Miguu ya Tulya inanng'ang'ania chini kama imeota mizizi.kwani Kila akijaribu kupiga hatua anajikuta miguu haitaki kusogea.Anamwona Lindiwe akiongea na kutabasamu kama mtoto kaokota kibuyu Cha asali.anakumbuka siku aliyomwambia atamfanya ajute 'alikuwa anamaanisha hiki au ' anajiuliza.lakini hata kama Lindiwe aliamua kujisogeza karibu na mumewe bado maamuzi yanabaki kwa Nzagamba endapo amwache awe karibu nae ama laa. lakini kama anazidi kuwa karibu naye na Nzagamba amemwacha basi ameridhika na Hali hiyo hata aongee ama awafume pale bado maamuzi yatakuwa kwa Nzagamba yeye hawezi kuzuia anachotaka kukifanya.
Miguu yake inageuza mwelekeo na kurudi alikotoka mkono wake ulioshika kikapu ukiking'ang'ania utadhani Kuna mtu anataka kumnyang'anya,mkono wake mwingine ukienda usoni kufuta machozi yaliyotoka pasipo ruhusa yake "unalia nini Tulya wakati unafanya maamuzi ya kuolewa uliyajua yote haya" anapiga hatua kadhaa lakini kabla hajafika mbali anamwona mama Nsio akiwa na mwanamke mwingine wakija maeneo Yale" Hawa wanawake ..." anajiuliza afanyeje maana wakiwaona Nzagamba na Lindiwe pale hadithi itakuwa nyingine kabisa.
Anageuza haraka haraka na kuelekea walipo Nzagamba na Lindiwe " Wanaongea tu pasipo wasiwasi" anawaza akiongeza mwendo.
" afadhali nimekukuta hapa maana mwendo wa mpaka mtoni na jua hili" anaongea baada ya kuwakaribia,wote wanageuka na kumwangalia huku Lindiwe akitoa tabasamu la kinafiki " subiri tuone kama tabasamu lako litabakia usoni baada ya kuwaona chiriku wa Kijiji hiki" anawaza Tulya akiweka mkono wake kwenye paji la uso wake kujikinga na jua " habari yako Lindiwe" anasalimia kwa tabasamu pana huku akisogea na kusimama karibu na Nzagamba.
Na pasipo kusubiri Lindiwe amjibu anamgeukia Nzagamba " kumbe afadhali nilipita njia hii ningepita kule ningefika mtoni nisingekukuta" wakiwa bado wanamshangaa Tulya wanasikia sauti za watu wakija na punde anafika mama Nsio na mwenzake.
" hamjambo?" mama Nsio na mwenzake wanawasalimia na wote wanaitikia " hatujambo shikamoni" " Marahaba" mama Nsio anamwangalia Tulya aliyebeba kikapu " naona umemletea mumeo chakula" Nzagamba na Lindiwe wote macho Yao yanaenda mkononi kwa Tulya ambaye yeye mwenyewe alikuwa anakiangalia kikapu chake na kabla hajajibu Mama Nsio anaendelea " inavyoonekana ulianza kumtafuta mpaka umemkuta huku" anaongea huku akimwangalia Lindiwe.Tulya anatukana kimoyomoyo na kuamini kuwa huyu mama kweli ni mmbea na sio mmbea tu anajua kuchambua mambo.
Anamwangalia Lindiwe anayetetemeka kama kalazwa nje usiku kucha wakati wa masika na Kisha macho yake kwenda kwa Nzagamba aliyekuwa ametulia kimya na asiye na hofu kama hajakutwa kwenye Hali ya mtafaruko .Anatabasamu na kumwangalia Mama Nsio " hapana sijamtafuta,Mimi na mume wangu tulikuwa tunaelekea mtoni tumekutana na Lindiwe hapa tukawa tunasalimiana" anaongea na kumfanya Nzagamba amwangalie na asishangae kwani mwanamke huyu anajua kudanganya hawezi hata kushangaa tena,na inamkera zaidi kwani uongo wake unaaminika na yeye alikuwa anaelekea kuanguka kwenye mtego wake " Mimi naondoka" anaongea na kuanza kuondoka akiwaacha wanawake waendelee na gumzo lao." haya tangulia nakuja sio mda" anamsikia Tulya akiongea lakini hajibu anaendelea kutembea tu.
" Lindiwe mbona hukuja kuchukua zile shanga " mwanamke mwingine anamuuliza Lindiwe wakati huo Mama Nsio akiwa makini kuisoma hali aliyoikuta " mambo yalikuwa mengi kidogo nitakuja Leo jioni kuchukua" anaongea Lindiwe akijichekesha " ohh,vizuri nikajua umepata kwingine" " hapana,nilizipenda sana shanga zako" anaongea Lindiwe akiendelea kujichekesha Ili kuficha woga wake usionekane lakini Tulya na Mama Nsio wanauona vizuri ' kumbe unaogopa eee' anawaza Tulya akiendelea kumkazia macho Lindiwe anageuza macho yake na kukutana uso kwa uso na macho ya Mama Nsio,Tulya anampa tabasamu na Mama Nsio analirudisha."Naona mmekuwa marafiki?" anauliza Mama Nsio akiwaangalia wote wawili.
" ndio tunajuana, kidogokidogo nadhani sio mda tutafika huko Mama Nsio" anajibu Tulya akiendelea kuokoa jahazi " ndio" Lindiwe naye anaitikia." vizuri,kwa sababu mke wa Nzagamba ni mgeni ni bora akajuana na vijana wenzake" anaongea mwanamke na Mama Nsio anadakia " ndio ni vizuri,ila uangalie tu marafiki wengine wanaweza kukuchoma mkuki mgongoni" anaongea huku akimwangalia Lindiwe " asante nitaliweka hilo akilini" Tulya anamjibu macho yake yakiwa kwa Lindiwe."twende Mama Nsio, Lindiwe usisahau basi Nina shida na hiyo ngozi" anaongea mama nkwasi huku akimvuta rafiki yake waondoke " sawa mama nkwasi" anajibu Lindiwe na macho yake yakiwasindikiza wanawake hao mpaka walipopotea katika upeo wa macho yake na kuvuta pumzi ndefu ya ahueni.
" kumbe unaogopa eee, ila kwa nini ufanye vitu vinavyokuweka katika hali Tete" anashtushwa na sauti ya Tulya anageuka na kumwangalia na Kisha kutoa tabasamu la kinafiki" vipi kuhusu wewe,unaogopa ee,kwamba mumeo anaweza kurudi kwangu"
Tulya anatabasamu na kumwambia " nakuonea huruma sana,kwa hiyo ulivyosema utanifanya nijute lengo lako lilikuwa ni hili?" anaongea kama sio kitu cha kumtisha lakini moyo wake pekee ndio unaojua hali yake halisi na hayuko radhi kumuonyesha nyoka huyu mwenye mabaka woga wake anawaza Tulya.
" mumeo anajua kama unajitupa kwa mwanaume wako wa zamani?" anatulia kidogo akiangalia jinsi sura ya Lindiwe inavyomshuka na hiyo inampa nguvu " nilisikia kwa wakulima kuwa wakivuna mtama huuweka chini wanachukua fimbo wanaupiga na kuhakikisha unatoka kwenye makapi Kisha huyatoa na kuyatupa,lakini ninavyomjua mumeo anavyojua kupiga akisikia hizi habari Nina uhakika kuwa hatutapata hata makapi ya kutupa wala mtama"
Lindiwe anatetemeka lakini anajikaza asitake kushindwa na Tulya " wewe hofia kuhusu mumeo wewe kukukimbia na sio Mimi kupigwa"
"mume wangu hawezi kunikimbia Lindiwe wewe ruka utue mume wangu atabaki na Mimi milele zaidi atakachopata ni maneno ya watu tu ambayo sidhani kama atayatilia manani kwani ameshazoea kusemwa na baada ya muda yatapita na mimi hapa.." anatulia kidogo na kumsogelea Lindiwe anapiga hatua nyuma Tulya anatabasamu."....Mimi nitakuwa mwanamke anayetia huruma zaidi duniani Kila mtu atanionea huruma kwani nitakuwa ni muhanga katika usaliti wenu,tuje upande wako Lindiwe,nadhani sina haja ya kukwambia utakuwa wapi katika hadithi yetu pendwa,kwa hiyo acha upumbavu wako kabla maji uliyochota hayajarudi mtoni ukakosa kutofautisha ni yapi yaliyokuwa kwenye kibuyu chako" anamsogelea na kumnyoshea kidole " Kaa mbali na mume wangu Lindiwe kwani sitakuacha umharibie heshima yake aliyobakisha"
Anaweka kikapu chake vizuri na kuanza kuondoka anapiga hatua chache na kusimama anageuka na kumwangalia " tafuta njia ya kumfunga mdomo mama Nsio maana sidhani kama amenunua uongo wangu niliomwambia si unamjua" Tulya anaondoka akimwacha Lindiwe aking'ata meno kwa hasira,aibu na woga.
Tulya anaendelea kuchanja mbuga akipita vichaka kuelekea Nzagamba alipo miguu yake ikikanyaga ardhi kwa nguvu kama ardhi ingekuwa na mdomo Nina uhakika ingemwambia nionee huruma hujagombana na Mimi wataka kuniua bure na chakula kwenye kikakapu kingesema taratibu nitaanguka.miguu yake inasimama ghafla baada ya kusikia sauti ya karimba ya Nzagamba." nyimbo hii tena?" anajiuliza nakuanza kutembea tena "atakuwa kakumbuka mapenzi yake ya zamani" anaongea huku akitembea akihisi kitu kikimkaba koo na angekuwa karibu na kipeo Cha maji angekunywa funda kubwa kwa kisingizio Cha kukabwa na kiazi.
Anafika na kumuona Nzagamba akiwa amekaa chini ya mti akipiga karimba anaweka kikapu chini.Nzagamba anaacha kupiga kariba baada ya kuona kikapu mbembeni yake na pasipo kugeuka anajua ni nani aliyekuja anachukua anataka kupiga tena lakini vidole vyake vinasimama baada ya kusikia sauti ya Tulya." mama kasema nikuletee chakula" Tulya anaongea akimwangalia "kwa hiyo mama asingesema asingeleta" anawaza Nzagamba na kuendelea kupiga karimba yake Tulya anasimama kwa mda nakuamua kuondoka.
Baada ya kusikia hatua za Tulya zikipotea Nzagamba anaangalia alikoelekea "ulikuwa unategemea nini?" anaangalia kikapu na Kisha macho yake yanaelekea mtoni kwenye mtego wake uliokuwa umenasa ndege watatu kwa mda mrefu na alikuwa bado hajaenda kuwatoa.Anaiweka karimba yake pembeni na kusimama lakini kabla hajapiga hatua anasikia hatua za mtu akija anageuka na kukutana na Tulya macho kwa macho.
" ulikuwa unafanya nini na yule mwanamke ?"
anamwangalia kwa mshangao kama haelewi Tulya anazungumzia nini.
" nimekuuliza ulikuwa unafanya nini na Lindiwe?"