Akiwa ofisini, Ed alikaa mara kadhaa akijaribu kufikiri nini atafanya Aretha atakapofika ofisini kwake. Akainuka kuangalia kwenye jokofu na kuona lilikuwa na maji na juisi. Akajiuliza nini kingine kingefaa, akaamua kumpigia Allan ambaye alitoka nje ya ofisi kuonana na washirika wa SGC.
"Naomba unichukulie boksi mbili za biskuti wakati unarudi" Ed alimwambia Allan.
"Za aina gani bro" aliuliza Allan
Ed akapata kigugumizi, "zozote nzuri"
Allan ambaye wakati huu alijaribu kuhoji ili kujua nini boss wake huyu aliwaza, akaongeza swali lingine huku akitabasamu,
"Ahh....bro kwa ajili ya watoto au mtu mzima"
"Allan....leta biskuti usiniulize tena" Ed akakata na simu
Allan alicheka sana maana alijua hizo biskuti sio kwa ajili ya Ed maana anamjua asivyopenda vitu vyenye sukari. Mara zote hutumia maji, juisi zilizomo kwenye jokofu lake hutumiwa na wageni hasa.
"This is amazing, let's roll with the drama" akacheka kwa raha Allan huku akimpigia Linus simu kumwambia mambo yalivyo.
*****************************
Masaa yalikimbia na mchana ulifika, muda wa chakula Ed hakutoka ofisini alimwagiza Loy kumchukulia matunda kwenye mgahawa uliopo ghorofa ya pili ya jengo hili.
Hakuwa na hamu ya kula na alijishangaa maana alihisi moyo wake kukosa utulivu mara zote alipofikiria kumuona Aretha.
Matunda yalipoletwa alikula huku akitazama saa yake mara kwa mara. Ghafla simu ya mezani iliita na alijua ni Loy, mapigo ya moyo ni kama yalisimama ghafla. Akabonyeza kitufe kumsikia..
"Boss una mgeni, kaka Linus yuko hapa" ilikuwa ni sauti ya Loy.
Ed akashusha pumzi ambayo aliibana kwa kuwaza mgeni wake amefika.. na kumbe la! Hisia za kuvunjika moyo zikampata... akajikaza na kujibu
"Okay, mwambie aingie"
Linus akaingia na kumsalimia Ed huku akimtazama kusoma hisia zake. Alijua kuwa bro wake alitarajia mtu mwingine maana ni kama hakuwa na furaha kumuona.
"Vipi masoko ya fedha yanaendaje?" Aliuliza Ed kwa uchovu akiwa ameegama kwenye kiti chake.
"Cool bro, vipi mbona kama umechoka sana" aliuliza Linus
"Mmmm" aliguna Ed kisha akaangalia saa yake. Oooh dakika kumi na tano Aretha bado hajafika katika muda alioahidi. Aliwaza Ed na wakati huo alitamani kumuondoa mbali Linus ili asijemfikiria vibaya. Kwani naogopa nini? Alijiuliza Ed
"Bro uko mbali eeh?" Aliuliza Li huku akitabasamu maana alijua hasa kaka yake hataki awepo pale.
"Mmmh no! Niambie mbona uko hapa mchana huu?" Aliuliza Ed huku akimkazia macho Li.
"Nimepita tu kukuona lakini niko na Allan kuna mambo tunahitaji kuboresha kutoka kwa washindani wetu" alijibu Li kuonesha kuwa alikuja kikazi zaidi huku ukweli alikuja kumuona Aretha.
"Oooh basi sawa, tutafanya tathmini soon kuona hiyo system mpya ya kutuma na kupokea fedha... I see it's working... good job Li" Ed alimwambia na kurudisha macho kizembe kwenye kioo cha kompyuta yake.
"Asante, Bro. Usisahau basi kuongea na Derrick, it will help. Please!" Li alimsihi kaka yake
Mhhhhh! Ed alishusha pumzi kisha akaitikia was kichwa.
"Basi ngoja nikuache, tuonane baadae home" aliaga Li na kuinuka
"Sawa Li, asante" alishukuru Ed, huku moyoni akihisi wepesi maana hakutaka Linus ajue chochote kuhusu mkutano wake na Aretha.
Lakini kabla ya kufika mlangoni simu ya mezani kwa Ed iliita, akainua macho kumuangalia Linus ambaye naye alisimama akiwa ameshika kitasa kusikiliza....."Oooh please let it be Aretha" alijisemea Li.
Ed aliangalia simu na akaamua kuinua mkonga wake badala ya kubonyeza kitufe kilichomruhusu kumsikia Loy. Alifanya hivi makusudi ili Li asijue, hakujua kumbe uwepo wa Li pale ni sababu ya kumuona Aretha.
"Mmm" aliitikia Ed
Upande wa pili Loy alimjulisha boss wake kuwa Aretha yuko ofisini tayari.
"Okay, mruhusu aingie" Ed alimjibu Loy na kurudisha mkonga mahali pake. Akainua macho na wakati huo Li alishatoka nje.
"Yuko hapa" akilini Ed alikuwa akijisemea, ni kama mbegu isubiripo maji ndivyo ambavyo alimsubiri Aretha. Akajiuliza asimame au akae na macho yake yalielekea kwenye mlango.
Dakika mbili zilipita bila kumuona Aretha, akahisi labda kuna kitu kimemzuia, akainuka ghafla ili kuelekea mlangoni kumuangalia. Wakati anashika kitasa cha mlango kufungua, akasikia ukigongwa taratibu. Ni kama dunia ilisimama na yeye pekee ndie alikuwa akikimbia maana alihisi mapigo ya moyo kuongezeka.
Na kwa sababu alikuwa tayari mlangoni, alifungua mlango na macho yake yalikutana na yale ya Aretha na kama kawaida, binti huyu aliwahi kuyaepusha ya kwake kutomwangalia Ed.
"Uko hapa" ndilo neno lililoweza kutoka katika kinywa cha Ed.