Chereads / KIZAZI DHALIMU / Chapter 5 - SURA YA TANO

Chapter 5 - SURA YA TANO

Siku ya kujiunga na shule ya upili ilipofika, aliabiri gari na mamake alfajiri na mapema kuelekea mjini Makoma.

Walipofika ilikuwa saa mbili, wakapata safu ndefu ya wanafunzi ambao pia walikuwa wamefika kwa shughuli iyo hiyo ya kujiunga shuleni humo. Wanafunzi waliokuwa karibu na usajili ulipofanyika walichungulia dirishani, walionekana wenye furaha.

Japo alikuwa pale kwa safu, macho yake yalikuwa kwa wanafunzi waliokuwa wakipita karibu yao nia yake kuu ikiwa kumuona Mziwanda. Alipokua akiangazia wanafunzi waliokuwa katika darasa moja, macho yake yalikutana na macho ya Shata akaangalia chini kwa uoga.

"Mwanangu, nahisi miguu yangu haitaniruhusu kusimama nikapita hapa. Ni heri nirejee nyumbani," mamake alimwambia akiketi kwenye fomu iliyokuwa kando yake.

"Lakini mama, huna budi," alitoa lalama akimsogea.

Saa zilisonga, ilipofika saa saba, mamake alimuita mwalimu mmoja akamnong'onezea jambo fulani, mara moja mwalimu aliita mwanafunzi akamuagiza.

Baada ya dakika kama ishirini hivi, Mziwanda alifika.

"Mwanangu, nimekusubiri sana," Bi. Linda alimwambia akiinuka.

"Nimefika mama."

Tumaini alipogeuka na kumuona mwenzake, mara moja alitoka kwa foleni akamkumbatia kwa furaha.

"naomba unisaidie kukamilisha wajibu uliosalia," Bi. Linda alimuomba Mziwanda akifikia mkoba wake mkuukuu akatoa not ya shilingi mia mbili na hamsini, "mamake 'kauza jogoo wako kisha' kanipa nikukabidhi."

"shukrani zangu zimfikie mama," Mziwanda alimwambia akipokea kwa heshima.

"kisha umwangalie mkeo," Bi. Linda alimtania, "ni kanakwamba ameshamuona mwana wa Bw. Makali, uoga umemvaa."

"nitamwangalia mama," Mziwanda alimpa ahadi akifikia mkono wa mwenzake.

Walizungumza machache kisha Bi. Linda akawaaga, machozi yalimtoka alipokumbuka kwamba hatakuwa karibu yake tena. Kwa huzuni alimpungia mkono. Shughuli ya usajili ilienda kwa kasi ikafikia zamu yake.

" fungua sanduku lako," aliagizwa kwa haraka na mwalimu.

Kwa uoga alisonga nyuma, Mziwanda akafungua. Mlikuwemo sare moja, kitana na mafuta. Mwalimu aliangalia vilivyokuwemo akamuagiza asonge kitengo kingine. Kitengo cha pili alipoagizwa kutoa kamusi, kamusi ya kiingereza, seti na vitu vingine vya kusoma alisusuwa. Aliagizwa asonge kando kumpisha aliyekuwa nyuma yake.

"ni mnuna wangu, tafadhali mwalimu, vitu vitaletwa kesho. Leo alitoka kwa haraka asikose nafasi yake," Mziwanda alimtetea.

"usajili utakamilika kesho vilivyoagizwa vitakapokuwa tayari," mwalimu alisusia ombi lake akiandika kwenye kijikaratasi.

Mziwanda kwa ujanja wake alijua hatafaulu asipofanya chochote, akatoa noti aliyekuwa amepewa na Bi. Linda akamkabidhi mwalimu.

'Kweli hongo ni adui wa haki,' Tumaini aliwaza baada ya kuona kitendo kile.

Kwa haraka walisajiliwa, Mziwanda akapewa kijikaratasi kilichokuwa kimeandikwa "cleared" kwa vitengo vilivyokuwa vimesalia.

Kwa furaha, Mziwanda alimsaidia kubeba sanduku mpaka kwenye bweni alilokuwa amepangiwa.

"Maisha huku ni magumu kweli," Tumaini alimwambia akimwangalia usoni kwa imani.

"si magumu hata, siku baada ya nyingine utazoea," mwenzake alimwambia kumpa tumaini.

"shule nzima nakujua wewe na Shata, ila Shata sitaki hata nikutane naye."

"hakuna haja ya kumchukia," Mziwanda alimshauri, "ila kuhusu kufahamiana, utakuwa na marafiki siku zitakavyosonga. Kwanza utakuwa na wenzio wa darasa kisha baadae hata madarasa mengine.

****

Asubuhi na mapema Bw. Makali alipofika afisini, aliwakuta wavyele watatu wameketi nje ya afisi yake. Alipowaangalia, moyoni alihisi kisebusebu. Alipita kwa haraka pasipo hata na kuwasalimu.

"Mwanangu yuko wapi?!" mwanamke mmoja kati yao alimuuliza alipoona anapita bila kuwasalimu.

"Mwana yupi unayezungumzia?!" Bw. Makali naye aliuliza akigeuka na kuwaangalia.

"Mziwanda, mtendakazi wako. Niwie radhi kwa kutojitambulisha mwanzo. Mimi ni Bi. Zena, mamake Mziwanda, huyu ni mume wangu Bw. Rufai kisha mwenzetu ni Bi. Linda, mamake Tumaini."

Bw.Makali aliwapa mtazamo kama anayetilia shaka kujitambulisha kwao.

"Ni miaka mingi Bw. Rufai. Nilipotoka kijijini mpaka sasa," Bw. Makali aliwaamkua baada ya kujitambulisha kwao akawaelekeza afisini.

Bi. Linda na Bw. Rufai walinong'onezana wakimfuata kwa karibu. Walipofika afisini, mwenzao aliwakaribisha wakaketi kwenye makochi yaliyokuwa pale afisini.

"Namlilia mwanangu Tumaini, wiki ya tatu sasa sijamuona, mwanangu wa pekee," Bi. Linda alimlilia Bw. Makali, "tafadhali, mtoeni kituo cha polisi atafute mkewe. Ikiwa ni deni mtachukua shamba langu lililoko kijijini, lakini kwanza muachieni awe huru."

Bw. Makali aliangalia kwa mshangao kama asiyeamini kinachosemwa na mamake Tumaini.

"Mimi sina taarifa kama Mziwanda yuko katika kituo cha polisi!"

"Kipi usichojua kuhusu wafanyakazi wako!"

"Nipo gizani kabisa, ndo' napata mwanga kuhusu haya," Bw. Makali aliwasisitizia, "wakati mwingi mimi humuachia binti yangu kuendesha kampani hili nikiwa kwa shughuli nyingine."

Mara moja alichukua simu akabonyeza nambari fulani kisha akaagiza aliyepigiwa kufika afisini. Baada ya dakika kama tatu hivi, bintiye alifika, alisita akasimama mlangoni alipowaona wageni wa babake. Muonekano wake ilikuwa ishara kwamba alikerwa na uwepo wao pale afisini.

"Huyu ni binti yangu, Shata," babake alimtambulisha kwa wageni wake, "hawa ni wazazi wa Mziwanda na mkewe."

"Saseni," Shata aliwasalimu kwa kuwapungia mkono.

"Hatujambo," walimjibu kwa pamoja, lakini walikuwa washaona dosari katika tabia zake.

"Msitie shaka, hawa ni watoto wa kisasa," Bw. Makali aliwaambia kuficha tabia chanya za bintiye.

"Hakuna neno."

"Atawatembeza mahali hapa kisha mkisharidhia atawapeleka kumchukua Mziwanda. Poleni kwa kutojua kwamba mwenzake yuko katika kituo cha polisi."

"Aka! Mimi nina shughuli chungu nzima, mtaniruhusu nizishughilikie. Labda utamtafuta Rehema," Shata alimpinga babake akatoka akiwa amesonya.

Wageni wake waliangaliana kwa mshangao kwa tabia za Shata mbele ya mzazi wake.

"Hizo ndizo tabia za huku mjini, Mziwanda akiwa hivyo nitamdona na bakora hii kichwani hata katika utu uzima wake," Bw.Rufai alisema kwa hasira baada ya kutoridhika na tabia za Shata.

"Hapana neno, nitamtafuta rafikiye."

Wageni wake waliinuka wakampa mkono wa kwaheri kisha wakatoka nje na kuketi nje wakimsubiri aliyeahidiwa na Bw. Makali.

Pale ndani palionekana penye shughuli nyingi na mabadiliko makubwa. Vyombo vya kiteknolojia vilikuwa vikiingizwa kwa magari makubwa makubwa.

***

Rehema alivyokuwa ameagizwa na Bw. Makali alifika kwa wakati akawakuta wameketi chini ya mti wakizungumza. Alipofika akawaona, Mara moja aliwatambua.

"Shikamo," aliwaamkua baada ya kuwafikia.

"Marahaba mwanangu. U hali gani?" Bi. Zena alimuamkua.

"'MI nipo salama."

Bi. Linda alikuwa akimwangalia kwa makini.

"Wewe ndiye ulinipigia simu kunijuza kuhusu kukamatwa kwa Mziwanda!"

"Ndimi," Rehema alikubali akitabasamu.

"Basi tuondoke, hatuna wakati wa kupoteza," Bw. Rufai aliwaambia wenzake akiinuka tayari kwa safari.

Waliandamana mpaka barabarani wakaabiri taksi kuelekea walipokusudia. Bw. Rufai aliketi kando ya dereva akimuwaza mwanawe, mara ya mwisho alipomuona ilikuwa alipofika nyumbani kwake akiwa na mkewe.

"Mimi ndiye mamake Tumaini," Bi. Linda alijitambulisha kwa mwenzako, "huyu naye ndiye mamake Mziwanda."

"Nimefurahi kuwafahamu, nami ni rafikiye Shata."

"Ah...," Bi. Zena alimaka, "basi mfunze mwenzio staha angalau awe kama wewe."

"Ila nilimfahamu Mziwanda nikiwa chuoni."

"Unamjua Tumaini?!"

"Ndiyo, namfahamu."

"Umesikia lolote juu yake tangu kupotea kwake?!"

"Ndiyo, juzi tumepata taarifa kwamba yupo kisiwani Mawe."

"Mwezi huu kwa upande wangu umekuwa lindi ya shida. Mwanangu kupotea, shamba langu kupigwa mnada na watu wa benki bila kuniruhusu kuvuna chochote, mara mumewe niliyetarajia mengi kutoka kwake kukamatwa pasipo na sababu."

Bi. Linda alipoanza kuhesabu masaibu yake kila mtu akawa kimya. Rehema aliwaza kuwaambia kiini cha kukamatwa kwa Mziwanda lakini akasusia baada ya kusikia shida za bibi yule. Walipokaribia njia ya kuingia katika kituo cha polisi, Rehema aliona gari la Shata likitokea kituoni. Shata alishusha kioo cha gari lake akamwangalia kwa kijicho walipopitana. Walienda mpaka kituoni wakashuka kisha wakaelekea kwenye mapokezi.

"Shikamoo," Rehema aliyekuwa mbele alimuamkua afisa aliyekuwepo.

"Hivi uzionavyo, leo kwa kwa nini hujaandamana na mwenzio!"

"Aka! Yupo kazini, nimewaleta wazazi wa Mziwanda."

"Mfungwa ana wazazi!" Yule askari alishangaa, "dadake 'katoka hapa sasa hivi. Kwa nini hakuja na wazazi wake."

"Haa...!" Bi. Zena alimaka baada ya kusikia kwamba Mziwanda ana dadake, "mwanangu nikamzaa pekee yake."

"Kama hana dada basi yule msichana ambaye m'mekutana naye akiondoka kwa gari ni nani!"

"Sisi hatumfahamu."

Mkuu wa kituo kile alitoka nje baada ya kusikia majadiliano yaliyokuwa yanaendelea kwenye masjala.

"Mnataka nini?!" Aliwauliza kwa amrisho.

"Nimefika kumuona mwanangu," Bw. Rufai alijibu.

"Dadake mfungwa ametoka hapa sasa hivi akasema yeyote asije hapa akatuhadaa."

"But sir..."

"Mziwanda hana ndugu yeyote, tena kufungwa kwake huenda kukafanya ampoteze mkewe," Bi. Linda alimwambia afisa Baada ya wazo kuhusu bintiye kupita akilini.

Pasi na neni jingine, afisa alirudi afisini waliofika kwa ajili ya mfungwa wakasalia hawajui cha kufanya. Bi. Zena alimwangalia mumewe, mara moja Bw. Rufai akainuka na kuelekea kwa afisa aliyekuwa kwa mapokezi akampa ruhusa ya kumuona mkubwa wake.

Kwa uoga, Bw. Rufai alielekea afisini kwa yule afisa akakomoa mlango bila kubisha.

"Unataka nini! Nishakwambia kwamba hakuna kumuona mfungwa yeyote," yule mkuu alimfokea, "now get out before I order you to be put behind bars."

"Lakini huyu ni mwanangu," Bw. Rufai alimwambia kwa heshima, "sina chochote cha kukupa."

"Hapa hatupokei hongo," afisa alimwambia akifikia mkono wake uliokuwa na saa ya dhahabu.

Bw. Rufai hakusubiri kuambiwa akatoa na kumkabidhi kisha yule askari akaagiza Mziwanda aitwe.

"Mwanangu, ukafanya nini kuwekwa gerezani?!" Bi. Zena alimuuliza baada ya kumuona kwenye tundu lililokuwa mlangoni.

"Hakuna mama," Mziwanda alimjibu akitokwa na machozi. Kwa mara ya kwanza Rehema aliona machozi ya mwenzake.

"Mimi babako nilikuonya kufanya kazi mahali pamoja na kisichana kile," babake alimushutumu, "ukasema ni kazi. Mkeo kwa sasa hujui alipo."

"Nikitoka hapa korokoroni, hilo ndilo litakuwa tendo la kwanza kuishughulikia."

"Utatoka vipi?!"

Mziwanda alimtupia Rehema jicho la kupasha ujumbe fulani, wakizungumza kwa dakika chache kisha yule mkuu akaagiza aondolewe.

"Rehema njoo," Mziwanda alimuita alipoona wanaondoka. Aliyeitwa alirudi nyuma akanong'onezewa maskioni kisha akawafuata wenzake.