Chereads / KIZAZI DHALIMU / Chapter 7 - SURA YA SABA

Chapter 7 - SURA YA SABA

Tumaini alikaa nje ya kijumba cha Bi. Tabitha akiangalia watu waliokuwa wakienda katika pilka zao za kutafuta riziki asubuhi. Kando yake kulikuwa na vijana watano waliokuwa wakila gumzo wakisafisha nyavu zao.

"Nilifikiri bintiye Bi. Tabitha atatuauni na hujuma ya Bw. Mfarika," alimsikia mmoja wao akiwaambia wenzake.

"Msichana yupi unayezungumzia..."

"Yule pale, alianzisha madarasa ya kuwafunza wana wetu lakini Bw. Mfarika akamkatiza."

"Nasikia aliponea kukamatwa na vibaraka wake Bw. Mfarika."

"Chifu alikuwa wapi!"

"Alikuwepo lakini hakufanya lolote."

Kwa maneno yale, Tumaini aliondoka asiwasikilize tena, yalikuwa yanamzidishia chuki moyoni. Alienda mpaka upande wa kijumba kile cha makuti. Alipofika aliketi kivulini kumuondokea Tabby aliyekuwa anamjia. Upweke wake ulimrejesha nyuma miaka kadha akiwa katika shule ya upili.

Baada ya majuma mawili ya kujiunga na shule ya upili ya Hodari, ilikuwa kanakwamba alifungulia zimwi lililotaka kumuangamiza.

Asubuhi moja juma la tatu, kinara wa darasa lao alisimama mbele ya darasa lao akatangaza kuwa daftari lake limepotea. Upekuzi ulipoanza miongoni mwa wanafunzi, uoga ulimvamia mara moja. Kinara alipekua madawati ya wanafunzi wawili wa mbele, akaruka madawati mengine mpaka kwake.

"Hebu fungua dawati lako," kinara wao alimtolea amri kwa hasira.

"Aka...mie sina daftari lako," alikana akifungua dawati kisha akasonga nyuma.

Kinara alimwangalia kwa hasira kisha akaanza kupekua dawati lake akitupa vitabu sakafuni. Kwa ghafla alisimama akamwangalia, kisha akainua daftari.

"Hiki ni nini?" alimuuliza akimpigia daftari aliloshikilia usoni, "ukatoa kijijini wivi wa familia yenu kutuibia sisi."

Tumaini alimwangalia kwa mshangao, hakujua atakavyojitetea, kupatikana kwa daftari dawatini mwake ilikuwa ithibati kamili. Machozi yalianza kutoka, kinara wao aliendelea kumzomea. Kisa hiki kilifanya darasa likagawanyika mikondo miwili. Wapo waliomuunga kinara mkono kisha kukawa na waliomtetea Tumaini.

Kwa kiburi kinara alirejea kwenye dawati lake kisha akaanza kufungua daftari lake, baada ya dakika kama mbili hivi alisimama mbele ya darasa na karatasi mkononi. Alimwangalia Tumaini akatoa tabasamu la kumchokoza.

"Kwa labibu, Tumaini," alianza kusoma mbele ya darasa, "ua la moyoni, wangu habuba. Tangu ulipoondoka juzi usiku kurejea shule nimekumisi...hope to see you soon..."

Wanafunzi wote waligeuka wakamwangalia kwa mshangao;

"Nimemisi kuona mato yako yenye ulegevu wa mahaba..." kinara alikatizwa na rafikiye Tumaini kwa jina Terry.

"Hapana, namjua Tumaini kutoka tulipoingia humu shuleni," Terry alimtetea mwenzake aliyekuwa amefunika macho kwa aibu akilia. Tumaini alihisi macho ya wenzake yakimchoma kama mkuki uliochoma maini.

Siku hiyo ilipokamilika alishukuru Maulana akifikiri labda ilikuwa tu sadfa. Huo ndio ulikuwa chanzo cha masaibu yake pale shuleni. Siku zilivyosonga ndivyo matatizo yalivyomuandama kama mjalaana.

Siku moja rununu ilipatikana katika dawati lake iliyoishia kutalikiwa majuma mawili na shule yake. Alipotoka nyumbani alipata fununu kwa Terry kwamba simu kupatikana katika dawati lake ulikuwa mpango wa Shata. Alipopata ujumbe, alienda akamtafuta Mziwanda na kumweleza yaliyokuwa yanaendelea.

Wakiwa wanazumgumza, mlangoni alisimama mwalimu wa zamu na Shata kando yake.

"Njooni," mwalimu aliwaamuru, "shuleni mlikuja masomo siyo mapenzi."

Pasipo na kupewa nafasi ya kujieleza, walitolewa mpaka afisini wakaadhibiwa, siku iliyofuata jina lake lilikuwa kati ya wanafunzi walioruka ua wa shule kwenda kukutana na wapenzi wao, hili lilifanya akaandikiwa talaka ya wiki mbili na mwalimu mkuu.

Kabla hajaondoka alienda kutafuta Mziwanda, mwenzake alipopata ujumbe, alimchukua mpaka katika afisi ya mwalimu mkuu. Hapo walikesha kwa masaa matatu wakimuomba mwalimu msamaha kutomtuma nyumbani. Mwalimu alikubali ombi la Mziwanda baada ya kupewa mlungula wa elfu mbili.

"Usingempa hela hizo," Tumaini alilalama walipokuwa wanaondoka.

"Ni heri kumpa hela kushinda wewe kwenda nyumbani."

"Thanks for care."

"For one day I'll need yours too," Mziwanda alimwambia kama utani lakini akiwa anamaanisha alichosema.

Alimsindikiza mpaka darasani mwake kisha akaondoka, alipokuwa anapita karibu na darasa la kina Shata, alimkuta mlangoni akiwa amesonya.

"Nimewaona," Shata alimwambia alipoona anapita bila kusema lolote.

Alisimama akamwangalia kwa sekunde kadha kisha akaondoka bila kusema lolote. Maisha yaliendelea vivyo hivyo akawa anaangamia siku moja na kuokoka nyingine mpaka Shata alipokamilisha mtihani wake wa kidato cha nne na kuondoka.

***

Mazonge hayakumpa nafasi ya kufanya chochote pale afisini, hakuamini kwamba Shata alitaka kumpindua babake kibiashara alivyokuwa amemweleza kwa kinywa chake. Alishika kalamu kujaza fomu fulani lakini kalamu ikamtoroka mkononi. Tangu alipotoka gerezani alikuwa amejifanya kibaraka wa binti wa bosi wake ili mwenzake asiwe na wahka juu yake.

Siku iyo hiyo ndiyo aliyokuwa amepanga kupatana na Ali kujadiliana naye kuhusu safari ya kuelekea kisiwani Mawe kumtafuta mkewe.

Kwa mara ya kwanza, Shata alipomsemea nia yake ya mageuzi pale kwenye kampani la babake alichukua kama mzaha, lakini kwa wakati huo alianza kuona ukweli ukidhihirika.

Miondoko kati ya Shata na sekritari wa babake ilikuwa imezidi kushinda hapo awali, wakawa wanaonekana na mwekahazina wa lile kampani wakinong'ona chemba, kisha mwanasheria wa lile kampani akawa anamtembelea kila jioni afisini mwake kwa siku tatu mtawalia.

"Hasidi hana utu," alijisemea alitikisa kichwa kama asiyekubaliana na mawazo yake.

Alimjua Shata kama banati mtukutu lakini hakutarajia tabia hizo kuvuka mipaka mpaka kwa babake aliyemuamini kama mboni ya jicho lake. Mawazo yale yalimkosesha amani. Nafsi yake ilimsuta kwenda kumshitaki kwa Bw. Makali na kumweleza kilichokuwa kinaendelea mgongoni mwake, lakini akahofia kwamba huenda mpira ukadunda akatupwa gerezani kwa mara nyingine.

"Ndugu wakigombana, shika jembe 'kalime," alisema akitikisa kichwa, "... no, hilo si zuri kabisa. Ni kweli kwamba rafiki anaweza kuwa adui kama adui anavyoweza kuwa rafiki kwa wakati mmoja."

Alipoangalia saa yake ya mkononi, ilikuwa saa tano thenashara, akachukua koti lake na kutoka kwa haraka. Alienda mpaka afisini kwa bosi wake akiwa na nia ya kumweleza njama ya mwanawe. Alipofika afisini na kumuamkua bosi wake, maneno yalimkauka kinywani kwa sababu alijua Bw. Makali hangemuamini.

"Mziwanda, nakusubiria. Nina kazi nyingi za kufanya kama uonavyo," Bw. Makali alimwambia baada ya kumuona kimya.

"Sir...it's about y...our daughter," Mziwanda alimwambia kwa uoga.

"What about her! Kama ni mizozo yenu 'kasuluhisheni wenyewe, mshakuwa watu wazima."

"Hapana boss, anapa...," Mziwanda alikatizwa kwa mlango uliofunguka kwa ghafla kisha mwekahazina, Bw. Baraka na bintiye wakasimama mbele yao.

Wote walivaa nyuso za wasiwasi, maongezi yaliyokuwepo kati ya mtu na bosi wake yalikatika wote wakawaangalia waliofika.

"Kuna nini kati yenu?" Bw. Makali aliwauliza baada ya dakika mbili, wote wakanyosheana vidole vya lawama.

"I was in the process of transferring money from company account and she interrupted!" Bw. Baraka alijitetea.

"Hapana baba, ni ujinga wake tu," Shata alimtukana mwekahazina mbele ya babake, "he has transferred 200,000, 000 instead of 20000. We have tried to retrieve the process but it has failed."

"Umenifilisi mwanangu..."Bw. Makali alimlilia,"badala ya kutuma elfu ishirini umetuma milioni mia mbili...hiyo kandarasi haitarudisha hata nusu ya pesa hizo. Nendeni benki."

"Hakuandika hundi, ilikuwa through electronic money transfer," Shata alimfahamisha babake.

"Basi niitieni bwana Mkombozi, tupeleke kesi mahakamani."

Wote waliinama kwa heshima kisha wakatoka, kabla ya kuondoka, Shata alimpa Mziwanda mtazamo wa kumkashifu.

Baada ya kuondoka kwao, Mziwanda alianzisha mazungumzo na mkubwa wake lakini akaambiwa arudi baadae.

***

Shata alimwangalia mwenzake kwa jicho la chuki, alijua kilichokuwa kimempeleka katika afisi ya babake. Mziwanda hakupendezwa na uamuzi wa mwenzake, lakini hakuwa tayari kumweleza.

"Pilipili usiyoila yakuashiani!" Shata alianza kumtenda.

"Ah! Mimi niliamua kuwa mkweli," mwenzake alijitetea.

"Ukweli wako hautakufukisha popote. Unajua kilichotokea kati ya wazazi wangu mpaka babangu kupata mali anayoogelea ndani kama ziwa!"

"Hapana."

"Basi usiingilie uamuzi wangu. Baba akiwa na mamangu, walichuma mali hii wakiwa pamoja, ila baada ya muda usiokuwa mrefu wakatalakiana baada ya baba kugundua kwamba mamangu alikuwa kirukanjia," Shata alimsimulia mwenzake kwa uchungu, "mamangu alikuwa akichepuka na mmoja wa rafiki za babangu."

"Lakini hi..."

"Usinikate usemi," Shata alimkatiza mwenzake, "baba alimtaliki pasipo na huruma. Mamangu alianza kuishi na mchepuko wake ila baada ya vipesa vyake kuyeyuka kwa anasa, mwenzake alimtoroka. Alirudi kwa mumewe kuomba radhi lakini baba akala yamini kutomsamehe, wakati huo nilikuwa mdogo wa umri lakini yote nilijionea na kuyaelewa. Siku moja mama alifika nyumbani lakini akazuiliwa kuingia na babangu, alitoka langoni machozi yakimtoka, hiyo ndiyo ilikuwa siku yangu ya mwisho kuonana naye. Kwa muda usiozidi juma ndipo tukahamia kijijini kwenu baba akiwa na nia ya kumuondokea kabisa."

Baada ya Shata kumaliza masimulizi yake, machozi yalimtoka, hapo ndipo Mziwanda akajua chanzo cha tabia chanya za mwenzake akijua alirithi kutoka kwa mamake na tabia zake za kufanya uamuzi wa haraka bila kufikiri matokeo yake.

" Nipe nami sababu ya kutomtenda uroho aliomtenda mamangu," Shata alimwambia mwenzake akicheka kicheko cha uchungu.

"Usiwe mwepesi wa kufanya uamuzi mzito namna hiyo," Mziwanda alimshauri, "nakushauri kumtafuta mamako kisha upange watakavyopatana kwa maongezi. Kwa sasa, nafikiri babako atamuelewa kwa sababu wakati huo alifanya uamuzi kwa hasira. Nijuavyo ni kuwa babako anakupenda na kwa sasa anaona ungali mdogo kutua usukani wa kampani lenu."

"Hayo ni ya kwako. Safu niliyonayo itanisaidia kuendesha kampani hilo kwa ustadi mkubwa mno nawe ukiwemo," Shata alimtupia jicho.

"Usiamini insi yeyote kati yao," Mziwanda alimuonya, "kama wameamua kumuangusha babako, kuna asilimia kubwa kwamba huenda nawe wakakusaliti."

"Hayo ni yako."

"Ushauri ni mgeni, ukimpokea atakesha usiku kucha, ila usipompokea anaondoka dakika iyo hiyo."

Walipokuwa wanaendelea na safari ndipo wazo lilipompitia akilini kwamba alikuwa na miadi na Ali. Mara moja alimwambia mwenzake aliyempeleka mpaka kwa sahibu yake kisha akaondoka