia mtegoni,

"Nani Li?" aliuliza huku akimkazia macho Li

Sasa Li aliamua kumlipua kaka yake kutoka mafichoni alikojificha. Hakutaka kumpa nafasi ya kuendelea kuogelea katika mashaka ya hisia zake.

"Aretha Thomas, miaka 28, mwanafunzi CU, kozi Art of Drawing, anaishi na wazazi wake Moon street nyumba namba 13, namba ya simu 0545 522 512." Alimaliza Li huku akimwangalia Ed machoni kumuonesha uhakika wa yale aliyoyasema pasipo shaka.

Midomo ya Ed ilibaki na 'O' ya mshangao, hakuamini maneno yaliyotoka kinywani kwa mdogo wake. Alimwangalia tena akitamani kumshukuru lakini wakati huo akipata taabu kujua mdogo wake ameamua kumfuatilia.

Akageuka na kuanza kupanda ngazi pasipo kuongea chochote alijua hakuna namna ya kujificha kwa Li ikiwa ameweza kukusanya taarifa hizo kwa muda huo mfupi. Alijiuliza ni kwa kiasi gani hisia zake zimekuwa wazi hata kusomeka kwa wengine. Alipofika chumbani badala ya kuelekea bafuni alijitupia kitandani akiwa na viatu.

Kwa dakika kadhaa alichakata kile alichoambiwa na Li, tabasamu laini lilionekana usoni kwake. Taarifa ilikuwa njema hata kama hakutaka kuipokea kutoka kwa Li.

"Aretha Thomas'' alisema taratibu na kufumba macho, alihisi uzito mdogo kupungua katika mawazo yake. Akainuka kuelekea bafuni.