Ni wiki mbili Sasa zimepita tangu Tulya ameota ndoto ya Ndesha na anashukuru haijajirudia tena kwa sababu hataki hata kuifikiria.Maisha yake na Nzagamba yamekuwa ni mazuri kuliko awali wamekuwa wakiwasiliana vizuri kama mke na mume isipokuwa Mmoja bado analala sebuleni mwingine chumbani. Tulya hajui hii Hali itaendelea mpaka lini kwani ameshatoa ishara zote za kutaka Nzagamba aamie chumbani kwake lakini mwanaume bado anataka kulala sebuleni.
" sijui nimwekee nyoka pale chini usiku?"
" umesahau kama mumeo ni mpiganaji Nina uhakika atamsaga kama unga kabla hata hajamfikia"
" asante kwa kunikatisha tamaaa" anajibu Tulya akijitupa kitandani.kwa wakati huu yupo na binamu yake na rafiki yake Sinde siku ya Leo ameamua Kuja kumtembelea ikiwa shamra shamra za harusi yake zikiendelea.
" phuuuu" anatoa pumzi Tulya macho yake yakiwa kwenye dari.
" au hujabobea kumtega tu,kwa urembo wako huo ni mwanaume gani rijali wa kuangalia tu asifanye kitu"
" nimeshafanya Kila kitu Sinde" anaongea Tulya kwa sauti ya kuchoka utadhani kabebeshwa Dunia nzima mabegani mwake pasipo kujua ni jinsi gani anamtesa mtoto wa Bibi sumbo anayesubiri mwaliko wake Kila siku.
" una bahati sana Sinde,mumeo mtarajiwa atakuwa anaona siku zinaenda polepole"
" usijali,Nina uhakika hata kwako mambo yatakuwa mazuri tu" Sinde anampa moyo.
"au kwa nini usimwambie tu unachotaka"
" ingekuwa wewe ungesema au unaongea tu,kwanza alisema nimpe mda labda bado anataka muda zaidi"
" si umesema mnaongea vizuri tu na ulishamwambia unampenda bado anataka nini?" anauliza Sinde akimwangalia Tulya akiwa amelala.
" nimepata wazo nina uhakika litafanya kazi" anaongezea na kumfanya Tulya aamke na kukaa.
" wazo gani?" anamuuliza.
" kwa nini usisubiri muda wa usiku akiwa sebuleni ujifanye unaenda kuoga uangushe kaniki kama bahati mbaya"
Tulya anamwangalia kwa mda na kusimama.
"naondoka,mama mkwe wangu hajisikii vizuri mkono unamuuma kwa hiyo inanibidi niwahi kurudi leo"
" na wazo langu je umelionaje?"
" kalitumie kwako na Tinde kwani Mimi sijakosa aibu namna hiyo" anamjibu.
" ehhh!,Nina uhakika hiyo ndio njia pekee rahisi"
"Sinde, Nzagamba ni mume wangu nataka anitake kwa hiari yake mwenyewe siwezi kufanya vitu vya kujidhalilisha mpaka anione Mimi mwanamke nisie na stara,kwa sasa nitamwacha kama alivyo" anatulia kidogo.
" ila nitamfanya ajute kwa haya yote siku akijilengesha we mwache tu" anaongea uso ukiwa na hasira
" unanitisha,kama namuona atakavyoteseka" anamalizia Sinde kwa kucheka akimwangalia Tulya akiondoka.
"namuonea huruma Nzagamba,sio kwa hasira hizo" anaendelea kucheka Sinde.
" usikose Kuja kesho" anapiga makelele kwa nguvu Ili Tulya amsikie huko nje.
Baada ya shughuli zake za siku jioni ya saa kumi Tulya anaamua kwenda mtoni anafika na kumuona Lindiwe akiwa amesimama mbali kidogo na mto na kibuyu chake." kakosa maji au" anajiuliza Tulya akiendelea kusogea kadri anavyozidi kwenda anasikia sauti za wanawake wengine.
" yaani hata sijui ana matatizo gani,inakuwaje aanze kujipendekeza kwa Nzagamba tena" anamsikia mwanamke akiongea baada ya kukaribia alipo Lindiwe na kuwasikia vizuri kabisa.
"huwa sipendi namna anavyojisikia,hivi umesikia kuwa mumewe analala na wanawake kibao huko nje?" anaongea mwanamke mwingine.
"ndio, nashangaa uzuri wake unafaida gani kama mumewe hamuoni,na ile kupigwa Kila siku ndio inanifurahishaga" wanaongea wanawake na kuangua kicheko.Haikumchukua mda mrefu Tulya kugundua kuwa walikuwa wanazungumzia Lindiwe lakini Cha ajabu zaidi wale wanaozungumza hivyo ni marafiki zake,ubinadamu kazi anawaza Tulya akimwangalia Lindiwe anayelengwa na machozi.miguu yake ikiwa imeganda chini asijue awakabili marafiki zake au arudi nyuma anatikisa kichwa kwa masikitiko,amesimama hapa kwa mda gani anajiuliza Tulya
" kwa hiyo rafiki hata usimwambie chochote kuhusu huo ujauzito huwezi jua wivu ni kitu kingine"anaongea rafiki yake mwingine ambaye Tulya amemjua kama mke wa Nsio.
" mwenzako hapa nakaa kimya atashtukia tu tumbo linajitokeza,naweza nikamwambia akanuna ama akaona namringishia kwa sababu yeye hazai"
" anune?kwani sisi ndio tumemfunga tumbo la uzazi,Kila mtu na bahati yake yeye kajaliwa uzuri lakini mizimu imemnyima Cha muhimu zaidi" anamalizia kwa kucheka mke wa Nsio.
Tulya anamwangalia Lindiwe na kummwonea huruma zaidi.
" kwani wale sio marafiki zako?" anamuuliza na kumfanya Lindiwe ashtuke kwani hakumuona wakati anafika.wanawake wanaendelea kuongea na kucheka utadhani wamemiliki mto wote.
" mizimu haikupi vyote" anaongea mwanamke mwingine.
" yaani Mimi huwa sipendi anavyokuja kujieleza kwetu,sema namvumilia tu kwani nataka kujua Kila mateso anayopitia kutoka mdomoni kwake" anaongea mke wa Nsio na kumfanya Tulya kubaki mdomo wazi na angekuwa kwenye nafasi ya Lindiwe wanawake wote wawili wangekuwa wanaogelea kama kambare mtoni muda huu anawaza Tulya.
" bado una hasira naye tu,kwa sababu alikunyang'anya Manumbu,lakini hakujua kama unampenda angekuwa anajua labda asingeolewa nae" mwanamke mwingine anamtetea Lindiwe lakini mke wa Nsio hajakubaliana nae anasema.
" hata kama angejua,angefanya velevile kwa sababu anataka vya thamani na unajua alimwambia baba yake atumia madaraka yake kumlazimisha Manumbu amuoe baada ya kuona kwa Nzagamba haiwezekani,naomba mizimu asizae kabisa Ili awe kiburudisho changu siku zote za maisha yake"
Sasa hii imezidi anawaza Tulya na pasipokujali anapiga hatua kuwafuata wanawake mtoni " hamna hata aibu" wanashtushwa na sauti ya Tulya wanageuka na kumwangalia lakini macho yanawatoka pima baada ya kumuona Lindiwe akiwa amesimama umbali kidogo na walipo.
" mnamfanyanyiaje rafiki yenu ukatili wa namna hiyo,mateso yake yanawafanya mlale usingizi mnene itakuwaje siku yakiwakuta nyie mmmm?" anawauliza Tulya akiwashikia kiuno baada ya kuweka kibuyu pembeni.
" Lindiwe!" anaongea mwanamke mwingine baada ya Lindiwe kusogea mahali walipo.
" nimewakosea nini Mimi mpaka mnitakie mabaya" anawauliza Lindiwe machozi yakimtoka.
" usitake kujifanya hujui,na mengine umesikia mwenyewe" anajibu mke wa Nsio akiwa Hana aibu kabisa baada ya kukamatwa anaamua kuonyesha rangi yake halisi.
" kwamba nimekuibia Manumbu sikufanya ki..." lakini mke wa Nsio anamkatisha.
" acha hizo wewe Kila mtu anajua kama ulimwambia baba yako akamlazimishe Manumbu akuoe baada ya kumkosa Nzagamba"
" sio kweli mbu.."Lindiwe anajaribu kujitetea lakini mwanamke hamuachi anazidi kumkanda kwa maneno.
Mwanamke mjinga huyu si anatakiwa kushukuru hajaolewa na huyo Manumbu baada ya kuona maisha anayopitia mwenzake lakini bado analalamika anawaza Tulya akimwona mke wa Nsio mjinga wa mwisho au wivu umemtawala.
" Unamtetea huyu,hujui tu alikuwa anakuwazia nini,kama hujui Sasa mwenzio alikuwa na mpango wa kumtega Nzagamba Ili akunyang'anye,ndivyo alivyo,mbinafsi huyu sana huyu mwanamke" Tulya anamwangalia mke Nsio anayemwingiza na yeye katika mkumbo wa ugomvi wao akitamani asingeingilia na kumwacha Lindiwe apigane vita yake mwenyewe kwa sababu yeye hawezagi kuongea na watu wasiojitambua kama mke wa Nsio maana unaweza kupasuka kichwa Bure kwa kujaribu kulinganisha mawazo lakini hasira zilimpelekesha na kujikuta Yuko hapa.
" hayo ni kati yangu na Lindiwe,na hata kama Lindiwe angeniibia mume wangu bado nisingekuwa na mdomo mchafu kama wako wa kufurahia mateso yake na kumtakia mabaya," anajibu Tulya na kutulia kidogo " na kingine Lindiwe ni Bora kuliko wewe unajua kwa sababu gani?" anamuuliza akimsogelea mke wa Nsio " kwa sababu hafichi uhalisia wake kuliko wewe unayejifanya una ngozi Moja tu kumbe unazo nyingi ikikomaa hii unaitoa na kuvaa nyingine kama chatu"
" unamwita nani chatu?" anakuja juu mke wa Nsio.
" wewe,unataka kufanyaje Sasa" anajibu Tulya na yeye akija juu rohoni akitamani kupasua ubongo wa nyumbu huyu.
" mwache,tuondoke" rafiki yake anamvuta mke wa Nsio lakini mwanamke huyu hakutaka kupoteza kwa Tulya anausukuma mkono wa mwenzake na kusema.
" sijui hata unaringia nini? wakati maisha yako yote utakula ndege mpaka utoke manyoya"
Mwanamke anajua kugusa panapouma huyu anawaza Tulya lakini hajui kuwa vitu kama hivyo huwa havimsumbui anaamua kufuta tabasamu lake la ushindi mapema.
" Mimi nimeridhika na Hali yangu lakini ninavyokuona wewe hata umezeshwe mto mzima kiu yako ya uchu na kutaka vingi haviwezi kukatika" anamjibu na kuona jinsi uso wa mke wa Nsio ulivyosuuzika kama mrina asali aliyekosa asali baada ya shida zote za kupambana na nyuki.
" tuondoke bwana" rafiki yake anafanikiwa kumvuta mke wa Nsio na kubeba vibuyu vyao waondoke.
" pwiiii"
Kina sikika kibuyu Cha mke wa Nsio baada ya kukutana na ardhi kinapasuka na maji yanamwagika.
" ohh inabidi urudi tena mtoni" Tulya anamwambia akitabasamu.
" umenitega" mke wa Nsio anakuja juu akimwangalia Tulya.
"usinisingizie Mimi,ilaumu mizimu kwa kukupa madole yamebebana kama uyoga,isitoshe wewe ndo ulisema mtu hawezi kupewa vyote,ohh nilijisi nimepamiwa na kifaru" anajibu Tulya kistaarabu akikagua mguu wake na ukweli ni kuwa yeye ndiye aliyesogeza mguu wake baada ya kumuona mke wa Nsio akipita karibu yake na kumfanya anesenese na katika harakati za kujiokoa anapoteza kibuyu chake.
mke wa Nsio na mdomo wake wote kajikuta anamwangalia tu Tulya asijue Cha kumfanya hivyo kuamua kuokota ngata yake na kuondoka.