Jioni ya Ijumaa hii, Ed aliwapa Allan na Loy nafasi wa kuondoka mapema, wakati huo alikuwa na mazungumzo binafsi na Brian, rafiki yake ambaye tayari alikutana naye Sunset Lounge.
Muda wote wa kazi alikuwa busy akipitia ripoti mbali mbali zilizopita mikononi mwa Allan na kuishia kwake. Lakini hakuacha kutafakari kile alichoambiwa na Li kila mara akiachia tabasamu, akishangazwa na umahiri wa mdogo wake kuweza kufanya utafiti mfupi kwa Aretha. Sio kwamba ni mara ya kwanza kwa Li kutafiti na kutoka na taarifa zinazohusu mtu, bali kule kujua hitaji la kaka yake na kuchukua hatua kabla yake ilimshangaza sana.
Wakiwa hapa, Sunset Lounge, Ed na Brian waliendelea na vinywaji huku wakisubiri oda yao ya chakula, mazungumzo yao yaliendelea
"Siku hizi nakupata kwa nadra sana mkuu, inakuwa hivi na ukioa itakuwaje!" Brian alimtania Ed baada ya kushusha glasi yake ya mvinyo mezani
"Ha ha ha unanichokoza maana unajua wewe ndio hunitafuti siku hizi. Mkeo ndio kabisa... Yaani Rose ndio siamini kabisa...!" Alilalamika Ed ambaye ni rafiki wa wanandoa hawa Brian na Rose. Ukaribu wao ulikuwa wa kumfanya mtu kudhani ni ndugu wa damu.
Brian alicheka taratibu na kumtetea mkewe, "Rose bado anasumbuka kidogo na homoni atakuwa vizuri soon utamuona."
Ed alirudisha glasi ya mvinyo kabla ya kuweka mdomoni, akamuangalia Brian kwa jicho la 'usinitanie'
"Ha ha ha Ed nini kwani! Tuna zaidi ya miezi nne ya ndoa, unashangaa nini tena!" Brian alijitetea huku akiachia kicheko chepesi
"Well done champ! Hii ni good news aisee!" Ed alisema kwa ukunjufu wa moyo. Upendo wake kwa marafiki hawa ni usiobeba unafiki wowote. Aliwaona ni sehemu ya familia yake.
"Asante champ, niambie upande wako, mnaendeleaje na Lyn? Muda unasogea sana" aliuliza Brian kuonesha kujali usoni kwake.
Ed aliinua glasi na kunywa kidogo mvinyo kisha akashusha pumzi
"Champ kuna lolote tulizungumze kusaidiana?" Maneno ya Brian yalitoka katika wasi wasi kwa kuwa Ed aliyemfahamu hakuwa mtu wa kusimama njia panda muda mrefu.
"Ndio lengo langu kukuona Brian. Champ ninahitaji ushauri wako" Ed alivunja ukimya hakuona shida maana karibia mambo mengi yeye na Brian walishirikiana.
"Niambie champ" alikaribisha usikivu wake kwa rafiki yake, lakini kabla ya Ed kuanza kujieleza mhudumu alifika na sinia lililobeba oda zao za chakula. Alipomaliza kuweka chakula na kuwakaribisha alitoka akiwaacha wafurahie oda zao.
"Champ kuna jambo ambalo natamani unisaidie kulielewa." Alisema Ed kabla ya kukata kipande cha nyama kilichokuwa kwenye sahani yake.
"Bila shaka wawili tutaling'amua" aliongeza Brian na kwa pamoja wakaendelea kula chakula
"Ni kuhusu hisia zangu, kuna msichana tangu nilipomuona hanitoki kichwani. Champ haikuwa hivyo kwa Lyn, nakwama kila nikimkumbuka. Nafsi yangu inamtaka nashindwa kuweka sawa kile nilijisikia kwa Lyn na sijui nakipa sura gani hiki ninachotaka kwa huyu msichana?"
Ed alizungumza kwa utaratibu na hakika mashaka yalionekana usoni kwake. Alirudisha mkono wake na kuchukua chakula ambacho alikisindikiza na funda la mvinyo.
Brian ambaye alimwangalia rafiki yake aliyahisi mashaka yake. Alijua kwa hakika Ed anampenda Aretha na amekwama kujua kipi asimame nacho. Alikumbuka kile alichokiona baada ya kuonana na Linus, na alijithibitishia kuwa Li alikuwa sahihi.
"Anaitwa nani?" Brian aliuliza wakati jina la Aretha alilifahamu, na tena alirudia kuangalia ila video baada ya Ed kumpigia simu na kumuomba waonane. Alichokihisi ndicho kilikuwa lengo la kukutana kwao.
"Aretha...Aretha Thomas, ni mwanafunzi wa chuo Bri, hata sijui najielezaje lakini msukumo wa ndani ni mkubwa sana, nafanya kila nachoweza kuwa busy Bri, what is happening to me? Is it normal?" Ed alifululiza akimhoji Brian.
Brian aliweka uma chini na kumuangalia Ed, alijua kwa hakika yupo njia panda. Si kawaida kumsikia Ed akiongea na kuonesha hisia hizi.
"Champ, ni wewe pekee unaweza kuchambua kile unachokihisi, lakini kuna mstari mwembamba unaotenganisha kile kinachoendelea ndani yako. Unahitaji kuiambia nafsi yako ukweli. Je ulimpenda Lyn kwa dhati ya moyo au la?"