"Derrick usijali, utaenda kukaa kwenye apartment za Heaven, kwa muda tu, mdogo wangu. Nadhani pale ni karibu na chuoni na nitakupa ile gari ndogo utumie ikiwa utataka tuonane au kumuona mama"
Linus alijaribu kumpoza mdogo wake ambaye alionekana kuathiriwa na kile kimetokea.
"Lakini kaka Li mbona big bro amebadilika sana jamani, mimi hadi naogopa kukaa hapa maana huyu Joselyn akija ni taabu tu"
Alilalamika Coletha..
"Kaka Li, hivi ulisikia big bro alichosema nimefanya?" Aliongea Derrick kwa sauti ya kukata tamaa
"Nimemsikia D, usijali hayo ni maneno ya huyu mwanamke, alichofanya ametuwahi mapema na kuhakikisha big bro hapati nafasi ya kuongea na sisi."
Linus akaendelea
"Wakati sisi tunamsubiri aje hapa sebuleni tuongee, tayari yule nyoka mwanamke alikuwa kashampa sumu ya kutosha"
"Lakini kwa nini hakunipa nafasi hata nijitetee yeye kanihukumu" alisema Derrick kwa masikitiko makubwa
"D mdogo wangu usimkasirikie big bro, tayari moyo wake ulikuwa umejeruhiwa. Wakati anaondoka alituambia tumwambie ikiwa kutakuwa na jambo lolote kwa Joselyn, hatukumwambia chochote tulitaka amalize mikutano yake salama. Sasa kule kutomwambia, moja kwa moja atakuwa amehisi tunakulinda wewe"
Alielezea Linus kwa wadogo zake hawa, waliendelea kujadili machache kuhusu nini wafanye maana Derrick hakutakiwa kuwepo katika jumba hili la kaka yake. Si kwamba alitaka sana kukaa hapa maana familia bado ilikuwa na safu ya nyumba kwenye maeneo tofauti ya mji huu. Pia mama yao alikuwa akiishi Rivers Estate kwenye jumba ambalo aliishi na mumewe kabla ya mauti kumfika.
Hawa ndugu waliamua kuishi na kaka yao sababu walitaka kujifunza biashara kutoka kwake.
"Lakini kaka Li, tutafanyaje sasa kumwambia big bro yale Derrick alimuona Joselyn akifanya, afadhali tungepata hata video maana sijui kama atatuamini"
"Usijali mdogo wangu, tutapata uthibitisho tena, ngedere akishajua kuna mahindi huwa haibi mara moja, atarudia tena. Najua ameamini kwa sababu Derrick siku zote ndie alikuwa akimpinga sana kuhusu mahusiano yake na Lyn. Atakuwa amehisi ulikuwa unamtaka wewe"
"Mmph" aliguna Derrick kisha akamgeukia Linus
"Kaka Li, nitaenda huko Heaven, naomba kitu kimoja, hili jambo tusimwambie mama, maana itabidi amuulize Big bro, kutatokea msuguano wa familia. Please" alisihi Derrick
"Ooh mdogo wangu, umekua vyema sana. Hatutamwambia mama, we all know hali yake. Coletha umesikia?" Linus alimuuliza Coletha ambaye alitabasamu na kuwahakikishia hatosema chochote.
"Good, kesho tumealikwa kwenye sherehe ya chakula cha jioni na Waziri wa Madini itakayofanyika Crest Hotel. Jiandaeni maana tuna kadi yenye reservation table kwa ajili ya familia" aliwaambia Linus
"Mimi naomba nisije, sababu kumuona huyo mwanamke ni sawa na kurudia matapishi" alisema Derrick
"It's okay D, tumia huo muda kumuona mama maana analalamika siku hizi tumemzira. Na vile anataka wajukuu basi sijaenda, nakimbia maswali" alisema Linus na kuwafanya wote kucheka hata hali ya huzuni ikaanza kutoweka.
"Yaani kaka kashuka airport saa kumi alfajiri na huyo kenge alishamsubiri huko huko na hakumpa hata nafasi ya kupumua , kaka Li tutafute njia mapema kabla big bro hajamvisha pete." Alisema Coletha huku akiinuka tayari kutoka.
"Naitafuta hiyo namna, unajua shida bro Ed alikuwa busy sana na biashara, mahusiano hakuyapa kipaumbele, ameamua kuanza mahusiano ndio kapata Delilah, yaani natamani hata Mungu ashushe malaika ambaye ataukamata moyo wake tofauti na huyu nyoka" alisema kwa kukereka Linus
"Kaka Li, si una marafiki wa kike ulisoma nao waalike basi kwenye issue mnazokuwa na kaka labda ataona wengine aaargh! Ananichosha sana huyu mwanamke" alisema Coletha huku akiwa kashika kitasa cha mlango
Wakacheka kwa pamoja, wawili hao wakatoka kumpisha Derrick aliyekuwa akipanga vitu vyake tayari kwa kuondoka baada ya Linus kumkabidhi funguo ya gari ndogo aina ya Hyundai.
Derrick alichukua simu yake na kumpigia rafiki yake wa kike, Emmy akimuomba amsainie chuoni maana leo asingeweza kufika. Ukweli tukio lote lilisababisha mpasuko wa hisia za Derrick, ambaye mara zote alionekana kupendana sana na kaka yake, Ed.
*********************************