Njiani katikati ya pori mwanamke wa makamo wa miaka takribani arobaini akiwa anatembea mwendo wake ukiwa wa haraka kama akikimbizana na muda.
Akiangalia jua la saa kumi ambalo sio muda mrefu jua litaanza kubadili rangi na kuwa ya dhahabu kuashiria machweo.Mwanamke huyo anaendelea kutembea huku akigeuka nyuma mara kwa mara.
Baada ya mwendo wa muda mrefu anasimama kwenye kivuli Cha mti na kuendelea kuangalia alikotoka. baada ya muda anafika Binti wa miaka ishirini akiwa amebeba furushi mgongoni kwake,akionekana kuchoka kutokana na kutembea kwa mda mrefu.Anafika na kusimama mama huyo anamwangalia kwa jicho la hasira "kwa mwendo huo unaotembea naona unataka tuwe vitoweo vya wanyama wakali Leo"anaongea mwanamke huku akimtathimini binti yake ambaye alikuwa anajiandaa kukaa kwenye majani lakini kabla hajafika chini mama anamzuia kwa kumnyanyua "hembe tembea huko unatembea kama kinyonga halafu bado unataka kukaa tena" anaongea huku akimsukuma binti yake kumuimiza kutembea.
Binti anamwangalia mama yake kwa huruma,"mama tupumzike kidogo tu nikiamka hapa nitatembea mpaka tunafika kweli tena " anaongea Binti huku akigoma kutembea.
"nimekwambia sitaki kuwa chakula Cha Simba na chui usiku huu haya tembea huko"mama anamsukuma binti na wanaanza kutembea ."eti bado unataka kupumzika utawazaje kupumzika kwa kile ulichokifanya Mimi na baba yako tutaficha wapi sura zetu,umetuharibia kabisa" Binti anaendelea kutembea huku akiivuta sura yake kuashiria kachoshwa na mazungumzo aliokuwa akizungumza mama yake "hivi akili yako huwa inawaza vizuri kweli,imekuwaje kujifanya unakifafa Mbele ya wageni wote wale"
Mama anaendelea kulalama kuonyesha kachoshwa na tabia ya Binti yake "yaani Mimi ndoa yangu iingie mchanga kwa sababu yako wewe siko radhi kabisa kwa hilo"
Binti anaendelea kutembea akimwacha mama yake nyuma kidogo huku rohoni akitamani angepata pamba Mahali Ili azibe masikio kwa muda maana mazungumzo ya mama yake yamemchosha na alikuwa hataki kuyatilia maanani hata kidogo "Sasa utakaa kwa mjombaako ukasugue gaga huko mi kwangu sikutaki kabisaa "
Mama anamwangalia mwanae akiendelea kutembea na kumwacha yeye akiongea peke yake kama kasuku,ananyoosha mkono na kumpiga mgongoni binti anaruka kwa mshtuko "aaaa!mama unaniumiza kwani nimekosa nini tena mbona natembea"
"umekosa nini?"wote wanasimama "hujui ulichokosa wewe,wewe tulya wakunifanyia hivi Mimi mama yako,Mimi na masomo wako wote tuonekane hatujakufunza vizuri wewe"
Tulya anamwangalia mama yake kirohoni akiwaza 'ohoooo! tumerudi tena kulekule naona maada hii ni kitafunwa Cha njiani'
Tulya anainama na kutengeneza viatu vyake vilivyoachia kamba akivikaza kwa ajili ya mwendo zaidi,viatu vya ngozi alivyovaa vilivyofungwa kamba za kupindisha pindisha mpaka usawa wa magoti mguu wake mnene ukiwa umekaa sawasawa kwenye kiatu hicho na kumpendeza sketi yake yangozi iliyoishia magotini ikimchora umbo lake zuri alilobarikiwa nyuma na kiuno chake chembamba kilichobebwa na tumbo lake dogo lililokuwa wazi likifuatiwa na kifua chake chenye Saaa sita mbili zilizonchongoka vizuri kifuani pake zikifunikwa na kitambaa Cha ngozi kilichozungushwa na kufungwa vizuri kabisa mgongoni pake kikiacha mabega wazi asingekuwa na furushi mgongoni pake mtu yeyote ambaye angemtia machoni Binti huyu lazima ageuke nyuma zaidi ya mara Moja kumtazama na mwanaume yeyote rijali asingeweza kujihimili pindi akimwangalia,sura yake ikijazwa na macho makubwa mazuri na ya kurembua yenye mboni nyeusi ya kung'ara,pua yake iliyomkaa vizuri ikifuatiwa na lips za ukubwa wa wastani na laini,kichwani akiwa amesuka nywele zake tano za kurudi nyuma zilizomfanya sura yake kuonekana vizuri na kumfanya kuwa msichana mzuri mwenye urembo wa kiasili.
Tulya ni mrembo sana na ukimwangalia vizuri mama yake utaona karibia robo tatu ya urembo wake ameupata kwa mama yake ingawa mama yake ameanza kuporomoka ngozi kutokana na umri na changamoto za maisha ila bado ukimwangalia unaweza kugundua kuwa alipokuwa msichana alikuwa kama Binti yake.
tulya ananyanyua sura yake baada ya kukaza viatu vyake vizuri kwani kwa mtazamo wake safari ilikuwa Bado ni ndefu sana "eeeh" anashtuka baada ya mama yake kumuita kumbe muda huo wote alikuwa akiongea na tulya hakusikia hata Moja "kwa hiyo unanifanya Mimi naongea peke yangu kama mwehu hapa njia nzima unanipuuzia"wanaanza kutembea huku zunde akitengeneza rundo la shanga zake za shingoni zilizokuwa zimevurugana na kutokueleweka mpangilio wake "we tulya si naongea na wewe inamaana hunisikii au" "mama nina kiu kwani bado sana"
mama anamwangalia tulya na kuchukua kibuyu chake kilichokuwa kimefungwa kwa kamba kiunoni na kuning'inia chini anatoa kijiti kilichokuwa kimeziba kama mfuniko kuzuia maji kumwagika anapeleka mdomoni na kuanza kunywa maji, tulya anasimama na kumwangalia mama yake akinywa maji kwa matumaini.zunde anakunywa na kumaliza maji yote tulya anamwangalia kwa mshangao "mama kweli umekunywa maji yote" analalamika tulya huku akijitahidi kukombeleza mate mdomoni mwake ambayo yalishakuwa mazito na kumeza "tembea huko yako ulipokuwa unakunywa kama chura wakati wa masika ulisahau kama Kuna kiangazi kinakuja" wanaendelea kutembea huku tulya akitaka kutokuiacha kabisa maada ya maji kwani alikuwa na kiu sana na mama yake kumnyima maji makusudi kumkomesha ilimuuma sana "ungenipa tone tu"
"bado unanguvu za kuongea kwa ulichokifanya na wakati nguvu za kutembea huna hembu punguza kuongea uhifadhi nguvu za kutembea kwani hii safari Kaisababisha nani kama sio wewe nyamaza huko" tulya anaamua kunyamaza na kuongeza mwendo huku rohoni akiwaza 'niongee shida nisipoongea nako shida oooh!hii safari nayo hatufiki tu'
kwa safari ambayo haikutarajiwa walioianza kwenye mida ya saa nne na hiyo ni baada ya tulya kufanya vitimbi nyumbani kwao Mbele ya wageni waliokuja kuleta posa.
tulya mwenye umri wa miaka ishirini Sasa amekuwa akifanya fujo za Kila aina ili kuwakimbiza wachumba waliokuwa wakija kutoa posa kuomba mkono wa ndoa kwake,amekuwa hataki kuolewa sababu Kila mwanaume aliyekuja amekuwa akimtaka yeye kuwa mke wa pili,sababu kuu ni kuwa umri wa tulya ulikuwa tayari umeshapita kuolewa hivo kumpata mwanaume wa kumchukuwa na kuwa mke wa kwanza ilikuwa ni vigumu.
waschana wengi huolewa wakiwa na miaka kumi na saba mpaka kumi na tisa, baada ya kutoka mafunzo ya mwali.
Waschana wote Wanaingia mafunzo ya mwali wanakuwa tayari wanawachumba hivo pindi wamalizapo mafunzo Moja kwa Moja hufunga ndoa na kwenda kwa waume zao.
lakini kwa tulya hali ilikuwa tofauti kidogo sio kwamba hakuwa na mchumba kabla ya kuingia mafunzo ya mwali la hasha, tatizo lilikuja pale baada ya mwaka Mmoja wa mafunzo nakuambiwa hakufuzu vizuri hivo ikambidi kukaa mwaka mwingine tena ndani na baada ya kumaliza akakuta mchumba ake tayari amekwisha kuoa.
mchumba hakutaka kumwacha tulya alienda na kusema atamuoa mke wa pili tulya alikataa kwani tayari ilikuwa inamuuma sana kwa mchumba wake kumsaliti kushindwa kumvumilia na kumsubiri kwa mwaka mwingine Mmoja vilevile alikuwa hapendi kabisa kuolewa mitala na Luila alilijua hilo na alimuahidi tulya kuwa atamuoa yeye tu.
baada ya tulya kuambiwa akae ndani mwaka mwingine aliamua kuoa akijua tulya akitoka atakuwa Hana namna nyingine zaidi kukubali kuolewa nae sababu umri tayari utakuwa umeenda na tulya alikuwa anampenda sana ila hakujua kuwa licha ya tulya kumpenda hakuwa radhi kuolewa mitala kwani alikuwa hapendi ugomvi wa wake wenza.
Hiyo yote aliiona kwa mama yake mateso aliyokuwa akiyapitia akiwa mke mdogo na wa mwisho kwa baba yake Mzee kijoola kati ya wake zake watatu.
Tulya alimkataa kwa nguvu zote luila,hii ilipelekea luila kuwa katika wakati mgumu kwani alikuwa anampenda sana tulya na hakutaka kumpoteza lakini tayari alishampoteza kwa tamaa zake,alimbembeleza mara nyingi lakini tulya bado alikuwa na msimamo wake uleule wa kutaka kuwa na mwanaume wa kwake mwenyewe,hapo ndipo tabia zingine za tulya zilipoanza kujitokeza ambazo hata mama yake hakuzijua,tulya akawa mbishi na mwenye msimamo mkali asiyetaka kuyumbishwa akitaka afanye maamuzi yake mwenyewe bila kupangiwa na mtu, akawa ni mtu wa kuongea fikra zake kutokujali mazingira gani.
Hiyo ikawa ni vigumu kwake watu wengi walimchukulia kama Hana adabu kwani mwanamke katika jamii hakuwa na lakusema zaidi ya kusikiliza Kila alichoambia na mwanaume au akiwa msichana anachoambiwa na wakubwa wake, lakini kwa tulya ilikuwa tofauti akawa hasikii la mhazini wala la mkwezi kwani alitaka kuwa huru yeye kama yeye.
Hii ilipelekea wachumba wengi kukimbia na waliokuja walitaka wamfanye mke wa pili au waliokuja kwa kumtamani kwa umbile lake zuri, na Kila walipokuja aliangusha kibwanga wanaondoka na hawarudi tena.
Tulya akawa gumzo Kijijini na vijiji jirani ikapelekea kupiga mwaka mwingine nyumbani ambapo wenzake wa umri wake wote waliolewa na walikuwa na watoto na wale wa chini yake nao waliolewa pia wakimuacha.
Sio kama Hali hii haikumsumbua,ilimsumbua sana na wakati mwingine ilimfanya asilale usiku akiwaza ikiwa atazeeka peke yake lakini aliamua kubaki na msimamo wake kwa sababu alijua kwa wakati kama huo akicheza ngoma kwa pupa ataangukia pua.
Hivo akaamua kujifanya hana haraka na kungoja kwa moyo wa uvumilivu kama mtu aliyevuna furu mbichi na kuamua kuzivundika kwenye majivu kwa uvumilivu akisubiri ziive zibadilike rangi kwa utaratibu ziwe nyeusi Ili aweze kula.
Lakini muda haukuwa upande wake kwa kuwa wazazi wake walikuwa na wasiwasi na maisha yake ukilinganisha na tabia yake alioianzisha wakaamua kumletea mchumba kwa kushtukiza asubuhi na mapema kabla hajawa na mpango wa kuwakimbiza.
Asubuhi ya Leo baada ya kurudi kisimani anakutana na umati wa wazee nyumbani wakija kutoa Mahari kabisa tayari kwa ndoa na kilichomchanganya zaidi ni kujua anaolewa na baba wa makamo kuwa mke wa tatu kwa muda Kila kitu alikiona kinazunguka akawa hana ujanja kweli akaona wazazi wake wamempatia.
Baada ya wazee kumwangalia na kuridhika nae wakianza kukubaliana kiasi cha mahari mama yake alimtuma jikoni kuleta togwa kwa ajili ya wageni,alipofika jikoni aliona nguvu zikimuishia na kukaa kwenye kigoda kwa muda machozi yakimtoka asijue cha kufanya,akijuta na ubongo wake ukimpigia makelele kuwa ni bora hata angeolewa na luila aliyekuwa akimjua na kuwa mke wa pili au na kijana yeyote wa pale Kijijini kwao kuliko kuolewa na mwanaume aliyemzidi umri kwa kiasi kikubwa na akawe mke wa tatu.
alijikatia tamaa na kuona Bora afe kuliko kukubaliana na Hali hiyo kwani angekuwa kichekesho kwa marafiki zake.
Akiwa na mawazo hayo anashtushwa na sauti ya mama yake ikimwita apeleke alichotumwa akanyanyuka na kuanza kutafuta kipeo Cha kuchotea ndipo alipokutana na kisonzo kilichokuwa na bamia na mrenda wazo likamjia kichwani akachukua bamia Moja akachanganya na mrenda na chumvi kidogo akatafuna na kutema akachota togwa na kuweka kwenye kipeo kikubwa akatoka.
Wakati anatembea akawa anakusanya mate mpaka anafika kwa wazee mdomo Wake ulikuwa umejaa mate,alipokaribia mama yake akapokea kipeo na kumwambia aondoke kabla hajazua Balaa kumbe angejua ndo alikuwa akilitengeneza.
Tulya akapiga hatua chache na kusikia baba yake akiulizwa kama karidhia Mahali iliyotajwa akaona huo ndio muda muafaka kwani baba yake akikubali tu tayari amekuwa mke wa mtu atake asitake.
Kabla Mzee kijoola hajajibu wakasikia kishindo kikubwa watu wote kugeuka wanamuona tulya yuko chini akitikisika kama tetemeka lililopita kwake tu wengine hawalioni povu likimtoka mdomoni macho yamemtoka kama ndulele mbichi juu ya kichuguu kirefu.
Mama yake anakimbia kwenda kumwangalia na baba yake akiwa ameduwaa kwa muda wazazi wake wakajua mtoto wao karogwa,wazee wakagadhabika wakimlaumu baba na mama yake kutaka kuwawozesha mtoto anayeumwa ugonjwa hatari kama huo "ndio maana hajaolewa mpaka Sasa licha ya kuwa mrembo kumbe anaumwa"alisikika Mzee Mmoja akisema "tuondokeni,hii sio familia ya kuoa kabisa" anaongea Mzee mwingine.
wazee wanaondoka,tulya anasaidiwa na kuanza kufumbua macho na kumuona mama yake akilia na baba yake akiwa amesimama ameshika kiono sura ikiwa na wasi wasi baada ya kumuona mwanae kaamka anasogea karibu na kumwangalia.
Tulya anakaa kitako chini "kalete maji" ilisikika sauti ya Mzee kijoola ikitoa amri zunde pasipokujifikiria mara mbili anaamka na kukimbia ndani kuleta maji.
kule ndani baada ya kuchota maji wakati anatoka akakutana na bamia chini kuangalia vizuri anaona ni mbichi na zimetafunwa akajua Moja kwa Moja kuwa tulya kawapiga tena.
Anatoka kwa hasira akiwa na kipeo Cha maji anafika alipo tulya na kumwagia usoni pwaaa! Kila mtu anashangaa"unafanya nini mama tulya mtoto anaumwa"anaongea Mzee kijoola kwa kukereka "haumwi huyu,ona" anaongea zunde huku akimwonyesha mumewe bamia alizookota chini jikoni "nini hiki" anauliza Mzee kijoola huku akionekana uvumilivu ukimshinda.
Tulya akiwa kimya akijua kakamatwa kwa kuwa alikuwa na haraka akili yake haikumtuma kuficha ule mchanganyiki aliotafuna hivo kufanya Siri yake kuwa hewani kwa muda mchache tu."bamia hizo baba tulya binti yako katafuna kachanganya na chumvi ndio maana ya povu hili lote hapa kaharibu tena mwanao"anafafanua zunde "nini"anabwata Mzee kijoola.
Zunde anashuka chini alipo tulya na kuanza kulia huku akimpiga "umefanya nini tulya mwanangu kwa nini unanifanyia hivi mama yako kwanini lakini,Sasa tutafanyeje safari hii umefika mbali nani atakuoa watu wote watajua unaumwa degedege sijui kifafa hata tukisema sio kweli hawatatuamini hata punje tukufanyeje wewe"
Mzee kijoola anakaa kimya tu akimwangalia mama na mwana pale chini,Mzee kijoola mwenye wake watatu akiwemo zunde akiwa mke mdogo na wa mwisho anawatoto wengi na wote wa kiume,kwa mkewe wa kwanza na mkubwa akiwa na watoto sita na wote wa kiume,mke wa pili akiwa na watoto watatu wote wa kiume na mwisho zunde ambaye alibahatika kuzaa mtoto wa kike mmoja tulya na wadogo zake wakiume wawili hivo kumfanya Mzee kijoola kuwa na watoto kumi na wawili wakiume kumi na Moja na wakike Mmoja.
Mzee kijoola anachoka kwani alikuwa anampenda sana Binti yake hivo alijitahidi kadri ya uwezo wake akapata posa iliyobora kabisa pale Kijijini kumuozesha kwa luila kijana aliyekuwa akigombewa na wengi Kijijini lakini yeye tu ndo aliweza kumpata.
Aliumia sana baada ya luila kuoa mke mwingine badala ya Binti yake kuchelewa kutoka mwali hata hivo bado alikuwa na matumaini baada ya luila kumuahidi kuwa hata mwacha tulya akitoka atamuoa tu lakini Mambo yote yalibadilika baada ya vimbwanga vya tulya kuanza na ya leo imekuwa kubwa kuliko.
"unamfundisha nini huyu mtoto na hao masomo wake pia,hembu ona balaa hili alilolizua nitaficha wapi sura yangu"
uvumilivu wa Mzee kijoola ukafika mimpaka na kuamua kumtumia lawama mkewe na masomo wa mwanae"Mambo yakienda hivi ufanye mpango uondoke wewe na mwanao"Mzee kijoola anatupia kaniki yake begani na kuacha bega moja nje anaelekea ndani.
Zunde kusikia hivo anaacha kulia "Mimi niharibikiwe kisa wewe,hataa haiwezekani kakusanye nguo zako upesi njoo huku nje"anaongea zunde huku akisimama,tulya aliyekuwa ameinamisha kichwa muda wote anatoa macho kwa mshangao inamaana wazazi wake wanamfukuza kweli au? na ataenda wapi? na afanyeje?
Anatolewa kwenye dimbwi la mawazo na mama yake ambaye tayari alishapiga hatua kadhaa kuelekea ndani kwake"haraka" tulya anaamka na kuelekea ndani kwake.
baada ya nusu saa walikuwa njiani kuelekea mpuli ambako wazazi wake waliamua kwenda kumuacha kwa mjomba ake.