Tulya anaamka mwili wote ukiwa umelowa jasho,macho yake yakiwa yameliwa machozi anaamka taratibu na kuketi kitako kitandani mapigo ya moyo yakiwa yanaenda mbio.Sasa hii inazidi anawaza Tulya asielewe kwa nini ndoto ya huyo Ndesha inamganda namna hii,akilini akijiuliza ilikuwaje mbona kama Ndesha alikuwa anaongea na yeye,na kingine hii ni ndoto lakini bado anahisi kama ni uhalisia.
Anameza funda la mate lakini anahisi koo lake limekauka.Anashuka kitandani na kuchukua kibuyu kilichokuwa na maji pembeni ya kitanda anamimina kwenye kipeo na kuyasukumiza kooni,anamaliza anaweka kipeo juu ya kibuyu anapanda kitandani na kuanza kujaribu kutafuta usingizi tena lakini usingizi ulishatokea dirishani na kukimbia mbali ukimwacha akigeuka pale kitandani,anafumba macho yake lakini masikio yake yanasikia sauti za mbwa wakimbeka nje wakitishwa na sauti za fisi wenye njaa wakilia kwa mbali kualikana Kuja kijijini kutafuta mabaki na mifupa." inaonekana bado usiku mnene" anawaza Tulya akijua bado ana masaa mengi ya kugeuka pale kitandani wakati kwa wakati huu yeye anatamani pawahi kupambazuka.
Tulya anageuka kitandani akijiweka vizuri lakini macho yake yanapigwa na mwanga mkali unaoingia kutoka nje,anafungua macho yake na kukuta ndani Pako peupe ikionyesha kupambazuka lakini sio mapambazuko tu kumekucha kabisa.
Haraka haraka anatupa kaniki yake kule anashusha miguu yake chini na kutoka nje kwa haraka anachokutana nacho kinamuacha mdomo wazi." ohh mama yangu! kulala gani huku?" anajiuliza baada ya kuona jua lipo juuu kabisa.Baada ya kushtuka ndotoni ilimchukua Tulya mda mrefu kulala kwani jogoo la tatu liliwika bado Yuko macho na usingizi ulipokuja ndio uliomfanya alale mpaka apitilize.
" umeamka?" anageuka na kumuona mama mkwe wake akiwa amebeba Kuni mkononi aibu inamshika asijue ajichimbie wapi.
" ndio,shikamoo mama" anamsalimia asijue hata Cha kufanya kwa anavyomjua mama mkwe wake atakuwa kafanya kazi zote za asubuhi anang'ata midomo yake akitamani akakipigize kichwa mahali kwa uzembe wake lakini haya yote ni makosa ya ile ndoto mbaya na kwanza ilitokea wapi na wakati Jana hakuzungumzia maada ya Ndesha kabisa na wakati anaenda kulala kichwa chake kilikuwa kimejaa mawazo ya Nzagamba tu,inakuwaje asimuote Nzagamba akaota mambo ya ajabu anawaza Tulya.
"unajisikiaje?" anamsikia Bibi sumbo akimuuliza akiwa bado amesimama na Kuni mkononi akimwangalia mkamwana wake.
" ehh?!" Tulya anaitikia kwa mshangao.
" mumeo amesema usiku hukulala vizuri,unajisikiaje?" anauliza Bibi sumbo na kumfanya Tulya kumtumbulia macho kwa mshangao asijue anamaanisha nini au kwa sababu kachelewa kuamka ndio maana Nzagamba akajua labda anaumwa.
" najisikia vizuri mama" anamjibu kwa sauti isiyo na uhakika.
" sawa pata kifungua kinywa,sisi tupo huku uwaani tunapanga hizi Kuni" Bibi sumbo anamjibu na kuanza kuondoka
" sisi?" anajiuliza na Kisha kusikia sauti ya panga ikitokea upande wa nyuma wa nyumba.
Anarudi ndani kwake na kuona kijiti cha mti mbichi uliokatwa na kuchomekwa ukutani pale alipoacha mswaki wake wa mti Jana,anatabasamu na kuchukua kijiti na kukiweka mdomoni anaking'ata na meno anakitengeneza vizuri na kuanza kuswaki akitabasamu akijua Nzagamba ndio kamtengenezea mswaki baada ya kuona kachelewa kuamka.Baada ya kumaliza kupata kifungua kinywa anaenda nyuma ya nyumba na kumkuta Bibi sumbo na Nzagamba wakiwa wanatengeneza kichanja Cha Kuni wakizipanda vizuri.Bibi sumbo akipanga na Nzagamba akizitengeneza vizuri kwa panga kabla ya kumpatia mama yake.Misuli ya mikono yake migumu ikijikaza Kila anaponyanya panga lake kukata Kuni nywele zake zilizojisokota kichwani zikitikisika,imekuwaje nimebahatika kupata mume mtanashati kama huyu anawaza Tulya na pasipo kujua tabasamu linatawala mdomoni kwake na kufika mpaka machoni.
Anasafisha koo kidogo kwa kukohoa kama kuwajulisha uwepo wake Nzagamba anageuka na kumwangalia " uko sawa?"anamuuliza uso ukiwa na wasiwasi.
" ndio,habari ya asubuhi" anamjibu akienda kuchukua Kuni nakuanza kumsaidia mama mkwe wake kupanga juu.
" nzuri,kama unajisikia vibaya kapumzike sisi tutamaliza hapa" anaongea Nzagamba akimwangalia kwa kumpima utadhani huo ugonjwa utaonekana kama tembo.
" Niko sawa" anajibu Tulya macho yake yakitoka kwa Nzagamba na kwenda kwa mama mkwe wake aliyekuwa anawaangalia au kufuatilia mazungumzo Yao,anampango wa kuniua Leo huyu anawaza Tulya.Anapata aibu asijue Nzagamba anafanya nini Mbele ya mama yake anaamua kuwa makini na kazi yeke.
" una uhakika uko sawa?" anasikia sauti ya Nzagamba karibu yake kabisa anageuka na kumwangalia na macho yake yakienda upande alipo Bibi sumbo asimuone.
" usihofu kuhusu mama,kama unaumwa kapumzike" anaongezea baada ya kumuona akiangalia huku na kule.
" Niko sawa,kilichokufanya useme naumwa nini?" anamuuliza macho yake yakimwangalia.
" nilikusikia usiku ukigeuka,karibua usiku kucha hujalala" na hukuja kuniuliza kama Niko sawa anamjibu kimoyoni.
" Niko sawa,nilikosa usingizi tu,ungeniamsha"
" Mimi nikaona nisikusumbue labda hujisikii vizuri" anamjibu.
" ningekuwa nimeshakufa na kukauka mda unakuja kuniangalia maana ukasubiri mpaka asubuhi" anajibu Tulya na Kisha kumkazia macho baada ya kumuona akitabasamu.
" kimekufurahisha nini?" anamuuliza macho yake makubwa yakiwa yametulia kwake kama bahari tulivu.
" una macho mazuri" anamjibu akiendelea kumwangalia huku akitabasamu maneno yake yanamshtua Tulya na pasipokujua anaangalia chini kwa aibu
" nenda kamalizie kukata Kuni" anamfukuza akijua Bibi sumbo akiwakuta atachimba shimo ajichimbie safari hii hatanii,na kama siyo mbaya anamsikia Bibi sumbo akija akiimba anageuka na kumwangalia Nzagamba aliyekuwa bado amesimama pale pale.
" nenda" anamwambia kwa sauti ya chini kama asitake mtu awasikie.
" kwani nimefanya nini?" anauliza Nzagamba akifurahia kumuona Tulya akihaha na kabla hajategemea anamuona Tulya akipiga hatua ndefu akihama mahali walipo. kama hataki kuondoka basi ataondoka yeye kama yeye amemzoea mama yake siyo yeye na tangu lini ameanza kuwa sina aibu namna hiii anawaza Tulya akisimama upande mwingine na kujifanya kazi yake ya kupanga Kuni ndio anayoiona maeneo haya.
" imekuwaje unazihamishia huku" anamuuliza mama mkwe wake akijifanya hajamuona Nzagamba anayehisi macho yake mgongoni kwake.
" siku zote zinakaaga huku,sababu ya kiangazi niliziweka kule,ila harufu ya Hali ya hewa imeanza kubadilika masika yanakaribia nimeona niziweke mahali pake" anajibu Bibi sumbo.
" mbona kule Mbele ndio kuzuri na tena karibu na jikoni" anaongea Tulya akiangalia umbali wa Kuja kufuata Kuni huku.
" ndio ni kuzuri,lakini wakati wa masika sio kuzuri,inaweza kuficha wanyama wakali"
" unamaanisha nini?" anauliza Tulya kwa mshtuko.
" unajua mvua zikianza kunyesha Kuna wanyama wengine huanza Kuja kijijini,na Kuna wakati wanaweza kupitiwa jua likachomoza bado hawajarudi porini wakaamua kujificha huko chini uvunguni au usiku ukiwa unaenda chooni si unaona pale zilipokuwa huwezi ona nyuma yake Kuna nini hivyo unaweza kushangaa umeshambuliwa na mnyama" Tulya anameza funda la mate macho yakimtoka pima asijue kama wanamtania au la.
" unatania si ndio?" anaamua kuuliza kilichopo kichwani pake kwa sauti ya juu macho yake yakitoka kwaBibi sumbo na kwenda kwa Nzagamba na kuwaona sura zao sio za utani kabisa.
" hapana mwanangu,Mimi nimewahi kukimbizwa na chui hivihivi sema niliwahi kuingia ndani,na ndio ikawa sababu ya kutokuweka Kuni kule." Bibi sumbo anamjibu.
Tulya anabaki amesimama asijue tahadhari aipokeeje maana kwa sasa tayari anayachukia masika ghafla tu na anaomba yasije kabisa lakini hajui kama ombi lake litajibiwa.Nzagamba anatabasamu baada ya kumuona Tulya ameduwaa utadhani Mbele yake tayari kasimama chui au Simba.
" masika ndio wakati wa kuwa makini sana huku" anamsikia Nzagamba akiongea na kugeuka kumwangalia rohoni akisema Asante kwa ushari ambao hadhani kama unasaidia.
Na kwake yeye tahadhari ni kukaa ndani tu mpaka masika yaishe kwani hayuko radhi kuwa kitoweo Cha wanyama wenye meno makali,kitendo Cha kuwaza kutafunwa na Simba au chui kinamfanya mwili kusisimka .Anaamua kukazana kupanga Kuni kwani hataki kabisa kuweka makazi ya wanyama hao.