"Huyu Senior bachelor ni mwanaume halisi au ana shida?"
"Ed atakuwa ni shoga, au ni gay"
"Utajiri wote huo hana mchumba, au ndio maagano yake na mganga nini?"
"Sasa anataka kutuambia yeye mke wake ni pesa tu hana habari na mambo ya wanawake?"
"Hawezi kuoa huo utajiri hautaki mke."
Haha ha haya ni baadhi ya maneno ambayo watu waliyasema nyuma ya pazia kwa kuona muda unaenda na Ed hajawahi kuonekana kwenye mahusiano na zaidi sana kukutwa na skendo yeyote ya kimapenzi.
Edrian ni moja kati ya watu wachache wenye misimamo thabiti linapokuja suala la mapenzi. Kwa sababu ya kutumia muda mwingi akiwa na baba yake hakuweza kutengeneza historia nzuri ya mahusiano ya kawaida na jinsia nyingine. Lakini hii haikuwa sababu kuu, bali ni moja kati ya mambo ambayo Ed hakuwa na msingi mzuri nayo. Ed na misimamo yake ya kimasomo ilimfanya asiwe na kipaumbele chochote kuhusu mapenzi. Aliyaona kama ni mambo ya ziada hasa kama hauna mpango wa kuoa wakati huo. Aliogopa sana kuwa na rafiki wa kike ambaye angepata shida kutokana na kukosa muda wa kukaa naye, kwa wakati huo alikuwa busy na kuweka msingi imara wa biashara.
Kutokana na msisitizo mkali kwa mama yake, Ed aliamua kuchukua hatua kwanza ya kuwa na rafiki wa kike, na baada ya miezi sita aweze kumtangaza rasmi kama mchumba wake. Wakati huo, msaidizi wa Ed, Allan alianza kumsaidia boss wake tips za muhimu katika kumpata msichana huku akishirikiana na Linus mdogo wake.
Wanasema wewe wapanga wenzio wapangua; taarifa hizo zikamfikia mmoja kati ya watu wenye uchu na fedha, Martinez Kussa. Akijua kuwa anaye binti wa miaka 28 ambaye ni mhitimu wa chuo mwenye degree ya Mahusiano ya Kimataifa (International Relation), Joselyn.
Hakusubiri apitwe akatengeneza namna ya kuwafanya wafahamiane. Baada ya kuchunguza ratiba za Ed, aliona fursa ya kumfanya Joselyn awe jirani yake katika ndege waliyopanda ambapo walikaa Business Class. Lakini hakuishia hapo, walipofika akamchukulia chumba kwenye hotel hiyo hiyo aliyofikia Ed, bado chumba kilikuwa mkabala na cha Ed. Martinez ni habari nyingine kabisa. Kwa ajali hizo Ed akajikuta anafahamiana na Joselyn na mwisho akajaribu kurusha ndoano ambayo kwa akili ya Martinez alimwambia mwanae ajifanye kama hana interest. Baada ya jitihada za mwezi ndoano ikashika samaki.
Maisha yakaanza kwa wapenzi hao wawili.
Kama nilivyokwambia Ed ni mtu wa misimamo, alimuomba Joselyn ajitunze na kumhakikishia kuwa atakuwa muungwana kwa kusubiri,
si vyema kukuchukulia kama mke kabla hujawa. Yalikuwa maneno ya Ed.
Kwa Joselyn asali aliisha ilamba kitu ambacho kilimuwia vigumu kukaa na Ed pasipo kuwa na ukaribu naye wa kimwili. Ed ni mwanaume ambaye mwili wake ulijengeka vyema, achilia mbali muonekano wake, weusi wake ulitoa mng'ao safi huku macho yake yakiwa ni kivutio tosha kwa mtu aliyemuona.
Uvumilivu ulimshinda Joselyn, mwezi wa tatu wa mahusiano yao aliamua kufanya alichokitaka, baada ya kwenda kwenye sherehe ya rafiki yake Ed, Brian, mwanamke huyu alitumia nafasi hiyo na kuweka kidonge cha kuamsha hisia kali za mapenzi kwa mwanaume. Ed asingeweza kuchomoka maana Joselyn aliandaa mipango yake sawa na hata kufanikisha alichotaka
Siku ya pili, Ed baada ya kugundua alichofanya alijilaumu sana na kuona yeye ndie tatizo pasipo kujua mpango wa Joselyn. Toka wakati huo alimchukulia Joselyn kwa dhati ya moyo wake, na aliazimu kumvisha pete katika muda alioupanga ambao ulikuwa ni miezi sita. Sasa yuko mbioni kutimiza kusudi lake, bado yuko kwenye hatua za uchunguzi juu ya Martnez Kussa, ambaye ni adui aliyevaa ngozi ya rafiki. Jukumu hilo alipewa Allan. Allan ni schoolmate wa Linus, hivyo shughuli hii kwa pamoja wanaendelea nayo. Taarifa ndogo tu itawapa ufunguo wa kumfichua Delilah na baba yake. Watafanikiwa??
***********************************
Edrian Simunge miaka 36,watu walipenda kumuita 'senior bachelor' kabla ya kukutana na Joselyn Martinez ambaye alibadilisha jina kongwe la mfanyabiashara huyu. Kijana ambaye ni maarufu sana kwenye biashara ya madini, the best and smart business man hapa A Town. Hii ni moja ya biashara ambayo tangu mtoto hata anakua ameiona ikifanywa na marehemu baba yake mzee Elvis Simunge. Alijifunza biashara katika umri mdogo hata kumfanya baba yake amuamini mapema na kumpa usimamizi wa mojawapo ya maduka ya Vito cha thamani aliyomiliki. Alijituma sana tangu akiwa elimu ya sekondari na alipoomba nafasi ya chuo tayari Ed aliamua kusomea elimu ya biashara. Alifanikiwa kupata scholarship na kusomea Chuo Kikuu cha Biashara cha Havard. Alikuwa mwenye bidii katika masomo yake huku simu sure akipanga kupata ufahamu wa namna ya kuendesha biashara za familia.
Uuzaji na ununuaji madini ilikuwa ni biashara ambayo ilimfanya mzee Elvis kujijengea jina katika ulimwengu wa biashara ya madini. Mzee huyu alijua namna ya kupata madini, kushawishi wanunuaji na wauzaji, kiufupi alijua in and out ya madini. Ed alikua chini ya uangalizi wake na hata biashara ya madini ikawa kama kiganja cha mkono wake. Alifahamika na serikali lakini makampuni ya wachimbaji, wauzaji na wanunuzi wa madini. Familia ilimiliki baadhi ya machimbo kwenye miji mitatu iliyofahamika kwa madini M-Town, G-Town na K- Town.
Ed alifahamika kwenye majukwaa mbali mbali ya biashara na hata kutoka kwenye baadhi ya magazeti yaliyozungumzia mafanikio yake. Alialikwa kwenye mikutano mbali mbali ya kuhamasisha vijana hata kumuongezea umaarufu mkubwa. Familia ilimiliki maduka mbali mbali ya vito vya thamani bila kusahau maduka ya fedha za kigeni
Baada ya baba mzee Elvis kufariki, Ed aliwekwa na familia kuwa msimamizi wa biashara zote za madini akisaidizana na mdogo wake Linus ambaye alikuwa amesomea uchumi. Linus alisimamia shughuli zote za maduka ya kubadili fedha za kigeni. Coletha na Derrick walikuwa mapacha ambao ni wadogo zake na Ed wa mwisho, wao walikuwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza chuo cha utalii hapa A- Town. Moja ya sababu ya wao kusomea kozi hiyo ni kusimamia wazo jipya la familia kuingia katika mambo ya utalii. Hili lilikuwa wazo ambalo Derrick alishawishi familia kulianza, na kwa support ya big bro Ed, walisajili kampuni ya Utalii ya Twin Safaris ambayo ilikuwa chini ya The Elvis Jewerly Gallery.
Mama yao, Mrs Simunge sasa alikuwa mjane ambaye muda mwingi aliutumia katika ufugaji wa ng'ombe wa maziwa huko River Estate nje kidogo ya A-Town ambako pia aliishi. Baadhi ya ndugu wachache walikuwa pamoja nae hata kuhakikisha wanamsaidia kulingana na umri wake. Mama huyu alikuwa sasa na ugomvi mwepesi na watoto wake wakubwa wa kiume yaani Edrian na Linus, mara zote aliwataka waoe maana hakutaka kuwaona wakidangayika na mafanikio pasipo kuona umuhimu wa familia. Alitaka pia wajukuu japokuwa vijana wake walimpinga na kusema wataoa wakiona inafaa.
Familia hii ilifahamika katika mji huu kwa kuwa na kituo kikubwa cha kulea watoto wenye ulemavu wa akili, ambacho kilishirikiana na hospitali kuu ya mji katika matibabu ya watoto hawa. Kwa ushirikiano na baadhi ya taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali watoto hawa walipata misaada mbali mbali ya kiafya, kielimu na hata kimalezi.
Ed alipenda kukaa na ndugu zake ili kuwapa nafasi ya kujifunza kutoka kwake mambo ya biashara. Japokuwa alikuwa mara was mara akisafiri lakini alitumia muda anaokuwepo nyumbani kujumuika na wenzie katika mambo ya biashara. Waliangalia masoko ya hisa, uuzaji na ununuaji wa bonds, mambo ya ubia na mengine mengi. Hakika aliendelea kuwakuza vyema kwenye biashara. Mazungumzo yao yalijaa maneno ya kibiashara hata kumfanya mgeni kati yao kutoelewa chochote.
Familia hii ingeweza kuitwa Happy family, japokuwa changamoto hazikosi na kila mara zilizaliwa hasa kutoka kwa washindani wapya katika maeneo yote. Maadui pia walikuwepo walioyakasirikia mafanikio yao na kutafuta mbinu za kuwashusha chini. Na sasa kipenzi cha Ed alikuwa ni mwiba kwa ndugu zake pasipo yeye kufahamu, Joselyn Martinez Kussa.
*************************************