Baada ya kuingia ndani Nzagamba anavuta pumzi ndefu ya ahuweni baada ya kutolewa kijasho Cha jioni na shemeji zake.
" nishushe" anamsikia Tulya akiongea mgongoni kwake na kumshusha harakaharaka.
Anageuka na kumwangalia Tulya aliyekuwa akinyoosha shingo yake akiwa amerudisha kichwa chake nyuma kidogo na mkono wake ukiwa nyuma ya shingo yake.
" vipi umeumia?" anamsikia Nzagamba akiuliza na kuacha alichokuwa akikifanya na kumwangalia.
Mwanga hafifu wa kibatari uliokuwa ukiwaka sebuleni hapo lakini hakuuona uso wake vizuri kutokana na yeye kuupatia mwanga mgongo na kumfanya Tulya asijue kama alikuwa na wasiwasi juu yake.
" hapana,shingo tu imechoka kutokana na kuangalia chini mda mrefu"
Anajibu akimwangalia Nzagamba usoni na kumfanya ayaone macho yake makubwa na ya kuvutia kwa ukaribu zaidi,kope za macho yake zikiwa ndefu kupitiliza yakifanya macho yake kufumba na kufumbua Kila baada ya sekunde kama tano au sita na yanapotulia macho yake yakiaksi mwanga wa kibatari kilichokuwa Mbele yake.
Pasipo kujua macho yake yanashuka kwenye midomo yake iliyokuwa ikicheza kidogo kama anatetemeka baridi ikimtamanisha,macho yake yanaganda hapo kwa muda na kufanya mawazo yake yakimbie kama swala anayekwepa kuwa kitafunwa Cha asubuhi Cha simba aliyelala njaa.
" Kuna nini?" anashtuliwa na swali la Tulya na kupiga hatua Moja kurudi nyuma akiukwepa ule ukaribu waliokuwa nao awali mapigo ya moyo wake yakimwenda mbio na mkono wake unaenda kifuani Mahali mdundo wa ngoma ya moyo ilipokuwa ikipigwa na kupashika asijue moyo wake ulikuwa unasherehekea nini.
Anakohoa kidogo kujaribu kurudisha akili, moyo na mwili na hali ya hewa ya mle ndani katika Hali ya usawa.
" karibu, hapa ndio nyumbani kwangu naanisha kwetu" anaongea akiangalia huku na kule mle ndani.
" hii ni nyumba yetu na ile ya pili ni ya mama nadhani utaiona vizuri kesho"
" asante" Tulya anaitikia macho yake yakiangaza pale sebuleni na kuona viti viwili vya miti vilivyoambwa ngozi sehemu ya kukalia na ya kuegemea vikichorwa mistari ya rangi nyeusi na vidoti kupendezesha.
Macho yake yanaenda upande mwingine na kuona mafiga matatu ya kukokea Moto na Sasa kukiwa na makaa kidogo ya moto yanayokaribia kuzima kutokana na kutokuchochewa kwa kuni kwa mda mrefu.
Upeo wa macho yake unampeleka juu ya ukuta wa mafiga hayo yakielekea juu kuangalia ukungu mweusi uliotanda ukutani ukiacha utando utando uliotokana na Moshi wa mda mrefu,akili yake inamtuma kuwa nyumba hii ni ya mda mrefu sana kutokana na moshi huo.
Katika ukuta huo anaona vibuyu vidogo vidogo vilivyokuwa vikining'inia kutokana na kamba zilizofungwa ukingoni mwa shingo ya kibuyu na kuning'inizwa kwenye vijiti vilivyopigiliwa ukutani na Moja kwa Moja anajua kuwa vitakuwa na dawa mbali mbali.Sebule haikuwa na vitu vingi vya jikoni akajua kuwa jiko litakuwa kwa bibi sumbo.
Akiwa anazungumza na mazingira ya mle ndani anamuona Nzagamba akienda karibu na mafiga anachuchumaa na kuanza kuuchochea Kuni zingine akiongezea na baada ya sekunde mafiga yanaanza kutoa Moshi yakionyesha uhai wa moto.Anasimama na kuchukua kibatari kilichokuwa juu ya ukuta.
" chumbani ni huku" anaongea akielekea chumbani na Tulya kumfuata nyuma kimya kimya mapigo ya moyo yakimwenda mbio mikono yake iliyoshikana Mbele kama imenaswa na ulimbo ikitoa jasho.
Wanaingia chumbani Nzagamba anaweka kibatari juu ya ukuta na kufanya mwanga wake kukiangazia chumba hicho.Tulya anaangaza macho yake mle chumbani na kuona kitanda kidogo Cha miti lakini Cha kutosha watu wawili kilichotengenezwa kwa kusokota kamba na kikiwa kimetandikwa ngozi juu yake.
Chumba hakikuwa kikubwa sana na hakikuwa na vitu vingi kutokana na aliyekuwa anakaa ni mwanaume tena kijana na sio kijana tu ni Nzagamba ambaye amejitupa na kujiona sio wa thamani kwa hiyo kuona vitu vingi humu ndani ni ingekuwa jambo la ajabu na angevitoa wapi.
Macho yake yanatoka alikokuwa anaangalia na kwenda kwa Nzagamba aliyesafisha Koo kumtaka amsikilize.Na Nzagamba alipoona anamwangalia akajua tayari anamsikiliza.
" utakuwa unalala hapa Mimi nitalala sebuleni"
Macho yanamtoka pima Tulya baada ya kusikia maneno ya Nzagamba " u-unamaanisha nini?" sauti nayo inaonyesha dhahiri mshtuko alioupata kwa kutoa kigugumuzi pale alipoongea mwili ukifa ngazi na kujihisi damu na maji vimepishana kazi.
Nzagamba anaona jinsi anavyomwangalia kwa mshtuko na woga " namaanisha nitalala sebuleni na wewe chumbani hapa kwa sababu.." kabla hajamalizia Tulya anamkatisha.
" kwa nini ufanye hivyo Mimi na wewe tumeoana tunatakiwa kulala chumba kimoja kitanda kimoja" anaongea mwili wake ukijawa ubaridi midomo yake ikimtetemeka macho yake yakijawa machozi yaliyotishia kuanguka na kumfanya aangalie ukutani huku akijikaza yasije yakamwaibisha kwa kufika kidevuni.
Lakini Nzagamba aliyaona hayo yote,akijua hakuna mwanamke ambaye angefurahi kukataliwa na mumewe usiku wa harusi yake lakini kwake yeye alikuwa na maana nzuri anayeijua mwenyewe kuwa ni nzuri kwa wote.lakini kabla hajaitoa Tulya anamshitua tena kwa kusema.
" Ndio unanichukia kiasi hicho"
Anaongea akihisi roho yake imepigwa mshale mara kumi,hakujua kama kukataliwa na mtu unayempenda Kuna maumivu kiasi hiki safari hii anaongea akimwangalia usoni pasipo kupepesa macho.
Roho ya Nzagamba inampwita asijue kwa nini maneno aliyoyaongea Tulya yamepita moyoni mwake kama sindano na kuchoma Kisha kuacha shimo dogo likivuja damu.
" ni kwamba tu Mimi na wewe hatujuani vizuri,nataka angalau Kila mtu awe na hisia na mwenzake ndio tuweze kupeleka uhusiano wetu kwenye hatua nyingine,sitaki kuwa na wewe kwa sababu natimiza wajibu wangu tu kwa sababu nimekuoa,pumzika utakuwa umechoka"
Hakumpa nafasi ya kuongea na kutoka chumbani akimwacha amesimama palepale,anausikia mlango wa nje ukifunguliwa na kufungwa akijua kuwa Nzagamba ametoka nje na kumwachia nyumba.Ni makosa ya nani hatujajuana vizuri kama sio yako,nilipokuwa ndani hukuja kunisalimia hata siku Moja Kila siku nilikuwa nakusubiri hukufika hata mara Moja hukufanya juhudi zozote Leo hii ndio unataka tujuane.
Ni maneno yaliyopita kichwani mwake akitamani angeyaongea kwa nguvu karibu na uso wake lakini aliamua kuyameza yote kwani anajua kwa namna hiyo angemkimbiza zaidi,angeenda mbali zaidi na hizo juhudi anazotaka kuzifanya zingekufa zote.
Licha ya Tulya kutokuweza kuuuzuia mdomo Wake anajua Mahali pa kurudi nyuma na wapi anatakiwa kusonga mbele,na vile vile mama yake na Somo wake walimfundisha vizuri kutokumpandishia mume wake sauti iwe ni kwa namna gani.
Sio kama huwa anamsikiliza mtu au ushauri wa mtu pale uvumilivu wake unapofika mwisho lakini Nzagamba ni wa tofauti sana kwake,ni mume wake,ni mwanaume anayempenda,ni mwanaume anayetaka kumfanya aanguke kwenye penzi zito kwake kama yeye alivyo,ni mwanaume ambaye anataka kumfanya aone Kuna mtu anayemjali kwenye dunia yake pweke hivyo anahitaji kumpatia heshima yake anayostaili.
" Angalau hajasema kama ananichukia kama hapo awali" anaongea kwa sauti ya chini.miguu yake inampeleka mpaka kitandani na kukaa,mawazo mengi yakipita kichwani kwake na mikakati mbalimbali yakuiendesha nyumba yake.
Nzagamba anasimama nje ya nyumba yake,mkono wake unaenda kifuani kwake Mahali ulipo moyo na kushika asijue kwa nini moyo unamuuma.sura ya Tulya inapita akilini mwake na kuona jinsi gani alivyokuwa ameumia lakini anafanya hivyo kwa ajili Yao wote,hataki kuwajibika kwa sababu tu amemuoa Tulya anataka kuwa sehemu ya maisha yake kwa kujipa nafasi kidogo ya kumtoa lindiwe moyoni mwake asije akamuumiza zaidi Tulya huko mbeleni.
Anaenda kwenye kitanda kama kichanja kilichopo uani kwake anapanda na kujilaza chali mkono wake mmoja ukiegemea kichwa chake macho yake anayafumba kidogo na kuyafumbua Moja kwa Moja yanaenda angani na huko yanakutana na anga lililojaa nyota tupu na mwezi mkubwa uliokuwa ukifanya usiku uonekane kama mchana.
Kwa mbali akizisikia sauti za ngoma zilizokuwa zikiendelea kupigwa sehemu walikosherehekea harusi Yao na watu wakiendelea kukesha wakinywa na kuufurahia harusi yao wakati wao wakipanga mikakati ya Mmoja kulala chumbani na mwingine sebuleni.wazo hili linamfanya acheke peke yake.Asijue amekaa hapo kwa mda gani mpaka alipoona mwili unapata baridi na kuamua kurudi ndani.
"umerudi" anamsikia Tulya akiongea chumbani baada tu ya kufunga mlango na sio mda anamuona anakuja sebuleni akiwa na kibatari mkononi.
" ulikuwa hujalala?" anamuuliza baada ya kumuona bado anamavazi yale ya mchana.
" mwanamke gani angelala usingizi baada ya mumewe kuondoka namna ile" tena siku ya usiku wao wa harusi anamalizia moyoni.
Nzagamba anamwangalia kwa mshangao hakujua kama alikuwa anamsubiri asijue kama alikuwa na wasiwasi au hakuwa na usingizi.
"sikuwa mbali nilikuwa tu hapo nje,vilevile ungelala tu kama hujui hata nitembee usiku wa manane hakuna kitakachonipata Mimi"
" hiyo haimaniishi Mimi nisiwe na wasiwasi juu yako tafadhali naomba usininyang'anye hata hiyo nafasi" anafumba macho yake na kufumbua akizuia hasira.
" nimewaza nimeamua kukubaliana na ulichokisena,nitakupatia hiyo nafasi unayotaka Ili tujuane zaidi,nitakusubiri kadri unavyotaka"
Nzagamba anamwangalia kwa mshangao zaidi kwani mwanamke huyu haishi kumshangaza Kila anapomuona.
" ngozi ziko wapi?"
" za nini?"
" Nahitaji kukutandikia hapo chini utalala kwenye sakafu tupu?"
" Haina shida nitaaanda mwenyewe wewe nenda kalele"
" kama umesahau ngoja nikukumbushe bwana Nzagamba,kwa Sasa umeoa na unatakiwa kuniacha Mimi kama mkeo kufanya majukumu yangu na mojawapo ni kuhakikisha uko sawa kwa hiyo naomba unionyeshe zilipo nikutengenezee Mahali pa kulala na Mimi nikalale kama hutaki tukeshe hapa"
" uvunguni mwa kitanda" anajibu haraka kupunguza maneno.
Tulya anarudi chumbani anaweka kibatari chake chini na kuinama uvunguni anavuta ngozi iliyokuwa humo na kuitoa,anaibeba na kutoka nayo sebuleni,anaweka kibatari juu ya ukuta na kutoka nje na ngozi, huko nje anaipiga piga kutoa vumbi.Ngozi ilikuwa na ukubwa wa kutosha kulala mtu Mmoja bila shaka anajua ni ngozi ya ng'ombe,anarudi nayo ndani na kutafuta Mahali pazuri anaitandika anageuka na kumuona Nzagamba tayari anakaniki mbili mkononi anajua alienda kuchukua alipokuwa nje.
Anachukua Moja na kuitanduka vizuri chini baada ya kumaliza anaangalia kama pamekaa vizuri baada ya kujiridhisha anaenda na kuuchochea moto uliokuwa unazima tena baada ya Nzagamba kuukoleza wakati wameingia,muda wote huo Nzagamba anamwangalia tu anavyofanya pilikapilika zake.
Anaupuliza moto na ulipowaka anasimama na kuchukua kibatari
" tayari,ila kesho itakubidi kuamka mapema maana sitaki mama akukute hapo"
Bibi sumbo au mtu yeyote angemkuta Nzagamba kalala chini sebuleni lawama zingeenda kwa Tulya Moja kwa Moja kwani yeye ndiye angeonekana kashindwa kumuhudumia mumewe hata kama angejitetea na kusema yeye ndio kaamua kulala sebuleni bado lawama zingekuwa zake kwamba kakosea ndio maana mumewe kamkimbia na hajafanya juhudi za kumrudisha chumbani,kwani siku zote mwanamke ndio mwenye makosa katika macho ya jamii na yeye hakutaka ndoa yake kutangaza kuwa na migogoro baada ya usiku Mmoja tu wa harusi.
Baada ya kuona haongei kitu anamtakia usiku mwema na kuelekea chumbani kwake akiwa na kibatari mkononi na kumwacha Nzagamba sebuleni akimulikiwa na mwanga wa moto aliokoka.Huko chumbani kwake anatoa shanga zake za shingoni na kichwani anapunguza na baadhi ya bangili alizovaa mkononi na kuweka juu ya sanduku lilitengenezwa kwa magome ya miti,anavua nguo alizokuwa amevaa na kubakiwa na nguo yake ya ndani kifua chake kikiwa wazi.akiwaza atabadilisha nini kwa sababu nguo zake hazijaja bado.Kwa Mila na desturi nguo zake zitaletwa kesho asubuhi na ndugu zake wanapokuja kusalimia na kutambulishana.kwa usiku wa ndoa bibi harusi huwa haruhusiwi kubadili nguo alizovaa kwani anatakiwa kuzivua Mbele ya mumewe wanapotimiza lengo la ndoa Yao na kesho kuzivaa tena kwenda kusalimia ndugu baada ya kurudi ndio abadilishe.
Lakini kwake ilikuwa tofauti kwani mumewe amelala sebuleni na yeye chumbani na hivyo anahitaji kubadili nguo Ili alale kwani hakuna mtu wa kumwangalia uzuri wa mwili wake hivyo hawezi kulala uchi.Macho yake yanaenda kitandani na kuona Kuna kaniki Moja tofauti na zingine zilizotandikwa kitandani na ile ya kujifunika.
hii ilikuwa imekunjwa vizuri na kuwekwa pembeni,anaenda na kuichukua anaifungua na kuikuata siyo kubwa sana kama zingine.Tabasamu linamtoka akijua Nzagamba atakuwa amemtolea kwa ajili ya kubadilisha,anafurahi moyoni na kujua angalau anamfikiria.anajifunga kaniki na kuzima taa anapanda kitandani na kulala.
Asubuhi ilipowadia Tulya anaamka mapema anavaa nguo zake za jana na kutoka sebuleni na kumkuta Nzagamba bado amelala anamfuata alipo na kumtikisa,Mara Moja tu na Nzagamba anafungua macho yake.
" kalale chumbani hapa mama atakuona nataka kufungua mlango.
Nzagamba anasimama na kutaka kuanza kukusanya virago pale chini lakini Tulya anamkataza.
" we nenda tu nitasafisha hapa,samahani kwa kukuamsha" Nzagamba anamwangalia kwa muda na Kisha kuitikia kwa kichwa na kuelekea chumbani.
Huku nyuma Tulya anakusanya kaniki iliyotandikwa na kuikunja baada ya kumaliza anaikunja na ngozi.anaingia Nazo chumbani na kuweka Kila kitu Mahali pake ikiwemo kurudisha ngozi uvunguni.Anajiangalia kama Yuko sawa na kutoka nje.kama mwanamke aliyeoleolewa au mwanamke yeyote ni wajibu wake kuamka mapema kabla ya watu wote wa nyumbani mwake kwa ajili ya kuchota maji,kufanya usafi na kuandaa kifungua kinywa kwa familia yake.
Ingekuwa kwa wafugaji na wakulima kazi za asubuhi zingekuwa nyingi zaidi,kukamua,kulima, na zinginezo lakini kwa wawindaji wanawake walikuwa na shughuli chache kidogo.Ile amesimama nje anajifikiria aanze na kazi ipi anamuona mama mkwe wake bibi sumbo akifika na kibuyu kichwani.
Macho yanamtoka pima Tulya akishangaa kaamka saa ngapi mpaka kaenda mtoni na kurudi ' naona Kuna kukimbizana riadha na mama mkwe Mimi nilijua nimewahi' anajiwazia moyoni lakini anajikaza na kwenda kumsalimia.
" shikamoo mama" anasalimia kwa heshima mguu wake mwingine akiukunja zaidi kupunguza makali ya kufokewa na mama mkwe kwa kushindwa kuamka mapema lakini mama mkwe wake anamshangaza.
" kwa nini umeamka mapema utakuwa umechoka,ungelala tu kazi zenyewe amna"
' ehh,mambo mbona yameenda tofauti na matarajio' anawaza Tulya.
" hapana mama Niko sawa,nikusaidie nini?"
" hauko sawa,ukifanya hivyo mjukuu nitapata mwaka gani"
" mjukuu?" Tulya anauliza kabla akili yake kufanya kazi na kujua anamaanisha nini,anainamisha kichwa kwa aibu moyoni akimjibu utasubiri sana kwa jinsi mambo yanavyoenda.
Bibi sumbo anacheka baada ya kumuona Tulya alivyoangalia chini kwa aibu " usijali nilikuwa nakutania tu,njoo huku nikuonyeshe ufanye usafi kwani ndugu zako watawahi kufika,mama yako aliniambia wanaondoka Leo hivyo ninauhakika itakuwa mapema zaidi"
Tulya anamfuata bibi sumbo ndani kwake moyo wake ukiwa mzito kidogo akiwaza kutokuwaona wazazi wake kwa mda mrefu na hii ikianza kumwingia akilini kuwa kweli ameolewa atakufa na kuzikwa huku.
Katikati ya milima inayoizunguka himaya ya Mpuli mwanga wa jua la asubuhi ukianza kuiangazia milima hiyo.Ndani ya pango Moja walikuwa wamekaa wanaume watatu wawili wakiwa ni wazee na kijana Mmoja.wakiwa wamevalia kaniki za ngozi wakifunga rubega, nyuso zao zikionyesha kuwa katika hali ya kuzungumzia jambo kubwa.
Na baada ya kimya kifupi Mzee Mmoja anaongea.
" Ameshao" na wengine wawili kumwangalia kwa mshangao na mshtuko.
" kweli? amefanikiwa kumpata yule mwanamke?" anauliza Mzee mwingine akimwangalia mwenzake kwa makini.
"ndio,nadhani sio sisi tu tuliokuwa tumechoka kusubiri hata wenzetu wa upande wa pili walikuwa wanechoka na wameharakisha mambo" anajibu Mzee wa kwanza aliyetoa taarifa ya uoaji na yule kijana akiwaangalia wazee hawa waliokuwa wanaonekana wanabusara kuliko yeye kutokana na nyuso zao zenye makunyanzi ya kuonyesha kuishi miaka mingi ya milima na mabonde.
" kwa hiyo itakuwa ni muda wa kuanza kazi Sasa" anaongea Mzee wa pili hii ikiwa kama siyo swali ila maelezo.
" hapana" anajibu Mzee wa kwanza anayeonekana kama kiongozi wao.
" kwa nini?kama kaoa si tayari ka kitu?" anauliza Mzee wa pili anayeonekana kutomuelewa mwenzake.
" kwa sababu hajaitimiza ndoa yake,angekuwa amefanya hivyo Kila kitu kingekuwa kimebadilika" safari hii kijana ndiye aliyeongea.
" ndio"Mzee wa kwanza anakubaliana na kijana na kuendelea "Mnelela nenda ukawe unamwangalia kama kutatokea mabadiliko yoyote utatuletea taarifa"
" ndio Manangwa"
anaitikia kijana kwa heshima na kusimama tayari kuianza safari yake.
" kumbuka unaangalia tu usifanye chochote kile" anaonya Mzee anayejulikana kama Manangwa ambaye ni mkuu wao na Mnelela anatoka mle pangoni na kuwaacha wazee wawili.
" je,wa upende wa tatu hawajajua?" Mzee wa pili anamuuliza Manangwa.
" bado,ila najua watakuwa wamehisi kwani Hali ya hewa imebadilika sana"
baada ya kimya kifupi Mzee Manangwa anasimama na kuvuta mkongojo wake na kusimama vizuri anavuta pumzi ndefu na kusema.
" sio muda Mambo yatabadilika,dhoruba kubwa kabla ya bahari kutulia"