Ed aliendelea kujikita katika kazi yake tangu alipoingia ofisini asubuhi hii. Alipiga simu na kupokea na mara kwa mara aliongea na Allan huku wakijadili maendeleo katika migodi iliyomilikiwa na SGC. Lakini hakuna aliyejua hisia zilizoufunika moyo wa Ed asubuhi ya leo. Nini kilitokea alfajiri kabla ya kufika kazini
*************************
Ed hakuelewa kwa nini anakosa usingizi mapema hivi, tangu ashtuke saa tisa usiku amebaki akigeuka geuka tu kitandani.
Akainuka kuelekea kilipo chumba chake cha kujisomea ambacho kiko ghorofa moja na chumba chake cha kulala. Aliingia na kujitupia kwenye sofa moja iliyokuwa ikitizamana na meza.
Ed alitabasamu baada ya kuwa njia panda akijishangaa maana mikono yake ilitaka kufungua kompyuta ili kuangalia kipande cha Aretha tena baada ya kuamua kuiacha simu yake chumbani. Sababu kubwa ni kutoshawishika kuangalia tena kipande hicho.
"Why Aretha, umenifanya nini, mbona sipati usingizi" alijisemea Ed. Akajicheka sana moyoni maana alijiona kama mtu asiyejielewa. Akaamua kuinua simu iliyokuwa mezani ili kumpigia Joselyn, lakini ilikuwa ni saa 10 alfajiri na simu yake ilikuwa imezimwa.
Baada ya jitihada za kujizuia kugonga ukuta alijikuta tayari yuko kwenye kompyuta akifungua tayari kuangalia tena. Akaipeleka mpaka pale alipomshika mkono Aretha, mara alihisi raha moyoni kiasi kwamba kona za mdomo wake zilitanuka na kuweka tabasamu binafsi usoni kwa Ed.
Aliposhtuka tena alishusha pumzi,"This is too much Ed" alijisemea na kuizima kompyuta akaamua kuelekea kwenye chumba cha mazoezi akijiapiza kutoruhusu hisia hizi kumtawala tena.
Alifanya mazoezi kwa nusu saa huku muda wote akiutumia kwenye kukimbia ambapo kwa wakati huo aliweza kuyaweka mawazo yake pale. Alipomaliza alielekea chumbani kwake tayari kuingia bafuni kujisafisha.
Baada ya kuoga, aliingia kwenye kabati la nguo kuchagua atakachovaa ghafla wazo la kuwa jumatatu hii ataonana na Aretha likapita kichwani tena. Akaamua kuvaa nguo simple, akatoa jeans nyeusi na shati ya mikono mifupi rangi ya mawingu
Muonekano wake akiwa amevalia na raba nyeupe chini ulimfanya Ed kuwa mwenye mvuto mkubwa. Bado moyoni aliamua kuonekana kawaida ajili ya Aretha. Bado alijaribu kulitupilia mbali wazo la hisia zake kwa msichana huyu lakini alijisaliti
Tayari muda ulikuwa saa 11 na dakika 30 akatoka huku manukato yake yakiacha harufu safi kwenye korido hadi sebuleni. Alikutana na Zena ambaye ni mhudumu wa jumba hili wanalokaa ndugu hawa aliyekuwa akifanya usafi sebuleni.
Zena alimsalimia Ed ambaye aliitikia na kutoka hadi sehemu yalipoegeshwa magari, akachukua gari ambayo huitumia mara chache kwenda kazini, SUV nyeusi.
Njiani aliamua kumpigia Joselyn, baada ya kupokea,mazungumzo yaliendelea
Edrian: Umeamkaje Lyn?
Joselyn: Salama babe, mbona asubuhi sana?
Edrian: Nilitaka kukusikia, uko wapi?
Joselyn: niko ndani nafanya mazoezi, na wewe uko barabarani?
Edrian: niko njiani naenda kazini. Jioni naweza kukuona?
Joselyn: mbali sana babe, nije lunch tule wote?
Edrian: mhm aaah hapana, iwe jioni tu Lyn.
Joselyn: Why Ed?
Sauti ya Joselyn sasa ilikuwa yenye hisia za kukasirika baada ya Ed kumkatalia
Edrian: Nothing Lyn, nina kazi hadi saa kumi, nitakuchukua kwa ajili ya dinner.
Joselyn: okay. Utanipitia dukani.
Edrian: sawa Lyn. See you soon.
Joselyn aliwahi kukata simu na kumfanya Ed ajisikie vibaya zaidi. Kwanza hakujua kwa nini alipata shida kufikiri Aretha kukutana na Joselyn. Na alihisi usaliti japokuwa hakujua anamsaliti Lyn au Aretha.
"Aaaaargh!" Alilalama Ed na kupiga usukani wa gari.
"What is this"
Alikanyaga mafuta na kuongeza mwendo hadi alipojikuta amesimama Ashanti Towers ikiwa ni saa 12 asubuhi. Alipoegesha alichukua begi lenye laptop yake na kuelekea kwenye lifti iliyompeleka ghorofa ya saba, ofisini kwake.
Baada ya kuingia alizama kwenye kazi, akitoka dakika chache kutengeneza kahawa kisha akarudi kwenye kiti chake na kuendelea na kazi mpaka Loy alipoingia.
Ndani ya moyo wake alitamani kumuomba Loy namba ya Aretha ili amuulize kama atakuja. Sio kawaida yake kufuatilia watu anaokutana nao. Lakini alifanya juhudi kuzimisha ile shauku yake ya kupata uhakika wa ujio wa Aretha.
*********************************