"Uko hapa" ndio neno pekee aliloweza kusema Ed baada ya kumuona Aretha.
Alipoangalia upande ilipo ofisi ya Allan aligundua Li alikuwa amesimama akimuangalia huku mdomoni akiwa na aina ya tabasamu ambalo Ed hakuelewa. Akashtuka na kuyaweka sawa mawazo yake na akaufungua zaidi mlango na kumkaribisha mgeni wake aingie ndani.
"Karibu" alisema Ed.
"Asante sana" alijibu Aretha na kuingia huku bado macho yake yakitazama chini.
Alipiga hatua chache na kuingia, Ed akaufunga mlango na kumuelekeza kwenye kochi la wawili huku yeye akikaa kochi lililoangaliana na lile alilokaa Aretha.
"Juisi?" alimuuliza mgeni wake huku macho yake yakiendelea kumwangalia
"Oh sawa" aliitikia Aretha. Alipoona Ed ameinuka, akainua macho yake kuutazama uzuri wa ofisi hii pasipo kuficha mshangao wake.
Aliyazungusha macho yake na kisha akainua kichwa kuangalia kwenye dari huku akionesha wazi kuvutiwa na mandhari hiyo. Aliporudisha macho yake mbele tayari yalikutana na ya Ed ambaye aliweka boksi la juisi ya embe na glasi huku akimwangalia.
"Ooooh asante sana. Ofisi yako nzuri sana" alisema Aretha kwa sauti ya chini huku akifungua na kumimina juisi kwenye glasi. Bahati nzuri Ed aliisikia na kutabasamu
"Asante"
Kimya kifupi kikapita huku Aretha akiendelea kunywa juisi yake. Ed alikuwa akijiuliza aanze kuuliza nini, na wakati huo Aretha alikuwa akitafuta namna ya kuanza mazungumzo...Mara kwa pamoja wakaanza kuongea, kitendo kilichowafanya kutabasamu na Ed akampa nafasi mgeni wake kuendelea
"Aaaah. ..ahm ulikuwa unafanya kazi nisije nikawa nimeharibu ratiba yako?" Aliuliza Aretha..
Ed alicheka ndani kumshangaa Aretha kufikiri anamchelewesha wakati alitamani kumuona, akamjibu
"Ndio, na hata sasa nafanya kazi maana uko kwenye schedule yangu leo"
"Eeeeh, kweli?" Aliuliza Aretha baada ya kuweka glasi kwenye meza ya mbao iliyokuwa mbele yake.
Ed alimuangalia kwenye macho na kutikisa kichwa chake kukubali.
"Aaahmm sawa, ila nisije kukuchelewesha na ratiba nyingine" alijibu Aretha
Ed alishtuka na kuwahi kumjibu
"Usifanye haraka kwanza, uko hapa nikujibu, hivyo nimeweka muda wa kutosha kukujibu kabla sija-resume na ratiba nyingine, sawa Aretha"
Aliposikia hivyo Aretha aliinama na kufinya vidole vyake akainua uso kumuangalia Ed ambaye macho yake hayakumpa hata sekunde na kumfanya Aretha kutazama pembeni.
"Ooooh. .. basi sawa." Akainua tena glasi na kunywa juisi
"Unachukua kozi gani chuoni?" aliuliza Ed
"Sanaa na Uchoraji" alijibu Aretha huku akichezesha vidole vyake kwenye glasi
"Sawa, unajua kuchora?" Aliuliza Ed huku moyoni akimshangaa huyu dada kwa namna alivyo huwezi dhania anaweza kuchora kweli.
"Najaribu, sijui sana, labda ukiona utaweza kujihakikishia naweza au la!" Alijibu na kuachia tabasamu
Oooh Ed hakuelewa kwa nini alitaka kumuona akitabasamu zaidi. Alisikia raha sana.
"Okay, una studio ya picha zako?" Aliuliza
Aretha akamuangalia na kutikisa kichwa akikataa akaendelea na kuchezea glasi yake na juisi ambayo ilikuwa imekaribia kuisha..
"Ongeza juisi" Ed alimwambia
"Aaah asante, inatosha kwa mchana huu" alijibu Aretha na kuinua glasi.
Ed akagundua hakumpa biskuti ambazo Allan alileta na mbaya zaidi hakumuuliza kama alikula chakula mchana.
"Amhhh... samahani Aretha ulipata chakula cha mchana?" aliuliza Ed huku akimkazia macho
"Mmmmh. ... usijali Edrian niko sawa" alijibu Aretha. Hakutaka kumsumbua maana ukweli ni kuwa muda aliotoka darasani ndio ulikuwa muda wa kuja huku na hakupata nafasi ya kula zaidi ya kula chungwa.
"Aaah hapana, it's okay niambie utakula nini nitaagiza mgahawa uko hapo chini tu" alisisitiza Ed
Ukweli ni kuwa Aretha alijua hata kama chakula kingekuja asingeweza kula mbele ya Ed.
"Aahm... hapana, juisi imenitosha"
Ed akainuka na kuchukua mfuko uliokuwa pembeni ya meza yake na kutoa biskuti boksi moja na kumletea Aretha.
"Tafadhali ongeza juisi na utafune walau hii biskuti" alimsihi
Macho ya Aretha yaling'aa baada ya kuona boksi lile, akaipokea kwa furaha na kuifungua
"Ulijuaje napenda Orange Biskuti?" Aliuliza huku akitabasamu
Ed alishtuka maana hakuwa ameangalia ni aina gani ya biskuti Allan alimletea. Alijisikia furaha
"Sikujua kabisa"