"Hukuona kipindi cha MBC?" Aliuliza kwa mshangao..
"Hapana Loyce, niambie"
"Okay nenda You Tube angalia Rising Star utamuona huyo Aretha" alijibu Loy ambaye hakutaka kuelezea zaidi maana alikuwa na dereva wa kampuni. Haikuwa sawa kwake kujadili mambo ya boss wake.
Loy alishtuka alipotupia macho nje tayari walikuwa wamesimama kwenye maegesho ya Ashanti Tower. Alipoangalia saa mkononi mwake ilikuwa saa mbili na dakika moja.
"Oooh Derrick baadae, ngoja niwahi" alikata simu na kushuka haraka kwenye gari huku akimlalamikia John ambaye ni dereva aliyemleta kwa nini hakumshtua. Loy alikimbia kuwahi lifti iliyokuwa na baadhi ya wafanyakazi wa jengo hili na kuingia ndani.
Kwa upande wa Derrick aliposikia habari hizo mara hiyo akaingia You Tube na kuanza kutafuta kama alivyoelekezwa na Loy. Muda mfupi baadae alikuwa amepata kipindi hicho na kuanza kuangalia. Baada ya dakika arobaini tabasamu lake lilionekana.
Alipomaliza alichukua simu yake na kumpigia rafiki yake anayesoma CU wakutane kabla hajaingia darasani maana alikuwa ana kipindi mida ya saa tano hadi saa saba.
Alijinyoosha Derrick na kuelekea bafuni. Dakika ishirini baadae alielekea Capital University japokuwa hakikuwa chuo anachosoma bali alienda pale kujua taarifa fupi za Aretha. Alijua atazipata kwa best yake huyo ambaye anasoma hapo, Charles.
Alipofika alielekea hosteli kama alivyomwambia.
"Hey kiddo vipi uko hapa asubuhi hii" alimpokea Derrick kwa swali, Charles alionekana ndio kaamka muda si mrefu.
"Huu uvivu utakupa umaskini Charlz na usinitafute" alijibu Derrick huku akiangalia wapi akae maana chumba kilikuwa hakina mpangilio huku nguo zikiwa kwenye viti viwili vilivyowekwa pembeni ya meza.
"Usijali kiddo nitakuomba kazi ya kutunza ndege pori he he he" alijibu Charlz na kuinuka, akatoa nguo kumpa nafasi Derrick akae.
Baada ya muda Derrick akamuelezea Charlz alichotaka amsaidie.
"Huyo Aretha, yukoje?" Aliuliza Charlz
Derrick akajaribu kumuelekeza kama alivyomuona kwenye ile video
"Sio mrefu wala mfupi, round face, beautiful eyes, na anaonekana kuwa mwenye aibu. Kiddo ni mzuri kawaida, lakini nahisi ana moyo mzuri zaidi." Alieleza Derrick ambaye hakutaka kumuonesha Charlz picha kwenye video maana alijua yatazaliwa maswali mengi na kuharibu mpango wake
"Kiddo kati ya hawa mamia ya wanafunzi hizo sifa ni za kawaida sana. Nipe moja itakayo mtofautisha na wengine."
Derrick alifikiria na akakumbuka kuwa Loy ana namba ya Aretha. Akamtumia Loy meseji akimuomba namba ya Aretha.
Loy aliyekuwa ametingwa na kazi za ofisi alishangaa kuona Derrick anamuomba namba ya Aretha. Akaamua kumtumia bila kuuliza kwa nini.
Derrick akamnyakua simu Charlz,
"Hey, umekuja kunifanyia fujo kiddo eeh" aliuliza Charlz
Derrick akaingiza namba za Aretha na kupiga. Simu ikaita sana na haikupokelewa.
Lakini meseji ikaingia
"In class, sorry will call later"
Derrick akatabasamu akatuma na yeye ujumbe
"Which lecture room?"
Baada ya dakika chache akajibiwa..
"Drawing Room"
"Okay" Derrick akamaliza na kumtupia simu Charlz ambaye alibaki akishangaa mfululizo wa tabasamu usoni kwa Derrick.
"Haya kiddo, nakuachia kazi, huyo mtu nayemtaka yuko Drawing Room. Unatakiwa kumfuatilia na utanipa mrejesho. Deal ni kukuachia Hyundai weekend hii" alipomaliza Derrick alimwangalia Charlz.
Charlz alifurahi, akaachia kicheko chake na kumuonesha alama ya kidole gumba.
"Nitaifanya haraka huwezi amini kiddo"
Alipomaliza Derrick alitoka na kuondoka maeneo ya CU akiamini atapokea simu ya Charlz muda si mrefu maana alimfahamu vyema rafiki yake.
Akaelekea chuoni kwake. Akamtumia ujumbe Loy kujua muda wa Aretha kuwapo Ashanti Tower.
*******************************