Jioni ulipowadia kila mmoja alijiandaa vyema, Ed alivaa suti safi ya rangi ya kijivu iliyomkaa vyema huku akivaa tai ya kipepeo kwenye shati yake nyeupe. Muonekano wake ungeweza kukamata macho ya mtu yeyote yule. Linus alivaa suti ya bluu iliyokolea na shati ya rangi nyeusi.. alivutia mno. Walielekea kwenye gari kumsubiri Coletha, huku Linus akikaa kwenye usukani na Ed alikaa nyuma. Coletha alipotokeza mlangoni macho yao yalimuangalia hadi alipoingia na kukaa nyuma na Ed.
"Hey bro, Coletha anahitaji bodigadi usiku wa leo" alitania Linus
"Mmmmm, kabisa Li, unaonaje ukimlinda wewe" alisema Ed
"Aaaargh acheni basi mbona mnanikorofisha" alilalamika Coletha
Ed akamshika mkono, "You are gorgeous baby sis"
Coletha alitabasamu kwa aibu, "asante bro" kisha akamuuliza Ed,
"Allan atakuja bro?"
"Atakuja ametangulia kumpitia Loy" alijibu Ed na kuchukua simu kumpigia Allan
Wakati huo uso wa Coletha ulijaa tabasamu na kufanya vidimple kuonekana kwenye mashavu yake. Linus aligeuka kumwangalia mdogo wake akarudisha tena macho yake barabarani akifikiri kwa nini Coletha amemuulizia best yake, au dada yao pekee ameanza kumpenda Allan? Linus aliamua kulitupia hilo wazo nyuma ya ubongo wake akaendelea kuendesha hadi walipoingia kwenye geti kubwa lililowakaribisha Crest Hotel. Walielekea kwenye maegesho baada kuelekezwa na mmojawapo wa walinzi waliokuwa eneo lile.
Hoteli hii yenye hadhi ya nyota tano ilikuwa na kumbi kadhaa za mikutano zilizofahamika kwa majina ya vito. Ukumbi wenye hadhi kubwa uliitwa The Golden Hall, ambapo ndipo sherehe as usiku huu ziliandaliwa. Ukumbi huu ulikuwa katika ghorofa ya 14 ya jengo hili, hivyo, matumizi ya "lifti" yalihusika.
Edrian, Linus na Coletha kabla ya kushuka waliwasubiri kina Allan ambao baada ya dakika tano waliwasili.
"Samahani bro, Loy alikuwa hataki kutoka kwenye kioo" alitania Allan na kuwafanya wacheke kwa pamoja huku Loy akiinama kwa aibu.
Baada ya kusalimiana ilikuwa ni wakati wa kupita kati ya waandishi wa habari waliokuwa kwenye mlango wa kuingilia.
"Umependeza sana Coletha" Allan alimwambia Coletha ambaye muda huu alirudisha macho chini
"Aaaaah, asante Allan" alijibu na kuendelea kupiga hatua. Linus aliyekuwa pembeni mwa Coletha aliangalia kisha akageuza shingo kuona wanakoelekea maana walishamuona Ed akibadilisha njia iliyoingia mlango mkuu wa kuingilia.
Wote walibaki wanashangaa huku wakiangaliana lakini waliamua kumfuata kimya kimya maana wote wanamjua Ed alivyo mtu wa matendo zaidi. Walipofika kwenye kona walikutana na mwanaume aliyevalia suti safi nyeusi ambaye aliwapokea
"Mr Simunge karibu sana" alimpokea Ed na kusalimiana na mikono na kisha akawasalimia wengine.
"Asante sana Mr Anthony, nilikuwazia tu baada ya kuona like jopo la paparazzi.. unaendeleaje?"
"Salama kaka, tuelekee huku" alijibu Mr Anthony na kina Ed wakamfuata nyuma. Baada ya kona mbili waka wamesimama kwenye mlango ambao mwenyeji wao aliweka kidole kwenye mashine ukafunguka na kulikuwa na ngazi ambazo ziliwapeleka mpaka chini (base), wakaingia kwenye lift kuelekea ghorofa ya 14.
Mr Anthony ni Meneja Utawala wa hotel hii ambayo Edrian ni mmoja kati ya wakurugenzi wa bodi ya hotel. Wakati wanamsubiri Allan, Ed alimtumia meseji ili kumuomba awasaidie kupita kwenye mlango wa ziada ambao mara nyingi unatumiwa na bodi ya wakurugenzi ambao huwa hawataki kuonekana mara was mara na wafanyakazi.
Walipofika, baada ya mlango wa lifti kufunguka, walitoka na kukata kona iliyowapelekea mpaka kwenye mlango wa The Golden Hall.
"Asante sana Anthony." Alishukuru Ed huku wengine wakionesha shukrani pia kwa kuinama.
Mr Anthony alimuita mhudumu aliyekuwa amesimama pembeni ya mlango akisaidizana na wengine kuwapokea wageni walioingia. Baada ya mhudumu kumuona Ed aliinama ishara ya heshima na kuwaelekeza wamfuate.
Ed alitangulia huku Linus na Coletha wakiwa nyuma, Allan na Loy waliwafuatia. Ukumbi uliandaliwa vyema, huku meza zikiwa zimepangwa vyema na viti vyake kuwa katika mpangilio wa kuvutia. Ed alisalimiana na watu kadhaa aliowapita katika meza zao na wengine walipomuona walisogea kumsalimia, naye hakusita kuwatambulisha aliokuwa nao.
Haikupita muda mrefu walikuwa wamekaa kwenye meza ambayo iliandikwa Simunges kuonesha watakaokaa hapo ni kutoka familia ya SGC. Waliendelea kupata vinywaji huku mazungumzo ya hapa na pale yakiendelea kati yao, mara kwa mara kukatishwa na watu waliowafahamu walipopita kuwasalimu.
Muda mfupi baadae aliingia Joselyn akiwa ameongozana na baba yake, Martinez pamoja na wanaume wengine wawili. Na kwa mpangilio wa meza jioni hii meza ya Martinez ilifuatana karibu kabisa na ile waliyoandaliwa kina Ed.
"Hello Mr Simunge" alisalimia Martinez na kuachia tabasamu pana katika midomo yake huku akinyoosha mkono kumuelekea Ed.
"Salama Mr Kussah, nimefurahi kukuona." Ed alijibu baada kuinuka na kushikana mkono na Martinez.
"Pleasure is mine, unamfahamu binti yangu Joselyn?" Aliendelea Martinez huku akimshika bega mwanae
"Yes, tumewahi kukutana hapa na pale, we are not complete strangers!" Alijibu Ed na kumpa mkono Joselyn ili kumsalimia.
Joselyn aliachia tabasamu lake na kuonesha mpangilio safi wa meno yake huku akisalimiana na Ed,
"You look lovely Lyn!" Ed alinong'ona waliposalimiana
Macho ya Joselyn yaliwaka kwa furaha na kwa ghafla akamkumbatia Ed ambaye hakuwa na namna zaidi ya kumpokea kwenye mikono yake.
"Thank you Ed, uko vizuri pia." Alisema maneno haya huku akimtupia jicho la dhihaka Coletha ambaye alitaka kuinuka na kutoka lakini Linus alimbana mkono kumuashiria asifanye hivyo.
Ed akiwa bado kwenye mshtuko mshereheshaji alianza kuongea kupitia kipaza sauti na kumfanya Joselyn amwachie na watu waliokuwa wamesimama ikabidi wakae kwenye viti vyao.
Wakati wanakaa Martinez alimshika binti yake begani na kunong'ona "Good move baby girl". Joselyn alitabasamu na kuketi.
Ed alirudi kawaida japokuwa hakupenda kitendo kile, akijua paparazzi kama walipata picha kesho lazima wataanza kupekua pekua. Sio kwamba hakutaka ifahamike lakini alijua utendaji kazi wa watu hao, wangeanza kufukunyua mambo ya nyuma ambayo hakutaka kuyajua kuhusu Joselyn. Alitaka tu kumvalisha pete na kuanza taratibu za ndoa bila kuwapa taarifa hawa pekua pekua. Alibaki akiomba isiwe imeonekana kwao.
Jioni hii ilienda vyema, huku Waziri wa Madini akitoa shukrani zake kwa makampuni na wadau kwa mchango mkubwa walioonesha kwenye sekta ya madini.
Baada ya chakula, mambo machache yaliendelea, Ed muda huu alikuwa kama mtu ambaye mawazo yake hayakuwepo hapa.
"Bro" aliita Coletha, lakini Ed hakuwa amesikia
"Bro Ed" alishtuliwa na Allan
"Naam" aliitikia na kumwangalia Allan,
"Sio mimi nakuita ni Coletha"
"Aaah, am sorry baby sisy, nambie" aliomba msamaha na kumpa masikio Coletha..Lakini alikuwa akijicheka moyoni kwa kuwa mawazo yake aliyapeleka siku ya Jumatatu ikiwa Aretha angefika ofisini kwake. "Kwa nini namuwaza" alijilaumu
"Nimeona haupo nasi nikakuita" alisema Coletha huku akitabasamu
"Mmmh, nipo, nahisi uchovu tu, nafikiri nitangulie" alisema Ed na kuinuka
Mara wote wakainuka ili kuondoka nae, "Hey vipi, mnaweza kubaki ni mimi tu nimechoka" Ed aliwaambia lakini wote walisisitiza waondoke pamoja, hakuweza tena kuwazuia.
Akaelekea meza ya Martinez na kumuaga Joselyn ambaye alimshangaa Ed,
"Vipi Ed haupo vizuri?" Aliuliza, Ed akamhakikishia kuwa alikuwa na uchovu tu.
Akaagana na wachache waliokuwa meza za karibu na pale alipokaa, kisha wakatoka kuelekea kwenye lift ambapo ilibidi kusimama dakika chache wakisubiri.
Lift ilipofika waliingia lakini kabla mlango kufunga Joselyn aliungana nao na kuwafanya wengine kubaki na mshangao.
Ed alimwangalia na kisha akatoa tabasamu dhaifu. Kimya kilitanda na hakuna aliyejaribu kusema chochote mpaka walipofika chini kwenye ukumbi wa mapokezi, wakatoka na kukutana na baadhi ya waandishi wa habari wachache.
Ed hakutaka kujibu chochote hivyo aliendelea kutembea akipuuzia maswali waliyouliza na hasa kuhusu uendeshaji wa migodi ya SGC. Alijua kama angesimama angesababisha maswali mengi.
Muda wote huo Joselyn alikuwa nyuma yake akimfuata mpaka walipofika kwenye maegesho ya magari. Hatua chache lilipokuwa gari la Allan, alisimamia Linus, Coletha na Loy, ambao waliwapa nafasi wapenzi hawa kuzungumza. Ed alisimama na kumgeukia Joselyn
"Lyn una wasi wasi mbona umenifuata?" Alimuuliza
"Yap, nafikiri hauko sawa, tuondoke wote" alisema na kuelekea kwenye mlango tayari kufungua.
Ed alimuangalia kisha akashusha pumzi,
"Basi sawa"
Joselyn aliposikia hivyo alifungua mlango na kukaa kiti cha nyuma ya dereva.
Ed akawapa ishara akina Linus kuingia kwenye gari, Coletha aligoma kuongozana na kaka yake.
Ed alipoona hivyo, alimuita Allan, akamuomba amsaidie kumrudisha nyumbani Coletha.
"Sitaki kum-upset mdogo wangu, i understand how she feels!"
"No problem Bro. Nitafanya hivyo." Alijibu Allan.
Linus aliposikia kile alichoamua kaka yake, na yeye akaamua kupanda gari ya Allan. Ed hakutaka kuwalazimisha maana alijua namna walivyojisikia baada ya tukio la Derrick. Wakaondoka The Crest Hotel huku kina Allan wakianza kwanza kumpeleka Loy.
"Jioni ilikuwa njema kabla ya Delilah kutokea arrgh!" Alilalamika Coletha aliyekaa kiti cha nyuma na Loy.
"Coletha usiseme hivyo" Allan alijaribu kumuweka sawa
"Nilifikiri ni mimi peke yangu kumbe na wewe" aliongeza Loy
"We Loy, usiongeze mafuta kwenye moto" Allan alimkemea Loy
"Hapana Allan, tuache tuseme ukweli, Lyn ni Delilah, au nadanganya kaka Li?" Coletha aliendelea kulalamika
Li alicheka kicheko chepesi, kisha akasema
"Kwa hiyo ladies mnataka tumtete Bro na mchumba wake eeeeh?"
"Aaaah hapana kaka Li, tunaongea tu" aliwahi Loy kujitetea.
"Njia rahisi ya kutokereka zaidi, tuache kabisa kumzungumzia, you will end up sleepless!" Linus aliwaambia
"Kabisa, comrade, Loy acha kumharibu Coletha." aliongeza Allan
"Mimi tena jamani" alijitetea Loy
"Usijali Loy, anakuonea tu, Coletha ndie aliyeanzisha." Linus alimtetea Loy.
Waliendelea na safari huku muda wote macho ya Coletha yaliibia kumuangalia Allan.
Baada ya kumfikisha Loy, Allan aliwapeleka kina Linus hadi nyumbani. Waliposhuka waligundua gari aliyoondoka nayo Ed haikuwepo sehemu ya maegesho.
"Afadhali daah! Sikutaka yule mwanamke alale hapa" alisema Coletha baada ya kuangaza kwenye maegesho. Kisha akamgeukia Allan aliyekuwa amesimama nje
"Asante Allan.Karibu upata hata matunda"
"Asante Coletha, wakati mwingine" alijibu Allan
"Usiku umeenda comrade" aliongeza Linus huku akimgusa begani
"Yap comrade. See you on Monday! Alimaliza Allan na kuingia kwenye gar huku mlinzi akimfungulia geti na akatoka.
Coletha alibaki amesimama hadi gari ilipotoka na geti kufungwa.
"Coletha mbona unamuangalia sana Allan, kuna kitu kinaendelea kati yenu sikijui" aliuliza Li
"Mhhh kaka Li, hebu niache, umeanza uchokozi" alijibu Coletha na kupiga hatua kuingia ndani
Li alibaki nje akitabasamu, akaamua kukaa kwenye kibaraza kumsubiri Ed huku akichukua simu yake na kumpigia.
Ed alimjulisha kuwa yuko njiani anarudi alimpeleka Joselyn nyumbani kwao.
********************