Mara zote Jumamosi kwa Ed huwa siku yenye mambo machache ya kazini na mengi huyaweka kwa ajili ya kuwa karibu na familia yake.
Asubuhi ya jumamosi hii Ed yuko ofisini kwa kuweka vitu vichache sawa. Lakini baada ya kugusa gusa kompyuta mpakato yake shauku ya kumsikia Aretha ilimvamia kwa nguvu. Akavuta simu yake na kuangalia mahali alipohifadhi namba ya Aretha, akaipiga namba ile na kusubiri. Simu iliita muda mfupi na ikapokelewa
"Hellow" sauti ya Aretha ilisikika na ilikuwa rahisi kwa Ed kujua Aretha alikuwa bado yuko kitandani.
"Aretha, habari ya asubuhi" Ed alisalimia huku usoni akiwa na tabasamu dogo la furaha
"Salama, naongea na nani, samahani?" Aliuliza Aretha
"Unaongea na rafiki ambaye alikupa kadi yake wiki mbili sasa na bado hukumtafuta" Ed alisema haya huku tabasamu la pembeni likionekana
Kimya kifupi kilipita hadi Ed akashtuka maana alisikia mtu akihema lakini hakuzungumza chochote..
"Aretha" aliita Ed
"Eeehhh ammmhhh..., samahani Edrian" ndicho alichoweza kusema Aretha.
"It's okay, ulisema utanitembelea mbona hukurudi?" Akaendelea Ed na maswali yake ya uchokozi.
Kabla Aretha hajajibu Ed akaongeza tena swali
"Au sikukupokea vyema?"
"Aaaah hapana Edrian, usiwaze hivyo, nimekuwa na ratiba ngumu lakini nitajitahidi nitakuja" Aretha alijitetea
"Lini utakuja?" Aliuliza Ed.
"Nikimaliza tu kuweka rangi kwenye picha" alijibu Aretha.
"Oooh, picha yangu au ya mtu mwingine?"
Ed alimuuliza huku ikiwa dhahiri kuwa anataka hiyo picha iwe ni yeye.
"Mhhhh, sitakuambia ni ya nani ila nitakuletea" alijibu Aretha.
"Aretha" aliita Ed
"Abeee" aliitika
"Naweza kupata muda wa kuona hizo picha unazochora?" Swali ambalo lilimpa kunyamaza kidogo Aretha
"Aretha" aliita tena Ed
"Aamhhh abee, samahani Edrian." Aliitika na kuomba radhi maana kimya chake kingekushtua hata wewe.
"Eeeh, sawa. Au nimeomba kitu kikubwa?" Aliongeza Ed
"Hahaha... hapana. Nitakuletea kwanza picha moja kabla ya kukuruhusu uone nyingine"
"Oooh.... basi sawa... kwa hiyo lini hiyo?" Ed aliuliza kwa shauku maana alitaka sana kuonana na Aretha.
"Jumanne... Edrian"
"Hahaha .....mbona mbali sana Aretha?"
"Nitakuwa nimeikamilisha ...tafadhali vumilia kidogo" maneno haya yalimfanya Ed kushusha pumzi na kukubaliana na Aretha ili asionekane kuwa na ajenda nyingine.
"Basi sawa Aretha, nina ombi moja..tafadhali"
"Eeeh. ..ombi lipi" sauti ya Aretha ilibeba wasi wasi baada ya kusikia Ed akisema ana ombi.
"Worry not.. naomba jumanne tukutane tofauti na ofisini kwangu. Itakuwa sawa kwako?"
Kwa sekunde kumi na tano Aretha alinyamaza lakini Ed alijua amemsikia na akampa nafasi atoe jibu kwa utashi wake mwenyewe.
"Sawa. Nitakupa ratiba yangu jumatatu." Aretha alijibu na kufanya Ed aseme 'yes' kwa sauti ya chini kufurahia jibu hilo.
"Asante Aretha. Hifadhi namba hii kwenye simu yako. Ni namba yangu binafsi. Naitumia na watu wachache walio karibu na mimi"
"Aaahhhm, haya nitafanya hivyo" aliitikia Aretha
"Nikutakie wikiendi njema Aretha."
"Asante sana"
Ed alikata simu akatabasamu kuonesha kuridhika na hatua alizochukua leo.
"I will get to know you Aretha.. " alisema moyoni mwake..
Baada ya muda, Allan aliungana na Ed na kwa pamoja wakaondoka kuelekea "The Base" moja ya mwamvuli wa usalama wa SGC. Mahali ambapo 4D walikuwa wakipatumia kufanya kazi zao.
Wakiwa kwenye gari Ed na Allan waliendelea kuzungumzia taarifa ya 4D iliyohusiana na Martinez Kussa. Waliamua kuonana na Captain kama ambavyo alijulikana na utaalamu wake wa kucheza na kompyuta kiasi kwamba huwezi kuiba taarifa za SGC kwa urahisi.
"Ukimuuliza Lyn unadhani atakuwa anajua njama za baba yake?" Allan aliuliza wakati wakielekea The Base.
"Kuna njia moja ya kujua, nitamuuliza lakini nategemea hata kama anajua hatoniambia anajua. Nafanya hivyo ili atakapomshtua baba yake ndipo nitajua ukweli wa uhusika wake" Ed alijibu na wakati huu alikunja usukani kuingia The Base.
The Base kwa nje imebeba muonekano wa duka kubwa la uuzaji wa kompyuta na vifaa vyake. Mmiliki halali wa duka hili ni Edrian lakini katika usajili ilionekana mmiliki ni Alexander Barnabas.