Kimya kifupi kilipita kisha Ed akaendelea
"Nashukuru kwa kuja na ile taarifa kuhusu Aretha, lakini usingesumbuka na mambo yasiyokuhusu Li" taratibu Ed alisema huku akimwangalia mdogo wake
Li alishtuliwa na maneno hayo maana hakutarajia kuwa Aretha anaweza kuwa kwenye mjadala.
"Samahani kwa kufanya hivyo lakini nilikuwa nasimamia nafasi yangu ya ndugu anayejali" aliomba msamaha Li japokuwa bado aliamini alichofanya ni sahihi.
"Asante bro, nitumie taarifa hiyo kwenye simu ninataka kuchukua hatua"
Aaah nini! Li hakuamini kama imekuwa rahisi hivyo. Tabasamu laini lilionekana usoni mwake. Akapapasa simu yake na sekunde chache alikuwa amemtumia kaka yake taarifa zilizokuwa na picha chache za Aretha.
"Asante Li" alishukuru Ed.
"Usijali bro, ndugu tunatakiwa kuwa hivyo"
"Nadhani mengine tutaendelea kuchunguza, kesho D atakuja. We will talk"
Ed alimfahamisha Li, kitu ambacho kilifanya furaha yake kuongezeka.
"Asante kwa hilo, we are brothers after all" alijibu Li na kuinuka tayari kutoka nje.
Ed alimtakia mdogo wake usiku mwema huku nafsi yake ikipata utulivu tofauti na wiki tatu nyuma. Hakika alihisi wepesi na moja kwa moja akarejea kwenye simu yake na kuangalia taarifa aliyotumiwa na Li. Akajitupia kitandani huku akitazama picha ya Aretha, alitabasamu
"Sijui una nini but I like you" alijisemea moyoni huku akichukua namba ya simu na kuihifadhi kwenye orodha ya namba alizonazo. Akainuka kuelekea bafuni.
Aliporejea, akavalia pajama zake za kulala na kuelekea kitandani. Lakini moyo wake ulisumbuka na kutaka kumsikia Aretha. Akashika simu na kuangalia ile namba, alipoinua uso kuangalia ukutani ilikuwa saa nne usiku.
"Nikimpigia sasa hivi atakuwa amelala au atanishangaa" aliwaza Ed.
"Aaaarghhh" akaitupa simu pembeni na kuamua kulala.
**************************
Derrick baada ya kuongea na Ed kaka yake, alitabasamu kwa furaha. Alishukuru walau mahusiano yao yatarejea upya baada ya kuyumbishwa na hila ya Joselyn. Aliwaza jinsi Ed alivyomkaba kwa hasira na kutompa nafasi ya kujitetea lakini akachagua kumsamehe kwa kuwa aliamini Joselyn hawezi kumdanganya.
Alichukua simu yake na kumpigia Aretha, simu iliita kwa muda na hatimaye ikapokelewa..
"Hellow Derrick" sauti laini ya Aretha ilisikika upande wa pili.
"Hellow rafiki yangu, vipi ulikuwa kwenye brashi eeeh?" Derrick alimtania
"Ahhhh hapana nilikuwa najisomea" Aretha alijibu huku kicheko chepesi kikimtoka
Derrick aliposikia hivyo akakumbuka sura ya Aretha anapotaniwa anavyoinama kwa aibu.
"Kesho nakuomba unisindikize mahali" Derrick alijua kumwendea moja kwa moja Aretha
"Eeeeh?" Mshituko wa Aretha ulikuwa wazi.
"Ndio Retha" Derrick alifupisha jina lake kama ambavyo alimsikia mama yake akimuita. Amekuwa na mawasiliano na Aretha ya mara kadhaa na ndio maana leo Aretha aliweza kupokea simu yake.
"Mmmh wapi huko Derrick?" Aliuliza kwa wasi wasi uliokuwa wazi kwenye sauti yake.
"Naenda kumuona ndugu yangu mmoja ambaye ameomba tuondoe tofauti zetu. Natamani unisindikize niwe na ujasiri wa kumuona" Derrick alijibu kwa msisitizo kuonesha hilo analotaka ni la muhimu
Kimya cha sekunde kilipita kwenye simu hadi Derrick akapata wasi wasi na ombi lake asiwe amemkera Aretha.
"Retha" aliita
"Oooh samahani Derrick, kesho nina wasi wasi nitashindwa ila kama nikipata ratiba tofauti nitakujulisha" alijibu Aretha
"Aaah sawa Aretha, ila nakuomba utafakari ni vile naamini nahitaji mtu mwingine kuwa nae wakati tunarejesha amani kati yetu. Tafadhali nakuomba. Ni jioni saa kumi. Nitapitia jibu langu" Derrick alijaribu kumshawishi
"Aah... amhhh basi sawa nitakwambia. Naomba niendelee na kusoma. Asante Derrick" Aretha alimshukuru na kumuaga
"Hapana shida Retha, fikiria ombi langu, jioni njema" Derrick alikata simu
Alishusha pumzi na kuachia tabasamu laini, hakika alikusudia kumsuprise kaka kwa kwenda na Aretha hadi nyumbani. Lakini alihitaji kumshawishi vya kutosha Aretha ili aweze kuongozana nae. Alikusudia asubuhi kupita kwao akichukulia nafasi aliyonayo kwa mama yake Aretha. Mara ya pili alienda pale na alifanikiwa kuuteka moyo wa mama huyo, sasa atatumia nafasi hiyo.