Tulya anamwangalia mama yake kwa mshangao "mama hupafahamu"anaongea kwa kunong'ona "shiiiii! kelele bwana unajua Nina siku nyingi sijaja huku" zunde anamjibu Binti yake kwa sauti ya chini huku akimwangalia yule mtu aliyefungua mlango akija karibu Yao "nyie kina nani mnaotafuta watu usiku huu mnene" anauliza yule mtu akiwa tayari ameshafika karibu Yao akijaribu kuwachungulia Ili apate kuona sura zao lakini bila mafanikio kutokana na kiza kizito.
"Mimi ni mdogo wake na huyu ni Binti yangu,najua alikuwa anaishi maeneo haya sijafika siku nyi...."kabla hajaendelea anakatishwa na sauti ya mtu aliyakuwa akiwasikiliza "shangazi zunde!" zunde na tulya wanapata moyo wa amani kuona huyo mtu anawajua "ndio wewe utakuwa nani" "karibuni,kulikoni usiku huu wa manane kwema shangazi" kijana anaacha kujibu swali la zunde anaanza kutoa miti iliyowekwa mlangoni akiwatengenezea njia ya kuingia bomani huku akiwakaribisha kwa furaha lakini moyo wake ukijawa na wasiwasi maswali mengi ya kwanini shangazi yake atembee usiku kwa usiku Kuna tatizo gani.
Kwa upande wa tulya aliona ni kama nyota ya jaaa imemwangazia na kuona shida zake zote zimekwisha,baada ya upenyo wa kuingia ndani kuonekana tulya anajisweka ndani kwa haraka haraka akimpita mama yake na yeye kuwa wa kwanza kuingia huku akivuta pumzi ndefu ambayo ikimwangukia mtu anaweza asiamke siku tatu.
Wanaingia bomani na tulya anamwangalia yule mtu aliyewakaribisha kwa karibu anaonekana ni kijana hivo akili inamtuma Moja kwa Moja kuwa huyo atakuwa ni binamu yake,"karibu shangazi shikamoo" anamsalimia kijana huku akijaribu kukaza macho yake kumwangalia shangazi yake vizuri lakini inakuwa ni vigumu kutokana na kiza "Marhaba hujambo"anaitikia zunde "sijambo shangazi kulikoni mbona usiku" anauliza tena kijana "tumetembea tu haraka hatukutaka kulala njiani ndio maana tumefika usiku"anajibu zunde akizitathimini nyumba nne zilizokuwa ndani ya boma Moja,lakini zikiwa zimeachiana umbali kidogo "nilijua nimepotea pamebadilika sana"anaongea zunde akiendelea kukagua " twendeni huku"anasikika kijana huku akiwaonyesha njia kuelekea nyumba kubwa kidogo kuliko zote na wote wanamfuata "ndio hujaja siku nyingi shangazi kipindi umekuja kulikuwa na nyumba Moja tu hii kubwa,Sasa ziko nne sisi vijana tumeoa na tunajitegemea na ile pale ya sinde analala huko"anaongea kijana huku akionyesha kidole nyumba ya mwisho "kwani wewe nani kilinge au zinge" anauliza zunde akimwangalia kijana "Mimi kilinge" anajitambulisha kilinge "ohh!hapo kweli ninavyomkumbuka zinge hakuwa mwongeaji alipokuwa mdogo labda ajifunze ukubwani" anaongea zinge huku akivuta kidogo taswira ya kilinge na zinge kipindi wakiwa wadogo.
Anamiaka kumi na miwili Sasa hajakanyaga nyumbani kwao mara ya mwisho alipokuja ilikuwa kwenye msiba wa baba yake na baada ya hapo hakupata nafasi ya Kuja tena."vipi sinde nae hajaolewa tu" anauliza zunde akisimama baada ya kufika nyumba kubwa, tulya anaona jiwe lililokuwa chini ya mti anaenda na kukaa hakuwa kwenye Hali ya kubadilishana mazungumzo kilichokuwa kinapita akilini mwake ni maji,chakula akautafute uchago wa kitanda alale kama marehemu aliyeondoka pasipokuacha Mali nyuma.
"bado, lakini anamchumba tayari,ndoa Yao itakuwa mwishoni mwa msimu huuu"anaongea kilinga huku akitembea na kwenda kusimama karibu na kidirisha kidogo nakuanza kuita"baba,baba,baba" anaita mara tatu na kusikilizia "kizinga Kuna nini usiku huu" inasikika sauti ya mtu ndani anayeonekana kukereka kuamshwa usingizini "Kuna mgeni baba" anajibu kilinge kwa adabu "mgeni? usiku huu wa jogoo la kwanza linakaribia kuwika" "ni shangazi baba,shangazi amekuja" kilinga anamjibu baba yake"shangazi?shangazi yako aje usiku huu kafukuzwa au" anajibu baba kilinga sauti ikiwa inakribia kufika mlangoni ikimaanisha alikuwa anakuja "ndio ni Mimi kaka na sijafukuzwa nimemkumbuka tu ndugu yangu nikaona nisilale" anaongea zunde akimhakikishia kaka yake.
mlango unafunguliwa anatoka Mzee wa makamo akiwa na kandili yenye mwanga hafifu akiangaza njee "zunde ni wewe kweli" anauliza Mzee huku akichungulia nje,na zunde pasipo kungoja anasogea karibu na mwanga kumefanya ndugu yake amuone vizuri "mdogo wangu jamani karibu ndani ingia,kulikoni usiku huu huyo kijoola kakufukuza au anajua nimezeeka siwezi kufika huko nitamuua mzima mzima"analalama mzee Shana kwa kujigamba.
Tulya anaamka alipokuwa amekaa na kuelekea ndani,wote Wanaingia ndani na tulya akimalizia Mzee Shana,ambaye hakumuona tulya hapo awali anageuza macho na kumuona "na huyu Binti je" anauliza Mzee Shana,zunde anamwangalia tulya wakati huo tulya akifungua furushi lake mgongoni na kuliweka chini"shikamoo mjomba" anasalimia tulya kwa heshima "Marahaba Binti yangu,mpwa wangu huyo" anaitikia Mzee Shana akimtathimini tulya "ndio binti yangu huyu tulya"zunde anamjibu kaka yake huku akikaa kwenye kigoda kidogo na wengine wakichukua vigoda na kukaa isipokuwa tulya ambaye alikaa chini akikunja miguu yake kwa namna ya kuipishanisha.
Mzee shana uso unamjaa hasira akijua mdogo wake atakuwa kafukuzwa na mumewe na kutembea usiku kwa usiku mpaka nyumbani kwake" huyu kijoola anataka nimuue kweli kabisa atawafukizaje mikono mitupu na kuwafanya mtembee mpaka huku peke yenu naona kanisahau safari..."kabla hajaendelea kutupia lawama kwa kijoola zunde anaamua kumkatiza "sio hivo kaka hatujafukuzwa ni sisi tu hatukumpumzika njiani tungelumzika tungefika kesho mchana lakini kwa sababu tulikuwa wepesi tukaamua kuunganisha tu leoleo" zunde anajieleza lakini kwa akili ya tulya ikimbishia mama yake ndani kwa ndani 'alikuwa ananikomesha mimi mjomba,kaninyima na maji"anawaza tulya hapo ndo anakuja kukumbuka kuwa anakiu anamwita binamu yake "kaka kilinge naomba maji" kilinge ananyanyuka na kuelekea chumba Cha pili ambako kwa harakaharaka tulya alijua ni jiko.
Wakati huo anatoka mwanamke wa makamo akitokea chumba kingine zunde anaamka na kumsalimia kwa heshima akiukunja mguu wake wa kushoto kidogo"shikamoo wifi" "Marahaba wifi yangu za Siku,naona Leo jua linachomozea magharibi" mwanamke anamtania zunde na wote wanacheka "shikamoo mama" wanakatishwa na sauti ya tulya ambaye alishasimama akisalimia kwa heshima kama mama yake "Marahaba mwanangu hujambo" anajibu runde mke wa Mzee Shani na tulya anaitikia kwa sauti ya chini akirudi kukaa alipokaa mwanzo kwa namna ileile "umekuwa mkubwa mara ya mwisho nilipokuona ulikuwa na miaka mitano, umeolewa?" anauliza runde akimfanya tulya ashtuke akijua mama yake lazima alianzishe tena anainamisha kichwa chini asijue ajibu au aache anaokolewa na kipeo Cha maji aliyoleta kilinge anakipokea na kukipeleka mdomoni harakaharaka kupoteza maada.
"usiku huu kwema wifi maana umekuja kama umeleta taarifa ya msiba"anauliza runde akiwa na wasiwasi "nimeshamuuliza kama hivo nikajua kafukuzwa kwake" abadakia Mzee Shana "Kila kitu Kipo sawa jamani tunaweza tukaenda kupumzika tukaongea kesho maana nimechoka kweli"anawatoa wasiwasi zunde,tulya kusikia habari ya kulala anashtuka akili yake ikilipuka 'na chakula je' anajuliza lakini anajipatia jibu yeye mwenyewe kwamba hakuwezi kukawa na chakula usiku huu mnene sio kama walijua kama walikuwa wanakuja wawabakishie chakula lakini akaona ni afadhali amepata hata maji kwani alivyochoka akienda kulala hataisikia hata hiyo njaa.
"kweli kabisa kilinge mpeleke tulya kule kwa sinde akalale wifi naomba nifuate huku"anaelekeza runde.Tulya anasimama na kumfuata kilinge nje na hii ni baada ya kuwatakia wengine usiku mwema.