Chereads / KIZAZI DHALIMU / Chapter 9 - SURA YA TISA

Chapter 9 - SURA YA TISA

Mziwanda alikuwa amesimama kando ya lori lililokuwa likipakiwa bidhaa kwa masaa matano. Kibegi chake mgongoni kilimka kama nundu ya ngamia, alimuona dereva wa lori alilosubiri kama mtu asiyependa urafiki wa kushtukiza kama wake.

"That cartoon contain fake batteries," alimsikia dereva akimwambia mwenye duka, "rudisha huo mzigo, sitaki lawama."

"Nami niliponunua nilipewa bidhaa feki, mchakato lazima iendelee vivyo hivyo mpaka kwa mtumiaji. Usipozipokea unataka nimuuzie nani!"

"Rudisha ulikonunua, kwa sababu mimi sitampelekea bidhaa hizi."

Mwenye duka hakuweza tena kushindana naye, akamuita kwa ishara ya mkono kisha akamnong'onezea maskioni. Dereva alionekana kuridhia alichoambiwa akaruhusu mzigo kupakiwa

Mizigo ilipomaliza kupakiwa ilikuwa saa mbili za usiku, dereva akagurumisha gari kisha akarudi dukani akapewa hela kisha akarudi garini tayari kwa safari.

Mziwanda kwa haraka aliingia garini tayari kwa safari aliyokuwa amesubiri kwa hamu, alikuwa amesusia kupokea simu za Shata na babake mchana kutwa akijua labda atapata mwito utakaomkatizia safari yake. Alipoketi, alimwangalia dereva aliyekuwa makini usukani.

"Naitwa Mziwanda," alijitambulisha kwa mwenzake.

"Nimefurahi kukufahamu," dereva alimwambia na kuwa kimya.

"Nawe ni nani?"

"Katika mapatano kama haya, kufahamiana na mwenzio si jambo la msingi kwa sababu huenda msipatane tena," dereva alimwambia akimpa mtazamo wa kumuarifu akae kimya.

Mziwanda alinyamaza baada ya kuhukumiwa, aliangalia nje akaona waja walivyokuwa wakiendesha shughuli zao kanakwamba ndipo kulikuwa kunapambazuka.

"Ukimpata mwanangu mwambie mamake anamsubiri," maneno ya Bi. Linda yalimpita akilini alivyokuwa akiongea akitokwa machozi.

"Mimi napendekeza hata ungeishi kuko huko unakoelekea, achia Shata jiji lake," mamake alimshauri, "huenda mkaondokea majanga yake. Kutoka utotoni mwana hasemezeki. Mwanangu, nataka uwe salama hata kama utakuwa mbali nami, lakini heri nijue mpo salama, si huko mjini maisha ya kubahatisha kama mchezo wa simbi."

"Nami mwanangu nakutakia safari njema," babake aliongeza alipokuwa anaondoka.

Walimsindikiza mpaka kwenye njia kuu alipoabiri gari akawa acha wakimwangalia kwa macho ya machozi.

Alipofika mjini alipitia kwa rafikiye walipozungumza mpaka saa nane kisha wakaelekea kule ambako angeabiri la kumpeleka mpaka alikotaka, hapo waliagana na mwenzake naye akasubiri kuanza safari. Kimya cha mle garini kilimpa nafasi ya kukumbuka alivyopatana na Rehema.

Alikuwa anaandmana na rafiki zake baada ya vipindi vya mchana, Rehema alitokea katika duka moja lililokuwa kando ya lango akafika na kuwaamkua kwa furaha. Baada ya salamu, alimshika mkono na kumvuta kumuondoa kwa wenzake.

"Nataka niwe nawe chemba," Rehema alimwambia baada ya kusonga hatua kadhaa kutoka kwa rafiki zake.

"Kuhusu nini?!" Alimuuliza kwa mshangao.

"Sahibu yako Ali, ningependa kujua kama kwa sasa una nafasi."

"Labda saa za jioni, kwa sasa naelekea chumbani kufanya kazi fulani."

Walibadilishana nambari za simu kisha wakaagana wakiahidiana watakapopatana. Mwendo wa saa kumi na mbili za jioni, Rehema alimpigia simu kumfahamisha kwamba ashafika walipoahidiana. Kwa haraka, aliondoka kuelekea alikoagizwa na mwenzake. Alipofika mkahawani akamuona Rehema na Shata alijua maongezi yao hayatafua dafu.

"Nimekusubiri tangu saa kumi na moja," Rehema alimwambia akivuta kiti kumkaribisha.

"Subira huvuta heri," alimwambia akimsalimu.

"You need something and is available, go for it. Sometimes we don't have to be patient," Shata alimwambia katikati ya kicheko. Rehema aliagiza vikombe vitatu vya kahawa.

"Nimekuita hapa kwa sababu wewe ndiye rafiki mkubwa wa Ali," Rehema alimwambia mhudumu alipokuwa anaanda kahawa mezani, "kwa sasa hasemezeki. Hasikii la mwadhini wala mteka maji msikitini. Nimemuonya zaidi ya mara moja kujihusisha na mambo ya siasa akakata. Anasema hawezi kusikia lolote kutoka kwa jinsia ya kike."

Mziwanda na Shata walijikuta wanacheka kwa lalama za mwenzako.

"Ni kweli, Ali si mtu wa kusikiliza sauti ya kike ila anawajali sana."

"Anatujali kwa namna gani ikiwa hata maingiliano yake na wenzake wa darasani hunirusha roho."

***

Mziwanda alimwangalia akamsikitikia kwa sababu alikuwa hajazoea "ustaarabu" wa chuoni.

Ustaarabu ambao kwa upande wake ulikuwa umevuka mipaka. Maingiliano kati ya watoto wa kike na wa kiume pale chuoni haikuwa na mipaka, jambo ambalo lilisababisha tabia hasi kuenea kama moto nyikani. Alijua vijana wengi waliokuwa "mumunye aliyeharibikia ukubwani" baada ya kufuata msemo wa kiingereza usemao, 'when you go to Rome, do what Romans do."

"Kijijini kwetu, msichana akipatikana amesimama na mvulana, kijiji kizima kitajua, ila hapa mambo ni kinyume. Hata watu wakapeana busu mbele ya hadhira, tena mbele ya wanaowazidi umri, ukijitenga na tabia zao utaitwa mshamba."

"Acha tabia za kijijini, staarabika aisee, kutakuwa na tofauti ipi kati yako na yule msichana wa kijijini," Shata alimwambia kumshusha hadhi.

"Akah! Kama huo ndo ustaarabu wa chuoni, basi heri kutostarabika," Mziwanda alimtetea Rehema kwa mwenzake.

"Nawe una mpenzi?" Rehema alimuuliza baada ya kushindwa kujizuia.

"Ndiyo," Shata aliropoka, "ana mpenzi kutoka shule ya chekechea mpaka chuoni. Kwa kifupi, she's a village girl."

"Am proud of her, because she's well mannered, not like other girls who are immoral even to their on parents," Mziwanda alijivunia mpenzi wake mbele ya wenzake.

Shata alimwangalia kwa kijicho kwa sababu alijua ndiye aliyelengwa na maneno yale, Rehema alipoangalia wenzake na kuona mara moja anga imebadilika, alibadili mada ya maongezi.

"Hayo siyo yaliyotuleta. Nilitaka kuzungumza nawe kama tu naweza kufanya lolote Ali arejee shule."

"Sina matumaini kama kuna lolote, sheria ishachukua mkondo. Kubadili uamuzi wao ni kama kuzuia mvua kwa utandabui."

"Kwa sababu huko nje ni kuangamiza tu talanta yake na utu kwa jumla. Ashaanza kutumia sigara, ukimuuliza atakwambia kwamba anajiondolea mawazo."

"Nitakuja ku..."

"Hamjambo," Mziwanda alikatizwa kwa sauti ya kike iliyotokea nyuma yake. Hata bila kugeuka, alijua sauti iliyotokea kwa heshima na adabu ni ya Tumaini.

Shata alipomuona Tumaini, aliinuka mara moja tayari kuondoka. Kutoka usoni, ungesoma dharau dhidi ya yule aliyewaamkua.

"Siwezi kuwa katika kikao na mtu ambaye hajastarabika, kuwa mjanja kama wenzako," Shata alimumwagia Tumaini maneno.

"'mi nimekosea wapi?!" Tumaini alimuuliza Mziwanda kwa mshangao.

"Achana naye."

"Haya yote yametokea wapi!" Rehema aliuliza kwa mshangao, "huyu ndiye mpenzi wako."

"Ndiyo..."

"Nitaacha kwanza mzungumze," Rehema aliwaambia akichomoa katika pochi lake noti ya shilingi mia tano na kumpa muhudumu.

"Bad company ruins good morals," Mziwanda alimwambia alipoona anaondoka.

"Sawa..."

Kumbukizi ilikatizwa na dereva aliyemgusa kuashiria ashuke garini.

Alipoangalia mbele yake, aliona wapo ufuoni mwa ziwa, mbele yake palikuwa na motaboti mbili zilizofika kusafirisha mizigo mpaka ilipotakikana. Dereva alishuka akaenda kuzungumza na mmoja kati ya wale waliokuwa wamefika kwa boti, kisha baada ya dakika thelathini akaondoka na kumuacha Mziwanda katikati ya watu asiofahamu.

Mizigo ilipakiwa kwa haraka kisha akaamurishwa aingie katika mmojawapo ya boti zile tayari kwa safari.

"Tuondokeni haraka tusikamatwe na askari kwa sababu leo hajatupa chochote cha kuwapa," nahodha alimwambia mwenzake, "nawe utaachwa kwa Bw. Mazoea usiku huu, kwa sababu bosi hapendi kuona tukiandamana na wageni katika biashara zake wala hapendi wageni kisiwani."

Mziwanda aliitikia kwa kichwa kukubaliana na matakwa ya mwenzake kisha wakang'oa nanga.