Chereads / KIZAZI DHALIMU / Chapter 3 - SURA YA TATU

Chapter 3 - SURA YA TATU

Tumaini alipoketi alionekana mwenye mawazo mengi, mwenyeji wake alimsogea pole pole akitumia mkongojo wake, akasimama kando yake nukta kadha hajanza kuzungumza naye, Tumaini hakuwa ametambua uwepo wake.

"Umeamka salama kweli?!" Bi. Tabitha alimuuliza kwa toni ya wasiwasi.

"Ah! Mama, shikamoo," Tumaini alimuamkua akionyesha mshituko.

"Sasa ni saa nne, lakini hujaanza vipindi vyako," mwenyeji wake alimkumbusha jukumu lake.

"Labda leo wapate mapumziko, aah...jana alikuwa!"

"Nani?"

"Bw. Mfarika, 'kaniambia nijiunge na shule yake. Nami kwa sababu nilijua azma yangu ya kuanzisha vipindi nilikataa lakini makataa hayo yalifanya akanionya."

"Jihadhari naye mwanangu, ni insi mui. Amewatenda mengi wanakisiwa hiki."

"Nimekusikia mama. Itanilazimu basi niache vipindi hivyo, huenda vikanizalia karaha. Mimi mwenyewe mtawa humu."

"Nitazungumza na chifu wetu, labda tutapata msaada wake. Umekuwa taa kwa watoto wetu, huna haja ya kufunika mwanga kwa sababu ya upepo uvumao."

Baada ya maneno yale, Bi. Tabitha alianza kuondoka kisha kando yake Tabby akatokeza na kopo la uji.

"Leo tumechelewa kuanza vipindi vyetu," Tabby alimwambia baada ya kimya cha sekunde kama tano hivi.

"Maamkuzi kwanza kabla ya chochote maana we," Tumaini alimkumbusha.

"Bibi amenda kwa Bw. Mazoea, lazima anaenda kuzungumza naye juu ya Bw. Mfarika."

"Amefanya nini cha kumzungumzia?."

"Si mwema anavyoonekana chini ya kofia yake na miwani."

"Kwa nini?"

"Yeye pekee hujitakia makuu kisiwani humu. Hataki kuona mtu yeyote akipiga hatua kumzidia. Atamtolea matisho ya barua au afanye kila jitihada kubadili taswira yake katika jamii."

Tumaini alimsikiliza Tabby kwa makini, japo alikuwa mdogo wa umri, alijua mengi kumzidia.

"Alifanya mwanabiashara mmoja aliyekuwa amepanga kuwekeza katika kisiwa hiki akatoweka asionekane tena. Yupo mwanabiashara alinunua shamba ufuoni, akaanza ujenzi mara moja. Lakini kila kukicha vifaa vyake vya ujenzi na raslimali zilikuwa zikipotea, na nyakati zizo hizo ndizo ambazo alijenga shule lake, watu wakasema mali ya yule mwekezaji ndiyo aliyotumia."

"Basi kwa nini watu wasiungane wakamtimua!"

"Ana wale wanaomuunga mkono kwa lolote," Tabby alimjuza, "kuna wazee wanne ambao wanao aliwapeleka mjini kutafuta riziki, hawaruhusu baya kusemwa kwake."

"Wanakisiwa wote wameamua kutawaliwa na vichwa vitano."

"Bw. Mazoea alitishiwa siku moja kwamba huenda akapoteza bintiye alipoanza kufuatilia habari za yule mwanabiashara niliyekufahamisha."

Baada ya maneno yale, kila mmoja alikuwa kimya, Tabby alipiga mafunda ya uji huku Tumaini akiwazia aliyosimuliwa.

***

Tumaini alipokuwa amelala, usingizi ulimpiga chenga akasalia kugaagaa kama mtu aliyeumwa. Mbalamwezi ilipenyeza mwanga mpaka alipokuwa. Tabby aliyekuwa kando yake alikuwa amelala fo fo fo, alikumbuka jinsi mjo wa Shata katika kijiji chao ulibadili maisha yake kwa kiwango kikubwa.

Siku moja aliandamana na Mziwanda kuelekea kwa kina Shata kucheza. Shata alipowaona, alienda akamvuta Mziwanda naye akasalia amesimama kama mlingoti. Mziwanda na Shata walianza kucheza kwa furaha.

"Njoo tucheze," Mziwanda alimuita baada ya kumwangalia na kuona alivyokuwa ametokwa na machozi.

"Aka! Shata atanifukuza," alikataa mwito wa mwenzake.

Mziwanda alichukua kigari kimoja walichokuwa wanachezea akampelekea. Shata alipoona vile, aliinuka akaenda na kumsukuma akanguka jiweni.

"Simtaki kwetu," Shata alimwambia Mziwanda, "sitaki kucheza naye."

"Lakini ni mwenzetu," Mziwanda alimtetea akimuinua, "muache acheze nasi."

"Ondoka," Shata alimwambia akinyakua kigari alichokuwa amepewa na Mziwanda, "we' ndiye tuendelee kucheza."

Alianza kulia akamlalia Mziwanda begani.

Shata alimvuta Mziwanda kumuondoa lakini mwenzake akakata kumfuata.

"Humfanyii vizuri," Mziwanda alimwambia Shata akijitoa mikononi mwake.

"Basi nawe kama hutaki kucheza nami ondoka kwetu."

Mara moja Mziwanda alimshika mkono wakaanza kuondoka. Shata alisimama akiwaangalia na vidude vyake mkononi.

"Basi shika," Shata alimwambia Tumaini akimnyoshea kigari.

"Nenda 'kachukue," Mziwanda alimshauri.

"Atachukua tena," alikataa wakiendelea na mwendo.

Maisha yaliendelea kuwa hivyo mpaka walipofika madarasa ya juu. Mziwanda alipokuwa katika darasa la nane, Shata alikuwa darasa la saba, naye akawa darasa la sita.

"Sifurahi kumuona karibu yako," alimwambia Mziwanda siku moja walipokuwa wanaelekea shuleni.

"Hakuna ubaya wowote akiwa nami," Mziwanda alimwambia katikati ya kicheko, "siwezi kumtimua, sote tunatoka mahali pamoja."

"I always feel insecure," Tumaini alimwambia akisonya kwa utani, "always feeling nitakupoteza kwake, kwa sababu hiyo sitaki uwe ukitangamana naye kila mara. Kumbuka tulikoanzia tukiwa wadogo."

"Nime...," kumbukizi zilikatizwa kwa sauti iliyotokea kando yake.

"Ndiyo, tunapaswa kujenga hapa zahanati, karibu na boma la Bw. Chifu tujenge shule wanetu watakapoenda kusoma," Tabby aliamba katikati ya usingizi akionesha kwa ishara ya kidole, "bosi alipata hundi wiki iliyopita kutoka kwa wafadhili wa benki la Vienna. Hundi ya shilingi milioni mia mbili."

"Tabby! Tabby," Tumaini alimuita akimtikisa kwa nguvu.

"Ndiyo, alipata lakini ninachoona kwa sasa ni vyuma vya ujenzi, simiti na mawe ya ujenzi vinavyopelekwa kwake. Hana mpango wowote wa kuanzisha ujenzi wa miradi tuliyokusudia."

"Makubwa haya," Tumaini alitikisa kichwa kwa maneno yale.

***

Jua lilisalimu siku mpya kwa furaha, nyuso zote mle ndani ziling'aa kwa furaha. Walikusanyika vikundi vidogo vidogo wakila gumzo kwa furaha. Mziwanda alifika katika manthari yale mwendo wa saa mbili, alikuwa amevalia suruali ndefu ya khaki na shati la mikono mirefu lilichorwa maua.

"How I wish my wife was here to witness this occasion," alijisemea kwa masikitiko.

Alipita akiwasalimu wenzake waliokuwa kwa mazungumzo ambayo hakujua kiini chake, alipomuona Shata mbele yake alipita njia nyingine kumuondokea. Alipokuwa anaelekea afisini alimuona Rehema mbele yake kitu ambacho hakikuwa kawaida kuonekana masaa yale.

"Leo umeniwahi," Mziwanda alimwambia akimpa mkono kwa salamu.

"Ndiyo, lazima nami nihudhurie uzinduzi wa Destined Logistics mpya," Rehema alimwambia kwa furaha.

"Unakaribishwa."

"Asante," Rehema aliitikia alianza kuondoka.

"Hundi itakuwa tayari saa ngapi?."

Rehema alimwangalia kwa mshituko, kisha upande mwingine kuepuka macho yake.

"Rehema nazungumza nawe," Mziwanda alimfikia.

"Itakuwa saa tano, laki...," Rehema alikata maneno yake akiangalia alipokuwa Shata.

Rehema alimwangalia mwenzake kwa wasiwasi kisha akaondoka kuelekea alipokuwa shoga yake. Mziwanda aliendelea na safari yake mpaka afisini akaanza shughuli zake. Kule nje, Rehema alimvuta Shata kumuondoa kwa wenzake akitaka kuzungumza naye.

"Unafikiri unachofanya ni cha haki kweli!" Rehema alianza akionekana mwenye wasiwasi.

"Nimefanya nini..."

"Kumtia Mziwanda mashakani."

"Hayo yanakuhusu vipi!"

"Waangalie, washafika kumchukua kwa sababu ya kutumia hundi feki."

"Huhitaji vidonge kwa ajili ya maumivu ya mtu mwingine," Shata alimwambia akimuondokea.

Rehema alipoona gari la polisi limeingia ndani ya kampani, alichukua simu akampigia Mziwanda. Mziwanda alipoona simu inakiriza na mwenzake ni Rehema, alisusia kuchukua kwa sababu alijua mwenzake anataka kumpa maneno ya uongo. Simu iliita mpaka ikakata. Pasipo na kukata tamaa, Rehema alimwandikia ujumbe mfupi.

"Unakujiwa na askari, kuna shida ilitokea kwa hundi uliyonikabidhi siku mbili zilizopita.

Mziwanda aliposoma ujumbe aliingiwa na kiwewe, mara moja akampigia.

" Shida ipi ilitokea," Mziwanda aliuliza baada ya simu kupokelewa.

"It was a fake cheque, am coming to explain right away," Rehema alimwambia kisha akakata simu. Mziwanda akiwa angali anawazia mazungumzo yake na Rehema, mlangoni palibishwa.

"Karibu," aliitikia kwa wasiwasi.

Mlango ulifunguka kisha askari akasimama mbele yake, baada ya sekunde kadha, wakili wa Bw. Makali aliingia kisha mlinzi wa benki.

"You are under arrest for trying to fraud Mr. Makali according to the cheque you deposited on 5th May 2021 at 13:00pm at Goodwill bank."

Mziwanda hakuwa na la kuongea, akaacha machozi yatoke. Mara moja alitiwa pingu wakaanza kuteremka vidato, wakiwa kwenye kona kutoka nje, alimuona Rehema. Alisimama kuzungumza naye lakini akasukumwa mbele kwa haraka. Aliingizwa ndani ya gari la polisi kisha wakaanza kuondoka, alipokuwa anatolewa ndipo mgeni aliyekuwa anamtarajia alikuwa anaingia kwa msafara wa kama magari ishirini hivi.

***

Mbele ya umati ule uliojaa wafanyakazi wa Destined Logistics waliketi wanaume watatu. Bw. Makali, aliyekuwa mkurugenzi wao, akafatiwa na mzungu mnene, kisha upande wa kushoto pakawa na kijana mmoja wa kiume aliyevalia suti ya samawati.

Watu walinong'onezana kwa sauti za chini, wengine wakamwangalia Bw. Brownson kwa mshangao.

"Anaonekana mwenye hadhi ya juu," Shata alisikia sauti ikidai kutoka alipokuwa ameketi.

"Akha! Mi' kwa kawaida siwapendi wazungu, hutuchukua sisi waafrika kama vinyago tusiojua lolote," sauti nyingine ilidai.

"Si wote, acha kasumba."

"Angalia maandalizi aliyofanyiwa, angekuwa mwafrika mwenzetu hata Bw. Makali hangetumia zaidi ya laki moja. Huyu kwa sababu ni mtu wa kutoka "majuu", nimesikia kwamba ametumia milioni tano."

Bw. Makali aliinuka kitini, umati ukawa kimya, hakuna aliyeshubutu kusema lolote.

"Namkaribisha Bw. Brownson mara moja, muda ushatupa kisogo. Hatuna budi kuendana nao kwa kasi," alimkaribisha akimpa mkono.

Watu walipiga makofi mkurugenzi wao alipompisha mgeni wao jukwani, makofi yalipigwa kwa dakika moja mfululizo kabla aliyekaribishwa hajawanyamazisha kwa ishara ya mikono.

"Kwa majina ni Bw. Michael Brownson, nafanya kazi na kampani la kiteknolojia la Natius Technologies lililoko na headquater zake nchini Uholanzi," mgeni wao walianza kuhutubu, "wengi hapa mlipo mshasikia mengi kuhusu sayansi na teknolojia, wengi wakawa na mtazamo hasi kwa kuzihusisha na nguvu za kishirikina."

Watu walimwangalia na kumsikiliza kwa makini, wengine walichukua vitabu vyao vidogo vidogo wakaanza kunakili.

"Kutoka kwa karne za nyuma, kumekuwa na mabadiliko na maendeleo makubwa katika nyanja zote za maisha," aliendelea, "kuanzia mawasiliano, usafiri, biashara, elimu, matibabu na sehemu nyinginezo. Haya yote ni kwa sababu ya uvumbuzi wa kisayansi unaofanyika kila siku, leo nimefika kuwapa manufaa ya sayansi. Iwapo mtakubaliana na maneno yangu na mkubwa wenu kukumbatia sayansi na teknolojia, mtawapiku wenzenu pakubwa."

Baada ya maneno yale, watu walianza minong'ono ya chini kwa chini, askari waliokuwepo waliangaza macho kama kamera za kunasa wahalifu.

"Sayansi imetuwezesha kuishi kama ndugu dunia nzima," Bw. Brownson alianza kupigia debe sekta yake, "imefanya kazi kuwa nyepesi zaidi kwa kuunda mashine ambazo zitachukua nafasi za binadamu siku zijazo. Robots are taking over work done by men in advanced countries."

Mdogo wake alionyesha mwanga kwenye kitamba cheupe kisha pakatokea filamu. Ilionesha jinsi mashine alizorejelea zilikuwa zikiendesha kazi katika jiji moja na ndege za vita zilizokuwa zikiendeshwa pasipo na rubani na kuvamia maelfu ya wanajeshi.

Bw. Brownson alipoona filamu imeng'ata akili za wenzake, alinyamaza kwa sekunde kadha. Filamu ilikamilika baada ya sekunde arubaini, yule kijana akazima mtambo kisha mhutubu akaendelea.

"Si hayo tu, yapo mengi, kwa sababu ya teknolojia tunaweza kushare mawazo yetu kutufaidi na kutukuamua hata zaidi. Sayansi ni mungu wa pili."

"Aaah...," umati ulimaka.

"Nisikilizeni kwa mara ya mwisho. Mitandao ya kijamii imetuwezesha kufahamu mengi kutoka kwa nchi za nje, si kukumbatia tu utamaduni wetu uliopitwa na wakati na usiotufaidi chochote. Tusiwe watu wa kuogopa mabadiliko na mapinduzi ya wakati, tutaachwa nyuma na wenzetu, asanteni kwa kunisikiliza. Sasa ni wakati wa maswali. "

Umati mzima ulikuwa kimya, wengi walikuwa na maswali lakini wakakosa ujasiri wa kuuliza na jinsi taswira zao zitakuwa miongoni mwa wenzao kwa kuwa watasemwa washamba. Baada ya dakika kama nne hivi za Bw. Brownson kusimama pasipo na swali, alivuta kitu tayari kuketi. Mvulana mmoja katikati ya umati akainua mkono na kusimama.

"Mimi nionavyo mitandao ya kijamii imeleta uozo katika jamii," alitoa maneno yake kwa ushujaa, "mengi ambayo vijana tunaona katika mitandao imetufanya tuwe vipofu wenye macho. Tunaona uozo lakini tunaufumbia macho na kukumbatia. Katika filamu, tunaona watu maarufu na mashuhuri wakivalia nguo za kike, herini maskioni na kupaka rangi midomoni. Una maoni yapi kuhusu hayo!"

Bw. Brownson alitikisa kichwa kupinga hoja ya kijana yule.

" Wao hufanya hivyo wapate mauzo zaidi ya filamu zao na miziki," alimpinga, "wala si kila kipatikanacho mtandaoni ni cha kuigwa, wala mimi sijaona mwanamziki yeyote akiwa unavyosema."

"Huo uvumbuzi unaozungumzia nafikiri umetuongezea majanga mengi kushinda faida. Wanasayansi kwa sababu ya" akili" wakaishia kutengeneza magonjwa badala ya dawa. Majaribio ya utafiti wao wakafanyia kwa binadamu au mnyama na matokeo yake yakawa ndwele badala ya tiba," mvulana mwingine aliinuka bila hata ruhusa.

Aliyeulizwa alikaa kimya, hakujua namna ya kubadili fikra za msemaji wa maneno yale, alijua yaliyosemwa ni kweli lakini alikuwa pale kwa kusema uzuri wa sayansi na kuficha maovu yake.

"Sir! Sorry for interruption," banati mmoja naye aliinuka, "and our phones sometimes mislead us. When updating applications. Kama biblia, utakuta mistri mingine imedondoshwa. Biblia za simu ni tofauti kwa kiwango, haya yakiendelea hivi vizazi vijavyo huenda visimjue Mungu wao kwa sababu ya kupotoshwa na sayansi na teknolojia"

Mvulana mmoja aliinuka lakini kabla hajasema chochote akaketizwa na mkurugenzi wao aliyeona mgeni wake ameshindwa kujibu yale maswali ya kwanza na kuongea jingine litakuwa kama mzigo. Alisimama akatoa hotuba ya kufunga kikao kisha baada ya kama dakika tano kila mtu akaondoka.