Kinapita kimya kifupi mawazo ya Tulya yakifunikwa na Ndesha aliyepitia mambo magumu lakini hata hivyo hakuwa tayari kumpatia mtemi alichokuwa anakitaka.Alikuwa ni mwanamke shupavu sana anafikia muafaka Tulya.
" kwa nini wewe hukuwa mfinyazi?" anamuuliza akikumbuka kuwa alimwambia bibi yake alikuwa ni mfinyazi.
" nilikwambia kuwa udongo huchagua mtu wa kuushika,nilijaribu mwanzo nikaona sifanikiwi nikaacha,ukilazimisha vitu vingine utaingia tamaa tu"
Tulya anakubaliana naye akimkumbuka huyo mtemi aliyetaka madaraka kwa kulazimisha
"vipi wewe utaendelea kufinyanga?" anamsikia mama mkwe wake akimuuliza
" ndio,mama kasema siku akiwa anaenda porini ataniambia tuende wote"
" hivyo vyema"
Usiku huo Tulya akiwa amelala anaijikuta katikati ya pori,anaangaza huku na kule asione chochote,sauti za bundi na wadudu wengine wa usiku zikipenya masikioni mwake 'niko wapi?' anajiuliza.Baada ya muda anaanza kutembea akielekea hata kusikojulikana,miguu yake isiyokuwa na viatu inapiga hatua moja baada ya nyingine nyayo za miguu yake zikigusa majani yaliyokauka chini na kutoa sauti.
Anaangalia anga na kuona nyota nyingi angani zikiipamba mbingu angali ardhi ikiwa imetandwa na kiza kinene.' mbona kama usiku ulikuwa wa mbalamwezi wakati naenda kulala?' anajiuliza akiendelea kutembea mikono yake akijizungusha mabegani mwake akijikumbatia kujipatia joto kidogo kutokana na baridi iliyokuwa inampiga usiku huu.Baada ya mwendo wa mda mrefu anaona miale ya moto ikiangaza mbele yake,anapiga hatua za haraka mpaka anakaribia mahali pale.
Baada ya kufika anakuta idadi ya watu kama kumi wakiwa wamesimama chini ya mbuyu mkubwa na pembeni yake kukiwa na pango. mavazi Yao yakiwa tofauti na yake aliyovaa au ya watu wanaovaa kwa sasa.Watu Hawa wamevaa ngozi lakini zikiwa hazijatengenezwa vizuri kutoa manyoya yaani wamechuna tu ngozi kutoka kwenye mwili wa mnyama hawakuitengeneza kuifanya ilainike watoe na manyoya,wao wamevaa hivyo hivyo
" wanafanya nini Hawa usiku huu?" anajiuliza asipate majibu.Anasogea karibu na eneo lile na kujificha nyuma ya mti akiwaangalia.
" sijawajui hawa, ni akina nani?" anajiuliza huku akiendelea kuwaangalia " ngoja nikawaulize kama wanajua njia ya kuelekea nyumbani" anapata wazo.Lakini wakati anajiandaa kutekeleza wazi lake anafika mwanaume mwingine akiwa na mavazi tofauti na wale wengine " yule anaonekana kama mganga" anawaza baada ya kumuona akiwa ameshika vitu vya kiganga.
Mara anasikia makelele watu wengine wakiwa wanakuja eneo lile,punde anawaona wanaume wawili wakiwa wanamburuza mdada mdogo umri kama wake.
" niachieni,niachieni nimesema" anaongea yule dada.
" tulia wewe" anamnyamazisha mwanaume mmoja kati ya wale waliomshika.wanamfikisha mahali walipokuwa wengine na mwanaume mmoja kati ya wale wengine anamfuata Mahali aliposimama na yule dada akimwangalia yule mwanaume kwa chuki.
" hutakipata unachokitafuta nakuapia" anaongea yule dada kwa hasira.
" usijali kuhusu hilo kwani ukishaondoka huku nyuma Kila kitu kitakuwa sawa,usingejifanya mjanja haya yote yasingekukuta Ndesha,ulichotakiwa kufanya ni kukaa pembeni yangu tu ule mema ya nchi nawe ukaona ugumu,Sasa unaona hasara ya urembo wako" anaongea na kumshika uso wake.
Tulya anashtuka baada ya kusikia hilo jina na kujiuliza alisikia wapi lakini hakupata jibu nakuamua kuachana nalo.Anashtuliwa na yule dada kumtemea mate usoni yule mwanaume anayeonekana kuwa kiongozi
" ninakuhakikishia nikiwa marehemu au mzima hutakipata unachokita utakufa kwa tamaa zako"
Mwanaume anampiga Kofi Ndesha" kwanini usishuhudie hayo yote ukiwa kuzimu,mfungeni" anatoa amri mwanaume na kuangalia pembeni,wale wanaume wanamchukua na kumfunga kamba mikononi na miguuni kisha kumlaza juu ya jiwe lilikuwa na urefu kama meza kwa marefu na mapana hata kimo pia.
Punde wanatokea wanaume watatu wakiwa na mavazi yaliyotatuka wakiwa wamejifunga rubega." karibuni wakuu" anaongea yule mganga akiinamisha kichwa na wengine kufanya vilevile" yaani umefanya makubaliano na mizimu mibaya,mmelaniwa nyote" anaongea Ndesha baada ya kuwaona wale wanaume.
" kwa nini hamjamfunga mdomo huyu,ananipigia kelele" anaongea Mmoja kati ya wale wanaume akionekana kutokufurahishwa na kile alichokisema Ndesha" tusamehe mkuu,mnafanya nini mfungeni huyo" yule mganga anaamrisha na Mmoja kati ya wale wanaume anafanya haraka kwenda kumfunga.
" mmelaniwa nyote,nimesema" Ndesha anaendelea kuwalaani pale chini lakini wale hata hawakumsikia na yule mwanaume aliyeenda kumfunga alipomkaribia yule mwanaume aliyetoa amri afungwe mdomo anatoa ishara akiashiria wamuache.
" Kila kitu Kiko sawa mkuu" anaongea mganga
" nimeona" anajibu mwanaume aliyevaa nguo zilizotatuka.anazunguka na kupita upande wa kichwa cha Ndesha na kusimama,ananyoosha mikono yake juu na fumba fumbua kisu kinatua mkononi mwa yule mwanaume,anafumba macho yake na kunuia maneno ambayo hayakusikika hata kwa watu walio karibu yake itakuwa yeye aliyeko mbali.
Muda wote Tulya alikuwa anafuatilia kwa makini tukio lilikuwa linaendelea ' wanataka kumtoa kafara!" anawaza akiwa pale chini ya mti lakini kilichokuwa kinamshangaza ni yule mschana aliyelala pale juu ya jiwe pasipo kutoa sauti yeyote ile haogopi au anajiuliza, kwa hali kama ile pale anauhakika angekuwa yeye angeshajikojolea na makelele juu ya kuwapasua ngoma za masikio.
Wakati akiendelea kugombana na kihoro chake yule mwanaume aliyeshika kisu anakipitisha kisu kwenye Koo la Ndesha na kumkata koromeo damu nyingi zinaruka na kutapakaa juu ya jiwe na usoni kwa wale wanaume waliokuwa karibu.Tulya anashtuka pale alipo na mikono yake kukumbatia mdomo wake kuzuia asipige mayowe lakini kwa kushtuka kwake miguu yake inakosa nguvu kidogo aanguke anajizui na kurudi nyuma anakanyaga mti mkavu unatoa sauti na yule mwanaume kama amesikia anageuka upande wake kama amemuona anashtuka usingizini.
Tulya anakaa kitandani mwili ukimtetemeka jasho likimtoka mpaka kwenye fizi anahisi " kile kilikuwa nini?" anajiuliza akihema ndoto mbaya, lakini ilikuwa inaonekana kama kweli anajisemea kwani mwili ulikuwa unahisi Kila kitu kilichokuwa maeneo yale," lakini jina la yule dada mbona kama sio mara yangu ya kwanza kulisikia?" anajiuliza na akili yake inaanza kuzunguka alisikia wapi jina lile anakuja kukumbuka kuwa Bibi Sumbo alizungumzia mchana na yeye ameibeba hadithi kama ilivyo na kuipeleka kichwani kwake mpaka ameiota " hadithi za mama zitanitoa roho kwa namna hii" anawaza akijitupa kitandani na kujifunika kaniki yake gubi.
Asubuhi ilipowadia Tulya aliamka mapema zaidi kwani usingizi wake haukuwa mzuri,anatoka nje kufanya usafi baada ya kumaliza jua tayari lilikuwa limechomoza,anachukua kibuyu chake nakuelekea mtoni kuchota maji,njiani anakutana na wanawake wengine wa Kijijini wakimwangalia na kumjadili lakini hakujali,alichofanya ni kusalimia na kuchota maji aondoke zake anajua watu huongea tu hata usipowapatia sababu ya kuongea na itakuwa wakiipata huongea kama hakuna kesho.
Anarudi nyumbani na kumkuta mama mkwe wake na Nzagamba wakiwa wamekaa kwenye mkeka anamsalimia Bibi Sumbo.
" shikamoo mama"
" Marahaba,habari ya asubuhi?" anaitikia Bibi Sumbo
" asubuhi yangu ni njema mama" anaitikia
" hii ndio raha ya kuwa na mke mwana,siwezi kuamka asubuhi na mapema tena" Tulya anatoa tabasamu na macho yake kwenda kwa Nzagamba aliyekuwa akimwangalia muda wote tangu aingie bomani na yeye akajifanya kama hajamuona kwani angemwangalia sana anauhakika angeangusha kibuyu, kwani ndivyo uwepo wake na macho yake yalivyo na madhara makubwa mwilini mwake,moyoni na akilini hasa asubuhi hii iliyokuwa ikimfanya aonekane mtanashati zaidi,lakini mda wote huwa ni mtanashati machoni pako, moyo wake unamkosoa.Najua hilo kwani lazima unikumbushe naye anaujibu.
kuachana na hilo anamkazia macho na Nzagamba anaukimbiza uso wake na kuangalia kwingine kama mtu aliyekamatwa na kibuyu cha asali.Tulya anaachana naye na kuingia ndani kutua kibuyu chake na hakuchukua mda mrefu anatoka nje.
" angalia hivyo viazi jikoni kama vimeiva tuje kupata kifungua kinywa" Bibi Sumbo anamrudusha tena ndani.
Ndani Tulya anaangalia viazi jikoni na baada ya kuhakiki kuwa vimeiva,anachukua kisonzo kilichokuwa karibu na kuviweka baadhi humo mkono mwingine unachota maji kwenye kipeo na kutoka navyo nje.
wote wanakaa chini ya mkeka na kuanza kula.Lakini Tulya alikuwa anahisi viazi vikimkaba kutoka na macho ya mtu mmoja aliyekuwa amekaa pembeni yake.Macho ya Nzagamba yanamfanya kuhisi labda atakuwa ameamka na tongotongo kwenye macho yake lakini mbona nilinawa uso anajiuliza au Kuna kitu kimemganda usoni kwake bila kujua mkono wake unaenda usoni kujipangusa.
Kwa Nzagamba alikuwa anamuona Tulya akizidi kuwa mrembo Kila asipomuona hata kwa dakika tano akija kumuona anamuona ni mzuri kuliko ule mda mchache uliopita na asubuhi hii hali haikuwa tofauti na ukaribu waliyokuwa wamekaa ulikuwa hausaidii kabisa kwani Kila akijaribu kuyatoa macho yake kwake yanarudi hukohuko kama yanavutwa na sumaku." Nina matatizo gani Mimi?" anajiuliza akitikisa kichwa chake kujiridhisha kula viazi lakini hiyo haikuchukua hata dakika macho yake yanarudi kulekule yalikopata dawa ya kujisafisha kwani yamechoka kuona ulimbo na misitu huko mtoni Kila siku.Mabadiliko mara moja moja sio mbaya.