Asubuhi na mapema Rehema alifika kazini, lakini mtazamo aliopewa na askari mlangoni hukumpa furaha. Kwa haraka alimpa mkono kumsalimu kisha akafululiza mpaka ndani.
"Habari za asubuhi," alimuamkua mwanadada aliyekuwa kwa mapokezi.
"Njema, labda za kwako," alijibiwa na yule msichana ila si kwa furaha ilivyokuwa kawaida yake.
"Haupo salama kabisa," Rehema alimpinga, "hebu nieleze, hii si kawaida yako."
Kwa yale maneno, mwenzake alisalia kimya akionekana mwenye mashaka. Kwa haraka alipanda vidato kuelekea afisini mwake. Alipofungua mlango, afisi hiyo ilionekana ngeni sana kwake, vitu vyake vilikuwa vimepangwa katika kona moja. Baada ya sekunde kadha za kushanga, aliona labda ilikuwa tu kazi ya yule aliyefanya usafi mle ndani.
Aliketi kitini akaanza kazi yake kwenye tarakilishi, alianza kwa kukamilisha kazi iyokuwa haijakamilishwa. Kwa haraka, alifikia daftari jeusi lililokuwa mezani akitaka kuangalia biashara zilizoendelea baada ya kuondoka kwake, akiwa anapekuapekua daftari, kwa ukurasa mmoja alipata ujumbe uliomrusha roho.
"What's the meaning of this?!," alijiuliza kwa mshangao, "nini maana yake!"
Aliteremka vidato kwa haraka kuelekea katika afisi ya meneja wa lile benki. Alienda mpaka kwa katibu wa meneja na kutupa kijikaratasi kilichoandikwa;
"kwanzia sasa, hatuhitaji huduma yako."
"Nini maana yake!"
"Tulia, punguza hasira," katibu alimpoza.
"Nataka kuonana naye, nimefanya nini cha kunitia kitanzi namna hii!"
Katibu alichukua simu akampigia bosi wake akimfahamisha kwamba Rehema alitaka kuzungumza naye. Aliyakwepa macho ya mwenzake, baada ya kuzungumza kwa simu, Rehema aliondoka hata bila kungoja taarifa ya mwenzake kama ombi limekubaliwa au la.
Alipofika afisini, alimkuta meneja ameketa akionekana mwenye wasiwasi.
"Nini maana ya hiki kikaratasi?!" Rehema alimuuliza akikitupa mezani kwa hasira.
"" Kuwa mpole Bi. Mdogo," meneja wake alimtuliza.
"Kwa nini ukiwa umenitia kaa la moto mgongoni..."
"Jana ulikuwa wapi?"
"Wewe mwenyewe ulinipa ruhusa nikaondoka baada ya kupata mwito wa Bw. Makali, babake Shata."
Meneja alitikisa kichwa kama asiyekubaliana na maneno yake.
"Nafikiri mkataba wako na benki hii umefika mwisho," meneja alimwambia akimwashiria aketi.
"But...sir, I still have six months," Rehema alijitetea, "my contract is supposed to expire next year April."
Bila kusema neni jingine, meneja alitoa kitabu cha sheria na ma sharti ya lile benki akamuonesha sheria moja iliyokuwa imewekewa kinyota na sharti lake.
*manager has full authority to discontinue any contract with any worker if he/she is found to be incompetent and worker has to comply to any decision made whether he/she is favored or not.
Baada ya kusoma kifungu kile, Rehema alicheka kwa sauti, mwenzake akamwangalia kwa mshangao.
"Siku moja tutatia sahihi sheria na masharti yanayoruhusu viongozi wetu kutumia ujira wetu pasi kuulizwa," alijisemea baada ya kukumbuka alivyotia sahihi kwa haraka alipopewa karatasi lile, "lakini mimi nimefanya kazi yangu vizuri zaidi ya wote humu ndani!"
"Ujira wako ni ghali mno ilhali una astashahada tu," Meneja alitoa kisingizio.
"Lakini bwana wangu, nina mkopo. Nitaulipa vipi ikiwa nitaachishwa kazi!"
"Hilo si tatizo la...," meneja alikatizwa kwa simu yake iliyokiriza mezani.
Alisita kupokea baada ya kuona aliyempigia, Rehema alipoona jina la Shata, alijua ndiye chanzo cha yote. Alitoka akafunga mlango kwa kishindo akiondoka, alijua kwamba kama mwenzake ndiye chanzo chake kufukuzwa kazini, mle ndani hakuwa na lake.
"Vipi nitamaliza kulipia nyumba niliyonunua...mama na baba je! Wadogo wangu watasoma vipi...kweli dunia haina urafiki wala huruma," alijisemea akielekea afisini mwake kupakia vitu vyake tayari kuondoka.
***
Tumaini aliketi kando ya msingi uliokuwa umeanza kujengwa akiongea na Tabby. Kwa ghafla mwenzake alinyamaza akamuonesha kwa kidole waliokuwa wakija mbele yao. Kwa haraka aliamka akaenda mpaka palipokuwa pamejengwa kuwasubiri. Wajenzi walipofika, mmoja wao alitoa ramani mkobani akaanza kuwaonesha wenzake waliomsikiliza kwa majini.
"Hamjambo," aliwaamkua kwa pamoja.
"Salama, labda zako," aliyekuwa na ramani alimjibu.
"Samahani kwa usumbufu. Naitwa Tumaini."
"Tumefurahi kukufahamu."
Tumaini alisimama kwa muda baada ya kushindwa atakavyooanza kusema yaliyomsukuma pale. Wenzake walimwangalia kwa mshangao, kisha aliyekuwa na ramani mkononi akawaagiza wenzake kuanza ujenzi.
"Nani akawaruhusu kujenga mahali hapa," Tumaini alimuuliza yule mkandarasi baada ya kusonga karibu yake.
"Ukaniuliza swali hilo kama nani?" alijibiwa swali kwa swali.
"Nilipewa nafasi hii na chifu niwe nikiendeleza madarasa ya watoto, kwa hivyo ujenzi wenu utazuia shughuli zangu."
"Bw. Mfarika ndiye akanipa idhini ya kujenga mahali hapa klabu kwa manufaa ya jamii nzima."
"Asante kwa taarifa yako," alimwambia yule mkandarasi kisha akaanza kuondoka.
Akiwa anaondoka, alimuona Bw. Mazoea akiwajia na Tabby akaridhika. Bw. Mazoea alipofika palipofanyika ujenzi, aliwaamkua wajenzi kwa heshima.
"Nilimuomba Bw. Mfarika asiitumie nafasi hii," Bw. Mazoea alimwambia yule mkandarasi kwa sauti isiyo imara."
"Dakika chache tu kisha atakuwa hapa nanyi," mkandarasi alimjibu chifu akiandika kwa karatasi lililokuwa mkononi.
"Sir! Aren't you doing anything to stop this?!" Tumaini alimuuliza baada ya kumuona kimya.
Wakiwa wanazungumza, Bw. Mfarika alifika kwa gari lake jeusi akiwa ameandamana na askari wawili. Baada ya kushuka, alienda mpaka alipokuwa mkandarasi akaanza kuzungumza naye."
"Mkamateni,"Tumaini aliropoka baada ya kushindwa kuvumilia uchungu uliomzidia,"anatumia mali ya jamii kwa manufaa ya kibinafsi."
"Huu si ubinafsi," askari mmoja alipinga, "anajenga klabu hii kwa manufaa ya jamii nzima."
"Klabu kina manufaa yapi kwenye kisiwa kama hiki ila kuleta "ustaarabu"."
"Watu watapata ajira, pia patakuwa mahali pa kustarehe baada ya kuchumia juani mchana kutwa."
Bw. Mfarika alielekea palipokuwa na mvutano kati ya Tumaini na askari.
"Msichana, kipi kinakukanganya?" alimuuliza Tumaini akimvuta kando.
"Maendeleo yapi isipokuwa kuharibu jamii nzima. Najua vilabu, hapa kuna watoto wengi watakaopotoshwa na watakavyoona.
"Infact, I am trying to uplift the retarded economy of Mawe Island, it will be a tourist attraction."
"Kuweni na maono ya vizazi vijavyo, msijiangalie tu. Uozo utaenea kote kote, elimu humfungua mtu kutoka kwa minyororo ya utumwa. Angalieni wana wenu na wajukuu wao," Tumaini aliwageukia askari waliokuwa nyuma yao.
Bw. Mfarika alipoona Tumaini hasikizwi na yeyote, alitua noti ya laki tano akaweka mkononi mwake. Kwa haraka Tumaini aliachilia ikaanguka mchangani.
"Hilo ni kosa, kutoa kadhongo," askari mmoja alimwambia Tumaini akimsogea tayari kumtia pingu.
Alimwangalia yule askari kwa mashaka, alijua mbwa alitaka kuficha maasi ya msasi. Bw. Mazoea alisonga hatua chache mpaka alipokuwa Tumaini akawaomba asifungwe. Baada ya tukio lile, askari na Bw. Mfarika waliondoka kwa gari.
"Sheria ni utandabui, huwanasa wadudu pekee yao," Tumaini alimwambia akimfuata, "askari hao wanafurahia hongo kukandamiza jamii nzima ya kisiwa hiki pamoja na wana wao."
***
Mziwanda aliandamana na Shata mpaka afisini mwa mkurugenzi wake, japo walikuwa wanatembea pamoja, kila mmoja alionekana kutomfurahia mwenzake.
" Karibu sana mwanangu," Bw. Makali aliwaamkua akimkaribisha Mziwanda kwa furaha.
Kwa pamoja walivuta vitu wakaketi baada ya kumsalimu Bw. Makali. Kutoka alipokuwa ameketi, alikuwa akichunguza manthari yake, mazingira yale yalionekana mapya kwake.
"Hongera kwa hatua uliyochukua," Mziwanda alimpongeza Bw. Makali baada ya macho yake kuridhia na kila alichoona ndani ya lile kampani.
Bw. Makali aliwaangalia vijana waliokuwa mbele yake kwa shauku, japo walikuwa wamefika pamoja, wote walionekana wasio na furaha.
"Sorry for being arrested without my knowledge," Bw. Makali alimpa pole, "nini haswa kilichotokea mpaka ukakamatwa!"
"Sh...," Mziwanda alinyamazishwa baada ya kukanyagwa na mwenzake.
"Usihofu kunieleza, mimi ni kama babako."
"Yalikuwa mambo yao ya nyumbani," Shata alimhadaa babake mbele ya mwenzake, "hawezi akamwaga mtama penye kuku wengi."
"Lakini wazazi wake..."
"Haswa kufungwa kwake kunahusiana na kupotea kwa mkewe."
Bw. Makali alinyamaza akawatupia jicho kisha akaendelea na kazi aliyokuwa anafanya kabla ya ujio wa wageni wake.
Alikuwa alifanya hesabu aliyoonekana kumkanganya akili.
"let's embrace digitality with our souls and mind," Mziwanda alisoma maandishi yaliyokuwa kwenye kibao fulani mezani.
"Ndiyo mwanangu, ulimwengu unabadilika. Nasi lazima twende na wakati tusiachwe nyuma."
"Lakini ni heri ungefanya mabadiliko katika vitengo fulani tu kuona jinsi utandawazi utaendana nasi, haya mabadiliko ya kushtukiza ikiwa shida itatokea unahatarisha kuporomosha kampani lako."
"Kati ya wafanyakazi wangu, hakuna aliyefikiri kama wewe, wala hakuna kufu yako," Bw. Makali alimwambia akimpa mkono kwa pongezi, "ila watu wote wamekuwa katika vipindi vya kufunzwa jinsi ya kufanya kazi na mashine haya kwa siku mbili mtawalia, sitaraji kosa lolote kutokea."
"Siku mbili ni chache mno kuzindua kitu kipya na kuanza kufanya kazi, heri ungetafuta wataalamu au watu wenye uzoefu wa mambo ya kidijitali waje wafanye nao kazi wakiwafunza hatua moja baada ya nyingine."
"Gharama mwanangu!" Bw. Makali alilalama, "kwa siku mbili nimetumia laki saba...pesa nyingi mno, ila kurudi kwake wenyewe watagharamia. Kila mmoja alikuwa katika vipindi hivyo, kuanzia kwangu mwenyewe mpaka kwa chura aoshaye vyoo."
Shata alimwangalia Mziwanda kwa macho ya kuashiria waondoke, wakazungumza machache na bosi wao kisha wakamuaga. Nje ya afisi ndipo Mziwanda alipotambua msukosuko uliokuwepo. Watu walionekana kama waliopigwa na mawimbi ambayo hawakutarajia.
Walizunguka bila mpango baada ya wengine kushindwa kufanya kazi walizopewa.
Baada ya Mziwanda kuchunguza yale mazingira kwa muda, alitambua mabadiliko makubwa mno, watu wengine waliokuwa wakifanya kazi katika afisi walikuwa kwa kazi za kunadhifu mazingira baada ya kazi zao kubanwa katika afisi moja na hata wengine waliokataa kushushwa vyeo wakaachishwa kazi baada ya kupewa hela asilimia ndogo za kustaafu.
'Yajapo yapokee,' Mziwanda aliwaza baada ya kuona yale.
***
Alipokuwa ameketi alionekana mtulivu lakini kichwani alikuwa na mengi yaliyomsumbua. Baada ya kupoteza kazi kwa benki, maisha yalikuwa magumu. Pale mjini mtu aliyekuwa karibu yake kwa wakati huo alikuwa Ali, kumbukumbu ya jinsi walivyopatana chuoni ilimrudia.
Baada ya kuingia chuoni chaTini, mchakato wa masomo ulianza baada ya majuma mawili.
Asubuhi moja wakiwa darasani wamemsubiri mhadhiri, waliingia vijana watatu wa kiume waliovalia nadhifu. Wawili wao walikuwa wamevalia suti nyeupe, mashati mekundu na tai nyeusi, kisha yule wa tatu alikuwa amevalia suruali iliyofika kwa muundi, t-shati iliyoonekana kumpwaya na viatu vya kijeshi.
Wenzake pale darasani walianza kunong'ona kwa sauti za chini wakiwangalia waliowasili. Wageni wao waliwanyamazisha kwa ishara ya mikono, kisha baada ya kimya kutanda, wakanza kujitambulisha.
"Mimi mtanifahamu kama Peter Mbewa," mmoja kati ya waliovalia suti alijitambulisha, "ni mkuu wa idara ya kiswahili."
"Aaaa...!" Wenzake walishanga, "haiwezekani."
"Nami ni Mike Kisiga," wa pili alijitambulisha, "mimi ni mkuu wa idara ya Sayansi Jamii."
Waliohutubiwa walipiga makofi kwa furaha, lakini Rehema kwa upande wake alitilia shaka nyadhfa zilizotajwa na wageni wao.
"wanaonekana wadogo mno," alimwambia msichana aliyeketi kando yake, "siwaamini asilimia mia moja, au ndiyo wale wajifanyao wahadhiri kunasa mabanati wageni humu chuoni wasio na hatia."
Aliyeambiwa alionekana asiye na hamu ya kumsikiliza, macho yalikuwa jukwani. Rehema alipoinua kichwa, macho yake yalipatana na yule kijana wa tatu, kutoka kwa muonekano wake alimchukua kuwa mtundu. Bila kupoteza hata sekunde, mwenzake alimkonyezea jicho, naye kwa haya akaangalia chini.
"Nami ni Ali Sudi," yule wa tatu alijitambulisha, "mimi ni mkuu wa maktaba. Ukifika maktabani uniulizie popote utanikuta."
Wanafunzi wote walimwangalia kwa mshangao, walianza kuondoka kisha baada ya hatua mbili Ali akawasimamisha wenzake na kuwanong'onezea ujumbe fulani.
Walisita kisha aliyejitambulisha kama mkuu wa idara ya kiswahili akatoa kikaratasi mfukoni, alisoma majina kisha akaagiza mabanati waliosomwa wawakute nje. Rehema alikuwa miongoni mwa wale waliosomwa, akainuka kwa uoga na wasiwasi. Hayo ndiyo yalikuwa mapatano yao ya kwanza.
Kadri siku zilivyosonga ndiyo alivyozidi kumuelewa Ali. Kwanza alitambua kwamba wote hawakuwa katika nafasi walizotaja, ila walitumia mbinu hiyo kuwanasa.
Alijua kwamba Ali hakuwa mtukutu alivyomchukulia kwa mara ya kwanza, alikuwa kijana mkarimu na mwenye kuwajali wenzake hata zaidi yake mwenyewe, sifa iliyosababisha kutalikiwa kwake chuoni. Urafiki wao ulizidi kunoga siku baada ya nyingine akawa anamuonea wivu alipomuona karibu na binti yeyote.
"Urafiki na ukaribu wako na hao mabinti wa chuo sipendi kabisa," Rehema alimwambia siku moja katika baadhi ya mafaraghano yao, "nahisi watakunyakua wafanye unisahau kabisa."
Ali aliposikia maneno yale alicheka kwa sauti iliyomdhalilisha akainuka kwa hasira tayari kuondoka lakini akazuiliwa.
"Ni vyema kuwa na marafiki," Ali alimwambia baada ya kicheko, "kuwa mpweke si hali nzuri."
"Sijataja kuwa marafiki ni wabaya, ila lazima urafiki uwe na mipaka. Kukumbatiana, busu za mara kwa mara na salamu za kila wakati sipendi kabisa."
"They are not more than you when it comes to relation, neither are you than them," Ali alimwambia, kwa hasira aliinuka akaondoka. Siku nzima akazima simu asitake kusumbuliwa na yeyote.