Tumaini alifumbua macho kwa shida akiinuka juu ya jabali, alihisi maumivu mwili mzima. Alipoangalia alipokuwa, aliona amesimama juu ya kisiwa chenye urefu wa kama kilomita moja na upana wa mita mia tano.
"Nikafika vipi mahali hapa?!," alijiuliza kwa mshangao akishika kichwa kilichokuwa kinamuuma.
Nywele kichwani zilimtimka kama za mwendawazimu, rinda alilovalia lilikuwa limeraruka tumboni, miguuni hakuwa amevaa chochote.
Kwa mbali aliona motaboti ikienda akapiga mayowe yawafikie waliokuwa kwenye mtambo bila mafanikio. Aliangalia angani akaona Jua linaaga kupisha mbalamwezi.
Baridi ya pale kisiwani ilianza kumudhulumu bila huruma, akaotama, alipojiangalia aliihurumia nafasi yake. Aliinuka mara moja akaanza kuokota vikuni vya kuoka moto wa kuota na mwanga usiku huo kwa sababu matumaini ya kuokoka kutoka pale yalififia.
Alipokuwa anaendelea na kazi yake ndipo alipotambua pete iliyokuwa kidoleni. Hili lilimzidishia hata mashaka.
Mwendo wa saa mbili za usiku, aliwasha moto akaanza kuota alijaribu kuvuta kumbukizi ya kile kilichotokea mpaka kujipata katika lindi ya shida.
"Bila shaka mimi ni mke wa mtu," aliwaza akigusa pete, "naye alikuwa wapi nilipoletwa hapa...au alikuwa pamoja nao...hapana, mtu hawezi kumtenda mkewe hivi...au naye alipatwa na shida...yuko salama...hapana...lazima naye ananifikiria mimi..."
Mawazo yake yalikatizwa kwa kitu baridi kilichomteremka mgongoni, kwa uoga alifumba macho akifikiri ni nyoka. Kwa wasiwasi, alifikia kilichokuwa mgongoni akakivuta kwa nguvu na kukitupa mbele yake. Alipoona mkufu wa dhahabu alishanga, akashusha pumzi na kutabasamu. Uling'aa kwa ile miale ya moto na mwanga hafifu wa mbalamwezi.
Aliufikia na kufungua kidoti kilichokuwepo, akaona picha yake na mwanaume fulani ambaye bila shaka ndiye alikuwa mumewe. Picha yenyewe ilikuwa iliyopigwa wakiwa maharusi.
"Mziwanda...!" Jina lilimtoka kwa mshangao baada ya kuona picha ya yule mwanaume, "Mziwanda mume wangu...uko wapi...yapi yakatokea kututenganisha...mume wangu." MA chozi yalianza kutoka, yakatiririka mpaka kifuani.
Alivuta rinda lake na kuyafuta, alitaka kutoa ukwenzi akahofia labda atawaita wanyama wa majini watakaomvamia na kumuangamiza.
" Hapana, lazima nipambane kulinda ndoa yangu. Sitaruhusu mtu kunidhulumu mie...hapana mume wangu...no...sitaruhusu mume wangu kunyakuliwa na mashangingi wa hapa mjini,' alikumbuka yaliyokuwepo kati yake na mumewe,"ukaniahidi kwamba utamuondokea Shata, ila leo nimewafumania m' me banana ukutani."
"Hapana Tumaini, siwezi nikakutenda karaha."
"Unaka...," alikatizwa na mlango wao uliofunguka kwa nguvu kisha madume manne yenye misuli yakajitoma ndani kwa nguvu.
Walimvamia mumewe na kumshika kwa nguvu hata asiweze kutikisa unywele wa kichwa chake kufanya lolote, alipotaka kutoa siahi kuita usaidizi kutoka kwa majirani ndipo alipopata mkong'oto wa bunduki kichwani akapoteza fahamu. Mwisho we alikuwa amerudisha fahamu akiwa Mahali ambapo hapafahamu.
****
Mziwanda aliinuka alipolazwa kwa shida baada ya kuhisi mguso begani.
"Shata!" aliita kwa mshangao, "unafanya nini hapa?!"
"Nimekuja kukuona wewe," Shata alimjibu akionekana mwenye furaha.
"Kuniona kama nani...na mke wangu Tumaini yuko wapi?!."
"Yeye ana nini ninachokosa, niangalie kuanzia chini mpaka juu," Shata alimwambia akimsongea, "huyu Tumaini akakupa nini usichoweza kumsahau."
"'kanipa kitu nisichoweza kupata kwako. Akanipa wema na uaminifu wake."
"Hayo tu!" Shata alidakia akionekana mwenye hasira, "kumbuka hiyo kazi unayojifanyia na huyo kikaragosi wako ndimi niliyekutafutia."
Mziwanda alijilaza kwa upole na kufumba macho kumuondokea mwenzake. Shata aliketi kando yake akionekana mwenye fikra, hakujua kipi angefanya cha kumpiku Tumaini ili mumewe asimfikiri tena.
Baada ya kuketi pale kwa dakika thelathini, aliondoka akionekana aliyeghadhabika. Zilikuwa zimepita siku tatu baada ya Mziwanda kulazwa pale hospitalini baada ya kupata jeraha kwenye mguu wake wa kushoto alipojaribu kumuokoa mkewe kutoka kwa nduli wale.
Alipoona Shata ameondoka aliinuka tena;
"Ndiyo, alinisaidia nikapata kazi lakini haya hayakuwa makataa yetu," alijisemea baada ya swala la Shata kumpita akilini, "ningejua haya...," alikatizwa na mbisho uliosikika mlangoni, akafumba macho akifikiri ni Shata. Mlango ulifunguka, mwanamke mmoja akaingia na kuketi kando yake.
"Mwanangu yuko wapi!?!" aliamshwa kwa swali lile, "Mwanangu ukamtupa wapi?!"
"Shikamoo mama," Mziwanda alimuamkua baada ya kuinuka kitandani.
"Marahaba mwanangu, nakutakia ahueni ya haraka ili ushughulike kumtafuta mkeo."
"Ndiyo mama, nitakuwa salama, siku chache kisha nitatoka katika majengo haya na kumtafuta kote kote, usitie shaka."
"Pole kwa yaliyowakuta," Bi. Linda alimpa pole akifuta machozi.
"Tushapoa mama, tutakuwa salama."
"Nilifika hapa mjini siku mbili kabla nikakupata wewe si wa kufa si wa kuishi."
Mziwanda alitoa tabasamu hafifu kwa maneno ya ma-mkwe wake.
"Na wazazi wangu je?!" alimuuliza baada yao kumpita akilini.
"wapo salama, ila kwa sasa wanashugulika kumtafuta Tumaini."
"Watamtafuta vipi ikiwa hawafahamu aliko...hawajui kilichotokea."
"Wanajaribu bahati mwanangu...naumia moyoni kumkosa mwanangu, naumia. Fanya haraka uanze kumtafuta asipotee kabisa."
"Nitamtafuta mama, usilie."
"Akipotea nitapata wapi mwana mwingine kufu yake, sitakuwa na chochote kilichosalia kuitwa changu hapa duniani."
"Hapana mama, usiseme hivyo. Ningekuwa na uwezo ningetoka hata sasa hivi, lakini nazuiliwa na wauguzi."
"Akha!" Bi. Linda alimaka, "usiwe na haraka mwanangu, vipi ukiharakisha kisha nawe tukakupoteza, tutakuwa wageni wa nani katika nchi yetu ya Mapuuza. Lakini ni heri ukipona usianze kazi yako kabla hujajua aliko mwanangu."
"Nimekupata mama."
"Kumbuka, mwana ndiye zawadi ya maisha. Nikimpoteza nitakuwa nimepoteza tunu yangu kutoka kwa Mungu."
****
Tumaini aliamshwa na sauti nzito aliyosikia kwa mbali. Alikuwa hoi kwa sababu ya kukosa kula chochote usiku uliotangulia, alifumbua macho kwa shida kumuona aliyekuwa kando yake.
Nguvu zilikuwa zimemuishia, alimuona mnenaji kuanzia kwa miguu yake mpaka kiunoni.
"Anaonekana mgonjwa," alisikia sauti ikidai.
"Hebu mchukue tumpeleke kisiwani kwetu kwa matibabu, labda tutaokoa maisha yake," alisikia sauti nyingine ikitoa amri.
"Ndiyo chifu."
Baada ya maneno yale alifumba macho, wavuvi wakamchukua pasi kujielewa mpaka kwenye kisiwa chao. Alipelekwa mara moja hadi kwa daktari wao wa mitishamba alipoanza kuhudumiwa mara moja.
"Atapata nafuu kweli?!" Chifu wa kisiwa alimuuliza daktari akionekana mwenye wasiwasi.
"Ni kwa neema," Bi. Tabitha alimjibu kwa toni ya mashaka.
Wanakisiwa cha Mawe walikuwa wamekusanyika kwa Bi. Tabitha wakimwangalia mgonjwa wao. Tabibu alitia juhudi katika kazi yake, alipoona jeraha lililokuwa tumboni, alitikisa kichwa.
"Huyu 'kadhulumiwa kweli," alimwambia chifu Bw. Mazoea alitikisa kichwa, "walomtia jeraha walikusudia kumuangamiza kwa kumuacha avuje damu pole pole mpaka kifo chake."
Yote Bw. Mazoea alisikia na kujionea, hakuwa na la kuongeza wala kuondoa. Siku iliaga, usiku ukaingia wenyeji wakatawanyika kurejea manyumbani kwao.
Siku zilisonga pasipo na Tumaini kuonyesha dalili yoyote ya kupata nafuu, kila asubuhi Bw. Mazoea akifika kwa tabibu wao kumwangalia.
Siku ya sita, Tumaini aliamka akaketi kwenye mkeka alokuwa amelalia, akaona kando yake kisichana kidogo kama cha miaka misaba hivi.
"Salamu aleikhum," alikiamkua kwa sauti ya unyonge. Pasipo na kujibu, kilitoka nje mbio kikiita bibiye aliyeingia baada ya sekunde kadha.
Bi. Tabitha alisimama mlangoni akimwangalia Tumaini kama mtu asiyeamini alichokiona.
"Shikamoo mama," Tumaini alimuamkua akiinuka kutoka alipoketi.
"Marahaba mwanangu," Bi. Tabitha aliitikia akimfikia kuzuia asiinuke, "keti mama, hujapata siha njema."
Baada ya kumlaza mgonjwa wake, alitoka nje akamwagiza mjukuu wake kumuita chifu.
Bw. Mazoea alipopata taarifa kwamba anatakiwa na Bi. Tabitha, aliacha uji wa wimbi aliokuwa ameandaliwa. Alipofikia mlango wa Bi. Tabitha, alilakiwa kwa tabasamu kitu ambacho hakikuwa cha kawaida kwa siku tano zilizotangulia.
"Mola akatujalia kuokoa maisha yake," Bi. Tabitha alimwambia akimpisha kuingia ndani.
"Yuko salama kabisa?!" Bw. Mazoea aliuliza akionekana mwenye mashaka.
"Ndiyo."
Aliingia ndani akampata Tumaini ameketi akiwa ameegemeza mgongo ukutani.
"Kweli Mungu hamuachi mja wake," chifu alimwambia akimpokeza mkono kumsalimu.
Tumaini alimtolea tabasamu hafifu akimsalimu, wakazungumza kwa dakika kadha kisha akatoka. Tumaini alisalia pale akiwa haelewi chochote, mara akasikia mlio wa baragumu uliomshitua.
" Mwito ni wa nini?," alimuuliza yule msichana aliyekuwa kando yake.
"Ni babu anaita watu," alimjibu kwa haraka.
Yule msichana alionekana kuvutiwa na mgeni wao, mara kwa mara akimtupia jicho la upekuzi.
Bi. Tabitha aliingia ndani ya nyumba yake ya msonge na kumpa taarifa kwamba mwito aliosikia ni chifu anawaita wanakisiwa kuwaarifu kwamba kutakuwa na sharehe.
"Tutaanda sherehe ya kukulaki mwanangu," Bi. Tabitha alimwambia kwa ukarimu.
"Kunilaki mimi!"
"Ndiyo, tulikuwa tumekupoteza lakini kwa sababu ya upendo wa Mola juu yetu akakurejesha. Sasa ni lazima tushereheke afya yako."
"Asante mama."
****
Siku ya saba masaa ya matlahi, wanakisiwa wakiwa wamesharudi kutoka kwa pilka pilka zao za kutafuta riziki, sherehe ilianza. Boma la Bw. Mazoea lilijaa halaiki, vyakula vya kitamaduni na vileo havikuachwa nyuma. Watu walionekana wenye furaha kupita kiasi, kila sura iling'aa kwa tabasamu.
Mwendo wa saa moja, Bw. Mazoea alisimama mbele ya hadhira kutoa hotuba na kuanzisha sherehe rasmi.
"Nawakaribisha nyote katika boma hili kwa furaha, nawakaribisha kwa sherehe ya kumlaki mwenzetu," umati uliangusha mvua ya makofi, "nawashukuru kwa kuitikia wito wangu na kwa sababu ya kuniheshimu kama kiongozi, wala si kiongozi tu bali pia kama jamaa yenu."
Watu walipiga makofi kwa mara nyingine. Tumaini, Bi. Tabitha na mjukuu wake walikuwa wameketi mbele ya hadhira na chifu wao.
"Usisahau kuwa ulikuwa baharia baada ya kuwa nahodha," Bw. Mazoea aliendelea, "nawaenzi nyote. Siku moja nami nilikuwa kama ninyi ila baba akaniachia ukoka nami sikuwa na budi kujivika, wala si mimi nifanyavyo hivyo bali ni kwa msaada wenu. Kumbuka asiyeti ushauri na amri hawezi kuamrisha au kuwa kiongozi, nami kwa sababu ya ndugu, baba na babu zetu nimefanikiwa kuwaongoza kwa hekima. Ni jukumu la kisiwa kizima kumlea mwana, nasi hapa tumemchukua kama msichana wa kisiwa hiki baada ya kupatana naye."
Baada ya maneno yale, Bw. Mazoea aliketi akampa Tumaini nafasi ya kuzungumza na wanakisiwa. Alipoinuka, mvua ya makofi ilinyesha, akajitambulisha kwa hadhira yake, akasema macha kisha akaketi, mfawidhi bila kupoteza wakati akawakaribisha watumbuizaji.
Wanaume wawili wenye miraba minne waliingia katikati ya mviringo kushindana maguvu, watu walionekana kufurahia mchezo, baada yao waliingia wasichana watatu walioimba wimbo wa kumkaribisha mgeni wao katika jamii yao na pia kusifia utajiri wa utamaduni wao. Sherehe iliendelea kwa furaha, Tumaini alifurahia umoja uliokuwa pale kisiwani. Mwendo wa saa tano, sherehe ilikamilika watu wakajikusanya makundi madogo madogo kushtaki njaa. Baada ya kula na kunywa kwa saa nzima, kila mtu alianza kuondoka kuelekea kwake.
"Kuwa kiongozi ni lazima uwe kama Mbalamwezi wala si Jua," Tumaini alimsikia mvulana mmoja akimwambia mwenzake wakiwa wanaondoka.
"Lazima uwe tayari kutoa kwa watu wako."
Hima hima, Tumaini alimfuata Bi. Tabitha mpaka kwake. Alikuwa mtawa asiyemjua yeyote pale kisiwani ila Bw. Mazoea, Bi. Tabitha na mjukuu wake ambaye ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuonana naye.
***
Mziwanda alikuwa afisini kiwiliwili, lakini kifikra alikuwa mbali na manthari yale. Alishika kalamu akashindwa kuandika barua aliyokuwa ameambiwa atayarishe na bosi wake kuhusu mwaliko wa mkurugenzi wa kampani la Natius Technologies.
"Shata akampeleka wapi mke wangu?!" Alijiuliza akiweka kalamu chini, "au 'kamwangamiza...hapana, hawezi kufanya kitendo kama hicho... siku tatu nimemtafuta Chokocho nzima bila mafanikio...wala sijapata ujumbe wowote kutoka kwa Rehema wala hajafika hapa kutafuta."
Bi. Linda alivyofika hospitalini kumuuguza, alionekana mwenye wasiwasi kutoka usoni mwake. Alikuwa amempa ahadi kuwa akitoka hospitalini jambo la kwanza litakuwa kumtafuta mkewe lakini alikuwa pale ofisini akilazimishwa kuandika barua kwa jambo ambalo hakuna manufaa yake.
"Ahadi ni deni," alijisemea baada ya yale kupita akilini, "lakini nitaanza kwa namna gani kumtafuta mtu nisiyejua aliko."
Alianza kukumbuka jinsi urafiki wake na mkewe ulivyoanza wakiwa wangali wachanga wasiojielewa.
Mwenyewe alikuwa katika darasa la pili, Tumaini akiwa katika shule ya chekechea.
Ilikuwa adhuhuri moja akiwa anatoka shuleni baada ya masomo yao, alimpata Tumaini akilia kando ya barabara huku daftari lake nusu likiwa katikati ya barabara na penseli upande mwingine.
Alienda akaotama kando yake kisha akaanza kumbemba, akaokota kitabu na penseli yake na kuweka ndani ya mkoba wake ulioshonwa kwa uzi.
Alipokuwa anaondoka, Tumaini alimshika nguo na kumuonesha kwa kidole kundi la vivulana kama tano hivi wa rika lake.
"Wakakufanyia nini?."
"Wameninyang'anya embe langu," Tumaini alimjibu kwa kusinasina.
"Twende nikununulie jingine, hao ni watu wabaya achana nao," alimwambia akimuinua.
Walipokuwa wanaelekea kwa mnada kununua embe, wale wavulana walisimama mbele yao.
"Tupisheni," aliwaambia kwa upole.
Kwa ghafla wale wavulana waliwazunguka, akamuacha Tumaini, lakini kwa sababu ya uoga alijificha mgongoni pake.
"Njoo basi nikupeleke," kivulana kimoja kati ya wale watano kilimwambia Tumaini akimvuta mkono.
"Niache," Tumaini alilia akimvuta kwa nguvu shati lake.
Kwa hasira Mziwanda aligeuka na kumng'ata yule mvulana kwa meno ikawa hana budi kumuachia Tumaini. Kitendo hicho kilisababisha pakazuka vita, watano dhidi ya mmoja.
Tumaini alisimama kando akilia na kuwavuta wale wavamizi. Mmoja wao alimpiga teke lililomuangusha uani akawa hana msaada mwingine wa kumtolea mwenzake ila kilio. Wale wavulana walimzidia Mziwanda nguvu wakampiga na kurarua vifungu vya shati lake na kifungo kimoja cha kaptura yake. Walipoona mwalimu anawajia, walitoka mbio kama mshale wakamuacha Mziwanda akiuguza majeraha.
***
Mwalimu alipowafikia, bila hata maelezo yoyote, alimlaza chini Mziwanda na kumtia adabu.
"ninyi ndiyo mfikao shuleni kupiga wenzenu?!" Alimuuliza baada ya kumpiga viboko vitatu.
"Hapana, Walimvamia," alijitetea akimuonesha Tumaini kwa kidole.
"Nawe ukaamua kupigana nao, kwa sababu wewe ndiye mtemi wa makonde?" mwalimu alimuuliza tena akimlaza chini kumtia adabu. Alitikisa kichwa akimzuia mwalimu kumcharaza kiboko kingine.
"Ushamaliza kazi uliyopewa na mkurugenzi wako?," kumbukumbu zake zilikatizwa na sekritari wa Bw. Makali.
"Hapana," alimjibu kwa haraka akifikia kalamu, "lakini hawezi akanielewa kwamba kwa sasa hali yangu si nzuri!"
"Ni heri ufanye ulivyoagizwa, huenda atakaporejea hatakuwa katika hali nzuri nawe atakapoona hujatimiza alichokuagiza."
"Nipe dakika ishirini hivi nikamilishe kisha upige chapa na kumpa," Mziwanda alimuagiza akianza kuishughulikia."
Baada ya kuandika anwani ya kampani lao, alikaa akamtazama sekritari aliyekuwa ametulia kando yake akibonyeza simu.
" Haya ndiyo ambayo mkuu wangu anataka ndani ya kampani lake," alijisemea baada ya kumuona alivyozamia simu yake.
Baada ya kama dakika tano, ndipo mwenzake alipoinua kichwa akamuona amemuangalia kwa kuzuba.
"Ushamaliza bwana wee!" alimuuliza akionekana aliyeghadhabika.
"Hapana," Mziwanda alimjibu akicheka kwa sauti ya chini, "nimekuona umezamia simu yako nikafikiri mara moja manufaa na madhara yatakayoletwa na utandawazi ndani ya kampani hili."
"Kwa njia ipi? Mi' kwa mtazamo wangu hata mambo yatakuwa mepesi zaidi. Hapatakuwa na panda-shuka nyingi, kutoka afisi moja hadi nyingine."
Mziwanda alimwangalia kwa makini akamuona anayeangalia upande mmoja tu wa sarafu. Kila kitu kina uzuri na ubaya wake, lakini kwake teknolojia hiyo ilikuwa na madhara mengi kushinda mazuri.
" Hali hiyo itapunguza kutangamana kwetu kama jamii moja," Mziwanda alimpa wazo lake, "kuzunguka kwetu ndiko hufanya tukajua hali za wenzetu humu ndani. Utokapo afisi yako ukaenda nyingine kushughulikiwa, angalau unazungumza na mwenzako. Utangamano ndiyo nguvu ya chochote."
Yule katibu aliinua kichwa akamwangalia kwa mara nyingine.
"Ndo haswa nionavyo, uvivu utapungua. Kuhusu mahusiano kuna masaa ya kustaftahi, kupata cha mchana na jioni kila mtu anapoenda nyumbani kwake, hapo mnaweza mkaonana mpaka keshoye asubuhi."
"Kitu usichofahamu ni kuwa, mwanadamu ni kiumbe-jamii, ana hisia ambazo lazima amuoneshe mwenzake na pia anahitaji mapumziko."
"Sijafika hapa kujadili uzuri na ubaya wa teknolojia, andika barua unipe niondoke."