Tulya anageuka na kumuona Lindiwe akiwa amekaa chini akilia.
" unalia nini na kuwafaidisha watu,hivyo ndivyo walivyotaka wakuone dhaifu na ukiwa umevunjika" anamwambia akimwangalia anamuonea huruma sana.
" maisha yako nayo ni magumu tu mwenzangu" hata kama Lindiwe amemfanyia mambo mengi ya ajabu Tulya hakuwa mtu wa kumwacha mtu mwenye matatizo,isitoshe hapa mtoni asije akafika nyumbani akasikia Lindiwe amekufa kwa kuzama kwenye mto kwani Hali yake kwa sasa sio ya kumwacha peke yake.
Anakaa na kumsikia Lindiwe akilia kwa kwikwi mpaka pale alipotulia.Tulya anasimama anashika kibuyu chake anaingia mtoni anachota maji anatoka na kuweka pembeni anachukua na kibuyu Cha Lindiwe anachota na kutoka,anatengeneza ngata yake na kuiweka kichwani.
" amka tuondoke,unataka watu watukute hapa waseme tumegombana kwa sababu ya Nzagamba,kama bado una nguvu za kupambana na umbea mwingine kaa lakini Mimi sina mwenzako,kwa hiyo simama tuondoke" anaongea huku ameshika kiuno chake.
" kwa nini umenisaidia?" anauliza Lindiwe akifuta machozi.Tulya anacheka kidogo na kusema" sijakusaidia,ila niliona kilichokuwa kinaendelea hakikuwa sahihi hivyo kama binadamu nikaamua kutoa maoni yangu"
Lindiwe anasimama nakuweka ngata yake kichwani anainama na kuweka kibuyu chake kichwani Tulya naye anafanya hivyohivyo.
" hujui hata kuchagua marafiki,ulikuwa unaishi nao vipi pasipo kujua rangi zao halisi" anaongea Tulya wakianza kutembea.
"sikujua kama Mbula alikuwa anampenda Manumbu" anajibu Lindiwe,hata wewe utakuwa na akili nzito tu au huyo rafiki yako Yuko vizuri kuficha makucha yakeanawaza Tulya ,subiri kidogo anasimama Tulya na kumwangalia Lindiwe.
" umesemaje?" anamuuliza.
" sikujua kama alikuwa anampenda Manumbu" anasema Lindiwe akikereka kidogo kurudiarudia maneno " hapana,jina lake anaitwa nani?"
" mke wa Nsio, Mbula"
Tulya anabaki mdomo wazi akimkumbuka Mbula wa kijijini kwao aliyefanya figisu za kuolewa na Luila.Itabidi nikae mbali na watu wenye majina haya anawaza Tulya akianza kutembea.Safari yao inatawala ukimwa mda wote Kila mtu akiwaza lake.
"jioni njema" anamuaga Lindiwe Baada ya kufika njia panda ya kuachana.Anapiga hatua kadhaa na kusimama.
" Lindiwe" anamwita, Lindiwe anasimama na kugeuka kumwangalia.
" usiache maneno Yao yakunyime raha,Nina Imani Kila kitu huja kwa wakati wake,jifunze kuwa mvumilivu na mwenye subira,nakwambia hivi kwani yamewahi kunikuta,kingine Kaa mbali na watu kama wale ni sumu iliyo hewani unaweza kuvuta ikakuua,uwe na jioni njema" anampa tabasamu na kuondoka,.
Lindiwe anasimama akimwangalia Tulya akipotea macho yake yanajaa machozi tena na pasipo kujua yanaanguka kwenye mashavu yake yakitiririka mpaka kidevuni kwake na hatimaye kufika chini.Hajaamini kama marafiki zake wa suku nyingi walikuwa hawamchukulii kama rafiki kawakosea nini siku zote alichokifanya ni kuwa nao pale walipomhitaji pasipokujua walifurahia mateso yake na kumuombea mabaya,anawaza Lindiwe akizidi kulia labda na yeye atakuwa anamkosi watu hawajui tu.
Tulya anafika nyumbani anaweka maji,anaingia ndani kwake anatoka na shanga kwenye kisonzo anakaa nje kwenye mkeke na kuanza kuzitengeneza kwa ajili ya kuvaa siku ya harusi ya Sinde iliyokuwa ni siku Sita zijazo pamoja na siku ya sherehe ya vijana kutoka lindoni.Baada ya kuona Giza limeanza kuingia anarudisha shanga ndani na kuelekea jikoni kuandaa Cha jioni.
" mama sijui kaenda wapi?" anajiuliza akiingia ndani maana mama mkwe wake amekuwa akitoka sana siku hizi sio kama zamani na Hali hii inamtia wasiwasi Tulya kwani afya yake sio nzuri na mara kwa mara amekuwa akilalamika maumivu ya miguu,ataongea naye Leo akirudi apunguze kutembea.Anakoka moto na kuchukua chungu anatoka nacho nje kwenda kuosha.akiwa ameinamana anaosha chungu anasikia sauti ya mbiu.
" rombo" anaongea baada ya kusikiliza sauti yake vizuri." watakuwa wanaenda kuwinda,sijui watafika wapi maana wamesema wanyama wamefika mbali" anaongea mwenyewe akiendelea kuosha chungu baada ya kumaliza anaelekea ndani lakini anasimama baada ya kumuona mama mkwe wake.
" ulikuwa wapi mama?" anamuuliza akiweka chungu chini na kwenda kumpokea furushi lilojaa ukili." unalalamika miguu inauma inabidi upunguze kutembea" anaongea akibeba furushi.
" nipo sawa mwanangu,Nzagamba karudi?" anamsikia Bibi sumbo akimuuliza anaweka furushi kitandani na kugeuka kumwangalia.
" bado,kuna nini?" anamuuliza baada ya kuona uso wake una wasiwasi.
" mmmh" anaguna Bibi sumbo
" Kuna nini mama?" anaongea Tulya akija kusimama alipo akianza kupata wasiwasi
" niletee kigoda" Tulya anamkimbia ndani upesi na Kisha kurudi na kigoda anakiweka karibu na ukuta Bibi sumbo anaenda kukaa.
" aiiiaiiii" anapiga makelele Bibi sumbo akinyoosha miguu yake vizuri iliyokuwa inavuta kwa maumivu kutokana na kutembea.
" ndio maana nakwambia upunguze kutembea" Tulya anamwambia akishika kiuno.
" hilo sio la muhimu kwa sasa,tutafanyeje Tulya?" anaongea Bibi sumbo akimwangalia mkamwana wake .
" Kuna nini kwani mama?"
" umeisikia mbiu ya rombo?" anamuuliza
" ndio,kwa mbali kwani haijapita karibu na huku"
" wanaume wote wenye umri wa kwenda kuwinda waliooa wanatakiwa kwenda kuwinda,hivyo Nzagamba naye anatakiwa kwenda" mikono iliyokuwa kiunoni mwa Tulya inashuka yenyewe na kukaa Kila upande ikikosa nguvu.
" unasemaje?"
" ndio hivyo mwanangu, tutafanyeje hawezi kukwepa hili" anauliza Bibi sumbo utadhani Tulya anauwezo wa kuzuia.
" lakini si wanajua tatizo lake hawezi kwenda?" anauliza Tulya asijue jaribu hili kimetokea wapi.
"Ndio,lakini Sasa kaoa na rombo hii ni kwa ajili ya vijana wanaotoka lindo,wao wataachiwa kesho kwa ajili ya kupimwa kama wanaweza kuwinda na Kisha siku ya sherehe kabisa ambayo ndio watu wengine wote wanatakiwa wakawinde kuleta chakula Cha sherehe,tutafanyeje Tulya sitaki kumuona kijana wangu akivunjika moyo tena,hili litamuumiza mwanangu" anaongea Bibi sumbo na kumfanya Tulya midomo yake kukauka asijue asemeje au Cha kufanya hawezi kumuona Nzagamba akiwa na huzuni tena baada ya Kila kitu alichofanya kuona tabasamu lake.
" wanatakiwa kuondoka lini?" anajikuta akiuliza kama siku itasaidia kutatua tatizo.
" kesho kutwa" anaongea Bibi sumbo sauti yake ikikwaruza na roho inamuuma Tulya kwani hajawahi kumuona Bibi sumbo akiwa hajiwezi namna hii siku zote amekuwa akimuona ni mwanamke imara na shupavu,je Nzagamba atakuwa katika hali gani anajiuliza na atafanyeje?Mtihani wa aina gani huu uliomkuata.
Anaingia ndani ana andaa chakula lakini kinakosa mlaji,anamlazimisha mama mkwe wake kula kidogo na kumpeleka kitandani anahakikisha anapitiwa na usingizi ingawa ilimchukua mda lakini kwa sasa anashukuru kuwa alienda kutembea kwani uchovu umemsaidi kulala mapema la sivyo ana uhakika angekesha akimuwaza kijana wake.
Sasa anaelewa ni mateso gani walikuwa wanapitia Nzagamba na mama yake kama kwa sasa Iko hivi kipindi kile ilikuwaje?
Anakaa nje akimsubiri Nzagamba arudi lakini usiku unaenda Nzagamba hajarudi." uko wapi Nzagamba?" anajiuliza akiendelea kukaa na kusimama pale kitandani akimsubiri,ingekuwa ni mchana anauhakika Sasa hivi angeshazunguka Kijiji kizima kumtafuta.
anaamua kuingia ndani kumsubiri kwani nje kumekuwa panamtisha sana.
Akiwa amekaa sebuleni anaona mlango unafunguliwa na Nzagamba anaingia,anasimama alipokuwa amekaa mapigo yake ya moyo yanaenda mbio huku akivuta na kutoa pumzi ndefu kwa ahueni aliyoipata baada ya kumuona Yuko salama. lakini moyo wake unavuja damu baada ya kuona sura ya Nzagamba ikiwa na huzuni,ukionekana kuchoka kwa masaa machache tu baada ya kusikia mbiu kwani asubuhi alivyoondoka mume wake hakuwa hivi na hii inaonyesha ni jinsi gani hili linavyomsumbua.
" hujalala?" anamuuliza akigeuka na kufungu komeo la mlango.
" nitalalaje mme wangu hajarudi nyumbani" anajibu Tulya akimpatia tabasamu.
" nikuwekee chakula?" anamuuliza akisogea kumwachia kiti akae.
" hapana,nataka kulala nimechoka" Tulya anaelewa hataki kuzungumzia hili na hivyo kuheshimu maamuzi yake na wanamuda mwingi siku ya kesho kuzungumzia tatizo linalowakabili kwa sasa amuache kwani itakuwa imekuja kwa kushtukiza kwao wote na ana uhakika kama Nzagamba akitakakulizungumzia hili atamwambia anacho kiwaza na safari hii hataki kumfuata anataka Nzagamba aje mwenyewe kama anaona yeye ni mtu muhimu kwake.
" naweza kupata maji ya kunywa?"
" ndio" anaitikia tulya na kwenda haraka haraka kilipo kibuyu na kumimina maji anampatia.Baada ya kumaliza kunywa Tulya anachukua kipeo na kukirudisha.Anatoa ngozi na kutandika wakati huo Nzagamba akimwangalia tu.
" tayari" anaongea Tulya akisogea pembeni Ili Nzagamba apite kulala.
" Asante" anaitikia akimwangalia.
" usiku mwema" anamwambia na kugeuka kuelekea chumbani lakini miguu yake inakufa ganzi baada ya kusikia maneno ya Nzagamba sauti yake ikiwa imejaa maumivu na kuelemewa,sauti ya mtu aliyepotea asijue njia,moyo wake unakuwa kama umeangukia kwenye shimo lenye sindano nyingi nazo zimeushambulia.
"Nifanyeje Tulya?"