Tumaini aliketi nje ya nyumba ya Bi. Tabitha akiota Jua asubuhi, aliangaza macho akaona nyumba nyingi za msonge. Palikuwa na nyumba moja ya mabati mekundu iliyojengwa kwa mawe. Kilichomshangaza zaidi ni kuwa, kisiwa kile kilikuwa mali ya jamii nzima, hapakuwa na mipaka ya kuonyesha umilisi wa mashamba ya watu binafsi.
"Naitwa Tabby," mjukuu wa Bi. Tabitha alimfikia na kumsalimu akijitambulisha.
"Nami naitwa Tumaini," Tumaini akijitambulisha akifikia kikono chake.
"Jina hilo ni la kupanga au ndilo ulilopewa na wazazi wako?!"
"Ndilo nililopewa, ni zuri au!"
"Ndiyo, nimelipenda. Je! Ukitoka hapa tutaenda nawe unakotoka, 'mi maisha katika kisiwa hiki siyapendi," Tabby alilalama, "sipati kwenda shule kama watoto wengine, nataka niende huko mjini nione magari, ndege, ninunue nguo nzuri, viatu, nimjengee bibi nyumba kisha nimnunulie ndege."
Tumaini alimwangalia kwa upendo, alifurahi aliposikia yaliyokuwa akilini mwake, lakini mwenyewe alijua huko alikotaka mambo hayakuwa mepesi alivyofikiri.
" Nyumba ile ya mabati mekundu ni ya nani?," Tumaini alimuuliza.
"Ni ya Bw. Mfarika, ndiye mwenye duka lililoko kule," Tabby alimweleza,"watoto wake hutoka kila asubuhi kwenda shule. Nataka niwe kama wao. Utanipeleka huko...bibi husema hana hela za kunipeleka shule."
"Ndiyo, nitaandamana nawe. Unataka kuwa nani ukiwa mkubwa?."
"Nataka niwe daktari, nitibu watu kama bibi, ila sitaki kutumia dawa za kienyeji kama yeye. Wakati mwingine huangalia watu wakifia mikononi mwake kwa sababu ya kushindwa kuwatibu."
'Mtambua ndwele ndiye mganga,' Tumaini aliwazia baada ya kusikia maneno ya kitoto kile, kilikuwa kidogo lakini kilikuwa kishatambua ndwele za kila namna katika jamii yao.
"Huu mkufu wa dhahabu ukatoa wapi?," Tabby alimuuliza akifikia mkufu uliokuwa shingoni mwake.
"Nawe utamuudhi mgeni kwa maswali na ujuaji wako," alivutwa akaondolewa na bibiye kabla hajajibiwa.
"Shikamoo mama," Tumaini alimuamkua akiinuka.
"Marahaba mwanangu, unaendelea vipi?."
"Niko salama, naendelea kupata nguvu na kupunguza maumivu."
"Nimefurahi kusikia hayo."
"Ameniambia kwamba hajaanza kuhudhuria vipindi vya shule!"
"Ndiyo mwanangu, hela za kumpeleka 'mi sina."
"Mamake yuko wapi?!"
"Mamake akapotelea mjini kwa kazi za uyaya, akirudi huonekana hata dhaifu kushinda alivyoondoka."
Walipokuwa wanaendelea na soga yao, wanakisiwa walipita pale wakiwaamkua kisha wakaenda katika kazi zao za kila aina.
Wengi wao walikuwa wavuvi, walipita na suruali kuukuu wakiwa wamebeba nyavu zao kwenda kutafuta riziki.
"Kati ya marafiki wa kweli, hata maji ya kunywa pamoja ni matamu," Tumaini alimwambia Bi. Tabitha baada ya kuwaona vijana fulani wa kiume.
"Ndiyo, usinihukumu mie. Nimekosa leo nitapata kesho, Mungu ndiye mpaji riziki, hana mawaa. Wanafurahia kazi waliyorithi kutoka kwa baba na babu zao."
"Ni hivyo, ila nimefurahia umoja wa jamii hii."
"Haya basi tuondoke," Bi. Tabitha alimshauri akimshika mjukuu wake tayari kuondoka.
***
Baada ya Bi. Tabitha na mjukuu wake kuondoka, Tumaini alisalia pale kwenye jabali akimfikiria mumewe na maisha yao ya mapenzi yalipoanzia.
Alikumbuka jinsi baada ya Mziwanda kucharazwa viboko na mwalimu alianza kuondoka kwa haraka, alikimbia akamfikia, akashikilia mkono wake kwa mikono miwili.
"Naogopa kwenda pekee yangu," alimwambia akiwa amemwangalia usoni kwa wasiwasi.
"Nipishe mie," Mziwanda alimwambia akijinasua, "unaiona nilivyoumizwa juu yako."
Bila neno jingine, alianza kuondoka. Tumaini alipoamuangalia usoni, alimuona anaonekana aliyeghadhabika. Aliinama chini akaanza kulia, baada ya sekunde kadha hivi, alihisi mguso begani, alipoinuka na kumuona Mziwanda amemnyoshea mkono alifarijika.
Walianza kuondoka kila mmoja akiwa kimya, Mziwanda alitembea kwa mwendo wa kasi kumzidia kulikofanya awe anakimbia na kutembea kwa wakati mmoja.
Mkono wa kulia wa mwenzake ulikuwa umeshika daftari lake na kaptura iliyotishia kuanguka, kisha mkono wa kushoto ukamshikilia. Baada ya kufika njia panda, Mziwanda aliacha mkono wake naye bila kusema lolote akaonesha njia ya kuelezea kwao kwa kidole, alipoamuangalia usoni alisoma mshangao uliojiandika.
"Nasi kwetu ni kuku huku," Mziwanda alimwambia akifikia mkono wake. Naye alimwangalia kwa tabasamu, akaanza kumfuata, walienda sako kwa bako mpaka kijijini kwao.
Kwa furaha alimpungia mkono kumuaga kisha akaondoka. Alipofika nyumbani kwao alimkuta mamake ameketi nje ya nyumba yao akionekana mwenye wasiwasi.
"Mwanangu! Leo ukachelewa ukifanya nini?!" mamake alimuuliza akimshika shavuni kwa utulivu baada ya kuona michirizi ya machozi.
"Nilipigwa na wavulana tusomao nao," alimwambia mamake akilia.
"Pole mwanangu, kesho nitakupeleka mwenyewe usipigwe tena."
"Mvulana aliyenisaidia nimemuachia pale," alimwambia mamake akimuonesha kwa kidole.
"Huyo ni Mziwanda, mvulana wa Bi. Zena."
"Aka! Hata mimi simfahamu."
Walianza kuelezea huko, walipokaribia alimuona mwanamke fulani mwenye umbo la kifaru na mwanawe wakiwa wamesimama, alimuona mwenzake akiwa amelazwa chini ka kucharazwa viboko.
"Huyu mwanao ana tabia mbi," alimsikia yule mwanamke akinung'unika, "mpige ndiposa apate adabu. Samaki mkunje angali mbichi."
Baada ya kucharazwa na mamake viboko kama saba hivi, Mziwanda alitorokea nyuma ya nyumba yao alikolilia.
"Kuna nini kumpiga mwanao?!" Mamake alimuuliza Bi. Zena baada ya wale asiowafahamu kuondoka.
"Ameniambia kwamba mwanangu 'kamvamia mwanawe barabarani wakirejea nyumbani."
"Hayo si kweli, mwanangu amenieleza kwamba mwanao ndiye akamuokoa kutoka mikononi mwa wavulana waliokuwa wamemvamia."
Tumaini aliwaacha wakizungumza akazunguka nyumba mpaka alipokuwa Mziwanda, lakini mwenzake alipomuona alimuondokea. Alimsogea kwa mara nyingine lakini matokea yakawa yale yale, akiwa mwenye huzuni aliondoka akamuendea mamake kisha wakaondoka.
" Amekataa kuongea nami," alimwambia mamake, "nimeenda alikokuwa akaondoka."
"Labda ni kwa sababu ya hasira tu, atapoa mwanangu. Usitie shaka kwa hilo," mamake alimpa imani.
Alimwangalia mamake usoni na kutabasamu akitarajia aliyoambiwa kuwa ya kweli.
***
Yalikuwa masaa ya adhuhuri, Mziwanda akiwa anapanga afisi yake akiwa tayari kuondoka kuelekea mkahawani angalau kushitaki njaa iliyokuwa imemkaba, alisikia mbisho mlangoni.
"Ni masaa ya chamcha," alijibu akiwa tayari kuondoka, "kazi baadae."
Alifikia komeo ya mlangoni lakini kabla hajafungua ukakomolewa kwa nje kisha Shata akasimama mbele yake.
"Waambaje mpenzi," Shata alimuamkua kwa sauti ya kulegeza.
"Unataka nini?," alimuuliza akionekana mwenye maudhi, "bado hujaridhia, ungali unanigandia."
"Yote ni kwa sababu ya mapenzi."
"Mapenzi! Mapenzi! Mapenzi! Unajua mapenzi?! Mapenzi yapi ya kunidhulumu mimi na kukandamiza nafsi yangu."
"Nitaondoa kizingiti chochote kitakachozuia kukupata," Shata alimwambia.
"Mimi kwa sasa nina mke, masihara yako sitaki, ni heri unieleze aliko mke wangu au...," aliinua mkono kupiga kofi lakini akasusia.
"Hata ukinipiga, sitahisi vibaya kwa sababu wewe ndiye haluwa ya moyo wangu."
Mziwanda alipita kando yake tayari kuondoka, lakini akazuiliwa.
"Basi nimekuachia," Shata alimwambia akimkabidhi bahasha.
"Nini hii?"
"Baba 'kaniagiza nikupee hundi umpelekee benki baada ya kupata chakula chako cha mchana."
"Kwa nini hakumpa katibu wake...," alilalama akiweka mfukoni.
"Au kazi nyingi twende sote kwa gari langu ukihofia kuchelewa."
"Hapana, nitapeleka usitie shaka. Kwaheri."
Baada ya Shata kuondoka, Mziwanda alifunga mlango kwa haraka akaelekea barabarani na kuabiri teksi kuelekea alikoagana kupatana na rafikiye.
Alipoangalia saa yake mkononi, alikuwa nyuma kwa dakika kumi na tano kwa masaa waliyaokuwa wameahidiana na mwenzake. Gari lilibinginya masafa na baada ya dakika kama ishirini hivi akawa ashafika akalipa kwa haraka na kuondoka.
Alipofika mkahawani alimkuta Ali ashawasili, lakini kutoka kwa muonekano wake akajua hajafua dafu kwa kazi aliyokuwa amempa.
"Umesikia lolote kumuhusu?," alivuta kitu na kuketi.
"Salamu kwanza bwana wee, mwenye subira hakosi lolote."
"Mwenye subira hakosi lolote," alirudia maneno yake akimsalimu, "mi'mwenzio sina amani kabisa. Kila niwapo kazini, akili hunikumbusha kwamba kuna jukumu sijatekeleza."
Ali alimwangalia mwenzake akamuona amekonda kwa siku chache ambazo mkewe hakuwepo.
Baada ya kuagiza chakula, Mziwanda alikula kwa haraka kisha akainuka.
"Haraka za wapi!" Ali alimuuliza baada ya kuona mwenzake yuko tayari kuondoka.
"Nimeagizwa nifike benki na Bw. Makali," Mziwanda alijibu akiweka noti ya laki mbili mkononi mwake, "utanijuza chochote utakachosikia."
"Yetu mamoja," Ali aliitikia akiweka hela alizopewa mfukoni.
Mziwanda alipofika nje ya hoteli, alitembea haraka kuelekea alikokuwa ametumwa na binti wa mwajiri wake. Alipofika mlangoni na kuona safu iliyokuwepo alikata tamaa, aliangalia kwa saa yake ya mkononi akaona zimesalia dakika kumi na tano kabla ya masaa ya afisi. Alisimama kwenye laini akionekana mwenye wasiwasi.
"Mziwanda, kwa nini upo hapa saa za kazi," alisikia sauti ya kike ikimuuliza kando yake.
"Nimetumwa na bosi," alijibu akigeuka kuangalia aliyezungumza naye.
Alimtambua mara moja, alikuwa Rehema, rafikiye Shata. Alimkonyezea jicho kama ishara ya kumuita, mara moja akaanza kumfuata.
"Kuwa mpole kijana," Mziwanda aliambiwa na mlinzi wa benki akizuiliwa, "haraka haraka haina baraka."
"Ni mgeni wangu," Rehema alimwambia bawabu akirudi nyuma. Waliingia ndani, baada ya kuzungumza machache, Mziwanda alimpa hundi kisha akaanza kuondoka.
"Raundi hii ni ya sahihi moja," Rehema alimwambia baada ya kuichunguza, "ila usitie shaka, itakuwa tayari baada ya siku mbili."
"Asante," Mziwanda alimpa shukrani kisha akaondoka.
***
Alishika kalamu kujaza fomu zilizokuwa mbele yake, mlangoni pakabishwa kisha mlango ukafunguka na mkurugenzi wake kusimama mbele yake.
"Umechelewa wapi?!" Aliulizwa akiwekewa bahasha mbele yake, "mwaliko wetu imekubaliwa."
"Na nani?."
"Bw. Michael Brownson," mkurugenzi wake alimjibu akitoa ndani ya bahasha picha na kumkabidhi.
Ilikuwa picha ya mzungu mmoja mrefu na mnene wa umbo, kutoka ambapo picha ilichukuliwa palionekana watu wenye shughuli chungu nzima.
"I see," Mziwanda aliitikia akichukua picha. Bosi wake alianza kuondoka baada ya kumpokeza barua.
"Boss..."
"Ndiyo, hafla yenyewe itakuwa baada ya siku tatu kuanzia sasa hivi," Bw. Makali alimkatiza, "nataraji kwamba utafanya kila uwezalo kuifanikisha."
"Ndiyo boss," Mziwanda aliitikia lakini kabla hajamuuliza alichotaka akaondoka, "hakuna tatizo lolote, hata mwanawe mwenyewe ndiye aliyenipa."
Baada ya bosi wake kuondoka, Alishika fomu iliyokuwa mezani akashindwa kuandika chochote. Fikra zake hazikumpa uhuru wa kufanya chochote.
Alianza kukumbuka jinsi mapatano yake na Tumaini yalibadili maisha yake kwa asilimia kubwa. Kila asubuhi Tumaini akawa analetwa na mamake, Bi. Linda nyumbani kwao ili aandamane naye wakielekea shuleni.
Haya yakawa mazoea kiasi kwamba wakati mwingine Tumaini angechelewa, angemwendea mpaka nyumbani kwao.
"Nenda 'kamchukue mkeo," mamake alimkumbusha asubuhi moja alipomuona anaondoka.
"Lakini mama, atafanya nichelewe kufika shule," alitoa kisababu, "hutembea pole pole."
"Hapana mwanangu, ameshakuzoea. Nenda'kamchukue mkeo," mamake alimtania.
"Aka! Mimi nitakuwa padri."
"Nani akakuambia kwamba padri hawana familia. Siku hizi hata wao huoa," alisikia sauti ya Bi. Linda, "Wana wake zao na hata wengine huoana jinsia moja, tena wengine wana familia nzuri sana. Haya, nenda na mumeo shuleni."
Tumaini kwa aibu, alifunika macho yake kwa makofi yake madogo. Alimfikia akamshika mkono kisha wakaondoka. Vyakula walivyopewa na wazazi wao wale wakiwa shuleni masaa ya kupumzika, waliketi madukani wakala kabla hawajaanza kuelekea shuleni.
Haya yaliendelea mpaka wakapata majina tofauti tofauti shuleni. Wengine waliwaita chanda na pete, wengine wakawapa lakabu Uta na upote, wengine waliwaita mapacha, maharusi na hata wengine mume na mkewe. Hayo yote kwao ilikuwa kama kumsugua chui ukitarajia kuondoa madoa yake. Wakati wa mapumziko, Tumaini angeketi akicheza pekee yake au aonekane mpweke kama mwenzake hayupo.
****
Shata alikaa kochini akiangalia picha ya Mziwanda na mkewe, kwa hasira alichukua makasi akakata katikati, akachukua sehemu ya Tumaini akaitupa ndani ya ndoo iliyokuwa kando ya kutupa taka kisha akachukua sehemu ya Mziwanda na kuweka ndani ya pochi lake. Alisikia mbisho mlangoni lakini kabla hata hajaitikia wito, babake aliingia na kusimama mbele yake.
"Unaonekana mwenye mazonge!" Babake alimwambia baada ya kumwangalia kwa muda.
"'MI niko salama," alimjibu babake akiinuka, "karibu kitini."
"Sina wakati wa kuketi, nilikuagiza jana usherikiane na Mziwanda kwa ajili ya tamasha ambayo itaandaliwa hapa siku moja kuanzia leo."
"Ndiyo nimefika sasa hivi, najipanga kuenda kukutana naye."
"Fanya hala hala basi."
Bw.Makali alitoka afisini kisha bintiye akafuata baada kuchukua kicha cha funguo mezani na kufunga mlango, kwa ghafla babake alisita na kumtazama.
"Kwa majuma mawili sasa sijamuona Bi. Tumaini," Bw. Makali alimdakia bintiye.
"Aka! Yao mie hayanihusu."
"Usiwe mtu wa aina hiyo binti yangu," babake alimuonya, "kumbuka urafiki kati yenu kutoka mkiwa wachanga."
"Lakini baba, ya mtu na mkewe mimi yananihusu vipi!" Alimuuliza babake kwa utani lakini akiwa amemanisha alichokisema, "nikiwaingilia, utasema mwenyewe natishia kuvunja ndoa yao. Nitamuuliza basi."
"Sawa mwanangu, fanyeni kazi nzuri. Kumbuka matunda ya kesho yanatarajia upanzi wa leo."
Pasipo na kusema jingine, kila mmoja alienda zake. Bw. Makali alipanda ghorofani kisha bintiye akaenda hadi afisini mwa Mziwanda. Alipofikia mlango wa afisi ya mwenzake, aliingia ndani pasipo na kubisha.
" Salamu aleikhum," alimuamkua.
" aleikhum,"Mziwanda aliitikia salamu akiinua kichwa,"umekawia kufika, nilikutarajia mwendo wa saa tatu."
"Nilijua hutataka kufanya kazi nami."
"Shata, kufanya kazi nawe hakuna ubaya wowote, bora tusivunje mipaka yetu."
"Kwa nini usiheshimu hisia za mwenzio!" Shata alimuuliza akionekana kutoridhia na jambo fulani, "unajua hatuwezi kufanya kazi ikiwa hakuna maridhiano. Mimi sijaridhika kabisa, nikikwambia nimeridhia itakuwa nakusemea umbea."
"Hapa ni kazini Shata, mambo mengine tutazungumzia huko nje," Mziwanda alimwambia akiinama kushughulikia hisabati iliyokuwa mbele yake, "'mi mwenyewe nina mazonge, lakini Sina budi kufanikisha hafla hii na kuinua kampani la babako."
Shata alifikia pochi lake akatoa kipande cha picha akaweka mezani.
" Nitafanya nini juu yako uridhike kuwa nami! Ukauteka moyo wangu, ukanifanya mtumwa wa milele, ukaufunga kwa nyororo na kwa kuta zake jina lako likajiandika lisifutike tena. Kila nifanyapo kitu wewe u pale pale, chombo cha thamani kwangu. Mwenyewe nimetamani kukuondokea ila nafsi na hisia zangu zinanihukumu."
Mziwanda alimwangalia akatabasamu, labda kwa sababu aliona amesukumiwa mzigo na Bw. Makali. Alijua mwenzake hakuwa na ufahamu wa yoyote yaliyokuwa yanaendelea akilini mwake, alijua Shata anaendeshwa na choyo na tamaa iliyojaa moyoni akitaka kufanikisha mambo yake kwa maumivu ya wengine.
"Hata nami nakupenda, tena natamani kuwa karibu yako kila wakati," Mziwanda alimwambia. Shata alitabasamu kwa maneno ya mwenzake, "ila hisia zangu zina mipaka yake, ninataka kuwa rafiki yako na kukusaidia kila litakalotufaidi maishani."
"Kufanikisha na kufaidi maisha yangu, wewe pekee ndiye jibu kwa hayo yote."
"Mimi kwa sasa nina mke, nashindwa kwa nini huwezi kunielewa."
"Nitakuelewa vipi ikiwa mwenyewe umeshindwa kunielewa. kumbuka tulikoanzia maisha tukiwa wadogo."
***
Shata alifikia mikono yake akaishika na kuizika ndani ya yake kwa utulivu. Mara moja kama aliyetiwa kanda, alirudi nyuma kifikra miaka nyingi iliyopita.
Alikumbuka jinsi Shata alifika kijijini mwao na babake akiwa angali mdogo, babake alikodi nyumba kubwa iliyokuwa hapo kijijini mwao.
Asubuhi moja baada ya kufika kijijini, walifika nyumbani kwa Bw. Rufai na Bi. Zena. Waliletwa na mmoja wa wanakijiji ili wajitambulishe kwa wazee wa pale kijijini. Bw. Makali alifika na bintiye akiwa amemshika mkono.
"Hujambo," Bw. Makali alimuamkua babake.
"Sijambo, Mziwanda niletee kitu tumpe mgeni."
Kwa haraka alikimbia jikoni akarudi na kiti cha kukunja, baada ya kumkabidhi mgeni kiti, alisimama kando ya babake akimwangalia yule binti. Macho yao yalipokutana, Shata alimkonyezea jicho kisha akamnyoshea kibonzo kilichokuwa kwapani.
"Twende tucheze," Shata alimwambia akimvuta mkono kumuondoa walipokuwa wazazi wao, wakaenda mpaka nyuma ya kibanda chao.
"My name is Shata," alijitambulisha akimnyoshea mkono, "I am in standard one."
"Naitwa Mziwanda," naye alijitambulisha. Kizungu cha mwenzake kilimvutia, hakupata kuona pale kijijini kwao watoto wa rika lake wakizungumza kimombo kwa ustadi mkubwa namna hiyo, "nipo katika darasa la pili."
Kwa wasiwasi Shata aliangalia kila upande, alipoona hakuna mtu anayesogea, aliweka kidole chake mdomoni ishara ya kumnyamazisha kisha akafikia kaptura lake.
"Mnafanya nini?!" Walisikia sauti kando yao, wote wakashtuka.
"Huyu anaitwa Tumaini," Mziwanda alimtambulisha aliyewafumania akienda karibu yake.
Shata alionekana asiyefurahia kuwepo kwa Tumaini mahali pale. Kwa upole na uoga, Tumaini aliwasogea na kumnyoshea Shata mkono, kwa haraka aliyenyoshewa aliokota kibonzo chake kilichokuwa kimeanguka kisha akatoka mbio na kuelekea walipokuwa wazazi wao.
"Mlikuwa mnafanya nini?," Tumaini alimuuliza.
"Hata 'mi sijui alitaka kufanya nini, alifikia kaptura langu kisha akaanza kufungua."
"'we muongo. Naenda kumwambia mama m'mefanya tabia mbaya," Tumaini alimwambia akitoka mbio.
"Usifanye hivyo," Mziwanda alimkanya akimshika mkono kumzuia asiondoke.
"Niahidi hutafanya hivyo tena mkiwa naye."
"Nakupa ahadi yangu."
Baada ya yale, wote waliondoka wakaelekea walipokuwa Bw. Rufai na Bw. Makali. Tumaini alimnyoshea Shata mkono akitaka angalau apewe kibonzo lakini mwenzake akakificha mgongoni.
Shata alimwangalia Tumaini kwa kijicho, lakini mwenzake ilivyokuwa kawaida akajificha nyuma ya Mziwanda.
"Utakuwa ukija kucheza na mwenzio," Bw. Makali alimwambia Mziwanda akiinuka tayari kuondoka.
"Ndiyo," aliitikia akimpa mkono kuwaaga.
Alipomsalimu Shata, aliufinya mkono wake upande wa chini huku akitabasamu. Tumaini naye kwa uoga alimnyoshea mkono lakini Shata akasusia kumuaga.
"Kwa nini ananichukia?," Tumaini alimuuliza baada ya wageni wao kuondoka.
Machozi yalianza kumlengalenga machoni, Mziwanda akamfuta kwa shati lake. Siku ya kwanza waliyopatana aliona uhasama uliozuka Kati ya hao mabinti wawili.
"Let me hope you have finished to prepare the budget," Mziwanda alishtuliwa na Bw. Makali aliyekuwa amefika na kusimama mbele yake.
"Ndiyo boss."
"Kwa nini mkawa kimya?!" Bw. Makali alimgeukia bintiye.
"It's ok dad."
"Mwambie akufunze hivi anavyofanya, 'we ndiye director wa kesho hapa ndani."
"Safari ya kesho hupangwa leo," Mziwanda aliingilia kati, "nitamfunza madogo madogo kila siku mpaka atakapokuwa tayari pasi na kupungua chochote."
"Mfunze, nakutegemea baada ya kuondoka kwa meneja wako," baada ya maneno yale, Bw. Makali aliondoka akawaacha wakiwa wameangaliana.
***
"Mwalimu ndiye huyo anakuja," msichana mmoja aliwafahamisha wenzake waliokuwa wanaunda vyumba vya mchanga kando ya mti wa mbuyu. Kwa haraka wote walikimbia mpaka chini ya mti wakachukua madaftari yao tayari kwa masomo.
Tumaini alifika na pakiti ya pipi na kitabu mkononi, Tabby akainuka kufuta ubao ulioegemezwa mtini.
"Hamjambo," aliwaamkua kwa furaha.
"Hatujambo mwalimu," walijibu kwa pamoja.
Walikuwa wanafunzi kama thelathini hivi, japo darasa alikuwa ameanzisha siku iliyotangulia akiwa na wanafunzi wanne, idadi ilikuwa imeongezeka kwa haraka.
"Jemima, hebu tujuze wenzako unataka kuwa nani ukiwa mtu mzima," Tumaini alimuamsha msichana mmoja aliyekuwa ameketi mbele ya darasa lake.
"Nataka kuwa rubani," aliyeulizwa alimjibu kwa uchangamfu, "nataka kupaa angani kama ndege."
"Kikojozi hawezi kuendesha ndege," kivulana kimoja kutoka nyuma ya darasa kilimkejeli Jemimah.
Kwa aibu, Jemimah aliketi akaanza kulia, darasa zima liliangua kicheko kilichomfedhehesha.
"Msiwe watu wa kuwatusi wenzenu," Tumaini aliwaonya.
Wanafunzi wote walimsikiliza kwa makini alipoanza kufunza. Kwa mbali alisikia mgurumo wa pikipiki aina ya honda ikiwajia. Kwa utaratibu, mwenye pikipiki alikuja akasimama kando na darasa lake.
"Naona unawafunza watakaochukua nafasi zetu siku za usoni," mgeni wake alianza bila hata kumuamkua.
"Ndiyo."
"Kwa nini usije ukajiunga na shule yangu," mgeni wake alimshawishi, "naitwa Bw. Mfarika. Nitakulipa pesa nzuri kushinda hivi unavyolipwa hapa na hawa wavuvi."
"Mimi si mwalimu," Tumaini alimdanganya, "nabambanya tu kidogo nipate hela za kunitoa hapa nirudi kwangu."
"Aaaah! Wewe ndiye yule binti aliyepatikana majeruhi kisiwa jirani."
"Haswa."
Bw. Mfarika alitikisa kichwa kama anayekubaliana na jambo fulani kichwani mwake.
"Naomba ujiunge nami," Bw. Mfarika alimrai kwa mara nyingine.
"Hapana haja, hawa nawasaidia kwa sababu walishindwa kujiunga na shule yako kwa sababu ya karo."
"Nitakupa makazi na kila utakacho. Nimefurahishwa na kufunza kwako, nahitaji walimu kama wewe."
"Mimi hapana, nishapata makazi na kila kitu."
Bw. Mfarika alitoa miwani akafuta jasho kisha akagurumisha pikipiki tayari kuondoka, kwa ghafla aligeuka na kumwangalia.
"Kumbuka, pesa zina makali kushinda upanga," alimtolea kauli yake ya mwisho kisha akaondoka.
"Nimemkosea nini mie, natafuta hela niondoke," Tumaini alijisemea.
"Tunamuogopa," watoto wote walimwambia kwa pamoja baada ya mgeni wao kuondoka.
"Alikuja nyumbani akamchukua ng'ombe wa mama aliposhindwa kunilipia karo," Jemimah alilalama mbele ya
mwalimu wao.
Tumaini alishika chaki kufunza lakini akashindwa, japo alikuwa amemaliza pale majuma mawili, alikuwa ameshasikia sifa zake, ilikuwa kanakwamba ameshamtenda kila mwanakisiwa maasi.
" Haya tuondoke, tutasoma kesho,"alivunja kikao.
" Nawe unamuogopa?" Tabby alimuuliza akiwa amemwangalia usoni.
" Hapana, nahisi maumivu kichwani," Tumaini alimdanganya.
Kila mwanafunzi alipita akimsalimu kisha akaondoka.